Hesperian Health Guides

Dharura zinazohusiana na ugonjwa wa kisukari

Katika sura hii:

Kisukari ni ugonjwa ambao unaathiri uwezo wa mwili wa kuchakata sukari iliyopo kwenye chakula. Mtu mwenye tatizo la kisukari anaweza kuugua ghafla kiwango cha sukari kwenye damu yake kinapopanda sana au kupungua sana kulingana na kiasi kinachostahili. Ugonjwa wa kisukari hujitokeza zaidi miongoni mwa watu wanene, lakini mtu yeyote anaweza kupata kisukari.

Kama unajua mtu ana tatizo linalotokana na kisukari lakini huna uhakika kama tatizo hilo linatokana na kiwango kidogo cha sukari kwenye damu, au kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu, mtibu kama vile ana kiwango kidogo cha sukari na baada ya hapo mpeleke kupata matibabu kamili.

Kiwango kidogo cha sukari kwenye damu (hipoglisemia-hypoglycemia)

Kiwango cha sukari kwenye damu kinaweza kushuka sana kama mtu atakuwa anatumia dawa ya insulini, au tiba nyingine ya kisukari na kama atatumia kiasi kikubwa cha dawa, hali chakula cha kutosha, hajishugulishi kimwili au kimazoezi, hukaa muda mrefu bila kula, au ni mnywaji wa pombe.

Mtu mwenye kiwango kidogo cha sukari katika damu yake anaweza kuwa mzito au goigoi, kuchanganyikiwa, mwenye wasiwasi au kuudhika upesi. Anaweza pia kuwa anatokwa na jasho sana au kutetemeka. Hali hii inapotokea, anapaswa kula angalau chochote. Kama hatapata chochote, hali yake inaweza kuwa mbaya zaidi na kuanza kuonesha dalili za hatari zifuatazo:

Mwanaume akipata shida kutembea wakati mwanamke akimpita bila kujali.
Kiwango kidogo cha sukari kwenye damu kinaweza kujionesha kama mtu aliyelewa pombe na tatizo hili linaweza kupuuzwa au kutochukuliwa kama dharura.
Dalili za hatari
  • Shida katika kutembea au kujisikia mdhaifu
  • Uoni hafifu
  • Kuchanganyikiwa au kutenda mambo kwa njia za ajabu (unaweza kufikiria amelewa)
  • Kupoteza fahamu
  • Dalili zinazofanana na za kifafa


Matibabu

Kama bado ana fahamu, haraka mpe sukari: juisi ya matunda, soda, au glasi ya maji ambayo yamechangaywa na vijiko kadhaa vya sukari. Anapaswa pia kula mlo kamili baada ya hapo. Kama bado amechanganyikiwa au hajaanza kujisikia nafuu dakika 15 baada ya kumpa sukari, tafuta msaada.

Kama hana fahamu, weka kiasi kidogo (mfinyo mmoja wa vidole vyako ) cha chumvi au asali chini ya ulimi wake. Endelea kumpatia vitu hivyo kidogo kidogo. Mwili huchukua muda kufyonza sukari hiyo. Atakapoamka unaweza kumpa zaidi.

Kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu (haipaglisemia-hyperglycemia)

Mtu mwenye kisukari anaweza kuwa na kiasi kikubwa cha sukari kwenye damu yake kama atakuwa anakula chakula kingi kuliko kinachohitajika, hajishughulishi kimwili au kimazoezi, ana ugonjwa mkubwa au maambukizi, hatumii dawa za kudhibiti kisukari, au hupungukiwa na maji mwilini. Hali hii inaweza kumpata mtu hata kama bado hajajua kuwa ana kusukari. Tafuta msaada wa kitabibu utakapoona dalili zifuatazo:

Dalili
  • Kusikia kiu na kunywa maji mengi
  • Kukojoa mara kwa mara
  • Uoni hafifu
  • Kupungua uzito
  • Kichefuchefu na kutapika
  • Maumivu ya tumbo


Kama hatatibiwa, kiasi kikubwa cha sukari kwenye damu ni hatari na kinaweza kusababisha kuzimia au hata kifo. Unaweza kuokoa uhai wa mtu kwa kumsaidia kukabiliana na dalili hatari sana zifuatazo:

Dalili za hatari
  • Mapigo ya moyo kwenda mbio
  • Pumzi yenye harufu ya matunda
  • Ngozi kukauka
  • Shinikizo la damu la chini
  • Kuchanganyikiwa
  • Pumzi nzito za haraka
  • Kupoteza fahamu
Matibabu

Mpeleke haraka hospitalini au kwenye kituo cha afya. Kama ana fahamu, mpe maji mengi ya kunywa. Mpe kidogo kidogo kila wakati.

Kama una uhakika ana shinikizo la juu la damu na unajua dozi yake ya insulini, mpe kiasi kidogo cha insulini mnapokua njiani kuelekea hospitalini ili iweze kumpatia nafuu. Kumpa insulini mtu ambaye ana shinikizo la chini la damu ni hatari na kunaweza kusababisha kupoteza maisha.



Ukurasa huu ulihuishwa: 14 Feb 2024