Hesperian Health Guides

Maumivu tumboni au kwenye utumbo

Katika sura hii:

Kama kuna maumivu, muulize mgonjwa aoneshe hasa wapi maumivu yalipo. Mahali maumivu yalipo inaweza kutoa mwanga juu ya kisababishi. Pia ni muhimu kujua kama matumbo yanafanya kazi – kutembeza chakula na kukichakata. Kama hapana, hii inaweza kuwa dalili ya hatari hasa.

  1. Uliza: mgonjwa amekwenda haja kubwa au kujamba? Kama anapata choo kama kawaida ni dalili nzuri. Kama mgonjwa hajaenda chooni kwa siku kadhaa, anaweza kuwa na tatizo la kupata choo kigumu. Kama hajapata choo, hawezi kujamba, na ana maumivu, tatizo linaweza kuwa uzibe kwenye utumbo.
  2. Sikiliza: kuna sauti zozote kutoka kwenye utumbo? Sauti ni dalili nzuri kiafya za chakula kuchakatwa na utasikia sauti hata kama kuna tatizo la ugumu wa choo. Kutokuwa na sauti ni dalili hatari ya utumbo kuziba.
  3. Gusa: je tumbo ni gumu kama ubao? Unapogusa anasikia maumivu sana? Hizi ni dalili za hatari kubwa.
mwili uliowazi ukionesha sehemu yenye maumivu katikati ya tumbo
Maumivu sehemu ya katikati tumboni
smwili uliowazi ukionesha sehemu zenye maumivu katikati na upande wa chini tumboni kulia
Kwanza maumivu husikika hapa
Baadaye maumivu husikika hapa
mwili uliyowazi ukionesha sehemu ndogo yenye maumivu juu kulia yakielekea kulia kifuani
Maumivu mara nyingi hufika hadi mgongoni
mwili uliyowazi ukionesha sehemu kubwa yenye maumivu upande wa kulia chini ya mbavu za chini
Maumivu hapa, wakati mwingine huenea kifuani
mwili uliyowazi ukionesha sehemu zenye maumivu ubavuni na kwenye tumbo la chini yakizunguka mgongo
Maumivu mgongoni katikati au sehemu ya chini, mara nyingi yakienea kuzunguka nyonga hadi sehemu za chini tumboni.
 mwili uliyowazi ukionesha sehemu zenye maumivu kwenye tumbo la chini la mwanamke na yakizunguka mgongo
Maumivu sehemu ya upande mmoja wa bega au shingoni

Jinsi ya kusikilizia

Sikilizia kwenye tumbo kwa kutumia kifaa maalum cha kusikilizia au sikio lako, ili kujua iwapo mgonjwa yupo hatarini. Tumbo lenye afya hutoa sauti ndogo za kugugumia kila baada ya dakika chache. (Kama wewe ni mfanyakazi wa afya, fanya zoezi la kusikilizia tumbo za watu zenye afya ili ujue sauti za kawaida zinazotolewa na tumbo hizi. Inahitaji uzoefu kuzisikia sauti hizi ndogo.)

mtu akisikiliza tumbo la mwanamke

Sauti nyingi za kugugumia zinaweza kumaanisha kuwa chakula kinatembea haraka kupita matumboni. Je mhusika ana tatizo la kuharisha?

Sauti za juu, au kutokuwa na sauti kabisa kwa dakika 2, ni dalili ya maumivu makali ya ghafla tumboni pasipo kuharisha. Jaribu kuligusa tumbo. Kama ni gumu na linauma, nenda hospitali haraka.

Jinsi ya kuhisi

Mvulana akionesha kwa kidole sehemu yenye maumivu kwenye tumbo lake upande wa kushoto; mfanyakazi wa afya akibonyeza kwenye tumbo la mtoto sehemu ya kulia.

Mwambie mgonjwa aguse mahali panapouma.

Ukianzia upande mkabala na mahali anapoonesha, bonyeza taratibu kuchunguza kiungo ndani ya mwili ambacho huenda ndicho chanzo cha maumivu (sehemu inayouma sana ndiyo iwe ya mwisho). Bonyeza taratibu lakini kwa mkazo, na endelea kwa mpangilio ili uweze kuchunguza kwa kugusa kila sehemu ya tumbo.

Pia angalia iwapo tumbo ni laini au gumu, na iwapo mgonjwa anaweza kuachia na kulegeza tumbo lake. Iwapo tumbo limekakamaa kama ubao, inawezekana kuna uzibe kwenye utumbo.

