Hesperian Health Guides
Utapiamlo
Katika maeneo yenye watoto wengi wenye utapiamlo, unaweza kufikiri kuwa mtoto mwenye utapiamlo ni mtoto wa kawaida. Lakini udongo wa kimo, udhaifu, hali ya kutochangamka, na magonjwa ya mara kwa mara siyo viashiria vya afya njema wala hali ya kawaida. |
Yaliyomo
Dalili
- kukua polepole na udogo wa kimo
- kukonda
- misuli kupotea-“kubaki mifupa”: mwili hutumia misuli kutengeneza nishati
- kasi ndogo ya kufikiri na kusinziasinzia, kwa sababu ubongo haupati nishati inayohitajika
- magonjwa na maambukizi mengi
- kuharisha mara kwa mara, na kudhoofika zaidi kilishe
Utapiamlo ni tatizo sugu ambalo limeenea sana. Hii inamaanisha kuwa watu wengi huathirika kutokana na njaa kwa muda mrefu. Hivyo hawakui kufikia kipimo chao cha urefu, huugua mara kwa mara, hukumbwa na kuharisha, anemia na matatizo mengine ya kiafya mara kwa mara.
Matibabu
Unaweza kuutibu utapiamlo hata kama huna rasilimali nyingi, kwa kumpatia mgonjwa vyakula vingi zaidi na vyenye ubora unaostahili kilishe.
Kwa watoto kuanzia umri kuzaliwa hadi miezi 6: wapatiwe maziwa ya mama tu kwa wingi na siyo kitu kingine. Chakula kingine chochote huzidisha matatizo kwa mtoto. Kadri mtoto anavyokua, endelea kumpatia maziwa ya mama, na ongezea vyakula vingine.
Kwa mtu yeyote mwenye dalili za utapiamlo: mpatie uji wenye nguvu joto kwa wingi. Anza kwa kutengeneza uji kwa kutumia chakula kikuu cha wanga kinachopatikana eneo lako na kuongeza kwenye uji huo vifuatavyo:
- Protini: Unga wa karanga zilizosagwa,siagi ya karanga au aina nyingine ya njugu au unga wa mahindi. Au maharagwe yaliopikwa, mayai, au samaki. Au maziwa, mtindi, au jibini. Chagua protini yoyote yenye gharama nafuu inayopatikana kwa urahisi ambayo unaweza kumudu.
- Nishati: Ongeza kijiko 1 cha mafuta na kijiko 1 cha sukari, asali, au kiungio kingine kitamu. Au ongeza tunda.
- Vitamini na madini: Kuanzia mbogamboga ambazo zimepikwa au matunda.
Kuna wakati ambapo hakuna chakula cha kutosha kumpatia mtoto lishe inayofaa yenye protini na mbogamboga kila siku. Pamoja na hayo, jitahidi kumpatia mtoto vyakula zaidi ya wanga. Akila wanga tu, mtoto atajisikia kushiba lakini ataendelea kuwa dhaifu na kuugua. Ongezea kijiko 1 cha mafuta. Kijiko cha mafuta hakifidii ukosefu wa protini na mbogamboga. Lakini angalau kwa muda mfupi huweza kumpatia mtoto nishati ambayo hawezi kuipata kutoka wanga tu.
Pima watoto wote kujua iwapo wana utapiamlo
Utapiamlo sugu miongoni mwa watoto mara nyingi hauonekani dhahiri. Kupima utapiamlo, pima uzito wa watoto mara kwa mara na kufuatilia maendeleo yao kwenye kadi ya kliniki ya watoto kama ile ya Chati ya safari kuelekea afya bora (Road to Health Chart). Kama huna mzani, njia mbadala ni kupima sehemu ya juu ya mkono wa mtoto. Mara nyingi kuna huduma za kliniki kwa ajili ya watoto. Huduma hii inaweza kuwa njia nzuri ya kumsaidia mapema mtoto, kabla utapiamlo haujafikia kiwango cha hatari.
Kumpima mtoto mkono, tengeneza kipimio chembamba cha karatasi, plastiki au kitambaa hadi sentimita 25.
