Hesperian Health Guides

Dharura kutokana na baridi kali

Katika sura hii:

Hipothemia (hypothermia) - kupigwa na baridi kali

Kupigwa na baridi kali kwa muda mrefu ni hatari sana kwa maisha yako. Hali hii inaweza kusababisha kuchanganyikiwa, kuathiri uwezo wako wa kufanya maamuzi na kufikiri vizuri.

Dalili
 • Kutetemeka
 • Kupumua haraka na mapigo ya moyo kuongezeka
 • Kuongea kwa taabu, goigoi
 • Kuchanganyikiwa
 • Kukojoa mara nyingi zaidi


Kadri hipothemia inavyozidi kuwa mbaya, kasi ya mapigo ya moyo na upumuaji huweza kupungua. Mtu anaweza kukaa chini, kuacha kutetemeka, na katika hali hiyo ya kuchanganyikiwa anaweza kuvua nguo zake. Hatimaye, anaweza kuzirai au hata kufariki.

Matibabu

Mpe pumzi ya kuokoa maisha kama inahitajika. Mtu ambaye ameshikwa na baridi kali anaweza kukaa muda mrefu bila kupumua. Hivyo, anaweza kuhitaji pumzi za kuokoa maisha kwa saa 1 au zaidi.

 • Mhamishie sehemu kavu na yenye joto la kutosha.
 • Ondoa nguo zilizoloa.
 • Mfunike kwa blanketi kavu na lenye joto la kutosha. Hakikisha unamfunika kichwa, mikono na miguu.
 • Fanya kila unaloweza ili apate joto la kutosha wakati wote. Mkumbatie mgonjwa, tumia mawe ya moto na chupa za maji ya moto kumuongezea joto. Chukua tahadhari ngozi isiungue.
Mgonjwa akitibiwa hipothemia.
Nguo na blanketi kavu na kofia
Joto la mwili (mawe ya moto au chupa zenye maji ya moto)
Vinywaji vitamu vya moto
Blanketi zilizokunjwa au kadibodi kumkinga dhidi ya sakafu baridi.

Kama mgonjwa anaweza kukaa na kushika kikombe, mpe vinywaji vya moto, mfano chai. Usimpe pombe. Ingawa pombe inaweza kutoa hisia za joto kooni au tumboni, pombe pia husababisha mwili kupoteza joto. Pia mpe chakula. Peremende na pipi za kawaida zina umuhimu wa pekee. Mpe mlo mara baada ya hapo. Mtie moyo atumie maji mengi.

Kama mgonjwa ana hipothemia kali —joto la mwili nyuzijoto 32° sentigredi (90°Fareinheti) au chini ya hapo, amepoteza fahamu, hatetemeki tena—kuwa mpole kadri uwezavyo wakati unamsafirisha haraka kutafuta msaada wa kitabibu.

Ugonjwa wa kuganda misuli kutokana na jalidi au theluji kali (frostbite)

Vidole vya mikono na miguu, masikio, na viungo vingine vya mwili vinaweza kuganda. Mwishowe, ”hufa,” na kugeuka vyeusi. Kama utachukua hatua baada ya kugundua dalili ya kwanza ya ugonjwa wa jalidi, unaweza kuokoa viungo hivi ambavyo vingeweza kuondolewa.

Dalili

 • Ngozi baridi, inanata, imepauka, na kuweka alama au madoa madoa
 • Hisia za mchonjoto au kuwashwa, kufaa ganzi, au maumivu
 • Kiungo cha mwili kinaweza kuganda na kuwa kigumu


Ugonjwa wa jalidi wa kawaida hubadilisha mwili kuwa mwekundu. Baada ya siku chache ngozi huanza kutoa gamba. Kama madhara yameenda ndani, ugonjwa wa jalidi huacha ngozi ikiwa ngumu kwa juu, lakini laini kwa chini. Malengelenge yanaweza kujitokeza siku inayofuata. Msuli unapoganda, ugonjwa wa jalidi huenda ndani. Sehemu inakuwa ngumu. Inaweza kuwa na vipele pembeni tu, au isiwe na vipele kabisa. Malengelenge yanaweza kujaa damu.

Matibabu

Mwanamke amekunja mikono yake na kuiingiza kwenye shati.

Jiondoe kwenye mazingira baridi haraka na kuipasha joto sehemu iliyoganda. Kwa vidole, kitu rahisi zaidi kufanya ni mtu kukunja mikono yake na kuiingiza kwapani au katikati ya mapaja. Au funika sehemu iliyoganda kwenye nguo kavu zenye joto. Acha sehemu iliyoganda katika nafasi moja na epuka kutembeza miguu ambayo tayari imeathirika kutokana na ugonjwa wa jalidi.

Kwa ugonjwa wa jalidi ambao umeenda ndani, jaza beseni na maji yenye vuguvugu (siyo ya moto). Kama una kipimajoto, jaribu kupata maji yenye nyuzijoto 39° sentigredi (102°F.). Loweka sehemu iliyoganda kwenye maji. Kwa uangalifu, gusa maji kwanza kuzuia kuungua. Usisugue.

Sehemu iliyoganda inapaswa kuachia (kuyeyuka) ndani ya dakika 45. Kadri inapopata joto, itauma. Mpe dawa ya kupunguza. Usiruhusu viungo kuganda tena.

Ni bora kuruhusu sehemu ya mwili kubaki ikiwa imeganda kuliko kuyeyusha ubaridi na kuiachia kuganda tena.


Kadri ugonjwa wa jalidi unapokuwa unapona katika kipindi cha siku au wiki kadhaa, tibu kama jinsi unavyotibu jeraha la moto.

Mmea wa Alovera.
Alovera husaidia kutibu ugonjwa wa jalidi na majeraha ya moto.