Jinsi ya kuchunguza maumivu ambayo hujitokeza baada ya kuondoa mkazo wa mkono kwenye tumbo

Polepole lakini kwa mkazo bonyeza tumbo, juu kidogo ya kinena, hadi litakapoanza kuuma kidogo. Halafu ondoa mkono wako haraka. Maumivu makali ya ghafla mara utakapoondoa mkono wako-makali kuliko yale ya mwanzo unapoweka mkazo wa mkono wako-yanaweza kutokea. Kama maumivu hayo hayapo upande wa kushoto, jaribu upande wa kulia. Maumivu haya ni dalili ya kidole tumbo. Nenda hospitali mara moja.

mkono ukibonyeza chini kwenye tumbo la mwanaume upande wa kulia
mkono ukitolewa kwenye tumbo la mwanaume na kusababisha maumivu

Maumivu makali tumboni yanayoibuka ghafla

mwanamke amejipinda kwa maumivu, akishikilia tumbo lake

Maumivu makali yanaweza kuanza ghafla, na kuendelea pasipo kuharisha. Maumivu makali tumboni pasipo kuharisha yanaweza kuashiria uzibe kwenye utumbo, kidole tumbo, mimba kutunga nje ya mji wa mimba au kizazi au matatizo mengine hatari. Kama utaona dalili hizi, unaweza kunusuru maisha ya mgonjwa kwa kumsaidia kwenda hospitali mara moja.

Dalili
  • Maumivu makali endelevu - kama kuchomwa au kukatwa kwa kisu kali.
  • Kutapika
  • Kupata choo mara chache au kutopata choo kabisa
  • Tumbo gumu, na ambalo halitoi mgugumo wowote
  • Kuhisi unaumwa sana

Kawaida, mgonjwa mwenye maumivu makali tumboni anakuwa anajigaragaza kutokana na maumivu, hawezi kujisikia vizuri na anakuwa akiihami tumbo lake kwa mikono yake.

Utumbo kuziba

Iwapo kuna kitu ambacho kimeziba sehemu yoyote ile ya utumbo, chakula na kinyesi haviwezi kupita. Hii inaweza kusababisha maumivu na maambukizi.

Pamoja na maumivu, mtu huyu anaweza kuanza kupata choo kigumu au kutopata choo kabisa na kutapika. Tumbo linaweza kuwa kimya, au kutoa sauti nyingi zenye mlio wa juu.

mvulana akitapika kwa nguvu
Uzibe utumboni huweza kusababisha kutapika kwa nguvu.

Tatizo la utumbo kuziba linaweza kusababishwa na:

Kama unadhani kuna uzibe kwenye utumbo, fanya mambo 2:

  1. Mpeleke mgonjwa hospitali mara moja. Huenda upasuaji ukahitajika.
  2. Kama kuna minyoo mahali unapoishi, mpe dawa ya minyoo ya askarisi ukiwa unampeleka hospitalini, hasa kama minyoo ndiyo itakuwa imesababisha uzibe huo. Bonyeza hapa kwa ajili ya dawa za minyoo.

Ugonjwa wa kidole tumbo na uvimbe wa ngozi ya fumbatio (peritonitis)

mtu akiwa katika maumivu kutokana na kidole tumbo
Maumivu yanaweza kuanzia sehemu inayozunguka kitovu
Halafu yakaendelea chini upande wa kulia.

Ugonjwa wa kidole tumbo unatokana na maambukizi ya kimfuko kidogo kilichounganika na utumbo mkubwa sehemu ya chini upande wa kulia wa tumbo. Hakuna njia ya kuzuia ugonjwa wa kidole tumbo. Hujitokeza tu kwa baadhi ya watu.

Dalili kuu ya ugonjwa wa kidole tumbo ni maumivu makali tumboni ambayo huzidi kuongezeka. Mtu mwenye ugonjwa wa kidole tumbo kawaida hapendi kula. Kawaida hakuna kuharisha. Homa ni kawaida,na mgonjwa huumia sana anapotembea au kusafiri kupita juu ya matuta ya barabarani. Ukiweka mkono sehemu hiyo na kubonyeza halafu ukaachia, maaumivu makali hutokea.

Tafuta msaada wa daktari. Kama ugonjwa huu hautatibiwa, kidole tumbo kilichoathirika kinaweza kupasuka na kusambaza vijidudu ndani ya tumbo. Hii inaweza kusababisha uambukizo hatari kwenye ngozi ya fumbatio ujulikanao kama peritonitisi.

