Hesperian Health Guides

Matatizo ya kiafya kwa watoto

Katika sura hii:

Wakati mwingine, pamoja na juhudi zetu nzuri za kuzuia magonjwa, watoto huugua. Ugonjwa kwa mtoto unaweza kuzidi au kuongezeka haraka. Ni muhimu kugundua dalili za ugonjwa mapema na kuushughulikia mara moja.

  
Danger.png
 Dalili za hatari
Mtoto mwenye dalili mojawapo zifuatazo anahitaji matibabu haraka na uangalizi wakati wote. Akipatiwa huduma, anaweza taratibu kupata nafuu. Kama ana dalili zifuatazo zaidi ya moja, au iwapo dalili yoyote itazidi kuwa mbaya, mtoto yu hatarini:
  • Kupungukiwa na maji mwilini. Kukosa mkojo, mdomo kukauka, au utosi kwenye kichwa cha mtoto kubonyea ndani ni dalili za kupungukiwa na maji mwilini-tatizo linalotishia uhai wa mtoto. Angalia chini -sehemu ya kupungukiwa na maji.
  • Mashambulio. Mashambulio ya ghafla kwa mtoto ambayo hujumuisha kupoteza fahamu na kurusha maungo ya mwili au kutetemeka- kawaida huambatana na homa kali.
  • Ulegevu mwilini. Udhaifu na uchovu wa mara kwa mara mwilini siyo hali ya kawaida na wala dalili ya afya nzuri. Kukosa hamu ya kula na kuchanganyikiwa kimawazo hasa ni dalili zinazoibua wasiwasi. Kuugua sana ugonjwa wowote ule huweza kusababisha tatizo hili.
  • Kupumua kwa shida au kupumua haraka haraka. Hizi ni dalili za kichomi au nimonia - ugonjwa ambao ni hatari sana kwa watoto wadogo.

Kupungukiwa na maji mwilini

Watoto wengi wanaokufa kutokana na kuharisha hupoteza maisha kwa sababu ya kupungukiwa na maji mwilini. Tiba yake rahisi ni kumuongezea mtoto maji ambayo anapoteza kwa kunywa maji zaidi. Kumuongezea maji mtoto mwilini husaidia kutibu tatizo la kupungukiwa na maji kutokana na kuharisha, kutapika, au kufanya kazi muda mrefu katika hali ya hewa au jengo lenye joto. Kwa kuwa kupungukiwa na maji mwilini kutokana na kuharisha ni hatari sana kwa watoto, kila mara kuwa makini kuangalia:

Dalili
  • Kuharisha hata kama hakuna dalili za kupungukiwa maji.
  • Kiu (lakini watoto mara nyingi hawasemi wanapokuwa na kiu).
  • Mdomo kukauka (unapogusa ndani ya shavu la mtoto kunaonekana kukavu).
  • Kukojoa mara chache kuliko kawaida na mkojo ukiwa na rangi nzito.

Anza tiba mara moja kabla dalili hazijawa mbaya zaidi.

Dalili zinazoashiria kuwa hali ya upungufu wa maji mwilini inazidi kuwa mbaya:
  • Ulegevu: uchovu, kukosa nguvu
  • Mapigo ya moyo kwenda haraka
  • Pumzi nzito
  • Macho kurudi ndani pasipo na machozi
  • Ngozi ya mwili inapofinywa au kuvutwa hubaki katika hali hiyo hiyo kwa muda au huchelewa kurudi
Vuta ngozi nyuma ya kiganja au kwenye tumbo kati ya vidole vyako 2 kama ilivyoonyeshwa kwenye mchoro. Kama ngozi haitarudi katika hali yake ya kawaida, huenda mtoto amepungukiwa na maji mwilini.
Mkono ukifinya au kuvuta ngozi
Ngozi ikifinywa au kuvutwa kuelekea juu hubaki katika hali hiyo kwa muda

Hali ya upungufu wa maji mwilini inapokuwa mbaya kiasi hiki, mtoto anakuwa katika hatari. Tiba ya haraka inaweza kuokoa maisha yake.