Weka alama kwenye kipimio hicho sehemu ambazo zinaonesha mtoto anapokuwa amekonda sana, au ameongekeza vya kutosha mwili na msuli. Kwenye sentimita 0, andika “pima kuanzia hapa”, kwenye sentimita 11.5 andika “ amekonda sana”, na kwenye sentimita 12.5 andika “ anakua vizuri”. Au tumia rangi au alama ambazo zina mantiki zaidi kwako.
Tumia kipimio hicho kupima sehemu za juu za mikono ya watoto kati ya umri mwaka 1 na 5, kujua iwapo wanaongezeka uzito wa kutosha (vipimo vya mkono havisaidii sana watoto wanapokua na utapiamlo mkali, wanapokuwa wamevimba mikononi na sehemu zingine mwilini).
Kipimo cha mkono wa mtoto kinapokuwa chini ya sentimeta 11.5 (chini ya msitari wa “amekonda sana”), au anapoonekana kuwa nyuma katika “Chati ya safari ya kuelekea afya bora (The Road to Health Chart), au ana dalili za utapiamlo mkali ambazo zimeorodheshwa kwenye ukurasa ufuatao, atakuwa ameathirika sana kilishe kiasi kwamba utapiamlo umegeuka ugonjwa. Anahitaji tiba haraka na unaweza kusaidia kuokoa maisha yake kwa kumpatia chakula chenye kiwango kukubwa cha nguvu joto bonyeza hapa.
NJANO (yupo hatarini) Kama kipimo cha mkono wa mtoto kinaangukia hapa yupo hatarini kupata utapiamlo. Mpatie vyakula zaidi, fuatilia ukuaji wake, na mweke chini ya uangalizi wa karibu ili asipate utapiamlo. | Msitari wa "amekonda sana" | Angalizo: kipimio hiki kinaweza kuwa katika vipimo visivyosahihi kinapopakuliwa kutoka kwenye kompyuta, hivyo tumia rula kuhakikisha usahihi wa kipimio chako. |
Utapiamlo mkali (severe, acute malnutrition)
Utapiamlo mkali hutokea wakati wa vita, ukame, au maafa, hali ya upatikanaji wa chakula inapovurugika. Au unaweza kumpata mtu ambaye anapata lishe duni wakati wote, lakini jambo fulani likatokea na kupunguza zaidi chakula anachokula au kuongeza kiasi cha nguvu ambayo anahitaji. Kwa mfano, mtoto ambaye tayari ana njaa akifikia hatua ya ukuaji haraka na anahitaji nishati na nguvu zaidi. Au mtu mwenye lishe duni anapopata VVU, malaria, surua, au ugonjwa mwingine, na anahitaji chakula zaidi kwa ajili ya nguvu ya kupambana na maambukizi. Ghafla, kile chakula kidogo walichokua wanategemea kuishi hakiwatoshelezi tena.
Taarifa juu ya utapiamlo katika maelezo haya zimejikita hasa juu ya watoto kwa sababu wao ndiyo huathirika zaidi kutokana na tatizo hilo. Hupoteza uzito haraka zaidi na baada ya hapo hupoteza hamu ya kula. Wanahitaji msaada mkubwa zaidi kupona na kuendelea kuishi. Bila msaada, uharibifu unaosababishwa na utapiamlo unaweza kuwaathiri kwa maisha yao yote. Watu wazima pia huathirika kutokana na utapiamlo, na matibabu yao yanafanana na ya watoto.
Mtoto mwenye utapiamlo mkali anaweza kufanana kama kwenye kielelezo:
Nywele hupukutika kwa urahisi
Ngozi kavu, nyembamba — ngozi inaweza kuonekana imelegea
Aina hii ya utapiamlo huitwa unyafuzi (marasmus).
Misuli dhaifu ikiwa imekaukiana (wasting) sehemu za mikononi na miguuni
Amekonda sana na kuwa mdogo kwa kimo
Nywele kavu na nyembamba ambazo zinapoteza rangi yake na kugeuka nyekundu, njao au nyeupe
Ngozi iliopasuka pasuka ikijiondoa kama gamba
Tumbo lililovimba
Vidonda au mabaka meusi kwenye ngozi
Aina hii ya utapiamlo huitwa Kwashakoo.
