Hesperian Health Guides

Mshituko wa moyo

Katika sura hii:

Wanawake na wanaume pia hupatwa na tatizo la mshituko wa moyo. Mshituko wa moyo hutokea pale mtiririko wa damu kwenye moyo unaposimama kwa muda mrefu na kusababisha sehemu ya moyo kuanza kufa. Kawaida hii husababishwa na ugonjwa wa moyo. Kwa taarifa zaidi juu ya ugonjwa wa moyo, angalia Magonjwa yasiopona (kinaandaliwa).

Dalili
NWTND fa Page 27-1.png
  • Kusikia shinikizo, kubanwa, kukabwa, hisia ya kuugua, na maumivu kifuani, au kifua kujaa
  • Maumivu hayo yanaweza kuenea hadi shingoni, mabegani, mikononi, kwenye meno au taya
  • Maumivu kawaida huja taratibu lakini wakati mwingine yanaweza kuwa ya ghafla na makali
  • Pumzi nyepesi
  • Kutokwa jasho
  • Kichefuchefu


Maumivu kifuani ndiyo dalili kuu ya kawaida kwa ajili ya wanawake na wanaume, lakini wanawake mara nyingi hawahisi maumivu kifuani. Badala yake huhisi pumzi nyepesi, uchovu, kichefuchefu, kutapika, au maumivu mgongoni au kwenye taya.

Matibabu

Mpe kidonge 1 cha aspirini mara moja. Mwambie akitafune na kumeza na maji. Hata kama huna uhakika kwamba mtu anapata mshituko wa moyo, aspirini haitampa madhara.

Kama unayo, mpe dawa ya naitroglaserini (nitroglycerine) ambayo huwekwa chini ya ulimi ili iweze kuyeyuka na kufyonzwa na mwili. Mofini (morphine) pia husaidia kupunguza maumivu na woga. Mpe matumaini mgonjwa na tafuta msaada.