Hesperian Health Guides

Huduma ya kwanza: Dawa

Antibiotiki

Antibiotiki ni dawa za kupambana na maambukizi kutokana na bakteria. Hazisaidii dhidi ya maambukizi kutokana na virusi kama vile tetekuwanga (chicken pox), rubella, mafua makali (flu), au mafua ya kawaida. Siyo dawa zote za antibiotiki zina uwezo wa kupambana na maambukizi yanayosababishwa na bakteria.

Antibiotiki ambazo zina muundo wa kikemikali unaofanana huchukuliwa kuwa za familia moja. Ni muhimu kuwa na ufahamu juu ya familia tofauti za antibiotiki kwa sababu 2 muhimu:

 1. Antibiotiki kutoka familia moja mara nyingi huweza kutibu matatizo yanayofanana. Hii inamaanisha kuwa unaweza kutumia dawa tofauti kutoka familia moja.
 2. Kama una mzio na antibiotiki kutokana na dawa ya antibiotiki ya familia moja, utaweza kupata mzio pia kutokana na dawa zingine kutoka familia hiyo. Hii inamaanisha kuwa siyo tu kwamba utahitaji kutumia dawa tofauti, lakini dawa kutoka familia tofauti kama mbadala.


Dawa ya antibiotiki inapaswa kutolewa kwa dozi kamilifu. Kusimamisha dawa kabla kujakamilisha siku zote za matibabu, hata kama unajisikia nafuu, huweza kuyafanya maambukizi kurudi katika mfumo ambao ni mgumu zaidi kutibiwa.

Penisilini

Dawa kutoka familia ya penisilini ni miongoni mwa dawa muhimu sana za antibiotiki. Penisilini hupambana na maambukizi mengi, yakiwemo yale yanayosababisha usaha.

Penisilini hupimwa kwa miligramu (mg) au uniti (U). Kwa aina ya penisilini G, miligramu 250 = 400,000 U.

Kwa watu wengi, penisilini ni miongoni mwa dawa salama. Kutumia zaidi ya kiasi cha dawa kilichopendekezwa ni kupoteza fedha lakini mara nyingi haimuathiri mtumiaji.

Usugu kwa dawa ya penisilini

Baadhi ya maambukizi yamejenga usugu kwa dawa ya penisilini. Hii inamaanisha kuwa zamani penisilini ingeweza kumponya mtu mwenye maambukizi hayo, lakini kwa sasa haiwezi kumtibu akapona. Kama maambukizi hayatibiwi na penisilini ya kawaida, jaribu aina nyingine ya penisilini au antibiotiki kutoka familia nyingine. Kwa mfano, nimonia wakati mwingine ni sugu kwa penisilini. Jaribu kotrimozazo (cotrimoxazole) au erithromaisini (erythromycin).

MuhimuNBgrnimportant.png
Kwa penisilini za aina zote (ikiwemo ampisilini na amoksilini)

Baadhi ya watu hupatwa na mzio wanapotumia dawa ya penisilini. Mzio wa kawaida husababisha upele. Mara nyingi upele huo hujitokeza saa au siku kadhaa baada ya kutumia penisilini na inaweza kudumu kwa siku kadhaa. Simamisha matumizi ya penisilini mara moja mara utakapoona mojawapo ya dalili hizo. Dawa ya antihistamini (antihistamines) husaidia kupunguza mwasho. Mvurugano tumboni na kuharisha kutokana na kutumia penisilini siyo dalili za mzio na, ingawa ni kero, zisiwe sababu za kusimamisha matumizi ya dawa hiyo.

Kwa nadra, penisilini husababisha mshituko kutokana na mzio. Ndani ya dakika au saa chache baada ya kutumia penisilini, mtumiaji anaweza kuiva usoni, koo na midomo kuvimba, kupata shida katika kupumua, kujisikia dhaifu, na kuingia katika hali ya mshituko. Hii ni hatari sana. Anapaswa kuchomwa sindano ya epinefrini (adrenalin) mara moja. Kila mara weka dawa ya epinefrini tayari unapochoma sindano ya penisilini.

Mtu yeyote ambaye aliwahi kupatwa na mzio kutokana na penisilini hapaswi kupewa tena aina yoyote nyingine ya penisilini—ampisilini, amoksilini, au penisilini zingine, iwe kwa mdomo au kwa sindano. Hii ni kwa sababu akipewa dawa hiyo mara nyingine, mzio unaweza kuwa mkali sana na wenye uwezo wa kumsababishia kifo. Watu wenye mzio kutokana na penisilini wanaweza kutumia erithromaisini (erythromycin) au dawa za antibiotiki nyingine.

Sindano

Penisilini kawaida hufanya kazi vizuri inapotolewa kwa njia ya mdomo. Sindano za penisilini zinaweza kuwa hatari. Zinaweza kusababisha mzio mkali na matatizo mengine, na zinapaswa kutolewa kwa uangalifu. Tumia sindano ya penisilini tu kwa ajili ya maambukizi makali au hatari.

Ampisilini na amoksilini


Ampisilini na amoksilini ni penisilini zenye wigo mpana wa tiba, hii ikimaanisha kuwa zinaweza kuua aina nyingi za bakteria. Dawa hizi mbili zinaweza kutumika moja mbadala wa nyingine. Ukiona mahali ilipoelekezwa kutumia ampisilini katika kitabu hiki, unaweza kutumia amoksilini katika nafasi yake, kwa kuzingatia dozi sahihi.