Uvimbe wa fumbatio (Peritonitisi) unaweza pia kusababishwa na jeraha tumboni – kwa mfano kipigo kikubwa au kuchomwa na kitu chenye ncha kali tumboni.

Kama tumbo halitoi mgugumo wowote, ni gumu na linauma lote, huenda kuna ambukizo kwenye ngozi ya fumbatio.

watu 2 wamebeba mgonjwa kwenye kitanda cha kubebea wagonjwa

Kama unadhani mgonjwa ana ugonjwa wa kidole tumbo au maambukizi ya ngozi ya fumbatio(peritonitis):

  • Mpeleke hospitali.
  • Mpe dawa 2: metronidazo (metronidazole) NA sipro (ciprofloxacin) AU seftriazoni (ceftriaxone), AU ampisilini. Bonyeza hapa kwa maelekezo juu ya dozi.
  • Usimpe chakula chochote au kinywaji isipokuwa dawa na maji kidogo ya kumezea tu.

Chunguza kama kuna dalili za mshtuko kama vile pumzi dhaifu ya haraka haraka, rangi ya mwili kupauka, ngozi kuwa baridi; au kuchanganyikiwa au kupoteza fahamu. Angalia sura ya Huduma ya kwanza.

Mimba iliyotunga nje ya mji wa mimba au kizazi

mimba imetunga kwenye mrija wa uzazi
Kawaida, mimba hutunga ndani ya mji wa mimba au kizazi.
Mimba inayotunga nje ya mji wa mimba hukulia ndani ya mrija wa uzazi – lakini nafasi haitoshi. Kadri mimba inavyokua, mrija hupanuka na unaweza kupasuka. Hali hii husababisha maumivu makali na uvujaji damu ndani ya mwili.

Kama inavyokua mimba inapoharibika, dalili za mimba kutunga nje ya mji wa mimba hutokea mapema katika ujauzito — mara nyingi hata kabla mwanamke hajajua kuwa ana mimba. Kunakuwa na maumivu tumboni sehemu za chini, na uvujaji damu baada ya kutopata hedhi kwa mwezi 1 au zaidi.

Dalili
  • Uvujaji damu kidogo kutoka ukeni - (tofauti na uvujaji mzito wakati mimba inapoharibika).
mwanamke akiwa na maumivu ameshikilia tumbo na shingo lake
  • Maumivu yanaweza kuongezeka upande mmoja.
  • Kama ujauzito utapasua mrija wa uzazi, maumivu huwa makali zaidi.
  • Mwanamke anaweza pia kuwa na maumivu begani au shingoni.
  • Anaweza kusikia kizunguzungu au kupepesuka kwa sababu ya kutokwa na damu nyingi.

Maumivu makali tumboni sehemu ya chini yanaweza kusababishwa na mambo mengi, yakiwemo maambukizi kwenye kibofu, kidole tumbo, na mengine. Kama inawezekana, mshauri mwanamke apimwe kujua iwapo ni mjamzito. Kama kipimo kitaonesha ndiyo, au kama huwezi kupata kipimo hicho lakini unadhani anaweza kuwa na mimba ambayo imetunga nje ya mji wa mimba, msaidie afike hospitali – unaweza kuponya maisha yake. Kama Kipimo cha mimba kitaonesha hana mimba, basi hana tatizo la mimba ambayo imetunga nje ya mji wa mimba.

Mkiwa njiani kuelekea hospitali, tibu dalili za mshtuko kama vile pumzi dhaifu inayokwenda haraka haraka; rangi ya mwili kupauka, ngozi kuwa baridi; au kuchanganyikiwa au kupoteza fahamu. Angalia sura ya Huduma ya kwanza.

Mikakamao ya misuli ya tumbo inayoambatana na maumivu

Mikakamao nyingi siyo hatari sana.Inaweza kusababishwa na :

  • kula chakula ambacho kimeachwa nje muda mrefu au kimeharibika
  • kunywa maji yenye vijidudu ndani yake
  • minyoo
  • vidonda vya tumbo
  • msongo au wasiwasi
  • njaa
  • hedhi
kinywaji cha moto


Kawaida maumivu kutokana na mkakamao wa misuli tumboni hupungua bila tiba baada ya siku 1 au 2.

