Hesperian Health Guides

Vidonda

Katika sura hii:

  1. Simamisha uvujaji damu kwa mgandamizo..
  2. Safisha kidonda vizuri mapema kadri unavyoweza. Kadri utavyokisafisha, ndivyo hatari ya maambukizi itapungua. Kwa ajili ya vidonda vikubwa, toa mojawapo ya dawa za kupunguza maumivu kabla hujaanza kukisafisha na kukitibu. Choma sindano ya lidokeni (lidocaine) eneo linalozunguka kidonda na chini kidogo ya ngozi ndani ya kidonda. Au mpe aina nyingine ya dawa ya kupunguza maumivu na kuruhusu iweze kufanya kazi.
  3. Funga au funika kidonda, au kama ni kidogo, kiache wazi kiweze kupona.

Safisha vidonda vyote

Kidonda chochote, kiwe kikubwa au kidogo, kinaweza kupata maambukizi. Kila kidonda kisafishwe vizuri.


Nawa mikono yako vizuri kwa kutumia sabuni. Halafu safisha kidonda na lita 1 hadi 4 za maji yanayotiririka. Dawa za kuua wadudu hazihitajiki kila wakati, kwani baadhi huchelewesha uponyaji wa kidonda. Kama kidonda kinaonekana kichafu, tumia maji yenye sabuni na kusuuza kwa kutumia maji masafi ya kawaida.

Inua vipande vyote vya ngozi ambavyo vimefunika kidonda ili kusafisha chini yake. Kwa vidonda ambavyo vimeingia ndani, tiririsha maji kwa nguvu ndani ya kidonda, na kuruhusu yatoke nje.

a flap of skin held up with tweezers while water is squirted on the wound.


Au toa sindano kwenye bomba lake na kutitirisha maji kwa nguvu kwenye kidonda.

Au mwaga na kupitisha tu maji juu na ndani ya kidonda.

Safisha kitu chochote ambacho huenda kimebaki ndani ya kidonda, hasa uchafu wa kawaida, vijiti, au vitu vingine. Unaweza kutumia kipande cha shashi (gauze) iliyotakaswa au kitambaa kingine kisafi kusafisha kidonda, halafu kisuuze vizuri.

Kuhudumia vidonda

Kidonda kinapokuwa kinapona, hakikisha kuwa kinabaki kisafi wakati wote kuzuia maambukizi. Kama kitachafuka, kisafishe na maji mengi. Kufunga kidonda na bandeji, shashi iliyotakaswa, au kwa kutumia kitambaa kisafi husaidia kidonda kubaki katika hali ya usafi. Kuweka asali kwenye kidonda pia husaidia kuzuia maambukizi. Badilisha bandeji kila siku, na kila inapolowa au kuchafuka. Ni bora kutofunga bandeji kabisa kuliko kutumia bandeji chafu au iliyolowa.

Chukua tahadhari kuangalia dalili za maambukizi kama vile wekundu, ongezeko la maumivu, joto, kuvimba, au usaha eneo la kidonda. Kwa ajili ya dalili hizi, safisha kidonda vizuri. Unaweza kukifunua taratibu kukifanyia usafi. Kuwa mwangalifu ili maambukizi yasienee sehemu zingine za mwili.

Kufunika vidonda

Kidonda kidogo ni bora kiachwe tu ili kipone chenyewe. Kawaida hakihitaji kushonwa. Jambo muhimu zaidi ni kukitunza katika hali ya usafi.

Kidonda ambacho kina zaidi ya saa 12 kinafaa kusafishwa na kuachwa wazi ili kipone chenyewe.

Kidonda kikubwa zaidi ambacho angalau kimejifunika chenyewe kitapona vizuri zaidi kama kitafungwa.

Ili kufunga kidonda kisafi ambacho hakijaingia ndani, tumia bandeji, gundi au mishono.

Bandeji aina ya kipepeo

Tumia bandeji aina ya kipepeo kwa vidonda vidogo.

Jinsi ya kutengeneza bandeji aina ya kipepeo.
Ngozi inayokizunguka kidonda lazima isafishwe na kukaushwa ili bandeji iweze kushika.

Gundi

Ni bora kutumia gundi yenye nguvu (Super Glue) ambayo kawaida hufanya kazi vizuri kwa ajili ya vidonda vingi. Itumie unapoona kwamba pande 2 za kidonda zinafaa kuunganishwa. Huenda isifanye kazi vizuri kwenye mikono au maungio (jointi) kwa sababu viungo hivi hutembezwa sana. Usitumie gundi karibu na macho au mdomo. Gundi kali (mathalan Super Glue) inaweza kusababisha mwasho kwenye ngozi.

Tumia gundi kufunga kidonda

Hatua 1: Hakikisha kidonda ni kisafi na ngozi inayokizunguka imekauka.

Hatua 2: Sogeza pande zote za kidonda pamoja. Weka vidole vyako nje ya kidonda ili visishikwe na gundi. Msaidizi anaweza kutumia vijiti visafi kadhaa kushika pande zote za kidonda pamoja.

Hatua 3: Minya kasha la gundi na kupaka sehemu za kidonda zilizounganishwa.

Hatua 4: Shikilia kidonda kilichofungwa kwa sekunde 30. Halafu ongeza tabaka lingine la gundi. Subiri kwa wastani wa sekunde zingine 30, na baada ya hapo ongeza tabaka la 3. Kila tabaka linapaswa kufunika eneo kubwa zaidi kuzunguka kidonda kuliko tabaka lililopita.

Gundi itapungua na kuisha yenyewe. Hadi hapo, kidonda kitakuwa kimeishapona.

Mishono

Jeraha litafaa kushonwa kama halijaenda sana ndani - ni refu, au kama ncha za ngozi zinazozunguka kidonda haziwezi kushikamana zenyewe.

Nyosha ncha ya ngozi hizo. Ncha hizo zinapaswa kupanda juu ya ngozi badala ya kujichomeka kwenye kidonda.

Tengeneza kina na urefu wa mshono ili ulingane kila upande wa kidonda.

Kushona kwa kutumia sindano yenye muundo wa kizingo (iliyopinda).
Shona kupitia hapa
Siyo hapa

Hatua 1:
Shona kupita ndani ya jeraha siyo chini ya jeraha.

Kama huna sindano maalum yenye muundo wa kizingo, noa sindano ya kawaida ya kushonea nguo. Chemsha sindano hiyo, pamoja na uzi wa nailoni na koleo ndogo kwa ajili ya kuvuta sindano kupita kwenye ngozi ngumu.

Mshono ambao umefungwa.


Hatua 2:
Funga mshono vizuri.


Hatua 3:

Jeraha lenye mishono 5

Shona mishono ya kutosha kufunga jeraha zima.

Kidonda ambacho kimeingia sana ndani kinapaswa kushonwa ndani ya misuli kwa kutumia nyuzi maalum zinayoyeyuka baada ya muda,mishono ya kuunganisha ngozi pamoja. Kama huwezi kufanya hivyo kwanza, basi usifunge kidonda.

Ruhusu nyuzi zibaki ndani angalau kwa wiki moja (siku 10 kwa kidonda cha mguuni). Halafu kata kila uzi na kuuvuta nje. Kama huwa unatumia muda kushona nguo zako, utajikuta stadi yako ya kushona majeraha au vidonda ikiboreka pia.