Hesperian Health Guides

Majeraha ya uti wa mgongo na shingo

Katika sura hii:

Ndani ya mifupa ya uti wa mgongo kuna kini au uboho ambao ni mwendelezo wa ubongo. Jeraha kwenye kini au uboho linaweza kusababisha ulemavu wa maisha au hata kifo. Kama itatokea mtu akajeruhiwa uti wa mgongo, unaweza kumlinda dhidi ya majeraha zaidi kwa kuuweka mgongo na shingo lake katika hali isiyoruhusu kutikisika!

Chukulia kuwa mfupa wa uti wa mgongo unaweza kuwa umejeruhiwa baada ya ajali ya gari, pikipiki, au baisikeli, kuanguka, au ngumi nzito kwenye usogo au kichwani. Weka kichwa na mgongo wake katika hali isiyotikisika ili visiweze kugeuka upande mmoja hadi mwingine, hali ambayo inaweza kusababisha majeraha zaidi kwenye kini cha uti wa mgongo. Zungushia shingo nguo, vitambaa, sponji au vitu vingine laini ili shingo ibaki katika nafasi moja –bila kuyumba.

Shati ikikunjwa na kuzungushwa kwenye shingo la mgonjwa.


Usitoe dawa ya kupunguza maumivu hadi utakapokuwa na uhakika kwamba hakuna majeraha kwenye mfupa wa uti wa mgongo. Maumivu humkumbusha mgonjwa kubaki katika nafasi au mkao moja bila kujitikisa.

Dalili za jeraha kwenye mfupa wa uti wa mgongo
  • Maumivu au ulegevu kwenye shingo au uti wa mgongo
  • Kukosa nguvu au kupoteza uwezo wa kutembeza mikono au miguu
  • Ganzi kwenye mikono au miguu


Dalili zingine za jeraha kwenye uti wa mgongo ni kupoteza uwezo wa kudhibiti mkojo au haja kubwa, shida katika kupumua, au mshituko. Kama kuna shaka, ni salama zaidi kumtibu mgonjwa kama vile amepata jeraha kwenye uti wa mgongo.

Mwanaume aliyelalia mgongo akiwa ameinua juu mikono yake.

Kuchunguza iwapo kuna jeraha kwenye uti wa mgongo, mwambie majeruhi kulalia mgongo wake, kujinyoosha na kuinua magoti yake. Halafu mwambie kuinua mikono yake juu. Je, anaweza kuiinua? Anasikia maumivu? Kamata vidole vyake vya mikono na miguu. Je anaweza kuhisi kukamatwa sehemu hizo? Anaweza kuhisi unapomfinya?

Kama kuna sehemu kwenye mwili ambayo hawezi kutembeza au kuhisi, mifupa kwenye uti wa mgongo imevunjika. Lakini kwa msaada kutoka kwa watu wengine, unaweza kuzuia hali hii kuwa mbaya zaidi.

Mwanaume akiongea na wenzake 2 wakati wanajiandaa kumbiringisha mwanamke.
Haya biringisha mara “tatu”. Moja, mbili...
Shika kichwa ili kibaki kwenye laini moja na mwili, hakikisha shingo inabaki imenyooka.
Wanaume wakimbiringisha majeruhi, mojawao akiwambia jambo.
tatu

Kama bado ana hisia na uwezo wa kutembeza sehemu zake za mwili, chunguza uti wa mgongo wenyewe. Kwa uangalifu, mbiringishe kama gogo alalie upande kama kwenye mchoro ili kukagua mgongo wake mzima.

Kichwa, shingo na mgongo vibaki kwenye mstari mmoja wakati unambiringisha. Baada ya hapo, mwili usitikishwe, na taratibu chunguza kwa mkono wako kila mwinuko kwenye uti wa mgongo mzima kuanzia kisogoni hadi chini katikati ya makalio. Chunguza kwa kuhisi kwa vidole vyako mifupa ambayo imetoka katika nafasi zake, iliyovunjika, au maumivu.

Tumia juhudi ya pamoja ya timu yako kumbiringisha na kumrudisha katika nafasi yake ya awali. (Kama anatapika, sogeza mkono wake au weka kitu kinachofaa chini ya kichwa chake ili aweze kubaki kwenye upande aliolalia).

Kama kuna maumivu au ulegelege, mgonjwa anahitaji huduma ya eksirei kuona iwapo kuna sehemu za mifupa zilizovunjika. Atahitaji kupumzika katika nafasi moja, akibadilishwa kila baada ya saa chache lakini shingo na mgongo vikibaki bila kutikiswa hadi maumivu yatakapopungua ndani ya wiki moja au zaidi.

Kumsogeza, mbiringishe kama ‘gogo’ alalie upande na mweke kwenye ubao bapa, sawa na mlango wa mbao, chini yake. Halafu mbiringishe na kumrudisha kwenye ubao. Tumia kamba kadhaa ndefu za kitambaa au kitu kingine kufunga kichwa chake, kifua, na mapaja kwenye ubao.

NWTND fa Page 22-3.png

Kama itabidi mgonjwa abaki kwenye ubao huu kwa muda mrefu, unapaswa kumbiringisha alalie upande kila baada ya saa kadhaa.

Mtu ambaye amepata jeraha kwenye uti wa mgongo anahitaji huduma ya tiba ya mazoezi (fiziotherapi) kwa muda mrefu. Tafuta msaada kwa wengine wenye uzoefu.