Unaweza kupata nafuu kwa:

  • Kunywa chai iliyochemshwa na tangawizi, budalasini, au aina nyingine ya chai ambayo inaweza kusaidia kutuliza maumivu.
  • Kula papai. Husaidia uchakataji wa chakula kwenye utumbo.
  • Oga maji ya moto, au tumia kitu cha moto kukanda tumboni, au kupumzika tu kwenye sehemu iliyotulia. Angalia sura Huduma ya kwanza kujifunza jinsi ya kutengeneza kitu chenye vuguvugu cha kujikandia.
  • Epuka vyakula ambavyo vinaweza kuchochea tumbo kutengeneza gesi. Vyakula hivyo ni pamoja na maziwa, jibini, kabeji, pilipili, vitunguu, au maharagwe.
mwanamke akichua tumbo lake
Taratibu kanda tumbo, au chua polepole kwa kufuata mdwara wa mwendo wa saa.


Unaweza kuzuia maumivu mengi ya tumbo kwa kupika chakula kikaiva vizuri ili kuua vijidudu, kula chakula kiingali cha moto, na kunawa mikono yako kabla ya kupika na kula. Kwa taarifa zaidi juu ya uandaaji na uhifadhi wa chakula, bonyeza hapa.

mwanamke ameweka mkono kifuani, akionekana kutojisikia vizuri
Kiungulia husababisha hisia ya kuungua au maumivu kifuani, na wakati mwingine kooni.

Kiungulia na ucheuaji

Kiungulia, kushindwa kuchakata na kufyonza asidi tumboni na ucheuaji vyote vinahusiana na hisia ya kuungua au maumivu katikati kifuani au kwenye njia ya chakula ambayo husababishwa na asidi tumboni kupanda juu kooni. Inaweza kusababisha maumivu makali sana. Maumivu huwa yanatokea unapokuwa umelala chini au baada ya kula-hasa baada ya kula sana, au kula kitu chenye mafuta sana au kilichokolezwa viungo.

Dhana ya ‘kuungua moyoni’ (heartburn) inaweza kuchanganya: haina uhusiano wowote na moyo. Maumivu ya kweli moyoni huaambatana na uzito fulani au mkazo, au mbanano. (Angalia sura ya Matatizo ya moyo - inaandaliwa).

Matibabu na uzuiaji
  • Kula chakula halafu subiri angalau saa 3 kabla hujaenda kulala.
  • Kula milo kidogo, lakini mara nyingi zaidi.
  • Epuka vyakula vyenye mafuta na viungo vingi.
  • Epuka pombe na uvutaji sigara, ambavyo huzidisha kiungulia.
  • Jaribu kutumia dawa za kupambana na asidi tumboni ili kupunguza maumivu.
mwanamke aliyelala kitandani sehemu ya juu ya mwili wake ikiwa imeinuliwa kwa kutumia mito Kaa wima baada ya kula, weka miito kujinua wakati wa kulala usiku (au inua sehemu ya juu ya kitanda chako kwa kutumia matofali kadhaa). Hii husaidia kuifanya asidi ibaki chini tumboni.
nafasi ya tumbo na utumbo na michubuko inayosababisha vidonda vya tumbo ndani ya mwili
Kidonda cha tumbo ni mchubuko au kidonda ndani ya tumbo au utumbo

Kidonda cha tumbo

Maumivu tumboni ambayo huja mara kwa mara yanaweza kuwa yanasababishwa na kidonda cha tumbo. Maumivu ya kidonda cha tumbo kawaida yanakuwa kama vile yanaunguza au kukwaruza, kama njaa na husikika sehemu ya kati ya tumbo upande wa juu. Mara nyingi, kidonda husababisha maumivu kwa wiki chache, na hutoweka kwa wiki au miezi kadhaa kbala ya kurudi. Maumivu yanaweza kupungua mtu anapokula au kunywa. (Au kula kunaweza kuzidisha maumivu, kutegemea na mahali kidonda kilipo.)

Matibabu: kupunguza maumivu na kusaidia kidonda kupona
chupa ya vidonge ikiwa na alama kubwa ya X ikiashiria - hapana
Hapana!
  • Acha kutumia ibrofeni (ibuprofen), aspirini, na dawa zingine za kupunguza maumivu. Matumizi ya dawa hizi mara kwa mara huumiza tumbo, na ni miongoni mwa sababu za kutokea vidonda vya tumbo. Panado (Paracetamol) ni bora kwa watu wenye matatizo ya tumbo kwa sababu haiathiri tumbo, lakini haipaswi kutumika sana au kila siku.)
  • Usivute sigara. Watu wanaovuta sigara huwa na vidonda zaidi, na vidonda vyao huchukua muda mrefu zaidi kupona.
  • Ulaji wa milo midogo na kunywa maji mengi siku nzima kunaweza kusaidia kupunguza maumivu.
  • Unaweza ukakuta vyakula vingine vikikuzidishia maumivu. Jaribu kuepuka vyakula vyenye asidi kama vile ndimo na kahawa. Pilipili, vyakula vyenye mafuta, na pombe huzidisha maumivu kwa baadhi ya watu.
  • Msongo unaweza kuwa sababu mojawapo inayochangia watu kupata vidonda vya tumbo, na pia kuzidisha maumivu. Kutafuta njia mbalimbali za kupunguza wasiwasi na maudhi inaweza kusaidia. Kwa taarifa zaidi juu ya kustarehe na kupunguza msongo wa mawazo, angalia sura ya Afya ya akili (inaandaliwa).


