Hesperian Health Guides
Vyakula vipya, matatizo mapya
HealthWiki > Toleo Jipya: Mahali Pasipo na Daktari > Lishe bora hutengeneza afya bora > Vyakula vipya, matatizo mapya
Pipi, soda na asusa zilizofungashwa vimekolezwa kupita kiasi aidha chumvi, sukari, mafuta na kemikali za kuvihifadhi. Vitu hivi vilivyoongezwa ni hatari kwa afya na husababisha meno kuoza, kisukari, ugonjwa wa moyo, na baadhi ya saratani. Vyakula hivi pia vinakosa vitamini, madini, nyuzi nyuzi na protini-virutubishi ambavyo hupatikana katika vyakula vilivyoandaliwa kwa njia za kawaida bila kuchakatwa viwandani. Kwa sababu hizi, hujulikana kama vyakula visivyo na faida kilishe (junk foods).
Mkate mweupe uliotengenezwa kiwandani, vyakula vya kwenye makopo, biskuti, na paketi za tambi vinaweza kuonekana vinafaa kiafya sawa na vyakula vinavyofanana ambavyo vimetoka shambani na kupikwa nyumbani. Matangazo yanatuambia kuwa vinafaa.Lakini kawaida hukolezwa sukari, chumvi na kemikali kwa kiwango kinachotishia afya. Pia huwa havina virutubishi ambavyo hupatikana katika vyakula vilivyotengenezwa nyumbani. Hivyo, navyo pia ni vyakula visivyo na faida kilishe (junk foods) sawa na pipi na asusa zilizofungashwa.
Yaliyomo
Kisukari na ugonjwa wa moyo: magonjwa ya mfumo mpya wa ulaji
Kisukari na ugonjwa wa moyo ni matatizo ya kiafya ambayo yamesababishwa na mabadiliko katika jinsi watu wanavyokula na kufanya kazi. Magonjwa hayo ni nadra mahali ambapo watu bado wanasanya, kulima na kupika chakula chao wenyewe, na kujishughulisha kama wakulima au na stadi za kazi mbalimbali. Lakini kadri watu zaidi wanavyoshindwa kujishughulisha ipasavyo, na hivyo kupata mazoezi kidogo ya kimwili( mfano wakifanya kazi viwandani au kukaa mbele ya kompyuta saa nyingi), na kutegemea zaidi vyakula viliyotengenezewa viwandani, magonjwa hayo yamekuwa jambo la kawaida. Hayasababishwi na vijidudu au hayaenezwi kwa kwambukizwa. Hutokana na kushindwa kujishughulisha, kutegemea sana vyakula visivyo na faida kilishe( junk foods), na ongezeko la msongo na matabaka ya kijamii katika maisha yetu. Miili yetu haifanyi kazi vizuri katika mazingira haya.
Wakati kisukari na ugonjwa wa moyo ni magojwa 2 tofauti, sababu zake zinafanana. Kila ugonjwa moja unaweza kusababisha mwingine, na njia za kuyatibu na kuyazuia pia zinafanana.
Kisukari
Kisukari ni tatizo la mwili kushindwa kutumia sukari barabara. Kisukari kinaweza kusababisha upofu, kukatwa viungo, kuzirai, na hata kifo. Kwa taarifa zaidi juu ya aina tofauti za kisukari na jinsi ya kuzitibu, angalia Kisukari.
Ugonjwa wa kisukari umeenea sana katika nchi tajiri kama vile Marekani, na hivi sasa unasambaa dunia nzima. Sababu zake zinazohusiana na chakula ni pamoja na kula kupita kiasi, kula vyakula visivyofaa kiafya, na kukosa mazoezi. Kila mahali ambapo unga ulio chakatwa viwandani na kuwa mweupe, na vyakula vilivyokolezwa sukari vinapotawala, kisukari nacho hufuatia.
Ugonjwa wa moyo na mshituko wa moyo
- Shinikizo la juu la damu
- Ugonjwa wa moyo
- Mshituko wa moyo (heart attack)
Kimsingi, hizi ni sehemu tofauti za tatizo moja la kiafya: ugonjwa wa moyo.Vyakula visivyofaa kiafya na kukosa mazoezi(pamoja na uvutaji sigara na msongo) husababisha mafuta kulundikana ndani ya mishipa ya damu. Kutokana na hali hiyo, moyo hujikuta ukisukuma kwa nguvu zaidi kulazimisha damu kupita kwenye mishipa iliyojazana na kusababisha shinikizo la juu la damu. Moyo huanza kuchoka na kudhoofu kutokana na kazi hii. Damu ambayo haiwezi kupita kwa urahisi kwenye mshipa huanza kuganda. Na moyo ukiwa umechoka na bila kupokea damu, husimama kufanya kazi, na hivyo kusababisha mshituko wa moyo (heart attack).
