Hesperian Health Guides

Vitamini na madini ya nyongeza (mineral supplements)

Lishe bora hutengeneza afya bora: Madawa

Vitamini mchanganyiko (multi-vitamins)


Chakula chenye virutubishi ndiyo chanzo bora zaidi cha vitamini. Lakini katika hali ambapo hakuna chakula cha kutosha au wakati wa ujauzito mwanamke anapokuwa na mahitaji makubwa zaidi ya lishe, mchanganyiko wa vitamini mbalimbali unapaswa kutumika.

Vitamini na madini ya nyongeza huwa katika miundo mbalimbali, lakini vidonge ndiyo muundo wenye gharama nafuu zaidi. Sindano za mchanganyiko wa vitamini mbalimbali hazina ulazima, ni kupoteza fedha bure, na zinaweza kusababisha maumivu na maambukizi ambayo yanaweza kuepukwa. Dawa za kuchangamsha mwili (tonics) na dawa zinazodaiwa kutibu magonjwa mengi (elixirs) mara nyingi hazijumuishi vitamini ambazo zinahitajika zaidi. Dawa hizi pia ni ghali sana ukilinganisha na manufaa yake madogo.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpillspoon.png

Vidonge vingi vya vitamini mchanganyiko hutumiwa kwa kidonge 1 kwa siku. Lakini soma maelekezo kwenye dawa kabla haujaanza kutumia.

Vitamini A, retino (retinol)


Kuzuia uoni hafifu wa usiku na zerofthalmia
Katika maeneo ambapo matatizo ya uoni hafifu usiku na zerofthalmia (kukauka na kuongezeka ukubwa wa konea) yameenea sana, watu wanahitaji zaidi matunda ya njano na mbogamboga za kijani, pamoja na vyakula kutokana na wanyama kama vile mayai na maini. Kwa kuwa vyakula hivyo mara nyingi havipatikani – angalau kwa muda mfupi–ni bora kuwapatia watoto na mama zao matone ya vitamini A kila baada ya miezi 6.

MuhimuNBgrnimportant.png

Kawaida huwezi kupata Vitamini A inayozidi kiwango ambacho mwili unahitaji kutokana na chakula. Lakini kuzidisha vidonge vya vitamini au mafuta ni hatari. Usitumie zaidi ya kiwango ambacho kimependekezwa.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill-drop.png

Kwa watoto wadogo, unaweza kusaga vidonge na kuchanganya unga na maziwa ya mama kidogo. Au kata kidonge cha kapsuli na kukamulia majimaji yaliyomo mdomoni mwa mtoto.

Kuzuia upungufu wa vitamini A mwilini
Miezi 6 hadi mwaka 1: toa uniti 100,000 kwa njia ya mdomo mara moja.
Zaidi ya mwaka 1: toa uniti 200,000 kwa mdomo mara moja. Rudia baada ya miezi 6.
Kwa akina mama: toa uniti 200,000 kwa mdomo ndani ya wiki 6 baada ya kujifungua. Vitamini A itamkinga mama na pia kumfikia mtoto kupitia maziwa ya mama.

Kwa watoto wenye surua
Vitamini A huzuia nimonia na upofu, matatizo 2 ya kawaida yanayohusiana na surua.
Miezi 6 hadi mwaka 1: toa uniti 100,000 kwa njia ya mdomo, mara 1 kila siku kwa siku 2.
Zaidi ya mwaka 1: toa uniti 200,000 kwa njia ya mdomo, mara 1 kila siku kwa siku 2.

(Kama mtoto alipata dozi ya vitamini A katika miezi 6 iliyopita, mpe dozi hii kwa siku 1 tu.)

Iwapo mlengwa ana hali mbaya sana ya lishe au tayari ameanza kupoteza uwezo wake wa kuona, rudia dozi ya vitamini A baada ya wiki 2.

Vitamini B6, piridokisini (pyridoxine)


Watu wanaougua kifua kikuu ambao wanatibiwa kwa kutumia dawa ya isoniazid (INH) wakati mwingine hupungukiwa vitamini B. Dalili za kupungukiwa na vitamini B ni pamoja na: maumivu au hisia ya kutekenywa mikononi au miguuni, mshtuko wa misuli(muscle twitching), na matatizo katika kupata usingizi.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png

Mpe mtu anayetumia isoniazid vitamini B kila siku.

Kuzuia upungufu wa vitamini B6
Watoto wachanga na watoto wadogo: mpe miligramu 10 kila siku.
Watoto wakubwa zaidi na watu wazima: mpe miligramu 25 kila siku.

Kutibu upungufu wa vitamini B6
Watoto wachanga hadi miezi 2: mpe miligramu 10 mara 1 kwa siku, kutegemea kuendelea kuwepo kwa dalili za upungufu huo.

Watoto zaidi ya meizi 2: mpe miligramu10 hadi 20, mara 3 kila siku kutegemea kuendelea kuwepo kwa dalili za upungufu huo.
Mtu mzima: mpe miligramu 50, mara 3 kila siku kutegemea kuendelea kuwepo kwa dalili za upungufu huo.

