Hesperian Health Guides

Majeraha ya kichwa

Katika sura hii:

Kama mtu ataanguka, kupigwa na kitu kigumu kichwani,au amejeruhiwa katika ajali ya gari, chunguza iwapo kuna dalili za jeraha kwenye ubongo. Inaweza kuwa vigumu kubaini iwapo kuna jeraha kwenye ubongo kama majeruhi amekua akitumia pombe au madawa ya kulevya kwa sababu dalili za vitu vyote hivi zinafanana. Pia chunguza yeyote mwenye jeraha kichwani kama ana majeraha ya shingo au uti wa mgongo, kwa sababu majeraha hayo 2 yanaweza kutokea pamoja.

Dalili za jeraha lisilo kali kwenye ubongo
 • Kuchanganyikiwa au kupoteza fahamu, hali ambayo inaweza kupungua yenyewe baada ya muda mfupi
 • Kutokumbuka kilichotokea
 • Kutoona vizuri kwa muda au kuona maruweruwe
 • Kichefuchefu au kutapika ambako hakudumu muda mrefu
 • Maumivu ya kichwa, kizunguzungu au uchovu


Apumzike angalau kwa saa 24 na kutumia dawa baridi ya kupunguza maumivu kama vile parasetamo au asetaminofeni (acetaminophen), lakini asitumie ibuprofeni au aspirini kwa sababu inaweza kuzidisha uvujaji damu ndani ya kichwa. Mwangalie kwa karibu mgonjwa kwa saa 24 za mwanzo. Kama atalala, mwamshe kila baada ya saa chache kuona iwapo bado anaweza kujibu maswali na kufikiri vizuri. Ndani ya saa kadhaa baada ya kujeruhiwa, kama mgonjwa atazidi kuchanganyikiwa, kusikia maumivu kichwani ambayo huendelea kuzidi, au kupoteza fahamu, au kupatwa aina ya kifafa, kuna uwezekano wa uvujaji damu ndani ya fuvu la kichwa na msaada wa haraka utahitajika.

Dalili za jeraha kali kwenye ubongo

Tafuta msaada haraka kwa dalili zifuatazo:

 • Kupoteza fahamu
 • Maumivu makali ya kichwa, mabadiliko katika uoni, kupoteza uwezo wa kusimama au kutembea bila kuanguka
 • Kichefuchefu na kutapika
 • Kuchanganyikiwa, mabadiliko katika nafsi,ushari au ugomvi
 • Mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida (yanasuasua au kwenda kasi sana)
 • Pumzi fupi za haraka au kupumua kusiko kwa kawaida (wakati mwingine haraka na mwingine polepole)
 • Ngozi yenye joto kiasi ikiwa na upele
 • Dalili zinazofanana na za kifafa
 • Damu au majimaji yasiyo na rangi kutoka masikioni au puani


Dalili zifuatazo zinaweza kujitokeza saa kadhaa baada ya jeraha:

 • Mboni moja ya jicho inakuwa kubwa kuliko nyingine
jicho lenye mboni kubwa sana. jicho lenye mboni kidogo kuliko lingine.
 • Michubuko kuzunguka macho yote au nyuma ya sikio
NWTND fa Page 23-3.png
NWTND fa Page 23-4.png

Uvujaji damu kutoka kichwani

Vidonda vya kichwani hutoa sana damu. Kama una uhakika kuwa hakuna jeraha kwenye uti wa mgongo, mwambie mgonjwa akae wima au msaidie kumkalisha, ili kupunguza uvujaji damu. Tumia mgandamizo kusimamisha uvujaji damu, baada ya hapo safisha kidonda vizuri kabla ya kukifunga kwa kushonwa au na gundi. Kama huna vifaa na majeruhi ana nywele ndefu, unaweza kufunga nywele hizo juu ya kidonda na kukifunika kama kwenye mchoro:

Mafungu 2 ya nywele ndefu yakifungwa pamoja juu ya kidonda.


Kama kuna mpasuko kichwani, angalia kama umeendelea hadi kwenye fuvu chini yake. Kama unadhani kuna mpasuko kwenye fuvu, bonyeza kwa uangalifu kila upande wa kidonda, ukiepuka kubonyeza sana upande wa kichwa wenye jeraha.

Kutokwa na damu puani

Mtu ameinamisha kichwa mbele akiwa amefinya pua yake.

Finya pua kwa nguvu, chini kidogo ya mfupa mgumu wa pua.

Finya pua kwa nguvu kwa dakika 10 — usiachie kufinya hata kama ni kuangalia iwapo damu imesimama. Au kama sivyo damu itaanza kutoka tena. Kama pua itaendelea kuvuja damu baada ya dakika 10, endelea kufinya pua kwa dakika 10 zaidi.

Ingawa utokaji damu puani hatimaye hupungua wenyewe, ni hatari ukiachiwa bila kudhibitiwa. Kuwa mwangalifu na utokaji damu puani hasa miongoni mwa watu wenye umri mkubwa.

Uzuiaji

Kupaka mafuta ya jeli kidogo ndani ya pua kunaweza kupunguza hali ya ukavu ambayo inaweza kusababisha kutokwa na damu. Kuichokonoa pua kwa sababu yoyote ile ni chanzo cha kawaida cha damu kutoka puani.