Hesperian Health Guides

Kuhara

Katika sura hii:

"mtoto aliyekonda sana na kuonekana mgonjwa akiwa anaharisha"

Kujisaidia kinyesi chepesi chenye majimaji mara kadhaa kwa siku ni kuharisha.

Mtu anapokuwa anaharisha, hupoteza majimaji mengi na virutubishi haraka sana. Mtu mzima mwenye afya anaweza akawa na tatizo la kuhara kwa siku 1 au 2, na atapona haraka. Lakini kupoteza maji mengi kiasi hicho na lishe ni hatari kwa watoto, watu wazima, na watu wengine ambao tayari ni dhaifu kutokana na utapiamlo na magonjwa mengine.

Huduma kwa watoto wanaoharisha imeelezewa kwenye Kuwatunza watoto. Iwapo unamhudumia mtoto mwenye tatizo la kuharisha, au unaishi kwenye jamii ambapo vifo vingi vya watoto hutokana na kuhara, tafadhali soma sehemu hii inayofuata, halafu soma hapa.

Dalili za hatari
  • Kuharisha sana kinyesi chenye majimaji ndani ya muda mfupi. Hii inaweza kuwa dalili ya Kipindipindu. Bila kuzingatia sababu, kuharisha sana ndani ya muda mfupi husababisha upungufu wa maji mwilini.
  • Kuharisha kinyesi chenye mchanganyiko wa damu na kamasi huitwa ugonjwa wa kuhara damu.
  • Kuharisha kunakodumu wiki kadhaa. Aina hii ya kuhara kwa muda mrefu husababisha mwili kupoteza virutubishi na kudhoofisha utumbo. Kawaida husababishwa na utapiamlo au ugonjwa wa muda mrefu.
Matibabu
"mwanamke akimlisha mtoto na kijiko"
  1. Tibu upungufu wa maji mwilini. Upungufu wa maji mwilini ndio hatari hasa katika kuharisha, na ndiyo kisababishi cha watu wanaoharisha kupoteza maisha. Hivyo, hatua muhimu kwa watu wanaoharisha ni kutumia vinywaji kila mara unapoharisha. Unaweza kutengeneza kinywaji cha kuuongezea mwili maji nyumbani kufidia virutubishi ambavyo unahitaji. Kunywa vinywaji hakuzidishi kuharisha badala yake husaidia kuponya maisha.
  2. Mpe chakula. Mwanzoni, mtu anaposikia kichefuchefu, unaweza kumpatia vitafunwa vidogovidogo au chakula chepesi. Mtindi na ndizi hasa husaidia na vinaweza kuwezesha uponaji wa haraka zaidi. Mpe chakula zaidi kadri atakavyoweza kula zaidi. Watoto hasa wapatiwe chakula.
  3. Aamua kama dawa zitasaidia (kawaida, hazisaidii). Kukusaidia kuamua, bonyeza hapa.

Kuhara husababishwa na nini?

"Mwanamke akiwaza"
Kazi moja ninayoifanya ni kuwatibu watoto wanaoharisha.Huenda ningeutumia muda wangu vizuri zaidi kwa kuipigania jamii yangu kupata mfumo wa maji safi.

Kuharisha husababishwa na mambo mengi. Sababu za kawaida ni:

