Hesperian Health Guides

Muwasho au maumivu kwenye njia ya haja kubwa

Katika sura hii:

Bawasiri

Bawasiri ni uvimbe wa mishipa ya damu kwenye njia ya haja kubwa. Huonekana kutuna au kujaa kama jipu karibu na unyeo. Inaweza kutoa muwasho, hisia ya kuungua, au maumivu; hasa wakati wa kujisaidia. Wakati mwingine bawasiri hupasuka na kutoa damu kidogo nyekundu inayong’aa kwenye kinyesi.

Bawasiri ni tatizo la kawaida wakati wa ujauzito na miongoni mwa watu wanaokaa au kubeba mizigo mikubwa kutwa nzima, lakini kila mtu anaweza kuupata. Maumivu kutokana na bawasiri huzidi zaidi mgonjwa anapokuwa na tatizo la choo kigumu, kwa sababu kukitoa choo kigumu hulazimisha mishipa kwenye njia ya haja kubwa kupanuka zaidi.

Matibabu
  • Epuka tatizo la ugumu wa choo na bawasiri kwa kujenga tabia ya kunywa maji mengi, kula matunda kwa wingi na nafaka nzimanzima ambazo hazijasindikwa.
  • Baadhi ya juisi kutokana na mimea chungu ikipakwa kwenye bawasiri husaidia uvimbe kunywea.
  • Kaa kwenye benseni au bafu yenye maji vuguvugu kusafisha bawasiri na kupunguza maumivu.

Wakati mwingine bawasiri hujaa damu iliyoganda. Utahisi kitu kigumu kinachobonyea ndani na mshipa uliovimba. Uvimbe huu unaweza kutoa maumivu makali sana kiasi cha kutomruhusu mtu kukaa. Punguza maumivu kwa kuondoa damu hiyo iliyoganda:

kutumia kibanio kuondoa damu iliyoganda
Kwanza, safisha unyeo kwa maji safi na sabuni . Kama inapatikana, choma sindano ya asilimia 1 lidocaine miligramu 5 chini ya bawasiri.
Tumia kifaa cha kukatia kilichotakaswa kukata au kutoboa sehemu ndogo kwenye uvimbe huo. Tumia kibanio kilichotakaswa kuitoa damu iliyoganda. Bana sehemu iliyokatwa au kutobolewa na kitambaa au pamba hadi damu itakaposimama.


Usikate na kuondoa bawasiri. Hii inaweza kusababisha kuvuja damu nyingi.

Jeraha wazi au michubuko kwenye unyeo

Muwasho, uchungu kama mwiba, au uvujaji damu kutoka kwenye unyeo unaweza kusababishwa na mchaniko mdogo wa ngozi. Hii kwa fikra ya haraka inaweza kudhaniwa kuwa bawasiri au minyoo. Mara nyingi mtu mzima mwenye muwasho kwenye unyeo huwa hana minyoo.

Michaniko hiyo kawaida husababishwa na kujifuta baada ya kujisaidia. Hali hiyo huzidishwa na kutosafisha unyeo vizuri baada ya kujisaidia.

  • Usifute unyeo kwa kutumia mabunzi, gazeti, au vifaa vingine visivyo laini.
  • Badala yake, tumia karatasi maalum ya kutawazia (toilet paper) au chombo cha maji kwa ajili ya kusafisha unyeo baada ya kujisaidia. Baada ya hapo, nawa mikono yako kwa maji safi na sabuni.


maalum ya kutawazia na chombo cha maji
  • Oga mara kwa mara, na kusafisha unyeo wakati wa kuoga.
  • Unaweza pia kujaribu krimu ya hydrocortisone, lakini usitumie kwa zaidi ya wiki au itaathiri ngozi


Maumivu kwenye njia ya haja kubwa

Wakati mwingine, watu hupatwa na uvimbe mwekundu na wenye maumivu pembeni na unyeo. Hujaa usaha na unakuwa aina ya jipu. Jipu linaweza kusababisha tundu kati ya unyeo na ngozi na unapaswa kukamuliwa mara moja. Toboa njia ya kutolea usaha karibu na unyeo, kadri iwezekanavyo. Angalia sura ya Ngozi, kucha, na matatizo ya nywele (inaandaliwa) kuhusu jinsi ya kukamua jibu.