Hesperian Health Guides

Dawa za antibiotiki hupambana na maambukizi

Lishe bora hutengeneza afya bora: Madawa

Kotrimozazo (Cotrimoxazole), Trimethoprimu (Trimethoprim)/salfamethozazo (sulfamethoxazole), TMP-SMX


Kotrimozazo, ambayo ni muunganiko wa dawa 2 za antibiotiki, siyo ghali na hutoa tiba pana kwa maambukizi mbalimbali. Ni dawa muhimu kwa watu wanaoishi na VVU na inaweza kuzuia maambukizi mengi ambayo hutokana na maambukizi ya VVU. Angalia sura ya VVU na UKIMWI (inaandaliwa).

MuhimuNBgrnimportant.png

Epuka kutoa kotrimozazo kwa watoto wachanga chini ya wiki 6 na wajawazito ambao wamebakisha miezi 3 kujifungua. Mzio hutokea sana kuhusiana na dawa hii. Dalili za mzio ni homa, kupumua kwa shida, au upele. Simamisha dawa hii ya kotrimozazo kama atatokwa na upele au kama unafikiri huenda kuna mzio.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png
Kotrimozazo hutengenezwa ikiwa na nguvu tofauti za dawa 2 zilizomo ndani. Hivyo inaweza kuwa, kwa mfano 200/40 (ikimaanisha miligramu 200 salfamethozazo (sulfamethoxazole) na miligramu 40 za trimethoprimu (trimethoprim) au 400/80 au 800/160. Dozi wakati mwingine huelezewa tu kwa kiasi cha trimethoprimu (namba ya pili).
Kwa aina nyingi za maambukizi
Wiki 6 hadi miezi 5: toa salfamethozazo miligramu 100 mg na trimethoprimu miligramu 20, mara moja kwa siku kwa siku 5.
Miezi 6 hadi miaka 5: toa miligramu 200 za salfamethozazo (sulfamethoxazole) + miligramu 40 za trimethoprimu (trimethoprim), mara 2 kila siku kwa siku 5.
Miaka 6 hadi 12: toa salfamethozazo miligramu 400 + trimethoprimu miligramu 80, mara 2 kila siku kwa siku 5.
Zaidi ya miaka 12: toa salfamethozazo miligramu 800 + trimethoprimu miligramu 160, mara 2 kila siku kwa siku 5.

Amoksilini


Amoksilini ni dawa aina ya penisilini yenye tiba pana, maana yake ni kwamba huua aina nyingi za bakteria. Dawa hii mara nyingi inaweza kutumika kama mbadala wa ampsilini. Pale ambapo amoksilini imependekezwa kutumika katika kitabu hiki, unaweza pia kutumia ampisilini katika nafasi yake kwa kuzingatia dozi sahihi. Dawa zote 2 ni salama kwa watoto wachanga na watoto wadogo.

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Amoksilini inaweza kusababisha kichefuchefu na kuharisha(lakini siyo sana kama ampisilini). Epuka kutoa dawa hii kwa watu ambao tayari wanaharisha - kama unaweza wapatie dawa aina nyingine ya antibiotiki.

Madhara mengine ya kawaida ya pembeni ni upele. Lakini uvimbevimbe, mithili ya malengelenge, unawowasha ambao huja na kutoweka ndani ya saa chache huenda ni dalili ya mzio kutokana na penisilini. Simamisha utoaji wa dawa hiyo mara moja na usimpe mtu huyu penisilini tena. Matukio ya usoni yanaweza kuwa mabaya zaidi na hata kutishia maisha. Kwa baadhi ya matatizo, erithiromaisini inaweza kutumika. Upele unaoenea tambarare ukifanana kama wa surua, na kawaida ukionekana wiki moja baada ya kuanza kutumia dawa hii na ambao huchukua siku kadhaa kutoweka, mara nyingi siyo dalili ya mzio. Lakini siyo rahisi kujua fika iwapo upele huo unatokana na mzio au la,hivyo ni bora kusimamisha dawa.

MuhimuNBgrnimportant.png

Usugu dhidi ya Amokislini unazidi kuenea. Kutegemea na mahali unapoishi, dawa hii inaweza kutofanya kazi tena dhidi ya stafilokokasi (aina ya bakteria wanaosababisha uvimbe unaotunga usaha, kisonono, shigella, na maambukizi mengine.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png

Amoksilini hufanya kazi vizuri inapotumika kwa njia ya mdomo. Kumpa mtoto mdogo vidonge au kapsuli, saga kidonge au fungua kapsuli na kugawa unga wake ili kupata kiasi unachohitaji. Halafu changanya kwenye maziwa kidogo ya mama. Mlishe mtoto maziwa na dawa kwa kutumia kikombe au kijiko.

Kama zilivyo antibiotiki nyingine, kila mara toa dawa hizi angalau kwa siku chache kama ilivyooneshwa hapa. Kama mtu ataendelea kuonesha dalili za maambukizi, endelea kumpa dozi ile ile hadi dalili zote zitakaponekana kutoweka angalau kwa saa 24. Kama mgonjwa atakuwa ametumia dawa kwa siku zote zilizoelekezwa na bado anaendelea kuwa mgonjwa, simamisha kumpa dawa ya antibiotiki na tafuta msaada zaidi wa kitabibu. Kwa mtu mwenye maambukizi ya VVU, mpe dawa kwa siku zote zilizoorodheshwa.

Vile vile kiasi cha dawa ya antibiotiki mtu anachopaswa kutumia hutegemea umri na uzito wa wake na ukali wa maambukizi. Kwa ujumla toa dozi ndogo kwa mtu mweye uzito mdogo au maambukizi yasiyo makali sana, na dozi kubwa kwa mtu mwenye uzito mkubwa au kwa maambukizi makali.

Toa miligramu 45 hadi 50 kwa kila kilo kwa siku, ikigawanywa katika dozi 2 kwa siku. Kama huwezi kumpima mtoto, mpe dozi kulingana na umri:
Chini ya miezi 3: toa miligramu 125, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Miezi 3 hadi miaka 3: toa miligramu 250, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Miaka 4 hadi 7: toa miligramu 375, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Miaka 8 hadi 12: toa miligramu 500, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Zaidi ya miaka 12: toa miligramu 500 hadi 875, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.