Ampisilini na amoksilini kawaida ni dawa inayosaidia sana hususan watoto wachanga na watoto wadogo.

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Dawa hizi mbili, lakini hasa ampisilini, zina mwelekeo wa kusababisha kichefuchefu na kuharisha. Epuka kuwapa watu ambao tayari wanaharisha kama unaweza kuwapa antibiotiki mbadala. Madhara mengine ya pembeni ni ukurutu. Lakini vimbe kubwa zinazowasha ambazo huja na kutoweka ndani ya saa kadhaa huenda nazo ni dalili ya mzio wa penisilini. Simamisha utoaji wa dawa mara moja na usiwape dawa ya penisilini tena. Mzio utakaowapata siku zijazo unaweza kuwa mkali sana na kuhatarisha maisha. Kwa baadhi ya matatizo, erithromaisini (erythromycin) inaweza kutumika kama mbadala. Ukurutu uliyoenea ambao unafanana na ule wa surua, na kawaida ukijitokeza wiki moja baada ya kuanza dawa na kuchukua siku kadhaa kutoweka, usichukuliwe moja kwa moja kuwa dalili ya mzio. Hivyo, kwa vile ni vigumu kujua kwa uhakika iwapo ukurutu huo unatokana na mzio au la, ni bora kusimamisha dawa.

MuhimuNBgrnimportant.png
Usugu kwa dawa ya ampisilini na amoksilini unazidi kuongezeka. Kutegemea na mahali unapoishi, dawa hizi huenda zisifanye kazi tena dhidi stafilikokasi (staphylococcus), shigella, na maambukizi mengine.


Jinsi ya kutumiaNBgrninjectpill.png

Ampisilini na amoksilini hufanya kazi vizuri zaidi zinapotumiwa kwa njia ya mdomo. Sindano ya Ampisillini pia inaweza kutolewa dhidi ya magonjwa makali.

Kama ilivyo kwa dawa za antibiotiki zingine, kila mara toa dawa hizi angalau kwa siku chache zilizooneshwa hapa. Kama mtu bado ana dalili za maambukizi, msaidie aendelee kutumia kiasi kile kile cha dawa kila siku hadi dalili zote zitapokuwa zimepotea angalau kwa saa 24. Kama mtu atakuwa ametumia dawa kwa muda na dozi ya juu zaidi kama ilivyoelekezwa na bado anaumwa, simamisha kumpa dawa hiyo ya antibiotiki na tafuta msaada wa daktari.

Kwa watu wenye VVU, toa dawa kwa ajili ya siku zote zilizoelekezwa. Vilevile, kiasi cha dawa ya antibiotiki anachopaswa kutumia mgonjwa hutegemea umri au uzito wake na ukali wa maambukizi. Kuna kiwango cha dawa ambacho kinapaswa kutolewa. Kwa ujumla, toa dozi ya chini kwenye kiwango cha matibabu kilichopendekezwa kwa mtu mwembamba au kwa maambukizi yasiyo makali sana, na dozi ya juu kwa mtu mwenye mwili na uzito mkubwa au dhidi ya maambukizi makali sana.

AMOKSILINI (KWA NJIA YA MDOMO)

Toa miligramu 45 hadi 50 kwa kilo kwa siku, ikigawanywa katika dozi 2 kwa siku.

Kama huwezi kumpima mtu, mpe dozi kulingana na umri:
Chini ya miezi 3: mpe miligramu 125, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Miezi 3 hadi miaka 3: mpe miligramu 250, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Miaka 4 hadi 7: mpe miligramu 375, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Miaka 8 hadi 12: mpe miligramu 500, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Zaidi ya miaka 12: mpe miligramu 500 hadi 875, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
AMPISILINI (KWA NJIA YA MDOMO)
Toa miligramu 50 hadi 100 kwa kilo kwa siku, ikigawanywa katika dozi 4 kwa siku. Kama huwezi kumpima mtu, mpe dozi kulingana na umri:
Chini ya mwaka 1: mpe miligramu 100, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Mwaka 1 hadi miaka 3: miligramu 125, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Miaka 4 hadi 7: miligramu 250, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Miaka 8 hadi 12: miligramu 375, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Zaidi ya miaka 12: miligramu 500, mara 4 kila siku kwa siku 7.
AMPISILINI (KWA NJIA YA SINDANO)
Ampisilini inapaswa kutolewa kwa njia ya sindano tu kwa maambukizi makali, au iwapo mgonjwa anatapika au hawezi kumeza.
Choma miligramu 100 hadi 200 kwa kilo kwa siku, dawa ikiwa imegawanya katika dozi 4 kwa siku. Kama huwezi kumpima mgonjwa, mpe dozi kulingana na umri:
Chini ya mwaka 1: choma miligramu 100, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Mwaka 1 hadi miaka 5: choma miligramu 300, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Miaka 6 hadi 12: choma miligramu 625, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Zaidi ya miaka 12: choma miligramu 875, mara 4 kila siku kwa siku 7.