Ugonjwa wa moyo unaohusiana na rumatizimu (Rheumatic heart disease) ni kisababishi kingine cha kawaida cha ugonjwa wa moyo. Kinatokana na kuugua homa ya rumatizimu (rheumatic fever) wakati wa utotoni.
Tiba na kinga
Yapo mambo mengi ambayo tunaweza kufanya kama watu binafsi na ndani ya familia zetu kuzuia na kutibu kisukari na ugonjwa wa moyo. Lakini mabadiliko katika ngazi ya jamii na kitaifa pia yanahitajika.
Mazoezi: Kutembea haraka, kucheza muziki , michezo, au zoezi lolote ambalo huongeza kasi ya moyo wako kwa dakika 30 au zaidi kwa siku linahitajika kwa ajili ya kila mfumo katika mwili wako kufanya kazi yake vizuri. Mazoezi huimarisha mifupa, hurejesha nguvu mwilini, huboresha hali yako ya kisaikolojia, na kukusaidia kuishi maisha marefu zaidi. Mazoezi ni mkakati muhimu wa kuzuia na kutibu magonjwa yote 2-kisukari na ugonjwa wa moyo.
Chakula: Mlo wenye mbogamboga nyingi za majani kutoka shambani, nafaka ambazo hazijakobolewa, na maharagwe ni bora zaidi kwa ajili ya kuzuia na kutibu ugonjwa wa moyo na kisukari.
- Nyama nyekundu, bidhaa za maziwa, na mayai ni vyakula vizuri kiafya, lakini vikiliwa katika kila mlo au kila siku huongeza hatari ya ugonjwa wa moyo. Hivyo kula vyakula hivyo mara chache kwa wiki au kula kidogo.
- Pipi na vyakula vya wanga vilivyochakatwa viwandani havihitajiki hata kidogo, na kula bidhaa hizi kila siku kunaweza kusababisha kisukari.
- Mafuta yanahitajika kwa kiasi kidogo, lakini huchangia hatari ya ugonjwa wa moyo na kisukari yanapotumiwa katika kiasi kikubwa. Nyama nyekundu, mafuta ya nazi, vyakula vilivyokaangwa kwenye mafuta na vyakula ambavyo hutengenezewa viwandani ndiyo vyanzo vikuu vya mafuta yasiyofaa kiafya . Jitahidi kula kiasi kidogo cha bidhaa hizi. Njugu, parachichi, na samaki ni miongoni mwa vyanzo vya mafuta ambavyo vinafaa kiafya na pia hutupatia virutubishi vingine vingi. Hivi ndiyo vyanzo bora zaidi.
- Chumvi inaweza kuzidisha ugonjwa wa moyo iwapo itatumika kwa kiasi kikubwa.Kama una ugonjwa wa moyo au shinikizo la juu la damu, epuka vyakula vyenye chumvi nyingi vilivyofungashwa viwandani. Vyakula vya kwenye makopo kawaida huwa na chumvi nyingi mno. Unapounga chakula chako, tumia chumvi kidogo tu, au tumia majani yenye ladha au viungo vingine kama mbadala.
Soda na vinywaji vingine vitamu kwenye chupa na makopo hasa havifai kiafya. Bidhaa hizi kimsingi ni mchanganyiko wa maji na sukari tu, pamoja na kemikali ambazo huongezwa kuleta rangi na ladha inayokusudiwa. Kunywa bidhaa hizi kila siku huweza kusababisha au kuzidisha kisukari, meno kuoza, na shibe bila lishe.
Kama wewe ni mnene: Kupunguza uzito utakulinda dhidi ya vyote viwili-kisukari na ugonjwa wa moyo. Kupunguza uzito taratibu ni salama zaidi kuliko kupunguza uzito katika muda mfupi. Njia inayofaa zaidi kiafya na inayodumu katika kupunguza uzito ni kufanya mazoezi mara kwa mara( siku 5 kwa wiki au zaidi) na kula milo yenye ukubwa wa wastani. Jitahidi kuepuka vyakula visivyofaa kiafya ambavyo vimeorodheshwa.
Kuacha uvutaji sigara ni njia nyingine ya kuishi maisha marefu na mazuri zaidi. Kuacha uvutaji sigara kutakulinda dhidi ya ugonjwa wa moyo, kisukari na pia saratani. Kuhusu maelezo zaidi juu ya hatari za uvutaji, angalia Madawa ya kulevya, pombe na tumbaku (kinaadaliwa).
