Hesperian Health Guides

Antibiotiki (viuavijasumu)

Maumivu tumboni, kuhara, na minyoo: Madawa

Antibiotiki ni dawa za kupambana na maambukizi kutokana na bakteria. Hazisaidii dhidi ya maambukizi ya virusi kama vile tetekuwanga, surua ya rubella, mafua, au homa ya kawaida. Siyo kila antibiotiki inaweza kupambana na maambukizi ya bakteria. Dawa za antibiotiki zenye muundo wa kemikali unaofanana huchukuliwa kuwa katika familia moja. Ni muhimu kuwa na ufahamu juu ya familia za antibiotiki kwa sababu kuu 2:

  1. Dawa za antibiotiki kutoka katika familia moja mara nyingi hutibu matatizo yanayofanana.
  2. Kama una mzio kutokana na dawa moja ya antibiotiki kutoka katika familia moja, utapata mzio pia kutokana na dawa za antibiotiki zingine kutoka familia hiyo. Hii inamaanisha kwamba unatakiwa kutumia dawa kutoka katika familia nyingine ya antibiotiki.

Dawa ya antibiotiki lazima itumike “kwa dozi kamilifu.” Kukatisha dozi bila kukamilisha siku zote za matibabu, hata kama utakuwa umepata nafuu, kunaweza kusababisha maambukizi kurudia katika muundo ambao utakuwa mgumu zaidi kutibika.

Ampisilini na amoksilini


Ampisilini na amoksilini ni familia ya penisilini yenye tiba pana, maana yake ni kwamba huua aina nyingi za bakteria kuliko dawa zingine katika kundi hili la penisilini. Dawa hizi 2 mara nyingi ni mbadala wa nyingine. Pale ambapo ampisilini imependekezwa katika kitabu hiki, amoksilini inaweza kutumika katika nafasi yake kwa kuzingatia dozi sahihi.

Ampisilini na amoksilini ni dawa salama sana na ni msaada mkubwa kwa watoto wachanga na watoto wadogo. Inapotolewa pamoja na dawa zingine, ampisilini ni tiba muhimu kwa vidonda vya tumbo na kwa ajili ya maambukizi ya ngozi ya fumbatio(peritonitisi).

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Dawa hizi 2, lakini hasa ampisilini, huwa na tabia ya kusababisha kichefuchefu na kuharisha. Epuka kutoa dawa hizi kwa watoto ambao tayari wanaharisha - kama unaweza wapatie dawa aina nyingine ya antibiotiki.

Madhara mengine ya kawaida ya pembeni ni upele. Uvimbevimbe, mithili ya malengelenge, unaowowasha ambao huja na kutoweka ndani ya saa chache huenda ni dalili ya mzio kutokana na penisilini. Simamisha utoaji wa dawa hiyo mara moja na usimpe mtoto huyu penisilini tena. Matukio ya usoni yanaweza kuwa mabaya zaidi na hata kutishia maisha. Kwa baadhi ya matatizo, erithiromaisini inaweza kutumika. Upele ulioenea tambarare ukifanana kama wa surua, na kawaida kuanza wiki moja baada ya kuanza kutumia dawa na ambao huchukua siku kadhaa kutoweka, mara nyingi siyo dalili ya mzio. Lakini haiwezekani kujua kwa uhakika iwapo upele huo unatokana na mzio au la, hivyo ni bora kusimamisha dawa.

MuhimuNBgrnimportant.png

Usugu dhidi ya dawa hizi unazidi kuenea. Kutegemea na mahali unapoishi, dawa hizi zinaweza kutofanya kazi tena dhidi ya stafilokokasi(staphylococcus -aina ya bakteria wanaosababisha uvimbe unaotunga usaha, shigella, na maambukizi mengine.

Jinsi ya kutumiaNBgrninjectpill.png

Ifuatayo ni orodha ya dozi za amoksilini kwa njia ya mdomo, na ampisilini kwa njia ya sindano. Kila inapowezekana toa amoksilini kwa njia ya mdomo. Tumia ampisilini kwa njia ya sindano kwa magonjwa makali, au pale ambapo mtu anatapika au hawezi kumeza.