Amoksilini yenye asidi ya klavulaniki
(amoxicillin-clavulanate potassium)


Amoksilini yenye asidi ya klavulaniki ndani yake (clavulanic acid)huja katika vipimo vyenye nguvu tofauti ya kila dawa mojawapo. Kwa mfano inaweza kuwa 250/125 (maana yake miligramu 250 za amoksilini na miligramu 125 za asidi ya klavulaniki ) au 500/125, au 875/125. Dozi hufafanuliwa kwa vipimo vya amoksilini kama inavyooneshwa hapo:

Mpe kwa njia ya mdomo na chakula au maziwa.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpillspoon.png

Kwa majeraha ya kuumwa au kung’atwa na wanyama

Mpe miligramu 25 hadi 45 kwa kilo kila siku, ikigawanywa katika dozi 2. Kama huwezi kumpima uzito, mpe dozi kwa kuzingatia umri:
Chini ya miezi 3: mpe miligramu 75, mara mbili kwa siku 3 hadi 5.
Miezi 3 hadi mwaka 1: mpe miligramu 100, mara 2 kila siku kwa siku 3 hadi 5.
Mwaka 1 hadi 5: mpe miligramu 125, mara 2 kila siku kwa siku 3 hadi 5.
Miaka 6 hadi 12: mpe miligramu 300, mara 2 kila siku kwa siku 3 hadi 5.
Zaidi ya miaka 12: mpe miligramu 600, mara 2 kila siku kwa siku 3 hadi 5.

Penisilini kwa njia ya mdomo, penisilini V, penisilini VK


Penisilini kwa njia ya mdomo (badala ya sindano) inaweza kutumika kwa ajili ya maambukizi ya kawaida na maambukizi makali.

Hata kama ulianza na penisilini ya sindano kwa ajili ya maambukizi makali,unaweza kufuatisha penisilini kwa njia ya mdomo mara mgonjwa atakapoonesha dalili za kupata nafuu. Kama hapati nafuu ndani ya siku 2 au 3, fikiria kumuanzishia antibiotiki nyingine na tafuta msaada wa kitabibu.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png

Ili kuusaidia mwili kuitumia vizuri dawa, tumia dawa ya penisilini kabla hujala chochote, angalau saa 1 kabla au saa 2 baada ya kula.

Mpe miligramu 25 hadi 50 kwa kilo kila siku, ikigawanywa katika dozi 4, kwa siku 10. Kama huwezi kumpima mgonjwa, mpe dawa kwa kuzingatia umri:
Chini ya mwaka 1: mpe miligramu 62, mara 4 kila siku kwa siku 10.
Mwaka 1 hadi 5: mpe miligramu 125, mara 4 kila siku kwa siku 10.
Miaka 6 hadi 12: mpe miligramu 125 hadi 250, mara 4 kila siku kwa siku 10.
Zaidi ya ya miaka 12: mpe miligramu 250 hadi 500, mara 4 kila siku kwa siku 10.

Kwa ajili ya maambukizi makali, zidisha dozi juu mara 2. Usitoe zaidi ya uniti 4,800,000 kwa siku.

Kwa ajili ya kidonda ambacho huenda kimeambukizwa na tetanasi, baada ya kutoa penisilini G kwa siku 2, fuatisha penisilini V katika dozi iliyopendekezwa hapo juu kwa siku zaidi 5 hadi 8.

Kwa majeraha kutokana na kuumwa au kunga’twa na wanyama, mpe dozi iliyopendekezwa hapo juu kwa siku 3 hadi 5. Pia mpe metronidazo AU kilindamaisini.

Penisilini kwa njia ya sindano, penisilini G


Sindano ya penisilini inapaswa kutumika kwa ajili ya maambukizi makali yakiwemo tetanasi.

Penisilini kwa njia ya sindano huja katika miundo tofauti. Tofauti kubwa ni muda gani dawa hiyo hukaa mwilini: muda mfupi, muda wa kati, au muda mrefu.

Jinsi ya kutumiaNBgrninject.png

Prokeni penisilini (PROCAINE PENICILLIN, prokeni benzilpenisilini (PROCAINE BENZYLPENICILLIN) hukaa mwilini kwa muda mrefu kiasi.

Choma kwenye msuli tu, siyo kwenye mshipa wa damu.

Mpe uniti 25,000 hadi 50,000 kwa kilo kwa siku. Usitoe zaidi ya uniti 4,800,000. Kama huwezi kumpima mgonjwa mpe dozi kwa kuzingatia umri:
Miezi 2 hadi miaka 3: choma uniti 150,000, mara 1 kwa siku kwa siku 10 hadi 15.
Miaka 4 hadi 7: choma uniti 300,000, mara 1 kwa siku kwa siku 10 hadi 15.
Miaka 8 hadi 12: choma uniti 600,000, mara 1 kwa siku kwa siku 10 hadi 15.
Zaidi ya miaka 12: choma uniti 600,000 hadi 4,800,000, mara 1 kwa siku kwa siku 10 hadi 15.
Usitoe kwa watoto wadogo chini ya miezi 2 isipokuwa kama hakuna aina nyingine ya penisilini au ampisilini.Kama hii ndiyo dawa pekee iliyopo, choma uniti 50,000,mara 1 kwa siku kwa siku 10 hadi 15.

Kwa ajili ya maambukizi makali katika umri wowote ule, zidisha dozi iliopendekezwa juu mara 2. Usitoe zaidi ya uniti 4,800,000 kwa siku.

