Hesperian Health Guides

Dawa za minyoo

Maumivu tumboni, kuhara, na minyoo: Madawa

Dawa tu hazitoshi kuondoa minyoo mwilini au kudhibiti maambukizi yake kwa muda mrefu. Usafi wa mtu binafsi na jamii kwa ujumla pia unahitajika. Maambukizi ya minyoo yanaweza kuenea kwa urahisi miongoni mwa wanafamilia. Hivyo mwanafamilia 1 anapokuwa na minyoo, ni muhimu kutibu familia nzima.

Mebendazo (Mebendazole)


Mebendazo hufanya kazi dhidi ya safura, askarisi, mchangokiboko (trichuris au whipworm), mchangouzi (pinworm au threadworm), na aina nyingine ya mchango. Pia husaidia dhidi ya trikinosisi (trichinosis) lakini siyo sana. Ingawa kawaida haina madhara ya pembeni, mara chache huenda kukawa na maumivu tumboni au kuharisha iwapo mgonjwa ana minyoo mingi mwilini.

MuhimuNBgrnimportant.png

Epuka mebendazo wakati wa miezi 3 ya kwanza ya ujauzito kwa sababu inaweza kumuathiri mtoto aliyeko tumboni. Usitoe kwa mtoto mwenye umri chini ya mwaka 1.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png
Kwa ajili ya mchangouzi (pinworm au threadworm)
Mwaka 1 hadi mtu mzima: toa miligramu 100, mara 1 kwa njia ya mdomo. Rudia ndani ya wiki 2 kama inahitajika.
Kwa ajili ya askarisi, trikurisi (whipworm au trichuris) na safura
Mwaka 1 hadi mtu mzima: toa miligramu 100, mara 2 kila siku kwa siku 3 (jumla ya vidonge 6). AU
toa kidonge 1 cha miligramu 500, mara 1 tu.
Kuzuia askarisi (roundworm) mahali ambapo imeenea
Mwaka 1 hadi mtu mzima: toa miligramu 500, kila miezi 4 hadi 6.
Kwa ajili ya trikinosisi (trichinosis)
Mwaka 1 hadi mtu mzima: toa miligramu 200 hadi 400, mara 3 kila siku, kwa siku 3. Halafu toa miligramu 400 hadi 500, mara 3 kila siku kwa siku zingine 10. Kama kutakuwa na maumivu au hata matatizo ya kuona, pia toa dawa kutoka kundi la steroidi kama vile prednisoloni (prednisolone), miligramu 40 hadi 60, mara 1 kila siku kwa siku 10 hadi 15.

Albendazo (Albendazole)


Albendazo inafanana na mebendazo, lakini huwa ni ghali zaidi. Hufanya kazi dhidi ya safura, askarisi, trikinosisi, mchangokiboko (whipworm), mchangouzi (pinworm au threadworm), na aina zingine za mchango. Madhara ya pembeni ni nadra sana.

MuhimuNBgrnimportant.png

Epuka albendazo katika miezi 3 ya kwanza ya ujauzito kwani inaweza kumuathiri mtoto aliyeko tumboni. Usitoe kwa watoto chini ya mwaka 1.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png
Kwa ajili ya mchangouzi, askarisi, mchangokiboko (trichuris au whipworm), na safura.
Mwaka 1 hadi 2: toa miligramu 200, mara 1.
Zaidi ya miaka 2: toa miligramu 400, mara 1. Rudia ndani ya wiki 2 kama itahitajika.
Kwa ajili ya trikinosisi (trichinosis)
Toa miligramu 400, mara 2 kila siku kwa siku 8 hadi 14. Kama kuna maumivu au matatizo katika kuona, pia toa dawa kutoka kundi la steroidi ama vile prednisoloni (prednisolone), miligramu 40 hadi 60, mara 1 kila siku 10 hadi 15.

