Hesperian Health Guides

Maumivu tumboni, kuhara, na minyoo: Madawa

Maumivu tumboni, kuhara, na minyoo: Madawa

Dawa za Kuhara

Utaratibu wa kuuongezea mwili maji ndiyo tiba muhimu zaidi kwa ajili ya kuhara bila kujali kunasababishwa na tatizo gani. Katika matukio mengi, kuuongezea mwili maji na lishe bora tu ndiyo mahitaji pekee. Pale panapokuwa na maambukizi ya vijidudu vya giardia, kuhara damu(ameba au shigella), au kipindupindu, hasa miongoni mwa watoto wadogo na watu wazima, dawa za antibiotiki na dawa zingine zinaweza pia kusaidia.

Giardia

Metronidazo hufanya kazi vizuri zaidi; mpe kwa siku 5 hadi 7. Quinacrine inaweza pia kutumika na bei yake ni nafuu.

Kuhara damu kutokana na Ameba

Tumia metronidazo kwa siku 7 hadi 10. Pia tumia diloxanide.

Shigella

Shigella inausugu kwa baadhi ya dawa za antibiotiki. Hivyo ni muhimu sana kutafuta dawa ambazo bado zina uwezo wa kuitibu katika eneo lako. Tafuta ushauri kutoka kituo cha afya. Unaweza kutumia ampisilini, au kotrimozazo. Lakini katika maeneo mengi kuna usugu kwa dawa hizi, na seftriksoni (ceftriaxone) inaweza kutumika kama mbadala. Sipro (ciprofloxacin) inaweza kutumika kwa watu wazima, lakini epuka kuwapa watoto. Kwa dawa yoyote utakayotumia, kama hakutakuwa na mabadiliko baada ya siku 2, jaribu dawa ya antibiotiki nyingine.

Kipindupindu

Utaratibu wa kuuongezea mwili maji ni muhimu kuokoa maisha ya mtu mwenye kipindupindu. Endelea kumpatia kinywaji maalum cha kuuongezea mwili maji hadi atakaposimamisha kuhara na dalili zote za kupungukiwa maji kutoweka. Halafu endelea kumpa kikombe cha chai cha maji hayo kila baada ya kujisaidia. Kinywaji cha kuuongezea mwili maji ambacho kimetengenezwa kutokana na mchele au uga wa mahindi kinaweza kuwa bora zaidi.

Wagonjwa wa kipindupindu au wenye matatizo makali ya kuhara wanapaswa pia kupewa viongeza madini ya zinki mwilini (zinc supplements).

Dawa za Antibiotiki siyo tiba bora zaidi ya kipindupindu, na katika sehemu nyingi ugonjwa huu umejenga usugu dhidi ya baadhi ya antibiotiki. Toa dawa za antibiotiki pale unapokuwa unafahamu aina gani ambazo zinafanya kazi dhidi ya kipindupindu katika eneo lako. Anzisha antibiotiki kwa njia ya mdomo baada ya mgonjwa kuacha kutapika. Antibiotiki ambazo zinaweza kusaidia ni pamoja na doksaikilini (doxycycline), tetrasaikilini (tetracycline), kotrimozazo (cotrimoxazole), sipro(ciprofloxacin), na erithromaisini (erythromycin). Erithromaisini ni salama zaidi kwa mama wajawazito na watoto.

Kuna chanjo ambazo zinaweza kusaidia kuzuia kipindupindu. Hufanya kazi vizuri zaidi pale jamii nzima inapopatiwa chanjo hiyo kuzuia uneaji wa mlipuko.