Kama baada ya wiki chache za kufanya mabadiliko bado kuna maumivu mengi, jaribu kutumia dawa ya kupunguza asidi tumboni yenye bei nafuu. Maumivu yanaweza kupungua kwa kutumia kalsiamu kaboneti (calcium carbonate), mara 4 kila siku kwa wiki 1. Dawa kwa ajili ya kudhibiti uzalishaji wa asidi tumboni ziitwayo proton pump inhibitors (PPI), kama vile omeprazo, hufanya kazi vizuri zaidi. Hupunguza asidi tumboni kwa kiwango cha kuweza kupunguza maumivu na mara nyingi kusaidia kidonda kupona. Hata hivyo, kama maumivu yatarudia, utahitaji kutumia dawa ya antibiotiki kuponya vidonda hivyo.

Matibabu: kuponya vidonda vya tumbo

Kwa ajili ya vidonda vya tumbo ambavyo hupona na kuibuka tena, utahitaji kutumia kwa pamoja dawa za antibiotiki, dawa ya kudhibiti uzalishaji wa asidi tumboni (proton pump inhibitors), na dawa za kudhibiti asidi kwa wiki 2. Hizi ni dawa nyingi, lakini ikitumika kwa usahihi vidonda vya tumbo havitarudia tena. Bonyeza hapa.

Kama kutakuwa na maumivu tumboni baada ya matibabu haya, huenda kuna tatizo lingine-siyo vidonda vya tumbo. Tafuta msaada.

Dalili za hatari

Je kuna dalili za vidonda vya tumbo kutoa damu? Chunguza iwapo kuna damudamu au vitu vyeusi vinavyofanana na mabonge ya kahawa ya unga kwenye matapishi. Kinyesi pia kinaweza kuwa na damu au vitu vyeusi vinavyofanana na lami au mafuta mazito ya gari. Hii ni hatari. Tafuta msaada haraka.

sodiamu baikaboneti au hamira inayotumika katika kutengeneza mikate na bidhaa zingine ikimiminwa kwenye kijiko
Baadhi ya watu hutumia sodiamu baikaboneti (sodium bicarbonate) kwa ajili ya kutibu maumivu tumboni. Hii hufanya kazi haraka, lakini husababisha tumbo kutengeneza asidi zaidi baadaye. Hivyo, usiitumie mara kwa mara. Usitumie sodiamu baikaboneti kama una matatizo ya moyo au miguu ambayo imevimba. Inaweza kuzidisha matatizo haya.

Matatizo ya kibofu cha nyongo

Kibofu cha nyongo ni kimfuko kidogo ambacho hukusanya nyongo kwa ajili ya kusaidia uchakataji na ufyonzaji wa vyakula vya mafuta. Nyongo inaweza kubadilika na kuwa gumu, na hatimaye kusababisha uzibe ndani ya kibofu cha nyongo. Hii inaweza kusababisha maumivu ambayo huchukua saa kadhaa. Matatizo ya kibofu cha nyongo hujitokeza sana miongoni mwa wanawake wenye umri wa miaka 40 au zaidi, watu wanene, na watu wenye kisukari. Lakini mtu mzima yeyote anaweza kupatwa na tatizo hili.

Dalili
  • Maumivu yanayoendelea kwa muda sehemu ya kati na sehemu ya pembeni ya mbavu za kulia. Maumivu haya yanaweza kuenea hadi mgongoni sehemu ya juu kulia au kwenye bega.
mwanamke mwenye maumivu yanayoenea kutoka tumboni kuelekea begani
maumivu
  • Maumivu ambayo huzidi kuongezeka, halafu kubaki vilevile kwa muda, na baada ya saa chache hutoweka taratibu.
  • Maumivu ambayo huja baada ya kula vyakula vyenye mafuta. Maumivu haya yanaweza kumuamsha mtu ghafla usiku kutoka usingizini.
  • Kichefuchefu na kutapika.
  • Pale ambapo kutumia asipirini au parasetamo, kubadilisha mkao, au kunyampa hakusaidii kuleta ahueni.

