Hesperian Health Guides
Matatizo mengine ya tumboni
HealthWiki > Toleo Jipya: Mahali Pasipo na Daktari > Maumivu tumboni, kuhara, na minyoo > Matatizo mengi ya tumbo yanaweza kuepukika
Sura ya Maji na usafi wa mazingira: Funguo za kudumisha afya inaonesha jinsi ya kuyafanya maji kuwa salama zaidi kwa ajili ya kunywa, na usimamizi wa kinyesi cha binadamu ili kulinda afya ya jamii. Kama familia au majirani zako hupatwa mara kwa mara na maumivu ya tumbo, kuhara, au minyoo, soma sura hiyo. Sura ya Lishe bora hutengeneza afya bora inahusu jinsi ya kula vizuri ili kupata afya bora, hali ambayo husaidia kuzuia maumivu tumboni, kichefuchefu, na matatizo mengine ya tumboni.
Njia zingine za kuzuia na kutibu matatizo hayo bila kutumia dawa ni pamoja na:
- Kunywa angalau glasi 8 za maji kila siku, na zaidi unapokuwa unafanya kazi au ukitokwa jasho. Hii inaweza kusaidia kuzuia tatizo la kupata choo kigumu.
- Kula mboga za majani, matunda, na nafaka nzimanzima kila siku. Hii inaweza kuzuia kupata choo kigumu na ni muhimu kwa ajili ya afya kwa ujumla.
- Vyakula vyenye mafuta mengi, viungo vingi, au asidi vinaweza kusababisha maumivu ya tumbo. Kama una tatizo la kuumwa tumbo , epuka vyakula hivi kwa wiki kadhaa, hadi utakapojisikia vizuri.
- Baadhi ya watu hupatwa na tatizo la gesi inayouma tumboni au kuhara wanapokunywa maziwa au kula jibini. Jaribu kuepuka vyakula ambavyo vimetengenezwa kutokana na maziwa. (Kama hii haitasaidia, ndani ya wiki moja au mbili, basi hakuna sababu ya kuendelea kujinyima vyakula hivi.)
- Epuka matumizi ya sigara na pombe. Husababisha matatizo ya tumbo.
- Je unatumia dawa zozote? Aspirini, ibuprofeni, aina nyingi za antibiotiki , na dawa zingine zinaweza kusababisha maumivu ya tumbo. Kwa magonjwa machache, kama vile VVU, ni inabidi kuendelea kutumia dawa hizo zenye nguvu kwa muda mrefu. Lakini kwa magonjwa mengi, kawaida kuna dawa mbadala ambazo unaweza kutumia kama dawa ambayo umekuwa ukitumia inakusababishia maumivu ya tumbo. Huenda huhitaji dawa yoyote kabisa.
- Wasiwasi na msongo pia huwasababishia baadhi ya watu maumivu tumboni. Sura ya Afya ya akili (inaandaliwa) inatoa mawazo juu ya jinsi ya kupata utulivu unapokuwa katika kipindi kigumu cha maisha.