Hesperian Health Guides

Majeraha na vidonda kwenye tumbo

Kama tumbo limeumia kutokana na kipigo, mathalan kutokana na anguko kali, ajali ya gari, au kupigwa teke na kitu kingine, angalia kama kuna michubuko ambayo ni dalili ya uvujaji wa damu wa ndani ya mwili. Uvujaji mkubwa wa damu mwilini unaweza kusababisha mshituko. Pia angalia iwapo kuna dalili za jeraha kali kwenye tumbo:

Dalili za hatari
  • Maumivu makali
  • Kuchanganyikiwa
  • Tumbo kuwa gumu kama ubao, na kuvimba
  • Dalili za kupoteza damu: kujisikia kuzirai, rangi ya mwili kubadilika, mapigo ya haraka ya moyo


Kwa ajili ya dalili hizi za hatari, mpe matibabu ya mshituko na tafuta msaada haraka. Usimpe chakula wala kinywaji chochote. Angalia Maumivu tumboni, kuhara na minyoo kwa taarifa zaidi juu ya dharura kuhusiana na tumbo.

Jeraha tumboni - utumbo umejitokeza nje.
Kama sehemu ya utumbo itamwagika nje ya mwili, ufunike kwa kutumia kitambaa kisafi ambacho kimelowekwa kwenye maji yaliyochanganywa na chumvi kidogo na tafuta msaada haraka. Usisukume kujaribu kuurudisha ndani.

Kitu kilichojeruhi kikiwa kinaning’inia nje ya mwili

Iwapo kitu ambacho kimesababisha jeraha kinaweza kubaki kinaning’inia nje ya mwili, kawaida ni salama zaidi kukiacha ndani na kutafuta msaada. Hata kama msaada utapatikana baada ya siku kadhaa, usikiondoe kitu hicho. Kiimarishe katika nafasi hiyo kwa kutumia bandeji au vitambaa safi na kuwahi hospitalini.

a man bleeding from a wound caused by a stick in his abdomen.