Kwa ajili ya kidonda ambacho kinaweza kuwa kimeambukizwa tetanasi, mpe dozi iliopendekezwa juu kwa siku 7 hadi 10. AU, mpe dozi iliopendekezwa juu kwa siku 2, baada ya hapo fuatisha na penisilini kwa njia ya mdomo. Pia mpe dawa nyingine dhidi ya tetanasi - antitetanus immunoglobulin.

Kloksasilini (cloxacillin)


Kloksasilini ni aina ya penisilini, na ambayo wakati mwingine inaweza kutumika kwa ajili ya maambukizi ambayo yamekuwa sugu kwa penisilini, kama vile vidonda vyenye usaha kwenye ngozi, na maambukizi ya mifupa. Kama huna kloksasilini, diklosasilini inaweza kutumika kama mbadala.

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Kichefuchefu, kutapika, kuhara, homa, na maumivu ya viungo.

MuhimuNBgrnimportant.png
 • Usitoe kwa mtu ambaye ana mzio kutokana na penisilini.
 • Dawa hii inaweza kuathiri ufanisi wa vidonge vya majira. Kama inawezekana tumia njia nyingine ya kupanga uzazi (kama vile kondomu) utakapokuwa unatumia dawa hii.
Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png

Kwa ajili ya maambukizi mengi

Kwa watoto wadogo, toa miligramu 25 hadi 50 kwa kilo, ikiwa imegawanywa katika dozi 4 kwa siku. Kwa watu wazima toa miligramu 50 hadi 100 kwa kilo, ikiwa imegawanywa katika dozi 4 kwa siku. Kama huwezi kumpima mtu, toa dozi kwa kuzingatia umri:
Chini ya miaka 2: toa miligramu 75, mara 4 kwa siku.
Miaka 2 hadi 10: toa miligramu 125, mara 4 kwa siku.
Zaidi ya miaka 10: toa miligramu 250 hadi 500, mara 4 kwa siku.

Zidisha dozi hizi mara 2 kwa ajili ya maambukizi makali.

Kwa ajili ya vidonda kutokana na visu au risasi, toa dozi iliyoelezwa juu kwa siku 10 hadi 14. Kama kidonda ni kichafu au kiko tumboni, toa pia metronidazo.

Kwa mfupa uliovunjika na unajitokeza nje ya ngozi, toa dozi iliyoelezwa juu kwa siku 5 hadi 7. Kama kidonda ni kichafu sana, toa pia metronidazo.

Dikloksasilini (dicloxacillin)


Dikloksasilini (Dicloxacillin) ni aina ya penisilini, na wakati mwingine inaweza kutumika kutibu maambukizi ambayo yamekuwa sugu kwa penisilini. Kama huna dikloksasilini, kloksasilini (cloxacillin) inaweza kutumika badala yake.

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Kichefuchefu, maumivu ya tumbo, kukosa hamu ya kula.

MuhimuNBgrnimportant.png
 • Usitoe dikloksasilini kwa mtu ambaye ana mzio kwa penisilini. Usitoe kwa watoto wachanga.
 • Dawa hii inaweza kupunguza ufanisi wa vidonge vya majira. Kama inawezekana tumia njia nyingine (kama vile kondomu) unapokuwa unatumia dawa hii.
 • Acha kutumia dawa hii kama utaanza kutoa mkojo wenye rangi nzito, kinyesi chenye rangi ya grei au dalili za homa ya manjano (ngozi na macho kugeuka rangi ya njano).
Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png

Mpe pamoja na maji glasi nzima. Toa saa moja 1 kabla ya chakula, au saa 2 baada ya kula.

Kwa watoto chini ya kilo 40, mpe miligramu 12.5 hadi 25 kwa kilo, ikigawanywa katika dozi 4 kwa siku. Kama huwezi kumpima mtu, mpe dozi kuzingatia umri:
Chini ya mwaka 1: toa miligramu 20 kwa njia ya mdomo,mara 4 kwa siku.
Mwaka 1 hadi 5: toa miligramu 30 kwa njia ya mdomo, mara 4 kwa siku.
Miaka 6 hadi 12: toa miligramu 80 kwa njia ya mdomo, mara 4 kwa siku.
Zaidi ya miaka 12: toa miligramu 125 hadi 250 kwa mwezi, mara 4 kwa siku.

Kwa ajili ya kidonda chenye maambukizi, toa dozi ilioelezwa juu kwa siku 5 hadi 7. Kama kidonda ni kichafu sana, pia toa metronidazo.

Kwa jeraha la kuungua ambalo limeambukizwa, toa dozi iliyoelezwa juu kwa siku 5 hadi 7. Kama jeraha limeenda ndani, au mtu pia ana homa, mpe dozi iliyoelezwa juu kwa siku 10 hadi 14.

Antibiotiki zingine

Erithromaisini (erythromycin)


Erithromaisini hufanya kazi dhidi ya maambukizi mengi yanayotibiwa na dawa zilizomo katika kundi la penisilini au tetrasaikilini, na inaweza kutumika kwa watu wanaopatwa na mzio kutokana na penisilini.

Inaweza pia kutumika kwa ajili ya dondakoo na kifaduro.

