Hesperian Health Guides

Kupigwa na umeme

Kupigwa na umeme kunaweza kusababisha kuungua na moyo kusimama kufanya kazi.

Mwanaume ameanguka chini mkono wake ukiwa umekamata nyaya ya umeme.
Kwanza zima umeme au tumia kifaa kisicho cha chuma kuuondoa waya. Halafu mwondoe majeruhi. Hii hukulinda na wewe usipigwe na umeme.
  1. Kama mtu amepigwa na umeme: Usimuguse. Umeme unaweza kupita kwenye mwili wake na kumpiga yoyote atakayemgusa. Kwanza, zima umeme unaoingia kwenye mashine au kifaa kinachosababisha shoti. Kama huwezi kuuzima umeme, tumia nguo kavu, kamba au kipande cha ubao au fimbo kavu, kama vile mkono wa fagio, kumtenganisha majeruhi na chanzo cha umeme unaosababisha shoti. Usitumie kitu chochote chenye unyevu au kilicholowa na maji au ambacho kimetengenezwa kwa chuma. Kama majeruhi amelala kwenye maji, tumia ubao mkavu au nguo kavu kumuondoa, na usikanyage ndani ya maji la sivyo na wewe utapigwa na umeme! Halafu mwondoe majeruhi kutoka kwenye chanzo cha umeme.
  2. Shoti ya umeme inaweza kusimamisha upumuaji. Toa pumzi ya kuokoa maisha.
  3. Kama hakuna mapigo ya moyo jaribu kuushtua moyo kwa kutoa mibinyo kifuani (chest compressions) – bonyeza kwa nguvu na haraka sehemu ya kati kifuani. Inaweza kuchukua muda mrefu. Endelea kujaribu.
  4. Kama mtu anapumua na moyo wake unapiga, angalia iwapo kuna dalili za majeraha kutokana na kuungua. Kama jinsi kinavyokuwa kidonda cha risasi, kunapaswa kuwepo kidonda mahali shoti ilipoingilia na kidonda kingine shoti ilipotokea.
  5. Chunguza iwapo kuna majeraha mengine. Kuchanganyikiwa akili, neva kuharibika (matatizo katika kuhisi au kutembea), kupoteza uwezo wa kusikia, au matatizo ya mzunguko wa damu – yote yanaweza kuibuka. Kama mtu alianguka, anaweza kuwa alipata jeraha kichwani, mifupa kuvunjika, au kutokwa damu.


Kama shoti ilikuwa ndogo, na aliyepigwa shoti hana dalili za matatizo saa chache baada ya ajali, ataendelea vizuri. Kama shoti ilikuwa kubwa au kutokana na radi, au kama mtu ana tatizo la kutumia muda mrefu kuliko kawaida kuitikia au kung’amua jambo, kuwa mwangalifu zaidi. Majeraha ya moto wa umeme ndani ya mwili yanaweza kuwa makali zaidi kuliko yale juu ya ngozi mahali shoti ilipoingilia na kutokea. Dripu kwa ajili ya kumuongezea maji mwilini na tiba nyingine zinaweza kuhitajika. Inaweza kuchukua siku au wiki kadhaa kujua madhara halisi.