Kama ilivyo kwa dawa za antibiotiki zingine, muda wa kuendelea kutoa dawa hizo hutofautiana kutokana na sababu mbalimbali. Lakini kanuni ya msingi ni kuendelea kutoa dawa hadi dalili zote za maambukizi(ikiwemo homa) zitakapokuwa zimetoweka angalau kwa saa 24. Kwa watu wenye VVU, toa dawa kwa ajili ya siku zote zilizoorodheshwa. Vilevile, kuna kiwango kwa ajili ya kiasi cha dawa ambacho kinapaswa kutolewa. Kwa ujumla, toa kiasi cha chini kwa mtu mwembamba au kwa maambukizi yasiyo makali sana, na kiasi cha juu kwa mtu mwenye mwili mkubwa zaidi au dhidi ya maambukizi makali sana.

AMOKSILINI (MATUMIZI KWA NJIA YA MDOMONI)
Kwa maambukizi mengi miongoni mwa watoto
Toa miligramu 45 hadi 50 kwa kila kilo kwa siku, ikigawanywa katika dozi 2 kwa siku. Kama huwezi kumpima mtoto, mpe dozi kulingana na umri:
Chini ya miezi 3: toa miligramu 125, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Miezi 3 hadi miaka 3: toa miligramu 250, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Miaka 4 hadi 7: toa miligramu 375, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Miaka 8 hadi 12: toa miligramu 500, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Zaidi ya miaka 12: toa miligramu 500 hadi 875, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.

Endelea kumpa amoksilini hadi angalau saa 24 baada ya dalili zote kutoweka.

AMPISILINI (KWA NJIA YA MDOMO)
Toa miligramu 50 hadi 100 kwa kila kilo kwa siku, ikigawanywa katika dozi 4 kwa siku. Kama huwezi kumpima mtoto, mpe dozi kulingana na umri:
Chini ya mwaka 1: toa miligramu 100, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Mwaka 1 hadi 3: toa miligramu 125, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Miaka 4 hadi 7: toa miligramu 250, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Miaka 8 hadi 12: toa miligramu 375, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Zaidi ya miaka 12: toa miligramu 500, mara 4 kila siku kwa siku 7.

Endelea kumpa ampisilini hadi angalau saa 24 baada ya dalili zote kutoweka.

AMPISILINI (KWA NJIA YA SINDANO)
Ampisilini inaweza pia kutolewa kwa njia ya sindano, lakini kwa magonjwa makali tu, au mahali ambapo mtu anatapika na hawezi kumeza.
Choma miligramu 100 hadi 200 kwa kilo, zikigawanywa katika dozi 4 kila siku. Kama huwezi kumpima mtu, mpe dozi kwa kuzingatia umri wake:
Chini ya mwaka 1: choma miligramu 100, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Mwaka 1 hadi 5: choma miligramu 300, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Miaka 6 hadi 12: choma miligramu 625, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Zaidi ya miaka 12: choma miligramu 875, mara 4 kila siku kwa siku 7.

Erithromaisini (erythromycin)


Erithromaisini hufanya kazi dhidi ya maambukizi mengi yanayotibiwa na dawa zilizomo katika kundi la penisilini au tetrasaikilini, na inaweza kutumika kwa watu wanaopatwa na mzio kutokana na penisilini.

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Erithromaisini mara nyingi husababisha kichefuchefu na kuharisha, hasa miongoni mwa watoto. Usitumie kwa zaidi ya wiki 2 kwani inaweza kusababisha ugonjwa wa manjano.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png
Toa miligramu 30 hadi 50 kwa kilo, ikiwa imegawanywa katika dozi 2 hadi 4 kila siku. Toa kwa siku 7 hadi 10 au hadi saa 24 baada ya dalili zote kutoweka.
Watoto wachanga: toa miligramu 65, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Chini ya miaka 2: toa miligramu 125, mara 3 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Miaka 2 hadi 8: toa miligramu 250, mara 3 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Zaidi ya miaka 8: toa miligramu 250 hadi 500, mara 4 kila siku kwa siku 7 hadi 10.