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Erithromaisini mara nyingi husababisha kichefuchefu na kuharisha, hasa miongoni mwa watoto.Usitumie kwa zaidi ya wiki 2 kwani inaweza kusababisha ugonjwa wa manjano.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png
Toa miligramu 30 hadi 50 kwa kilo, ikiwa imegawanywa katika dozi 2 hadi 4 kila siku. Kama huwezi kumpima mgonjwa, toa dawa kwa kuzingatia umri:
Watoto wachanga hadi mwezi 1: toa miligramu 62, mara 3 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Mwezi 1 hadi miaka 2: toa miligramu 125, mara 3 au 4 kwa siku 7 hadi 10.
Miaka 2 hadi 8: toa miligramu 250, mara 3 au 4 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Zaidi ya miaka 8: toa miligramu 250 hadi 500, mara 4 kila siku kwa siku 7 hadi 10.

Kwa maambukizi makali, zidisha dozi iliyoelezewa juu mara 2.

Tetrasaikilini na doksisaikilini (doxycycline)


Tetrasaikilini na doksisaikilini ni antibiotiki zenye tiba pana ambazo hupambana na aina nyingi za bakteria. Hufanya kazi vizuri zinapotumika kwa njia ya mdomo (na sindano zake zinauma sana ). Hivyo, hazipaswi kutolewa kwa njia ya sindano. Kuna usugu mkubwa dhidi ya dawa hizi, lakini bado ni muhimu sana katika kupambana na maambukizi.

Doksisaikilini na tetrasaikilini zinaweza kutumika kama dawa mbadala. Lakini doksisaikilini kawaida ni bora zaidi kwa sababu kiasi kidogo huhitajika kila siku na madhara yake ya pembeni ni kidogo.

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Kiungulia, tumbo kusokota, kuhara, na maambukizi ya kuvu ni kawaida.

MuhimuNBgrnimportant.png
 • Wanawake wajawazito hawapaswi kutumia dawa hizi, kwa sababu zinaweza kuathiri au kusababisha madoa kwenye meno ya mtoto na mifupa. Kwa sababu hiyo hiyo, watoto chini ya miaka 8 wanaweza kuitumia kama hakuna dawa nyingine bora, na kwa vipindi vifupi tu. Wanaweza kutumia erithiromaisini.
 • Usitumie tetrasaikilini au doksisaikilini ambayo muda wake wa matumizi umepita.
 • Baadhi ya watu wanapokuwa wanatumia dozi ya dawa hizi wakikaa chini ya jua kali wanaweza kubabuka ngozi haraka au kutokwa na upele. Hivyo, kaa mbali na jua kali au vaa kofia pana.
 • Dawa hizi zinaweza kuingiliana na vidonge vya majira na hivyo hupunguza ufanisi wa vidonge vya majira. Kama inawezekana tumia njia nyingine ya kupanga uzazi (kama vile kondomu) utakapokuwa unatumia dawa hizi.
Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png

TETRASAIKILINI
Epuka maziwa, vidonge vya madini chuma, na dawa za kupambana na asidi tumboni angalau kwa saa 2 kabla ya kutumia tetrasaikilini. Vitu hivi vitaathiri utendaji wa dawa hii.

Tumia tetrasaikilini kabla hujala, na kunywa maji mengi angalau saa 1 kabla au saa 2 baada ya mlo.

Kwa maambukizi mengi:

Toa miligramu 25 hadi 50 kwa kilo kila siku, ikigawanywa katika dozi 4 kwa siku. Au toa dozi kulingana na umri:
Miaka 8 hadi 12: toa miligramu 125, mara 4 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Zaidi ya miaka 12: toa miligramu 250, mara 4 kila siku kwa siku 7 hadi 10.

DOKSISAIKILINI (DOXYCYCLINE)
Doksisaikilini hutumika mara 2 kila siku (badala ya mara 4 kila siku kama ilivyo kwa tetrasaikilini). Kwa maaambukizi makali, toa mara 2 kila siku.

Epuka maziwa, vidonge vya madini chuma, na dawa za kupambana na asidi tumboni angalau kwa saa 2 kabla ya kutumia doksisaikilini. Vitu hivi vitaathiri utendaji wa dawa hii.

Tumia doksisaikilini kabla hujala na kunywa maji mengi angalau saa 1 kabla au saa 2 baada ya mlo.

Kwa ajili ya maambukizi mengi:

Toa miligramu 2 kwa kilo kwa dozi, lakini usitoe zaidi ya miligramu 100 katika kila dozi au zaidi ya miligramu 200 kwa siku. Au toa dozi kulingana na umri:
Miaka 8 hadi 12: toa miligramu 50 kila dozi, kwa siku 7 hadi 10.
Zaidi ya miaka 12: toa miligramu100, kila dozi kwa siku 7 hadi 10.

Kwa ajili ya majeraha kutokana na kung’atwa na kuumwa na wanyama, toa dozi iliyopendekezwa juu kwa siku 3 hadi 5. Pia mpe metronidazo au klindamaisini.

Kotrimozazo (cotrimoxazole), salfamesozazo yenye trimethoprimu (sulfamethoxazole kwa trimethoprim), TMP-SMX


Kotrimozazo ni muunganiko wa dawa 2 za antibiotiki ambayo siyo ghali na hupambana na aina mbalimbali za maambukizi. Ni dawa muhimu kwa watu wanoishi na VVU na inaweza kuzuia maaambukizi mengi ambayo hujitokeza kwa sababu ya VVU.(Angalia Virusi vya UKIMWI na UKIMWI - inaandaliwa).