Matibabu na uzuiaji

Tiba ya tatizo la kupungukiwa na maji mwilini ni rahisi: mpe vinywaji. Angalia maelekezo juu ya kinywaji maalum cha kumuongezea mgonjwa maji mwilini. Iwapo mtoto hataanza kupata nafuu haraka, tafuta msaada zaidi.

Maziwa ya mama
Kama unanyonyesha mtoto ambaye amepungukiwa na maji mwilini,endelea kunyonyesha na pia kumpa kinywaji hicho. Mnyonyeshe mtoto mara nyingi zaidi kuliko kawaida-angalau kila baada ya saa 2. Mruhusu mtoto anyonye kadri atakavyohitaji.

Kuharisha

Kujisaidia kinyesi laini chenye majimaji kila baada ya muda mfupi kuliko kawaida huitwa kuharisha. Watoto huandamwa na tatizo la kuharisha kwa sababu nyingi, zaidi ni kutokana na vijidudu vinavyosambaa kupitia mazingira machafu na lishe duni. Mara nyingi, tatizo la kuharisha hupungua bila dawa. Lakini kuna tiba moja ambayo huhitajika kwa kila mtu ambaye anaharisha, na tiba hiyo ni kutumia vinywaj ili kufidia maji ya mwilini ambayo hupotea kupitia mharo. Bila kumpatia vinywaji, mtoto ambaye anaharisha anaweza kupoteza kiasi kikubwa cha maji mwilini na kufariki.

Nusuru maisha ya mtoto ambaye anaharisha kwa kumpatia vinywaji ili kufidia maji ya mwilini ambayo amepoteza.


Je, unaamini kumpatia mtoto vinywaji husababisha tatizo la kuharisha kuzidi? Ni rahisi kufikiria hivyo unapoangalia mharo ukimtoka mtoto. Lakini vinywaji havisababishi kuharisha.

Kuzuia kumpa vinywaji hakusaidii kupunguza makali ya kuharisha. Kitendo hicho badala yake kuyaweka maisha ya mtoto katika hatari.
Mtoto aliyekonda akiwa anaharisha
Kunywa vinywaji husaidia kukuongezea afya unapokuwa na tatizo la kuharisha.
Mtoto mwenye furaha na afya nzuri akiwa na kikombe cha maji

Bonyeza hapa kwa taarifa zaidi juu ya kuharisha. Taarifa zifuatazo zinahusu hasa watoto.

Matibabu

Mtoto mgonjwa ambaye amekonda sana akiwa amekaa kwenye shuka na kikombe mikononi

  1. Mpatie kinywaji maalum cha kumuongezea maji mwilini. Kwa mtoto chini ya mika 2, mpe angalau robo kikombe kila baada ya kuharisha. Kwa mtoto wa miaka 2 au zaidi, mpe nusu kikombe kila baada ya kuharisha. Kinywaji maalum cha kuongeza maji mwilini ni maji yaliyochanganywa na chumvi kidogo na sukari au nafaka zilizopikwa. Baadhi ya watu huongeza juisi ya ndimo kidogo kuleta ladha.
  2. Mwanamke akipika uji
  3. Mpatie chakula. Mara nyingi mtoto hatasema anasikia njaa, lakini kama hatakula atazidi kudhoofika na ugonjwa kuzidi. Kuwa na subira. Mpe vijiko vichache vya chakula, mara 6 kwa siku au zaidi. Ongeza kipimo cha chakula kadri hali yake itakapokuwa inaboreka. Boresha virutubishi kwenye uji wa mtoto kwa kuchanganya na vyakula vinavyoongeza sana nguvu mwilini kama vile karanga zilizosagwa, mayai, samaki wakavu au dagaa, maziwa ya mtindi, parachichi, au ndizi. Iwapo huna vyakula vya protini au mbogamboga, ongeza kijiko 1 cha mafuta kwenye uji.
  4. Mwanamke akimyonyesha mtoto wake
    Maziwa ya mama hufidia majimaji na virutubishi ambavyo hupotea wakati wa kuharisha.
  5. Epuka matumizi ya dawa dhidi ya kuharisha. Dawa hizi hufanya kazi kama vizuizi na kubakisha kinyesi na vijidudu vilivyomo ndani ya mtoto. Dawa za antibiotiki husaidia tu kwa baadhi ya maambukizi ya kipindupindu na kuharisha damu.
  6. Zuia ugonjwa wa kuharisha usitokee tena kwa kuboresha usafi wa mazingira na lishe.