Kwa maambukizi makali, zidisha dozi iliyoelezewa juu mara 2.

Kwa ajili ya kipindupindu( katika maeneo ambapo dawa hii bado ina uwezo dhidi ya kipindupindu): (where erythromycin works for cholera)

Toa dozi zilizoorodheshwa juu, lakini kwa siku 3.

Tetrasaikilini na doksisaikilini (doxycycline)


Tetrasaikilini na doksisaikilini ni antibiotiki zenye tiba pana ambazo hupambana na aina nyingi za bakteria. Hufanya kazi vizuri zinapotumika kwa njia ya mdomo( na zinauma sana zinapotolewa kwa njia ya sindano). Hivyo, hazipaswi kutolewa kwa njia ya sindano. Kuna usugu mkubwa dhidi ya dawa hizi, lakini bado ni muhimu sana katika kupambana na maambukizi.

Doksisaikilini na tetrasaikilini zinaweza kutumika kama dawa mbadala. Lakini doksisaikilini kawaida ni bora zaidi kwa sababu kiasi kidogo huhitajika kila siku na madhara yake ya pembeni ni machache.

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Kiungulia, tumbo kusokota, kuhara, na maambukizi ya kuvu ni kawaida.

MuhimuNBgrnimportant.png
  • Wanawake wajawazito hawapaswi kutumia dawa hizi, kwa sababu zinaweza kuathiri au kusababisha madoa kwenye meno ya mtoto na mifupa. Kwa sababu hiyo hiyo, watoto chini ya miaka 8 wanaweza kuitumia kama hakuna dawa nyingine bora, na kwa vipindi vifupi tu. Wanaweza kutumia erithiromaisini.
  • Usitumie tetrasaikilini au doksisaikilini ambayo muda wake wa matumizi umepita.
  • Baadhi ya watu wakikaa juani wanaweza kubabuka ngozi haraka au kutokwa na upele wanapokuwa wanatumia dozi ya dawa hizi. Hivyo, kaa mbali na jua au vaa kofia pana.
  • Dawa hizi zinaweza kuingiliana na vidonge vya majira na hivyo kupunguza ufanisi wa vidonge vya majira. Kama inawezekana tumia njia nyingine ya kupanga uzazi (kama vile kondomu) utakapokuwa unatumia dawa hizi.
Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png

TETRASAIKILINI
Epuka maziwa, vidonge vya madini chuma, na dawa za kupambana na asidi tumboni angalau kwa saa 2 kabla ya kutumia tetrasaikilini. Vitu hivi vitaathiri utendaji wa dawa hii. Tumia tetrasaikilini kabla hujala, pamoja maji mengi angalau saa 1 kabla au saa 2 baada ya mlo.

Kwa maambukizi mengi:
Toa miligramu 25 hadi 50 kwa kila kilo kila siku, ikigawanywa katika dozi 4 kwa siku. Au toa dozi kulingana na umri:
Miaka 8 hadi 12: toa miligramu 125, mara 4 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Zaidi ya miaka 12: toa miligramu 250, mara 4 kila siku kwa siku 7 hadi 10.

Kwa ajili ya kipindupindu (sehemu ambazo tetrasaikilini bado ina uwezo juu ya kipindupindu)
Miaka 8 hadi 12: toa miligramu 250, mara 4 kila siku kwa siku 3.
Zaidi ya miaka12: toa miligramu 500, mara 4 kila siku kwa siku 3.

DOKSISAIKILINI (DOXYCYCLINE)
Epuka maziwa, vidonge vya madini chuma, na dawa za kupambana na asidi tumboni angalau kwa saa 2 kabla ya kutumia doksisaikilini. Vitu hivi vitaathiri utendaji wa dawa hii. Tumia doksisaikilini kabla hujalapamoja maji mengi angalau saa 1 kabla au saa 2 baada ya mlo.