Ingawa dalili hizi zinaweza kusaidia kubainisha kuwepo tatizo la kibofu cha nyongo, kipimo cha kumulikwa ndani(ultrasound) au kupiga picha ya eksirei (x-ray) kinahitajika kupata uhakika.

Matibabu

Maumivu ya kibofu cha nyongo yanaweza kumkosesha mtu raha, lakini kama hakuna homa au dalili zingine za hatari zilizoainishwa hapa, hayana madhara ya haraka. Dawa ya iburofeni (Ibuprofen) inaweza kusaidia kupunguza maumivu.

Dalili za hatari

Kama mtu ana matatizo ya kibofu cha nyongo, kuwa mwangalifu katika kubaini mapema dalili za hatari zifuatazo. Mgonjwa atahitaji kufanyiwa upasuaji.

  • Maumivu ya kibofu cha nyongo ambayo hudumu zaidi ya saa 4 kwa wakati mmoja.
  • Matatizo ya kibofu cha nyongo ambayo yanaambatana na homa.
  • Maumivu ya kibofu cha nyongo yakiambatana na homa ya manjano (ngozi au macho kugeuka njano).
Uzuiaji

Epuka nyama zenye mafuta, vyakula vinavyoivishwa kwa kukaangwa kwenye mafuta, au vyakula vingine vyenye mafuta mengi ambavyo huchochea maumivu ya kibofu cha nyongo kwa mtu mwenye tatizo hili. (Haina tatizo kula kiasi kidogo cha mafuta kwenye chakula na kufanya hivyo husaidia kibofu cha nyongo kujisafisha. Mafuta yanayotokana na mimea ni bora kuliko mafuta ya nazi au ya wanyama).

Kama wewe ni mnene, kupunguza uzito kunaweza kusaidia, lakini fanya hivyo taratibu kwa kufanya mazoezi mara kwa mara na kula milo midogo midogo. Kupoteza uzito mkubwa haraka kunaweza kukusababishia tatizo la mawe tumboni.

watu wenye umri tofauti wakifanya mazoezi pamoja
Watu ambao hufanya mazoezi mara kwa mara angalau wako katika hatari kidogo ya kupatwa na tatizo la mawe tumboni, ukilinganisha na wale ambao hawafanyi mazoezi.

Mikakamao ya misuli na maumivu kuhusiana na hedhi

Wanawake wengi hupatwa na maumivu sehemu za chini tumboni kabla au wakati wa hedhi zao za kila mwezi. Pumzika, tumia njia ya kukanda, au tumia dawa yoyote ya kupunguza maumivu kama vile iburofeni. Kwa taarifa zaidi juu ya hedhi na jinsi gani ya kupunguza maumivu, angalia Miduara ya hedhi za wanawake (kinaandaliwa).


chupa ya maji ya moto na nguo nzito zenye uwezo wa kutia joto
Chupa ya maji ya moto au kujikanda na kitambaa chenye vuguvugu tumboni vinaweza kusaidia kupunguza maumivu.

Maambukizi sehemu ya nyonga

Mwanamke anapokuwa na maumivu sehemu ya chini tumboni, anaweza kuwa na maambukizi ya kizazi au mji wa mimba ambayo huitwa maambukizi ya sehemu ya nyonga. Kuna sababu kuu 2 zinazosababisha maambukizi ya sehemu ya nyonga, na zote ni hatari. Maambukizi yanaweza kutokea pale ambapo vijidudu hatari vinapoingia ndani ya mwili wa mwanamke, aidha baada ya kujifungua au baada ya mimba kutoka au kutolewa, au kama ugonjwa wowote unaoambukizwa kupitia ngono ukibaki bila kutibiwa na kuenea hadi kwenye kizazi au mji wa mimba.

Dalili
  • Maumivu sehemu ya chini ya tumbo –yanaweza kuwa ya wastani au makali.
  • Maumivu au kutokwa damu wakati wa tendo la ngono.
  • Tumbo la chini kuwa linauma unapolibonyeza.
  • Homa.
  • Uvujaji damu usio wa kawaida au majimaji yenye harufu mbaya kutoka ukeni.
Matibabu

Tibu maambukizi haya kwa kutumia antibiotiki haraka ili kuzuia ugonjwa mbaya zaidi, ugumba au hata kifo. Kama maambukizi haya yalianza baada ya kupata mimba au kujifungua, bonyeza hapa. Kama mwanamke hajawa na mimba siku za karibuni anahitaji dawa tofauti, zilizoorodheshwa katika Matatizo na maambukizi umeni na ukeni: Madawa (kinaadaliwa).