  • Kijidudu (kirusi, bakteria, au kinyemelezi) kinachosambazwa kupitia hali duni ya usafi wa mazingira. Zuia kuharisha kwa kutumia vyoo, kunawa mikono, na kupika chakula vizuri na kukila mara baada ya kutoka jikoni (badala ya kukiacha kikakaa wazi kwa saa kadhaa). Unaponunua chakula mitaani, omba kirudishwe kwenye moto tena. Angalia Maji na usafi wa mazingira kwa taarifa zaidi juu ya kuboresha usafi wa mazingira – njia bora zaidi ya kuzuia kuharisha.
  • Ambukizo lingine mwilini. Maambukizi ya sikio, maambukizi ya kibofu, malaria, au VVU vyote vinaweza kusababisha kuharisha. Kuharisha kutapungua mara utakapotibu chanzo chake kikuu cha maambukizi.
  • Utapiamlo. Utapiamlo hudhoofisha matumbo, na kuyapuguzia uwezo wa kufyonza chakula na majimaji ambavyo kulazimika kupita haraka na kusababisha kuharisha. Chakula bora, kila siku kinahitajika kutibu utapiamlo. Kwa mawazo zaidi jinsi ya kula vizuri hata unapokuwa na uwezo mdogo bonyeza hapa.
  • Antibiotiki (Viuavijasumu). Antibiotiki zinaweza kusababisha kuharisha na maumivu tumboni. Hutumika zaidi kuliko zinavyohitajika na magonjwa mengi yanaweza kupungua nguvu bila kutumia dawa hizo. Kwa mfano, hazisaidii chochote juu ya mafua ya kawaida au magonjwa mengine ambayo husababishwa na virusi. Kwa ujumla, epuka dawa za antibiotiki kwa ajili ya maambukizi ya kawaida, na tumia tu unapokuwa na uhakika kwamba ugonjwa unaoutibu unahitaji dawa hizi.
"mwanamke mwenye umri mkubwa akimsaidia mtoto wa kike kunawa mikono yake kwenye benseni, mvulana akinawa mikono yake kwenye bomba, na mwanamke akinawa mikono yake kwenye sinki bafuni"
Unaweza kuzuia visababishi vingi va kuharisha kwa kunawa mikono yako mara kwa mara kwa maji na sabuni.

Ulaji na kuharisha

Mtu ambaye anaharisha anapaswa kuanza kula tena mara baada ya kuharisha kadri iwezekanavyo. Kwa mtu ambaye anatapika, au anajisikia mgonjwa sana na hawezi kula, mpe chakula kidogokidogo mara nyingi kila siku. Kama anaharisha sana, mpe chakula kidogo kila baada ya saa 1 au 2 kufidia lishe iliyopotea. Jaribu kumpa supu au rojo ya wali, mahindi, au viazi. Pia changanya nyama kidogo ambayo imepikwa vizuri, mayai, au mbogamboga kama vinaweza kumkaa tumboni. Maziwa yaliyochachushwa au mtindi hutoa protini. Vyakula vilivyokaangwa na matunda mabichi havifai kwa mtu ambaye anaharisha.

Kwa kuhara ambako kumedumu kwa wiki 2 au zaidi – ugonjwa sugu wa kuhara – kula hasa ni muhimu. Ugonjwa sugu wa kuhara kawaida husababishwa na utapiamlo au ugonjwa amabao huchukua muda mrefu kupona, kama vile VVU. Katika hali yoyote ile, chakula zaidi kinahitajika kufidia kile ambacho kimepotea kutokana na kuharana kusaidia matumbo kufyonza chakula kinacholiwa.

Utapiamlo huzidisha tatizo la kuharisha.
Tatizo la kuharisha huzidisha utapiamlo.
Chakula huvunja mduara huu.


Mtoto mwenye utapiamlo anapaswa kula mara nyingi zaidi-mara 6 kwa siku au zaidi. Kila siku, anahitaji protini na mafuta, kufidia nguvu na nishati iliyopotea. Mboga za majani na matunda huulinda mwili na kusaidia kupambana na maambukizi – yakiwemo maambukizi ambayo huchangia kuhara. Bonyeza hapa kuhusu jinsi ya kutibu utapiamlo.

"maharagwe, maziwa, mtindi, jibini, samaki, nyama, mayai, njugu"
Watoto wenye ugonjwa sugu wa kuhara huhitaji vyakula vyenye protini kuliko kawaida.

Madawa

Kwa matatizo mengi ya kuhara, matumizi ya dawa hayatatibu maambukizi ambayo yalisababisha tatizo hilo. Ni kupoteza fedha bure na pia huenda matumizi ya dawa hizo yakasababisha hatari zaidi.

Kwa baadhi ya visababishi vya kuhara, antibiotiki zinaweza kusaidia. Antibiotiki husaidia dhidi ya ugonjwa wa kuhara damu na baadhi ya maambukizi ya kipindupindu. Lakini hata kwa ugonjwa wa kuhara na kipindupindu, kutumia vinywaji ndiyo tiba muhimu zaidi. Kamwe usimpe mtu anayeharisha dawa ya kulainisha tumbo.