Doksisaikilini hutumika mara 1au 2 kila siku badala ya mara 4 kila siku kama ilivyo kwa tetrasaikilini. Kwa maaambukizi makali, toa mara 2 kila siku. Lakini kwa ajili ya maambukizi mengi, toa dozi ya kwanza ya doksisaikilini, halafu baada ya saa 12 toa dozi ya pili. Baada ya hapo, toa dozi mara 2 kwa wakati moja kila siku. Kwa mfano, kama utatoa dozi ya kwanza jumatatu usiku, basi toa dozi ya pili jumanne asubuhi. Toa dozi mara 2 wakati moja jumatano asubuhi, na tena alhamisi asubuhi, na kuendelea.

Toa miligramu 2 kwa ajili ya kila kilo kwenye dozi, lakini usitoe zaidi ya miligramu 100 katika kila dozi au zaidi ya miligramu 200 kwa siku. Au toa dozi kulingana na umri:
Miaka 8 hadi 12: toa miligramu 50 kila dozi, kwa siku 7 hadi 10.
Zaidi ya miaka 12: toa miligramu100, kila dozi kwa siku 7 hadi 10.
Kwa ajili ya kipindupindu (sehemu ambazo doksisaikilini bado ina uwezo juu ya kipindupindu):
Toa miligramu 6 kwa kilo, mara moja tu. Au toa dozi kulingana na umri:
Miaka 8 hadi 12: toa miligramu 150, mara moja tu.
Zaidi ya miaka 12: toa miligramu 300, mara moja tu.

Metronidazo (metronidazole)


Metronidazo hutumika kutibu maambukizi tumboni ambayo yamesababishwa na ameba, giardia, baadhi ya bakteria.

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Kichefuchefu, tumbo kusokota, na kuhara ni kawaida. Matumizi ya dawa hii pamoja na chakula kunaweza kusaidia. Wakati mwingine husababisha ladha ya chuma mdomoni na hata maumivu ya kichwa.

MuhimuNBgrnimportant.png

Usitoe wakati wa miezi 3 ya kwanza ya ujauzito. Inaweza kusababisha madhara kwa mtoto aliye tumboni. Pia epuka kutoa metronidazo baadaye katika ujauzito, na wakati wa unyonyeshaji isipokuwa tu kama ni dawa pekee yenye uwezo iliyopo na inahitajika hasa. Usinywe pombe wakati unapokuwa unatumia metronidazo — na kwa siku 2 baada ya kumaliza dozi. Unywaji pombe wakati wa dozi ya metronidazo husababisha Kichefuchefu. Usitumie metronidazo kama una matatizo ya ini.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png

Kwa matatizo mengi, unaweza kutoa dozi kubwa ya dawa hii kwa siku 3, au dozi ya chini kwa siku 5 hadi 10. Wanawake wajawazito wanapaswa kuepuka matibabu kwa kutumia dozi kubwa.

Tiba kwa ajili ya giardia
Toa miligramu 15 kwa ajili ya kila kilo ya uzito kila siku, ikigawanywa katika dozi 2 hadi 3 kila siku, kwa siku 5 hadi 7. Au toa dozi kulingana na umri:

Chini ya miaka 3: toa miligramu 62 (¼ ya kidonge cha miligramu 250), mara 2 kila siku kwa siku 5.
Miaka 3 hadi 7: toa miligramu 62, mara 3 kila siku kwa siku 5.
Miaka 8 hadi 12: toa miligramu 125, mara 3 kila siku kwa siku 5 hadi 7.
Zaidi ya miaka 12: toa miligramu 250, mara 3 kila siku kwa siku 5 hadi 7.
AU toa gramu 2, mara moja kila siku kwa siku 3.

Kwa ajili ya kuhara damu kutokana na ameba
Tumia miligramu 30 kwa kila kilo ya uzito kila siku, ikigawanywa katika dozi 3 kila siku, kwa siku 8 hadi 10. Au toa dozi kulingana na umri:
Chini ya miaka 3: toa miligramu 62 (¼ kidonge cha miligramu 250), mara 3 kila siku kwa siku 8 hadi 10.
Miaka 3 hadi 7: toa miligramu 125, mara 3 kila siku kwa siku 8 hadi 10.
Miaka 8 hadi 12: toa miligramu 250, mara 3 kila siku kwa siku 8 hadi 10.
Zaidi ya miaka 12: toa miligramu 500 hadi 750, mara 3 kila siku kwa siku 8 hadi 10.

