Hesperian Health Guides
Dawa kwa ajili ya mzio au mwasho: Antihistamini (antihistamines)
HealthWiki > Toleo Jipya: Mahali Pasipo na Daktari > Huduma ya kwanza > Dawa kwa ajili ya mzio au mwasho: Antihistamini
Yaliyomo
Huduma ya kwanza: Madawa
- Antibiotiki
- Dawa za kuzuia tetanasi (pepopunda)
- Dawa za vidonda kutokana na kung'atwa au kuumwa na wanyama
- Dawa za vidonda kutokana na kuungua
- Dawa kwa ajili ya mzio au mwasho: Antihistamini (antihistamines)
- Dawa za mshituko wa moyo
- Dawa za kutibu sumu
- Dawa za kupunguza kaumivu
- Dawa za kutia ganzi
- Dawa za kupunguza wasiwasi, kukosa utulivu
Mwasho, chafya na ukurutu ambavyo vimesababishwa na mzio vinaweza kutibika kwa kutumia dawa za antihistamini. Dawa za antihistamini hufanya kazi vizuri kama dawa yoyote nyingine kutoka kundi hilo. Hivyo kama huna klorofeniramini (chlorpheniramine) au difenhidramini (diphenhydramine), tumia dawa nyingine ya antihistamini katika dozi sahihi (dozi itabadilika kwa kila dawa). Dawa zote za antihistamini zina tabia ya kulewesha, lakini baadhi hulewesha kuliko zingine.
Dawa hizi hazisaidii kwa mafua ya kawaida.
Antihistamini zinapaswa kuepukwa wakati wa ujauzito. Kama ni lazima zitolewe, chagua zile za mwanzoni kabisa kama vile klorofeniramini (chlorpheniramine) au difenhidramini (diphenhydramine), na zisindikizwe na maji mengi.
Kwa ajili ya mzio mkali ukiambatana na kupumua kwa shida, epinefrini (epinephrine/adrenaline) inahitajika sambamba na antihistamini.
Klorofeniramini, klorofenamini (chlorphenamine)
Klorofniramini (chlorpheniramine) ni aina ya antihistamini ambayo hupunguza mwasho, chafya, ukurutu, na matatizo mengine yanayosababishwa na mzio. Inaweza kutumika baada ya kuumwa na mdudu, mzio mdogo kutokana na chakula au dawa, au kwa ajili ya aina ya homa ya mafua ambayo inajumwisha kupiga chafya na kuwashwa macho kutokana na chavua kwenye hewa (hay fever).

Kusinziasinzia (lakini siyo sana ukilinganisha na antihistamini zingine).

Usitoe dawa hii kwa wanawake wajawazito isipokuwa kama hamna njia nyingine.Usitoe wakati wa shambulio la asma (pumu).

Miaka 3 hadi 5: mpe miligramu 1, kila saa 4 hadi 6 hadi mtoto atakapojisikia vizuri.
Miaka 6 hadi 12: mpe miligramu 2, kila saa 4 hadi 6 hadi mgonjwa atakapojisikia nafuu.
Zaidi ya miaka 12: mpe miligramu 4, kila saa 4 hadi 6 hadi mgonjwa atakapojisikia nafuu.
Kwa ajili ya mzio mkali
Kwanza choma epinefrini (epinephrine). Fuatisha na klorofeniramini (chlorpheniramine) kwa njia ya mdomo katika dozi zilizoelekezwa juu kuzuia mzio kurudia pale nguvu ya dawa ya epinefrini itakapokua imekwisha.
Difenhidramini (diphenhydramine)
Difenhidramini ni aina ya antihistamini ambayo husaidia kupunguza mwasho,kupiga chafya, ukurutu, na matatizo mengine yanayosababishwa na mzio. Inaweza kutumika baada ya kuumwa na mdudu, mzio wa kawaida kutokana na chakula au dawa, au kwa ajili ya homa ya mafua au “hay fever” (kupiga chafya na kuwashwa macho kutokana na chavua kwenye hewa).

Kusinziasinzia.