Uvimbe kuzunguka macho au miguu au vifundo
Uzito wa mtoto unaweza kuwa wa kawaida-mtoto haonekani kuwa amekonda
Uchovu au kutokuwa tayari kutembeatembea
|
Wakati mwingine watoto huonesha dalili kutoka aina zote 2 za utapiamlo.
Watu wenye VVU, kifua kikuu, minyooo, au magonjwa mengine yanayochukua muda mrefu nao wanaweza kuwa na utapiamlo hata kama watakuwa wanakula kila siku. Kama mtoto au mtu mzima anakula chakula kingi lakini bado akaendelea kuonekana mwenye utapiamlo, huenda wakawa na ugonjwa hatari. Mbinu muhimu ya kulinda afya unapokua unaugua ugonjwa wa muda mrefu ni kupata lishe bora na ya kutosha. Lakini jaribu kuchunguza chanzo cha tatizo.
Ashika alikuwa na utapiamlo mkali alipoletwa kwenye kliniki. | Baada ya wiki kadhaa, lishe bora iliweza kumtibu. |
Picha hizi 2 zinaonesha mtoto mmoja wenye umri wa miaka 2 aitwaye Ashika. Alifikishwa kwenye Kituo cha Kukarabati Lishe, jijini Kathmandu, Nepali akiwa na utapiamlo mkali. Baada ya siku 26 ya matibabu kwa kutumia maziwa maalum yenye virutubishi vya nyongeza na lishe bora yenye mchanganyiko wa vyakula vya kawaida kadhaa, aliongezeka uzito unaofaa umri wake kiafya, na kurudi nyumbani na mama yake. Kituo cha Kukarabati Lishe siyo hospitali-ni jumba kubwa lenye vitanda vingi, bustani ya mbogamboga, na watumishi wenye huruma. Huwahudumia wastani watoto 20 kila mwezi wenye utapiamlo mkali kutokana na umasikini, na magonjwa mengine, na ukosefu wa uelewa juu ya lishe, pamoja na vita na njaa. Hujifunza juu ya lishe ili waweze kuwasaidia wanaporudi nyumbani. Vituo vya lishe kama hiki huokoa maisha ya idadi kubwa ya watoto wanaopelekwa kwenye kituo hicho.
Tiba ya utapiamlo mkali
Mtoto mwenye utapiamlo mkali (Kwashakoo na unyafuzi) anahitaji msaada wa kiafya mara moja. Kama kuna kituo cha kukarabati lishe katika eneo lako, mpeleke mtoto huko, au unaweza kutoa huduma hii wewe mwenyewe. Mpe:
- chakula.
- vinywaji (kuongeza maji mwilini).
- joto (vuguvugu), hasa usiku.
- dawa.
Chakula
Mpatie vyakula vilivyoimarishwa ili apate nguvu na virutubishi. Uji wa kawaida peke hautoshi.
Unaweza kutengeneza mwenyewe chakula chenye kiwango kikubwa cha nguvu joto nyumbani. Chakula hiki chenye kiwango kikubwa cha - nguvu joto ni bora, sawa na vyakula-tiba maalum ambavyo vimetengenezewa viwandani, na wakati mwingine ni bora zaidi katika vipengele kadhaa (angalia hapa). Ni chakula kizuri sana pia kwa mtoto mdogo yeyote kwa sababu watoto wadogo wote wanahitaji vyakula vyenye nguvujoto na virutubishi ili waweze kukua na kustawi.
Changanya aina 4 za vyakula kwa kutumia vyakula asilia kwenye eneo unapoishi: uji, protini, mafuta, na mbogamboga.
- Tengeneza kikombe 1 cha uji kutokana na chakula cha wanga.
Chagua chakula chochote kati ya vifuatavyo:
Tumia chakula chochote cha wanga ambacho kawaida huliwa na familia yako, kipikwe na kitengenezwe kama uji mzito.- ulezi
- mahindi
- mchele
- ngano
- gimbi au kiyazi
- Ongezea chakula chenye protini kwa wingi.