Baada ya dozi ya mwisho ya metronidazo, tumia diloxanide furoate.

Kwa ajili ya kutibu kidole tumbo au maambukizi ya ngozi ya fumbatio (peritonitis)
Mpe, pamoja na antibiotiki nyingine. Bonyeza hapa.
Kwa ajili ya vidonda vya tumbo

Sipro (Ciprofloxacin)


Sipro ni antibiotiki yenye tiba pana kutoka kundi la quinolone. Hufanya kazi dhidi ya maambukizi mengi tofauti ya ngozi, mifupa, njia ya chakula na njia ya mkojo. Lakini kuna usugu dhidi ya sipro katika sehemu nyingi za dunia. Hivyo, tumia tu dhidi ya maambukizi ambayo yamependekezwa katika eneo lako. Siyo dawa nzuri kwa watoto.

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Kichefuchefu, kuhara, kutapika, maumivu ya kichwa, kizunguzungu, upele, au maambukizi ya fangasi.

MuhimuNBgrnimportant.png

Usitumie dawa hii iwapo ni mjamzito au unanyonyesha. Usitumie pamoja na bidhaa za maziwa.
Kwa nadra, sipro huathiri tishu zinazounga misuli kwenye mifupa. Isipokuwa katika matukio maalum machache, haipaswi kutolewa kwa watoto chini ya miaka 16 kwa sababu tishu zao hizo bado zinakua. Kama utapata maumivu kwenye misuli ya miguu nyuma ya miuundi unapokuwa unatumia dawa hii, acha kutumia mara moja.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png
Kwa ajili ya maambukizi mengi
Toa miligramu 250 hadi 750, mara 2 kila siku hadi angalau saa 24 baada ya dalili zote kutoweka.
Kwa ajili ya kutibu shigella
Toa miligramu 500, mara 2 kila siku kwa siku 3.
Kwa ajili ya kutibu kipindupindu (katika maeneo ambapo sipro ina uwezo dhidi ya kipindupindu).
Toa gramu 1 (miligramu 1000 ), mara moja tu.
Kwa matibabu ya kidole tumbo au maambukizi ya ngozi ya fumbatio (peritonitis)

Seftriaksoni (ceftriaxone)


Seftriaksoni ni antibiotiki yenye nguvu ambayo hutumika dhidi ya maambukizi makali na maambukizi yenye usugu kwa dawa ya penisilini. Tumia seftriaksoni tu kutibu maambukizi mahsusi ambayo yamependekezwa katika eneo lako. Hii itasaidia kuzuia usugu na kuiwezesha dawa hii kuendelea kutumika.

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Hutoa maumivu wakati inachomwa. Changanya na 1% ya lidocaine kama unajua jinsi ya kuichanganya.

MuhimuNBgrnimportant.png

Usitumie kwa mtoto mchanga chini ya wiki 1. Usitumie pia kama kuna homa ya manjano.

Jinsi ya kutumiaNBgrninject.png

Seftriaksoni haiwezi kutumika kwa njia ya mdomo. Wakati wa kuchoma, hakikisha sindano inaingia ndani sana ya msuli.

Kwa ajili ya maambukizi makali
Dozi hutofautiana kutegemea na maambukizi, lakini kwa ujumla unaweza kutoa miligramu 50 hadi 100 kwa kila kilo ya uzito miongoni mwa watoto, na gramu1 hadi 4 miongoni mwa watu wazima, mara 1 au 2 kwa siku.

Kutibu shigella
Choma miligramu 50 kwa kila kilo ya uzito, mara 1 kila siku kwa siku 5. Au kama huwezi kumpima mgonjwa, toa dozi kulingana na umri:
Wiki 1 hadi miaka 3: choma miligramu 250, mara moja kila siku kwa siku 5.
Miaka 3 hadi 7: choma miligramu 500, mara moja kila siku kwa siku 5.
Miaka 8 hadi 12: choma miligramu 1000, mara moja kila siku kwa siku 5.
Zaidi ya miaka 12: choma gramu 1 hadi 2, mara moja kila siku kwa siku 5.