- Difenhidramini (diphenhydramine) inaweza kusababisha kizunguzungu, kusinziasinzia au uoni hafifu. Usiendeshe gari au mashine kama unatumia dawa hii. Kunywa pombe kunaweza kuongeza hali ya kusinziasinzia inayosababishwa na difenhindramini.
- Usiwape watoto wachanga au wanawake wanaonyonyesha. Ni bora zaidi kutowapa kabisa dawa hii wanawake wajawazito isipokuwa tu kama hakuna mbadala.
- Ustoe dawa hii wakati wa shambulio la asma.

Miaka 2 hadi 5: mpe miligramu 6 kila saa 4 hadi 6. Usitoe zaidi ya miligramu 37 kwa siku.
Miaka 6 hadi 11: toa miligramu 12 hadi 25 kila saa 4 hadi 6. Usitoe zaidi ya miligramu 150 kwa siku.
Zaidi ya miaka 12: toa miligramu 25 hadi 50 kila saa 4 hadi 6. Usitoe zaidi ya miligramu 400 kwa siku.
Kwa ajili ya mzio mkali
Miaka 2 hadi 11: toa miligramu 1 hadi 2 kwa kilo, kila baada ya saa 6. Kama huwezi kumpima mtoto, toa dozi kwa kuzingatia umri, na toa sehemu ambayo ni kubwa zaidi. Usitoe zaidi ya miligramu 50 kwa wakati mmoja, au miligramu 300 kwa siku.
Zaidi ya miaka 12: toa miligramu 25 hadi 50, kila saa 2 hadi 4. Usitoe zaidi ya miligramu 100 ndani ya saa 4 au miligramu 400 kwa siku.
Epinefrini (epinephrine/adrenaline)
Epinefrini hutumika kwa ajili ya mzio mkali unaotokana na dawa, vyakula, kuumwa au kung’atwa na wadudu, au vitu vingine vinavyosababisha mzio mkali. Husaidia kudhibiti upumuaji wa shida, upumuaji wa kukorota, mwasho mkali wa ngozi na mabaka kwenye ngozi.

Woga, kukosa utulivu, wasiwasi, msongo, maumivu ya kichwa, kizunguzungu, kasi ya mapigo ya moyo kuongezeka.

Epinefrini huja katika vichupa vidogo vya miligramu 1 kwa kila mililita 1 ya majimaji. Epinefrini pia hupatikana katika sindano ambazo tayari zimechanganywa, lakini katika vipimo tofauti. Hakikisha unasoma na kufahamu kiasi gani cha epinefrini kilichopo kwenye sindano yako ambayo tayari imeandaliwa kwa ajili ya kuchoma ili uwe na uhakika kuwa unachoma kiasi sahihi.

Kwa ajili ya mzio mkali
Mwaka 1 hadi 6: Choma ¼ miligramu (miligramu 0.25).
Miaka 7 hadi 12: Choma ⅓ miligramu (miligramu 0.33).
Zaidi ya miaka 12: Choma ½ miligramu (miligramu 0.5).
Kama itahitajika, unaweza kutoa dozi ya pili ndani ya nusu saa, na dozi ya tatu ndani ya nusu saa baada ya hapo. Usitoe zaidi ya dozi 3.
Baada ya kutoa epinefrini, toa antihistamini kama vile klorofeniramini (chlorpheniramine) au difenhindramini (diphenhydramine). Hii itasaidia kuzuia mzio dawa ya epinefrini itakapopungua nguvu mwilini
Salbutamo (salbutamol/albuterol)
Salbutamo hufanya misuli kwenye njia ya kupumua kulegea na kuongeza kiasi cha hewa inayoingia kwenye mapafu. Hutumika kutibu upumuaji wa kukorota au pumzi fupi fupi ambazo zinatokana na asma (pumu), au kutokana na kuingiza moshi mchafu mwingi mapafuni kutokana na moto.

Kutetemeka, wasiwasi, kizunguzungu, mapigo ya moyo kwenda mbio, na maumivu ya kichwa.
Jinsi ya kutumia
Ni sawa kutoa kiasi zaidi kuliko kilichopendekezwa kama mgonjwa ataonekana kuhitaji zaidi.