Madini joto


Chumvi ambayo imeongezewa madini joto, na vyakula vya baharini ndiyo vyanzo bora zaidi vya madini joto. Mahali ambapo bidhaa hizi hazipatikani, na kukiwa na goita au hali ya kuwepo mapungufu ya ukuaji wa kijinsia na dalili zingine ambazo hutokana na ukosefu wa madini joto mwilini, unaweza kutoa madini joto ya nyongeza.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill-drop.png
Watoto wachanga hadi mwaka 1: mpe miligramu 100 mara 1 kwa mwaka. Kama una kapsuli ya miligramu 200, fungua kwa kukata, halafu kamulia vilivyomo kwenye kikombe kidogo, na kufanya uwezavyo kumlisha mtoto angalau ½ ya kimiminika hicho. Siyo rahisi kupima nusu yake, lakini usimpe mtoto mchanga kimiminika chote kilichomo kwenye kikombe.
Mwaka 1 hadi 5: mpe miligramu 200 mara 1 kwa mwaka.
Miaka 6 hadi mtu mzima: mpe miligramu 400 mara 1 kwa mwaka.
Kwa mwanamke mjamzito, kumkinga dhidi ya goita, na mtoto wake dhidi ya mapungufu ya kuzaliwa mbalimbali: mpe miligramu 400 mara 1 wakati wa uja uzito. Kumpa dozi hiyo mapema kabisa anapopata ujauzito ndiyo njia bora zaidi, lakini wakati wowote pia unafaa.
Kwa kutumia mafuta ambayo yameongezewa madini joto:
1 hadi 5: mpe mililita 0.5(miligramu 250) mara 1 kwa mwaka.
Miaka 6 hadi mtu mzima: mpe mililita 0.5 hadi 1 (miligramu 480) mara 1 kwa mwaka.
Wanawake waja wazito: mpe mililita 1 (miligramu 480) mara 1 mapema iwezekanavyo wakati wa ujauzito. Rudia mwaka 1 baada ya kujifungua.

Madini chuma, ferasi salfeti, ferasi glukoneti (iron, ferrous sulfate, ferrous gluconate)


Madini chuma ya nyongeza husaidia katika kutibu au kuzuia matukio mengi ya upungufu wa wekundu wa damu mwilini. Matibabu kwa kutumia madini chuma kawaida huchukua angalau miezi 3.

Madini chuma ya nyongeza hufanya kazi vizuri yanapotumika pamoja na vitamini C (aidha kwa kula matunda na mbogamboga, au kutumia kidonge cha vitamini C).

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Madini chuma ya nyongeza wakati mwingine huvuruga tumbo na ni bora kutumiwa na chakula. Vilevile, yanaweza kusababisha kupata choo kwa shida hasa kwa watu wazima, na kufanya kinyesi kuonekana cheusi.

Kunywa madini chuma ya nyongeza yenye muundo wa kimiminika huyafanya meno kuonekana meusi. Kunywa kwa kutumia mrija au piga meno mswaki baada ya kunywa.

MuhimuNBgrnimportant.png

Hakikisha dozi ni sahihi. Ukizidisha hugeuka sumu. Usitoe madini chuma ya nyongeza kwa watu walioathirika sana kilishe. Subiri hadi afya zao zirudi ndipo uwape madini ya chuma.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpillspoon.png

Miundo tofauti ya madini chuma ya nyongeza huwa na ujazo tofauti. Kwa mfano, kidonge cha ferasi salfeti chenye miligramu 300 huwa na miligramu 60 za madini chuma. Lakini kidonge cha ferasi glukoneti chenye miligramu 325 huwa na miligramu 36 za madini chuma. Hivyo, soma maelekezo kwenye kifungashio cha vidonge vyako, chupa ya dawa (au karatasi ya taarifa juu ya dawa), au taarifa juu ya madini chuma ya nyongeza mengine kujua kiwango cha madini chuma kilichomo.

KUZUIA upungufu wa wekundu wa damu(anemia) miongoni mwa akina mama wajawazito na wanaonyonyesha
Toa ferasi salfeti miligramu 300 (miligramu 60 za madini ya chuma) kila siku. Inapaswa kutumiwa kila siku na wanawake ambao wanapanga kupata mimba. Kuunganisha madini chuma ya nyongeza na asidi ya foliki (folic acid) ya nyongeza ni bora zaidi kwa sababu asidi ya foliki husaidia kuzuia hitilafu katika uzazi.
Kumtibu mtu yeyote mwenye upungufu wa wekundu wa damu (anemia):
Toa ferasi salfeti mara 1 kwa siku, au gawa katika dozi 2 iwapo kuna hofu kwamba itavuruga tumbo.
DOZI YA FERASI SALFETI KWA UMRI
KUNDI LAUMRI KIASI GANI KATIKA KILA DOZI VIDONGE VYA MILIGRAMU 300 VINGAPI JUMLA YA MADINI YA CHUMA
Chini ya miaka 2 Miligramu 125 za ferasi salfeti Tumia sairapu ya madini ya chuma, au saga ¼ kidonge cha ferasi salfeti chenye miligramu 300 kwenye maziwa ya mama Toa kiasi cha kutosha kutoa miligramu 25 za madini ya chuma
Miaka 2 hadi 12 Miligramu 300 za ferasi salfeti Kidonge 1 cha ferasi salfeti chenye miligramu 300 Toa kiasi cha kutosha kutoa miligramu 60 za madini ya chuma
Zaidi ya miaka 12 hadi mtu mzima Miligramu 600 za ferasi salfeti Vidonge 2 vya ferasi salfeti vyenye miligramu 300 Toa kiasi cha kutosha kutoa miligramu 120 za madini ya chuma

Zinki (zinc)


Madini ya zinki husaidia mtu anayeharisha kupata nafuu haraka. Madini hayo yanapaswa kutolewa pamoja na kinywaji cha kuongeza maji mwilini.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png
Kwa watoto, vidonge vinaweza kusagwa na kuchanganywa na maziwa ya mama au na maji kidogo. Pia unaweza kupata aina ya kidonge ambacho humomonyoka haraka na kuchanganyika kwa urahisi kwenye kimiminika.
Watoto wachanga hadi miezi 6: toa miligramu 10, mara 1 kila siku kwa siku 10 hadi 14.
Zaidi ya miezi 6: toa miligramu 20, mara 1 kila siku kwa siku 10 hadi 14.