Afya ni swala la jamii
Kile tunachokula na jinsi gani tunavyoishi maisha yetu ya kila siku kwa kiasi kikubwa ni matokeo ya uchaguzi wetu. Lakini pia ni matokeo ya vyakula, kazi na makazi ambayo yanapatikana, na kwa bei ambayo tunaweza kuimudu. Tunaweza kujaribu kujenga tabia za ulaji na mazoezi zinazofaa kiafya, lakini juhudi zetu zikawa zinakwamishwa na mapungufu mbalimbali katika mazingira yetu. Kwa mfano, kile tunachotaka kula na hata muda wa kukiandaa vizuri hutegemea mambo mengi ambayo siyo rahisi mtu mmoja kuyadhibiti: matangazo, jinsi ratiba zetu za kazi zilivyopangwa, na hata upatikanaji wa maji safi na jiko linalofaa. Mambo hayo yanawahusu watu wengi na yanaweza kubadilishwa kupitia juhudi za pamoja au kupitia sera za serikali.
Shughuli za wana harakati kwa ajili ya mabadiliko zinaweza kuwa na mtazamo mdogo au mtazamo mpana.Mtazamo mdogo ni pamoja na kuangalia swala moja, kama vile kupiga marufuku soda na vinywaji vilivyokolezwa sukari mashuleni, au kutoa chakula cha mchana kinachofaa kiafya kwa wanafunzi wote shuleni. Lakini mfano wa mtazamo mpana, ni kuangalia jiji zima kama vile madarasa ya mazoezi ambayo hutolewa na uongozi wa Jiji la Bangkok, Thailand bila malipo, au kama inavyoelezewa katika taarifa juu ya Ciclovía kutoka Bogota , Columbia. Sera za taifa na za serikali za mitaa zinaweza kutengenezwa kwa namna ambayo inawapendelea wakulima wadogo na masoko ya ndani badala ya sera zinazoyajengea makampuni makubwa ya kilimo mazingira ya kupata faida kubwa. Mabadiliko yanahitajika katika ngazi zote hizi ili kudhibiti na kutibu kisukari na ugonjwa wa moyo kwa mafanikio.
Ciclovía
Wakazi wa Bogota, Colombia (jiji kubwa katika bara la Amerika ya Kusini) walikatishwa tamaa na mitaa iliyosongamana na hali ya hewa iliyochafuliwa. Wakiongozwa na afisa mmoja mwenye mtazamo wa mbali kutoka Halmashauri ya jiji hilo, waliamua kuchukua hatua: walipanga kukomboa maeneo yao ya jiji ambayo yalikuwa yakitumika kwa ajili ya magari madogo na makubwa ili kulifanya jiji hilo kuwa sehemu bora zaidi ya kuishi kwa wakazi wake. Jiji liliondokana na mamia ya sehemu za kuegesha magari, zaidi ya kilomita 300 za njia za baisikeli zilijengwa, na idadi ya magari yanayotakiwa kuwa barabarani wakati wa saa zenye pilika nyingi ilidhibitiwa.
Uvumbuzi ulioleta shamrashamra zaidi (hivi sasa umeigwa na majiji kadhaa duniani) ni Ciclovía: Kila jumapili, barabara kuu hufungwa kuzuia matumizi ya magari. Waendesha baisikeli, wanamichezo wanaotumia viatu vyenye vigurudumu au vitelezaji (skaters) watumiaji wa baisikeli za miguu mitatu, na watembea kwa miguu ndio huchukua hatamu. Katika bustani za jiji hilo, muziki wa dansi na madarasa ya mazoezi hutolewa bure. Baisikeli pia huazimwa bila gharama.
Ingawa imebuniwa kutatua tatizo muhimu, Ciclovía pia ni burudani kubwa. Ni tafrija ya wiki ambapo kila mtu ndani ya jiji hilo amealikwa. Watoto na mababu/mabibi hucheza pamoja kwenye bustani na watu wa kila rika huendesha baisikeli, na kukimbia huru kupita barabara ambazo kawaida hazina mahali pa kupita. Ni fursa ya pekee kufanya mazoezi, kukutana na majirani na wafanyakazi wengine na kupata marafiki wapya.Ni njia tofauti na bora zaidi ya kuishi maisha ya jijini.
Mwanzoni, baadhi ya biashara zilipinga wazo hili kwa sababu lingesababisha msongamano wa magari na kuingilia shughuli za watu kutafuta mahitaji yao .Lakini Ciclovía ilijenga umaarufu kiasi kwamba waliacha kulalamika. Hivi sasa watu katika jiji la Bogota wanatafuta njia zaidi za kulifanya jiji lao kuwa salama, lenye afya na burudani zaidi, siku 7 kwa wiki.