Maambukizi ya kibofu na figo

Maambukizi ya kibofu (maambukizi ya njia ya mkojo)husababisha maumivu au hisia ya moto wakati wa kukojoa, au maumivu nyuma kidogo au juu ya mfupa wa nyonga sehemu ya mbele. Lakini iwapo maambukizi yataenea hadi kwenye figo, maumivu yanaweza kuanza kusikika sehemu mbalimbali ubavuni au mgongoni. Maambukizi ya kibofu kawaida hujitokeza zaidi kwa wanawake. Kwa taarifa zaidi juu ya maambukizi ya kibofu na figo, angalia Matatizo katika Kukojoa (sura inaandaliwa).

sehemu ya nyuma ya mgongo wa mwanamke, ikionesha maeneo yenye maumivu kutokana na figo
Kusikia maumivu unapogusa upande mmoja wa mgongo sehemu ya chini yanaweza kuashiria maambukizi au mawe kwenye figo.

Mawe ya kwenye figo

Mawe ya kwenye figo ni vijiwe vidogo ambavyo huota ndani ya figo, mrija wa mkojo, au kwenye kibofu na kusababisha maumivu makali wakati vikitoka nje pamoja na mkojo. Kawaida makali ya maumivu huongeza taratibu, na baadaye kusimama. Maumivu hudumu dakika 20 hadi saa 1 kila mara. Mara nyingi huzidi zaidi upande mmoja na yanaweza kusikika sehemu yoyote kuanzia mgongoni hadi kwenye mrija wa mkojo. Miongoni mwa wanaume, maumivu yanaweza pia kusikika ndani ya mapumbu. Damu inaweza kuonekana mwenye mkojo. Kawaida huwa hakuna homa na tumbo linakuwa laini. Tiba ya kawaida ni kutumia dawa za kupunguza maumivu na kunywa maji mengi hadi mawe yatakapotoka, lakini angalia Matatizo katika kukojoa (sura inaandaliwa) kwa maelezo zaidi juu ya kuzuia na kutibu tatizo hili.

Ugonjwa wa ini (Hepatitisi au homa ya manjano)

mwanamke akionesha mahali ini lake lilipo, sehemu ya kulia ya upande wa juu wa tumbo lake
Ini husafisha damu. Ini linapokua halifanyi kazi vizuri, sumu na mabaki mengine hulundikana kwenye mwili, na kusababisha kuugua.

Ugonjwa wa ini (Hepatitisi au homa ya manjano) husababisha ini kuvimba. Ugonjwa huu unaweza kusababishwa na kirusi, kunywa sana pombe, au kula sumu. Aina zote za ugonjwa huu zina dalili zinazofanana. Lakini mtu anaweza kuambukizwa aina tofauti za hepatitisi kupitia njia mbalimbali, na baadhi ni hatari zaidi au hudumu zaidi kuliko zingine. Hepatitisi A na Hepatitisi kawaida kutoweka ndani ya miezi michache. Lakini Hepatitisi B na Hepatitisi C zinaweza kudumu kwa miaka mingi na kusababisha saratani ya ini.

Dalili
  • Kichefuchefu na kutapika.
  • Ngozi kuwasha.
  • Mkojo mweusi-rangi ya Coca-Cola.
  • Kinyesi laini chenye weupe.
  • Maumivu upande wa kulia. Au maumivu ya misuli na viungo kote mwilini.
  • Udhaifu na uchovu ambao unaweza kuendelea kwa miezi kadhaa.
  • Unjano kwenye macho na ngozi.

Unaweza kuhisi ini lililovimba kutoka nje, upande wa kulia, chini kidogo na mbavu.