MuhimuNBgrnimportant.png

Epuka kutoa kotrimozazo kwa watoto chini ya wiki 6 na kwa wanawake katika miezi yao 3 ya mwisho ya ujauzito. Mzio kwa dawa hii ni kawaida. Dalili za mzio ni homa, kupumua kwa tabu, au kututumuka upele. Acha kutoa kotrimozazo kama mgonjwa atatokwa na upele au kama unafikiri kuna mzio.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png

Kotrimozazo huja katika vipimo tofauti kwa kila dawa 2 zilizopo kwenye muundo wake. Hivyo inaweza kuwa 200/40 (maana yake miligramu 200 za salfamethozazo na miligramu 40 za trimethoprimu) au 400/80 au 800/160. Dozi yake wakati mwingine huelezewa kwa kiasi cha trimethoprimu (namba ya pili).

Kwa maambukizi mengi:

Wiki 6 hadi miezi 5: toa salfamethozazo miligramu 100 + trimethoprimu miligramu 20, mara 2 kwa siku kwa siku 5.
Miezi 6 hadi miaka 5: mpe salfamethozazo miligramu 200 + trimethoprimu miligramu 40, mara 2 kwa siku kwa siku 5.
Miaka 6 hadi 12: mpe salfamethozazo miligramu 400 + trimethoprimu miligramu 80, mara 2 kwa siku kwa siku 5.
Zaidi ya miaka 12: mpe salfamethozazo miligramu 800 + trimethoprimu miligramu 160, mara 2 kwa siku kwa siku 5.

Kwa ajili ya majeraha kutokana na kung’atwa au kuumwa na wanyama, mpe kiasi kilichopendekezwa juu kwa siku 3 hadi 5. Pia mpe metronidazo au klindamaisini (clindamycin).

Klindamaisini (clindamycin)


Klindamaisini ni antibiotiki nyingine ambayo hutumika kutibu aina nyingi za maambukizi ambayo yamekuwa sugu kwa penisilini kama vile maambukizi ya ngozi na majipu.

MuhimuNBgrnimportant.png

Kama utapata mharo wa kawaida au ukiwa umechanganyika na damu wakati wa kutumia dawa hii, simamisha matumizi mara moja. Hii inaweza kuwa dalili ya maambukizi hatari ambayo yamesababishwa na dawa hii ya antibiotiki. Kwa sababu dawa inaweza kumuathiri mtoto anayenyonya kupitia maziwa ya mama, epuka kutoa dawa hii kwa mama ambaye ananyonyesha.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png
Mpe klindamaisini kwa njia ya mdomo.
Chini ya miaka 3: mpe miligramu 37.5 hadi 75, mara 3 kwa siku.
Miaka 3 hadi 7: mpe miligramu 75 hadi 150, mara 3 kwa siku.
Miaka 8 hadi 12: mpe miligramu 150 hadi 300, mara 3 kwa siku.
Zaidi ya miaka 12: mpe miligramu 150 hadi 450, mara 3 kwa siku.

Kwa ajili ya majeraha kutokana na kung’atwa au kuumwa na wanyama, mpe dozi iliyopendekezwa juu kwa siku 3 hadi 5. Pia mpe dawa nyingine kama vile doksisaikilini (doxycycline), kotrimozazo (cotrimoxazole) AU penisilini V.

Kwa ajili ya kidonda chenye maambukizi, mpe dozi iliyopendekezwa juu kwa siku 5 hadi 7.

Kwa ajili ya jeraha la moto ambalo limeambukizwa, mpe dozi iliyopendekezwa juu kwa siku 5 hadi 7. Kama jeraha limeingia ndani, au mtu huyu pia ana homa, mpe dozi iliyopendekezwa juu kwa siku 10 hadi 14.

Kwa ajili ya mfupa ambao umevunjika na kujitokeza nje ya ngozi, mpe dozi iliyopendekezwa juu kwa siku 5 hadi 7. Kama kidonda ni kichafu sana, pia mpe sipro (siprofloxacin).

Kwa ajili ya vidonda kutokana na visu au risasi, mpe dozi iliyopendekezwa juu kwa siku 10 hadi 14.

Metronidazo (metronidazole)


Metronidazo ina uwezo mzuri wa kupambana na bakteria na maambukizi mbalimbali inapotumika peke yake au pamoja na dawa zingine za antibiotiki.

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Kichefuchefu, tumbo kusokota, na kuhara ni kawaida. Matumizi ya dawa hii pamoja na chakula kunaweza kusaidia. Wakati mwingine husababisha ladha ya chuma mdomoni na hata maumivu ya kichwa.

MuhimuNBgrnimportant.png

Usitoe wakati wa miezi 3 ya kwanza ya ujauzito. Inaweza kusababisha madhara kwa mtoto aliye tumboni. Pia epuka kutoa metronidazo baadaye katika ujauzito, na wakati wa unyonyeshaji isipokuwa tu kama ni dawa pekee yenye uwezo iliyopo na inahitajika hasa. Usinywe pombe wakati unapokuwa unatumia metronidazo – hadi angalau baada ya siku 2 baada ya kumaliza dozi. Unywaji pombe wakati wa dozi ya metronidazo husababisha kichefuchefu kikali. Usitumie metronidazo kama una matatizo ya ini.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png
Mpe miligramu 30 kwa kila kilo, ikigawanywa katika dozi 4 kwa siku. Kama huwezi kumpima mtu uzito, mpe dozi kwa kuzingatia umri:
Chini ya mwaka 1: mpe miligramu 37, mara 4 kwa siku.
Chini ya mwaka 1 hadi 5: mpe miligramu 75, mara 4 kwa siku.
Miaka 6 hadi 12: mpe miligramu 150, mara 4 kwa siku.
Zaidi ya miaka 12: Mpe miligramu 500, mara 3 au 4 kwa siku. Usitoe zaidi ya gramu 4 ndani ya saa 24.