Chagua chochote moja wapo:
- vijiko 2 vya chakula vya maziwa ya unga
- yai 1
- ½ kikombe cha karanga ambazo zimekaangwa, kutwangwa au kusagwa
- ½ kikombe cha maharagwe, njegere au kunde zilizopikwa na kupondwapondwa
- ½ kikombe cha maharagwe yaliopikwa au unga wa kunde/njegere
- ½ kikombe cha samaki kavu waliopondwapondwa au kusagwa
- ¼ kikombe cha nyama au viungo vya ndani iliopikwa, ikacharangwa kwenye vipande vidogo.
- Ongeza vijiko 2 vya mafuta.
Chagua moja kati ya vifuatavyo:- Mbogamboga yeyote au mafuta ya karanga, siagi au mafuta ya nguruwe.
- Ongeza ½ kikombe cha mbogamboga zilizopikwa.
Chagua moja kati ya vifuatavyo:- nyanya
- mboga za majani
- maji ya matunda
- boga
- maharagwe mabichi
- kunde au
- njegere-mbichi
- bamya
- au mbogamboga nyingine
Mpe uji huu wenye kiwango cha juu cha nguvu joto mara 4 au 5 kwa siku.
Mtoto mwenye utapiamlo anaweza kutopenda kula au kuwa na nguvu tu ya kula polepole. Mpe chakula kidogo kidogo kila baada ya saa 1 au 2. Kuwa na subira na lakini usiache. Endelea kumpatia chakula hiki chenye nguvu hadi atakapoanza kuongezeka uzito na kurudisha tena nguvu na kuchangamka.
Nawa mikono yako kabla ya kupika au kutoa chakula, tumia vyombo visafi, na tumia chakula chote ulichoandaa ndani ya siku moja. Kama vilivyo vyakula vingine, chakula hiki chenye nguvu joto nyingi hatimaye kitaharibika, na kitaharibika haraka zaidi kama unaishi katika mazingira yenye joto.
Kama mtoto bado ananyonya, nyonyesha kwanza na baada ya hapo ndipo umpe chakula hiki. Mpatie maziwa ya mama mara nyingi zaidi-kwa sababu watoto wenye utapiamlo wanaweza kutokua na nguvu za kunyonya vya kutosha kila wanapopewa ziwa.
Pia mpe tunda kila siku. Kila tunda lina vitamini. Lakini kama unaweza, mpe aina tofauti ya matunda – ili mtoto aweze kupata vitamini mbalimbali.
Vinywaji vya kuongeza maji mwilini
Watoto wengi wenye utapiamlo huwa wamepungukiwa na maji mwilini kutokana na kuharisha. Kama mama atakuwa ananyonyesha, anapaswa kuendelea kunyonyesha, mara kadhaa kadri atakavyoweza.
Pamoja na maziwa ya mama, mpe kinywaji cha kumuongezea maji mwilini. Mtoto mwenye utapiamlo mkali huhitaji chumvi kidogo na sukari zaidi kidogo ya kiasi kinachowekwa kwenye kinywaji maalum cha kawaida kwa ajili ya kuongeza maji mwilini. Hivyo:
Katika lita 1 ya maji safi | |
Changanya ¼ kijiko cha chumvi |
|
Onja mchanganyiko huu. Unatakiwa kuwa na chumvichumvi kidogo kuliko machozi. | |
Halafu changanya vijiko vya chai 9 vya sukari Mpatie vijiko kadhaa vya mchanganyiko huu kila baada ya dakika chache. Mtu mwenye utapiamlo anaweza kutokuwa na nguvu za kutosha kunywa. Msaidie kuinua kichwa wakati utakapokuwa unamnywesha kwa kutumia kijiko. |
Joto
Mtu akiwa na utapiamlo, mwili unaweza kukosa nishati ya kuupatia joto la kutosha. Pima joto la mwili wa mgonjwa mara kwa mara. Muongezee joto kwa kumfunika na blanketi kwa siku kadhaa hadi atakapopona. Watu wengi huhisi baridi zaidi usiku, na kuhitaji blanketi za ziada.
Dawa
Utapiamlo mkali ni ugonjwa na unapaswa kutibiwa. Mtoto ambaye ana utapiamlo mkali yuko katika hatari kubwa ya kupatwa na maambukizi. Lakini kwa sababu mwili wake tayari ni dhaifu, inawezekana usioneshe dalili ambazo kawaida hutuambia mtu anapokuwa anaumwa. Kwa sababu hii, mpatie dawa za kupambana na maambukizi, hata kama hana homa au maambukizi ya kawaida. Watoto wenye utapiamlo mkali wapatiwe:
- amoksilini (amoxicillin) au dawa ya antibiotiki nyingine, mara 3 kila siku kwa siku 7.