Kusaidia ini kupona

Hivi sasa kuna dawa ambazo zinaweza kusaidia kutibu Hepatitisi B na C. Hata hivyo hazijaenea sana. Nenda katika kituo chako cha afya iwapo unaweza kuzipata eneo lako. Lakini hata bila dawa, kupumzika, kutumia vinywaji kwa wingi, na kuepuka baadhi ya vitu ambavyo huathiri ini vinaweza kusaidia.

mgonjwa akiwa amepumzika kitandani
Homa ya ini hukufanya ujisikie mchovu sana. Zingatia hali ya mwili wako na kupumzika kila inapobidi.
woman drinking liquid through a straw
  • Tumia vinywaji kwa wingi siku nzima – vikombe 8 au zaidi vya maji, maji ya matunda (juisi), na supu vyote vinaweza kusaidia afya yako.
  • Usinywe pombe angalau kwa miezi 6. Pombe ina madhara makubwa kwenye ini. Kama unahitaji msaada kuacha pombe, angalia Madawa, pombe na tumbaku (sura inaandaliwa).
  • Epuka parasetamo kwa sababu inaweza kujikusanya kwenye ini na kusababisha matatizo.
  • Tumia dawa ya aina nyingine ya kupunguza maumivu inapobidi. Kama una kifua kikuu, unaweza kutakiwa kusitisha kuanza dawa ya kifua kikuu hadi ini litakapopona. Tafuta msaada wa daktari. (Kama dalili za hepatitisi zitaanza kukutokea wakati wa kutumia dawa ya kifua kikuu, simamisha dawa mara moja na kutafuta msaada wa daktari.)
  • Kuwa muangalifu katika kutumia dawa. Epuka dawa ambazo siyo za lazima. Aina nyingi za dawa zina madhara kwenye ini, hasa zinapotumika katika vipimo vikubwa na kwa muda mrefu.
Uzuiaji

Hepatitisi A na E huenezwa kutokana na uchafu wa mazingira, hasa kuhusiana na kinyesi, na zinaweza kuzuiwa kwa kutumia vyoo kwa usahihi na kunawa mikono.

Nawa mikono yako mara nyingi kila siku kuwalinda wengine wasiambukizwe. Kila mtu ambaye anaishi kwenye nyumba yako anatakiwa kunawa mikono yake mara kwa mara pia.

Hepatitisi B na C hupatikana kwenye damu na majimaji kutoka ukeni na umeeni. Aina hizi za hepatitisi huenezwa wakati wa tendo la ngono au kupitia vifaa vya kuchanja, kukata au kutoboa vinapotumika kwa zaidi ya mtu mmoja bila kutakaswa kila mara. Hii huruhusu damu, na virusi ndani ya damu kuenea kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. Hepatitisi B na C inaweza pia kuenea kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wake wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua, au baada ya kujifungua.

Katika maeneo ambapo hepatitisi B imeenea, zikiwemo sehemu nyingi za Afrika na Asia, huwaathiri pia watoto na wanafamilia wengine bila hata kushirikiana damu. Hii inaweza kutokea hasa iwapo familia inaishi kwenye nyumba ndogo yenye mbanano na watu wanagusana kila mara.

Zuia hepatitisi B na C:

paketi la kondomu

  • Epuka sindano pale inapowezekana. Sindano yoyote ile na bomba lake viwe vipya. Kama huwezi kupata vipya, lazima uchemshe sindano na bomba lake kabla ya kutumia. Angalia Dawa, vipimo na matibabu (sura inaandaliwa).
  • Tumia kondomu kila unapofanya tendo la ngono.


Hepatitisi A na B zinaweza kuzuilika kwa kutumia chanjo. Chanjo ya hepatitisi B ni muhimu hasa kwa wale waishio katika maeneo ambapo homa hiyo na saratani ya ini vimeenea.

Kama unamhudumia mgonjwa mwenye hepatitisi, linda afya yako kwa kunawa mikono mara kwa mara na kujikinga dhidi ya damu na kinyesi chake.


Jipu kwenye ini

Jipu kwenye ini linaweza kusababishwa na ambukizo la ameba ambalo limeenea hadi kwenye ini. Kawaida hali hujitokeza zaidi miongoni mwa wanaume.

Dalili

Maumivu pale unapotomasa tumbo sehemu ya juu upande wa kulia, na homa. Maumivu yanaweza kuenea hadi upande wa kulia wa kifua. Maumivu huzidi sana mtu anapotembea. Linganisha ugonjwa huu na hepatitisi; sirosisi (cirrhosis-ugonjwa mwingine wa ini unaoambatana na uharibifu wa tishu za ini) (angalia Dawa, pombe, na tumbaku - sura inaandaliwa); na maumivu ya kibofu cha nyongo.

Kama mtu mwenye dalili za jipu kwenye ini ataanza kukohoa majimaji yenye rangi ya udongo, inawezekana jipu limeanza kuvujia kwenye mapafu yake. Hii inahitaji msaada wa daktari.

Matibabu

Toa tiba inayofanana na ya kuhara damu kunakotokana na maambukizi ya ameba. Halafu toa dawa ya diloksanaidi furoti (diloxanide furoate) kwa siku 10.