Kwa ajili ya kidonda ambacho kimepata maambukizi, mpe dozi kwa iliyopendekezwa juu kwa siku 5 hadi 7. Pia mpe dikloksasilini (dicloxacillin) AU sefaleksini (cephalexin).

Kwa kidonda ambacho kinaweza kuwa kimeambukizwa na tetanasi, mpe dozi iliyopendekezwa juu kwa siku 7 hadi 10. Pia mpe dawa nyingine dhidi ya tetanasi- antitetanus immunoglobulin.

Kwa ajili ya majeraha kutokana na kung’atwa au kuumwa na wanyama, mpe dozi iliyopendekezwa juu kwa siku 3 hadi 5. Pia mpe dawa nyingine kama vile doksisaikilini (doxycycline), kotrimozazo (cotrimoxazole), AU penisilini V.

Kwa mfupa ambao umevunjika na kujitokeza nje ya ngozi, mpe dozi iliyopendekezwa juu kwa siku 5 hadi 7. Pia mpe seftriaksoni (ceftriaxone), sefaleksini (cephalexin) AU kloksasilini (cloxacillin).

Sipro (ciprofloxacin)


Sipro ni antibiotiki yenye tiba pana kutoka kundi la quinolone. Hufanya kazi dhidi ya maambukizi mengi tofauti ya ngozi, mifupa, njia ya chakula na njia ya mkojo (kibofu cha mkojo na figo). Lakini kuna usugu dhidi ya sipro katika sehemu nyingi za dunia. Hivyo, tumia sipro tu dhidi ya maambukizi ambayo yamependekezwa katika eneo lako. Siyo dawa nzuri kwa watoto.

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Kichefuchefu, kuhara, kutapika, maumivu ya kichwa, kizunguzungu, upele, au maambukizi ya fangasi.

MuhimuNBgrnimportant.png
 • Usitumie dawa hii iwapo ni mjamzito au unanyonyesha. Usitumie pamoja na bidhaa za maziwa.
 • Kwa nadra, sipro huathiri tishu zinazounga misuli kwenye mifupa. Isipokuwa katika matukio maalum machache, haipaswi kutolewa kwa watoto chini ya miaka 16 kwa sababu tishu zao hizo bado zinakua. Kama utapata maumivu kwenye misuli ya miguu nyuma ya miuundi unapokuwa unatumia dawa hii, acha kutumia mara moja.
Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png

Kwa ajili ya maambukizi mengi:

Toa miligramu 250 hadi 750, mara 2 kila siku hadi angalau saa 24 baada ya dalili zote kutoweka.

Kwa ajili ya sumu ya vijidudu iliyoenea kwenye damu (sepsisi), mpe dozi iliyopendekezwa juu kwa siki 2 hadi 3 baada ya dalili kutoweka. Pia mpe klindamaisini (clindamycin).

Kwa mfupa ambao umevunjika na unajitokeza nje ya ngozi, mpe dozi kwa siku 5 hadi 7. Pia mpe klindamaisini.

Kwa kidonda cha moto ambacho kimepata maambukizi, mpe dozi iliyoelezwa hapo juu kwa siku 5 hadi 7. Kama kidonda kimeenda ndani, au ngonjwa ana homa, mpe dozi hiyo kwa siku 10 hadi 14.

Seftriaksoni (ceftriaxone)


Seftrikasoni ni dawa inayotoka katika kundi la dawa za antibiotiki za sefalosporini (cephalosporin). Sefalosporini ni dawa ya antibiotiki ambazo hufanya kazi dhidi ya aina nyingi za bakteria. Mara nyingi dawa hii ni ghali na haipatikani kwa urahisi. Hata hivyo, huwa ina madhara madogo yakiwemo madhara ya pembeni kuliko dawa nyingi za antibiotiki na inafaa sana kutibu baadhi ya magonjwa makali.

Seftriaksoni hutumika dhidi ya maambukizi makali yakiwemo sepsisi na homa ya uti wa mgongo na maambukizi yenye usugu kwa dawa ya penisilini. Tumia seftriaksoni tu kutibu maambukizi mahsusi ambayo yamependekezwa katika eneo lako. Hii itasaidia kuzuia usugu na kuiwezesha dawa hii kuendelea kutumika. Seftriaksoni ni muhimu hasa katika kutibu kisonono, ikijumuisha maambukizi ya kisonono kwenye macho ya watoto wachanga. Hata hivyo haipaswi kutolewa kwa watoto wachanga chini ya wiki 1 na ni bora kuwaepusha watoto wachanga chini ya mwezi 1.

MuhimuNBgrnimportant.png

Usitumie kwa mtoto mchanga chini ya wiki 1. Usitumie pia kama kuna homa ya manjano.