Madawa ya kupambana na kuhara kama vile bismasi (bismuth) au loperamidi (loperamide) hupunguza kasi ya kuharisha au kufunga tumbo kabisa lakini hayawezi kuzuia upungufu wa maji mwilini, ambao ndiyo hatari kuu katika tatizo la kuharisha. Hata kama maji hayatoki nje ya mwili, yanakuwa yanatoka kwenye viungo vyote ambavyo vinayahitaji kufanya kazi.Ingawa kwa nadra sana madawa husaidia, kwa mfano, kama utakuwa kwenye basi ukisafiri kwa muda mrefu, hupunguza uwezo wa mwili wa kuondoa bakteria zinazosababisha tatizo hilo na kufanya kuhara kuendelea kwa muda mrefu.

Epuka dawa hizi mgonjwa anapokua na homa, akiharisha damu, auakiharisha mfululizo (kipindupindu). Loperamidi (Loperamide) siyo salama kwa watoto.

"upside-down bottle with a plug that keeps liquid inside"
Madawa ya kupambana na kuhara hufanya kazi kama kizuizi. Huzuilia maambukizi ndani badala ya kuyaruhusu kutoka.
"chupa yenye kimiminika ndani ikiangalia chini, mdomo wake ukiwa umezibwa kuhakikisha majimaji yanabaki ndani "

Kipindipindu

Mharo mkubwa ambao huonekana kama maji yaliyooshea mchele unaweza kuwa kipindupindu. Ugonjwa wa kipindupindu huenea haraka na kuwaathri watu wengi kwenye jamii kwa wakati mmoja. Husababisha upungufu mkali wa maji mwilini ambao unaweza kusababisha kifo. Unaweza kunusuru maisha ya mtu mwenye kipindupindu kwa kumpa vinywaji ili kuuongezea mwili wake maji ambayo anakuwa anapoteza.

Matibabu

Tibu upungufu wa maji mwilini kwa kuendelea kumpatia kinywaji maalum cha kumuongezea maji mwilini. Muwezeshe mgonjwa anywe kadri awezavyo, bila kusimama hadi kuhara kutakaposimama na dalili zote za upungufu wa maji mwilini kutoweka. Hata kama mgonjwa anatapika, anapaswa kuendelea kunywa.

Antibiotiki zinaweza kusaidia katika baadhi ya matukio ya kipindupindu. Antibiotiki itakayotumika itategemea na usugu wa dawa katika eneo lako. Wasiliana na kituo cha kutolea huduma za afya cha karibu, na bonyeza hapa.

Kipindupindu ni tishio kwa kila mtu

Mlipuko wa kipindupindu ni dharura kwa jamii nzima. Bakteria inayosababisha kipindupindu huenezwa kupitia mifumo ya huduma ya maji na hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa kusimamisha ueneaji huo.

"tandiko la turubai likiwa na shimo lilitobolewa katikati, limewekwa juu ya ndoo"
Kitanda cha mgonjwa wa kipindupindu kinaweza kuruhusu watu angalau kupumzika na kubaki wakiwa wasafi kiasi.
  • Kuwa na uhakika kwamba kila mtu anajua tiba muhimu zaidi ya kipindupindu: kunywa vinywaji kwa wingi kadri uwezavyo. Sambaza ujumbe juu ya kinywaji maalum cha kuurudishia maji mwilini kupitia radio, kuwataarifu majirani, na kubandika taarifa kwenye mbao za matangazo.
  • Nawa mikono yako mara kwa mara kuwasaidia watu wote kuelewa umuhimu wa kuzingatia usafi katika kuzuia ueneaji wa maambukizi.
  • Wasaidie wahitaji kupata msaada wa kiafya. Huenda kukawa kumeazishwa kliniki au kituo maalum cha tiba au mahali ambapo watu wanaweza kupelekwa kupata huduma ya kuongezewa maji mwilini. Wakati mwingine dawa za antibiotiki husaidia na zinaweza kuwa zinatolewa kwenye kituo cha afya cha dharura.
  • Saidia juhudi za kuifanya huduma ya maji kuwa salama. Bonyeza hapa.
  • Milipuko ya usoni inaweza kuzuilika kwa kujenga vyoo na kuboresha usafi wa mazingira kwa ajili ya kila mtu. Kadri watu watakavyoendelea kukosa vyoo kwa ajili ya kujisaidia, au vyanzo vya maji ya kunywa kuendelea kuchafuliwa na vinyesi, kila mtu atakuwa katika hatari ya kuambukizwa kipindupindu na magonjwa mengine. Bonyeza hapa kwa taarifa juu ya jinsi ya kujenga vyoo sala.
  • Kuna chanjo ambazo zinaweza kusaidia kuzuia kipindupindu. Chanjo hizi hufanya kazi vizuri zaidi pale jamii nzima inapopewa chanjo kwa ajili ya kuzuia ueneaji wa mlipuko.