- Chanjo ya surua (isipokuwa kama una uhakika kuwa mtoto alipatiwa chanjo zote dhidi ya surua), angalia Chanjo (kinaandaliwa).
- Matone ya vitamini A.
- Viongeza madini ya zinki.
- Mebendazo (mebendazole)-kama maambukizi ya minyoo ni kawaida eneo unaposhi.
Mhudumie mtoto kwa uangalifu
Hali ya mtoto mwenye utapiamlo inaweza kubadilika na kuwa mbaya haraka. Hivyo, anahitaji uangalizi wa karibu.
Unapoanza kumnywesha na kumlisha chakula, pima kasi ya mapigo yake ya moyo na pumzi. Angalia Jinsi ya kumchunguza mgonjwa (kinaandaliwa). Kama kasi hizi zinaongezeka unapokuwa unampa kinywaji cha kuongeza maji mwilini, simamisha kumpa na tafuta msaada wa daktari. Moyo wake huenda ukawa unapata shida kupatana na majimaji hayo.
Je mtoto anapata nafuu? Kama hapati nafuu baada ya siku kadhaa, anaweza kuwa na maambukizi au ugonjwa ambao unasababisha matatizo zaidi. Unahitaji kwenda hospitali. Pia, tafuta msaada wakati wote mtoto anapozirai au kupoteza fahamu, anapopata shambulio (sezure), au ana homa ya nyuzi joto 38 sentigredi (100.4 farenheti) au zaidi.
Msaidie mhudumu mkuu wa mtoto kuelewa mtoto anachohitaji hasa ili kuishi na kupata nafuu. Elezea vizuri juu ya suala la kumuongezea maji mwilini, chakula, na dawa ambazo zinahitajika pamoja na jinsi gani ya kumsaidia mtoto kupata lishe bora siku zijazo. Mkumbushe mtoa huduma kuwa na subira na kushikilia yaliyo ya msingi kwa mtoto wakati wa kumlisha. Bila kuwa makini juu ya chakula cha mtoto na matunzo, mtoto anaweza kurudi haraka katika hali ya utapiamlo. Mwambie mhudumu wa mtoto kukuelezea kanuni za huduma kwa mtoto mwenye utapiamlo alizojifunza ili kujihakikishia kuwa ameelewa.Fanya chochote uwezacho kumsaidia. Kawaida huduma kwa mtoto mwenye utapiamlo iko mikononi mwa mama ambaye tayari ametingwa na kazi ya kuwaangalia watoto wake wengine, na kazi zingine za nyumbani. Wakati mwingine yeye mwenyewe hana lishe ya kutosha. Kumsaidia mama huyu ni kumsaidia mtoto.
Bila kuzingatia kiasi gani anaendelea kupata nafuu, a child mtoto ambaye amewahi kupata utapiamlo mkali anahitaji kuchunguzwa mara kwa mara kuhakikisha kuwa anakua kimwili na kisaikolojia na kupata nguvu.
Vyakula -Tiba Vilivyo Tayari kwa Matumizi
Katika hali ambapo watu wanashinda au kulala njaa, vyakula - tiba vilivyofungashwa tayari kwa matumizi (“Ready-to-Use Therapeutic Foods”). Vinaweza kusaidia. Vyakula hivi vyenye nguvu joto kwa wingi vinaweza kuokoa maisha iwapo hakuna ckakula chochote kingine, kwa mfano, katika kambi za wakimbizi. Lakini vina matatizo yake. Dk Massimo Serventi, daktari wa watoto Tanzania, alielezea wasiwasi wake juu ya Plumpy’nut, chakula tiba maarufu duniani:
(Baada ya kupewa changamoto na shirika la Médecins Sans Frontières, kampuni inayotengeneza Plumpy’nut ilikubali kuruhusu kampuni za ndani za nchi husika kutengeneza bidhaa zinazowafaa kwa kutumia fomula ya Plumpy’nut)