Jinsi ya kutumiaNBgrninject.png
Seftriaksoni haiwezi kutumika kwa njia ya mdomo. Wakati wa kuchoma, hakikisha sindano inaingia ndani ya msuli. Sindano hii inaweza kuuma sana. Hivyo, changanya na 1% ya lidokeni (lidocaine) kama unajua jinsi ya kuichanganya.
Toa miligramu 50 hadi 100 kwa kilo ya uzito kila siku, ikigawanywa katika dozi 2 kwa siku. Kama huwezi kumpima mgonjwa, toa dozi kulingana na umri:

Mwezi 1 hadi miezi 3: choma miligramu 150 mara 2 kwa siku
Miezi 3 hadi mwaka 1: choma miligramu 250, mara 2 kila siku kwa siku 5.
Miaka 2 hadi 4: choma miligramu 400, mara 2 kila siku kwa siku 5.
Miaka 5 hadi 12: choma miligramu 625, mara 2 kila siku kwa siku 5.
Zaidi ya miaka 12: choma gramu 1 hadi 2, mara moja kila siku kwa siku 5. Usitoe zaidi ya gramu 4 ndani ya saa 24.

Kwa ajili ya mfupa ambao umevunjika na unajitokeza nje ya ngozi, mpe dozi iliyopendekezwa juu kwa siku 5 hadi 7. Kama kidonda ni kichafu, pia toa metronidazo.

Kwa ajili sumu ya vijidudu ilioenea kwenye damu (sepsisi), mpe dozi iliyoelezwa juu hadi siku 2 hadi 3 baada ya dalili za maambukizi kutoweka. Kama kidonda ni kichafu au hakuna unafuu baada ya saa 24 ya kuanzisha dawa ya seftriaksoni, pia mpe metronidazo.

Sefaleksini (cephalexin)


Sefaleksini ni aina ya antibiotiki kutoka familia ya sefalosporini (cephalosporin). Kundi hili la antibiotiki lina nguvu sana na hufanya kazi dhidi ya aina nyingi za bakteria. Kawaida bei yake ni ghali na hazipatikani kwa urahisi. Hata hivyo ina madhara kidogo, yakiwemo madhara ya pembeni kuliko na kutumika kutibu baadhi ya magonjwa makali.

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Mharo wa kawaida au uliochanganyika na damu, homa, mwasho kooni, maumivu ya kichwa, ukurutu mwekundu kwenye ngozi wakati mwingine ukitengeneza malengelenge au kujitoa gamba, mkojo wenye rangi nzito, kuchanganyikiwa au mwili kukosa nguvu.

MuhimuNBgrnimportant.png
Usitoe dawa hii kwa mtu ambaye anapata mzio kutokana na dawa zingine za antibiotiki kutoka kundi hili la sefalosporini.
Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png
Mpe miligramu 50 kwa kilo kila siku,ikiwa imegawanywa katika dozi 4 kwa kwa siku. Usimpe zaidi ya miligramu 4000 ndani ya saa 24. Kama huwezi kumpima mgonjwa, mpe dozi kwa kuzingatia umri:
Chini ya miezi 6: mpe miligramu 100, mara 4 kwa siku.
Miezi 6 hadi miaka 2: mpe miligramu 125, mara 4 kwa siku.
Miaka 3 hadi 5: mpe miligramu 250, mara 4 kwa siku.
Miaka 6 hadi 12: mpe miligramu 375, mara 4 kwa siku.
Zaidi ya miaka 12: mpe miligramu 500, mara 4 kwa siku.

Kwa ajili ya kidonda chenye maambukizi, mpe dozi iliyopendekezwa juu kwa siku 5 hadi 7. Kama kidonda ni kichafu sana, pia mpe metronidazo.

Kwa ajili ya jeraha la moto lenye maambukizi, mpe dozi iliyoelezwa juu kwa siku 5 hadi 7. Kama jeraha limeenda chini, au kama mgonjwa ana homa, mpe dozi kwa siku 10 hadi 14.

Kwa mifupa iliyovunjika na kujitokeza nje, mpe dozi iliyoelezwa juu kwa siku 5 hadi 7. Kama kidonda ni kichafu sana, pia mpe metronidazo.

Kwa ajili ya vidonda kutokana na visu au risasi, mpe dozi iliyopendekezwa juu kwa siku 10 hadi 14. Kama kidonda ni kichafu sana, au kipo sehemu ya tumbo, pia mpe metronidazo.

Jentamaisini (Gentamicin)


Jentamaisini ni antibiotiki kali sana ambayo natoka kwenye kundi la aminoglaikosaidi (aminoglycoside). inaweza kutolewa tu kwa sindano au kwa dripu kupitia kwenye mshipa wa damu. Dawa hii inaweza kuharibu figo na uwezo wa kusikia. Hivyo inapaswa kutumika tu wakati a dharura.

MuhimuNBgrnimportant.png

Jentamaisini azima itolewe kwa kuzingatia dozi sahihi. Dawa ikizidi inaweza kusababisha uharibifu wa figo au uziwi wa kudumu. Ni bora zaidi kutoa dozi kwa kuzingatia uzito. Na usitoe jentamaisini kwa zaidi ya siku 10.

Jinsi ya kutumiaNBgrninject.png

Choma kwenye msuli au mshipa wa damu.

Kwa ajili ya sepsisi

Miezi 6 hadi miaka 12: choma miligramu 2.5 kwa kilo, mara 3 kwa siku.
Zaidi ya miaka 12: choma miligramu 1 hadi 1.7 kwa kilo, mara 3 kwa siku.