Kuhara damu

Ugonjwa wa kuhara damu kawaida husababishwa na bakteria ijulikanayo kama shigella, au vijidudu nyemelezi vinavyoishi kwenye utumbo vijulikanavyo kama ameba.

Dalili
  • Kinyesi chenye majimaji kikiwa na kiasi kikubwa cha kamasi na damu kwa kawaida.
  • Maumivu yanayoambatana na mikakamao ya misuli tumboni na hisia ya kutaka kwenda kujisaidia haja kubwa, hata kama hakuna kitakachotoka, au kutoa kamasi tu .
  • Maumivu kwenye unyeo.
  • Kuhara kukipishana na vipindi vya kutoa choo kigumu au kutopata choo kabisa.

Jinsi ya kubaini chanzo cha kuhara damu

Kama mtu anahara damu kwenye kinyesi, ni bora zaidi kupima choo hicho kwenye maabara kujua chanzo. Kama huwezi kupata kipimo cha maabara, dalili hizi zinaweza kusaidia kubainisha chanzo.

Shigella, (kuhara damu kunakosababishwa na bakteria) kawaida huibua homa. Kawaida huanza ghafla, na kusababisha mikakamao yenye maumivu na kinyesi chenye majimaji kikiwa na kamasi au damu.

Kuhara + kamasi au damu + homa = shigella (kuhara damu kunakosababishwa na bakteria)

Ameba, (kuhara damu kunakosababishwa na ameba), vinaweza kusababisha kutokwa na damu nyingi. Kawaida haiambatani na homa.

Kuhara + damu+ bila homa = ameba (kuhara kunakosababishwa na ameba)

Matibabu

Ni bora zaidi kutibu ugonjwa wa kuhara damu na dawa za antibiotiki, hasa kwa watoto wadogo au watu ambao tayari ni dhaifu au ni wagonjwa.

Tiba dhidi ya shigella

Shigella huzua haraka usugu kwa dawa. Hivyo hakuna dawa moja ambayo ni bora zaidi kwa maeneo yote. Angalia Dawa, vipimo, na tiba (sura inaandaliwa) kujifunza zaidi juu ya usugu kwa dawa. Katika matukio mengi, sipro (ciprofloxacin) hufanya kazi, lakini ulizia kwenye kituo cha kutolea huduma za afya cha karibu ili kujifunza zaidi juu ya tiba bora.

Tiba dhidi ya ameba Kutibu ameba, mapatie mgonjwa metronidazo (metronidazole).

Giardia

Giardia ni kijidudu kidogo nyemelezi ambacho huishi kwenye utumbo na ni chanzo cha kawaida cha ugonjwa wa kuhara, hasa kwa watoto.

Dalili
  • Gesi nyingi tumboni ambayo husababisha tumbo kujaa na kuvimba, kusokota, kichefuchefu, kujamba na kubeua mara kwa mara. Harufu mbaya kutokana na kubeua,inayofanana na ya mayai yaliyooza.
  • Mharo wa njano ukiwa na povu na harufu mbaya, bila damu au kamasi.
  • Kawaida hakuna homa.
  • Hali hii inaweza kudumu kwa wiki kadhaa, ikisababisha uzito kupungua na dhaifu.


Maambukizi ya kawaida ya giardia yanakera, lakini hupungua yenyewe ndani ya wiki 6. Lishe bora husaidia. Maambukizi ambayo huchukua muda mrefu, hasa kwa mtoto, ni bora yatibiwe kwa dawa ya metronidazo. Dawa ya quinacrine hupatikana kwa ] bei nafuu zaidi na mara nyingi hufanya kazi vizuri, lakini ina madhara makali ya pembeni.