Pamoti pirante (Pyrantel pamoate), Emboneti pirante (pyrantel embonate)


Pirante (pyrantel) hufanya kazi dhidi ya mchangouzi,safura, na askarisi, lakini inaweza kuwa ghali. Mara chache husababisha kutapika, kizunguzungu, au maumivu ya kichwa. Usitoe kwa mtu yeyote ambaye pia anatumia piperazini (piperazine) - dawa nyingine ya minyoo.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png
Kwa ajili ya safura na askarisi: toa dozi 1 tu.

Kwa ajili ya mchangouzi: toa dozi 1, subiri wiki 2, halafu toa dozi nyingine.
Toa miligramu 10 kwa kila kilo. Kama huwezi kumpima mtoto toa dozi kwa kuzingatia umri kama ifuatavyo:
Chini ya miaka 2: toa miligramu 62 (¼ ya kidonge cha miligramu 250).
Miaka 2 hadi 5: toa miligramu 125 (½ kidonge cha miligramu 250).
Miaka 6 hadi 9: toa miligramu 250 (kidonge 1 cha miligramu 250).
Miaka 10 hadi 14: toa miligramu 500 (vidonge 2 vya miligramu 250).
Zaidi ya miaka 14: toa miligramu 750 (vidonge 3 vya miligramu 250).

Kutibu mchangokamba (tapeworm)

Dawa ya Prazikante au niklosamaidi (niclosamide) hutibu aina yote ya minyoo katika kundi la chango. Kama maambukizi ya mchangokamba yatakuwa yameufikia ubongo na kusababisha mashambulio, mgonjwa atahitaji albendazo na dawa za kudhibiti mashambulio, na msaada wa haraka.

Prazikante (Praziquantel)


Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Prazikante (Praziquantel) inaweza kusababisha uchovu, kizunguzungu, maumivu ya kichwa, kukosa hamu ya kula, na kichefuchefu, lakini madhara haya ni nadra pale dozi ndogo inapotumika kutibu mchangokamba.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png
Kwa ajili ya aina nyingi ya michangokamba, ikiwemo inayotokana na nyama ya ng’ombe au nyama ya nguruwe:
Tumia miligramu 5 hadi 10 kwa kila kilo ya uzito, mara moja tu. Au toa dozi kulingana na umri:
Miaka 4 hadi 7: toa miligramu 150 (¼ kidonge), mara moja tu.
Miaka 8 hadi 12: toa miligramu 300, mara 1 tu.
Zaidi ya miaka 12: toa miligramu 600, mara 1 tu.

Kutibu mchangokamba fupi (H. nana)
Tumia miligramu 25 kwa kila kilo katika dozi 1. Halafu rudia siku 10. Au toa dozi kulingana na umri:
Miaka 4 hadi 7: toa miligramu 300 hadi 600 (½ kidonge hadi kidonge 1) kwa kila dozi.
Miaka 8 hadi 12: toa miligramu 600 hadi 1200 kwa akila dozi.
Zaidi ya miaka 12: toa miligramu 1500 kwa kila dozi.

Niklosamaidi (Niclosamide)


Dawa ya Niklosamaidi (Niclosamide) hutibu maambukizi ya mchangokamba kwenye utumbo, lakini siyo vifuko vyenye viluwiluwi vya minyoo hiyo nje ya utumbo.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png

Tumia niklosamaidi (niclosamide) baada ya kula mlo mdogo asubuhi. Vidonge vinapaswa kumumunywa vizuri na kumezwa. Dozi inaweza kutofautiana na aina ya mchangokamba. Hivyo, tafuta ushauri kutoka kituo cha afya eneo lako au kama hili haliwezekani tumia dozi ifuatayo:

Mumunya vizuri na kumeza dozi zifuatazo. Kama mtoto mdogo hawezi kumumunya, saga kidonge na kuchangaya na maziwa ya mama kidogo au chakula.

Chini ya miaka 2: toa miligramu 500, mara 1 tu.
Miaka 2 hadi 6: toa gramu 1 (miligramu 1000), mara 1 tu.
Zaidi ya miaka 6: toa gramu 2, mara 1 tu.