Utapiamlo na kuharisha

Watoto wenye utapiamlo hupatwa na tatizo la kuharisha mara kwa mara. Na kwao, ugonjwa huu unakuwa mgumu kupona. Hii ni kwa sababu magonjwa haya 2 hufanya kazi kwa pamoja katika mduara hatari wa kupokezana.

Mtoto mwenye utapiamlo
1. Kutopata chakula cha kutosha (lishe duni) huathiri mwili mzima, ukiwemo utumbo.
2. Utumbo ulioharibika kutokana na lishe duni au utapiamlo hauwezi kufyonza virutubishi vingi. Chakula hupita tu haraka. Hali hii ndiyo kuharisha.
3. Kuharisha mara kwa mara huchangia mwili kupoteza virutubishi. Mwili ukikosa virutubishi kutoka kwenye chakula husababisha utapiamlo.
Utapiamlo husababisha kuharisha – kuharisha husababisha utapiamlo.

Kuuvunja mdwara huu hatari kutasaidia kuzuia vifo kutokana na muunganiko wa kuharisha na utapiamlo, au kutokana na maambukizi mengi ambayo huwapata watoto waliodhoofika kutokana na kuharisha na njaa.

Kama una fedha kidogo tu, bora kuitumia kwa ajili ya chakula cha mtoto wako. Chakula kitamwongezea nguvu mtoto, kumsaidia kupona haraka, na kumpunguzia hatari ya kuharisha tena.

Kutibu utapiamlo mkali, bonyeza hapa.

Zinki husaidia kuzuia kuharisha
Madini ya zinki husaidia kupunguza tatizo la kuharisha miongoni mwa watoto. Kwa sababu hii, watoto wanaoharisha wanaweza kupatiwa zinki iwapo inapatikana.

Kwa mtoto wa miezi 2 hadi 6: Mpe miligramu 10 za zinki kila siku kwa siku 10. Saga kidonge na kuchanganya na maziwa ya mama kidogo.

Kuanzia umri wa miezi 6 hadi miaka 5: Mpe miligramu 20 kila siku kwa siku 10.

Kutapika

Baadhi ya watoto hutapika zaidi kuliko wengine. Lakini mtoto anapotapika sana au kuonesha dalili za kupungukiwa na maji, mpatie kinywaji maalum cha kumuongezea maji mwilini. Kwa kuanzia, mpe kijiko 1 tu kila baada ya dakika 15, hata kama anaendelea kutapika. Kama hatakitapika kinywaji, muongeze kijiko 1 kila baada ya dakika 5. Halafu mpe tena kipimo kikubwa zaidi. Kwa kumpatia vinywaji zaidi na chakula mapema kadri iwezekanavyo, unaweza kumsaidia mtoto kurudisha nguvu zake tena.

Homa

Watoto mara nyingi hupata homa miili yao inapokuwa inapambana na ugonjwa, na homa hizo wakati mwingine hupanda sana. Msaidie mtoto kupata nafuu kwa kumpatia dawa ya parasetamo au ibrofeni. Kumkanda na kitambaa chenye ubaridi kidogo kilicholoweshwa na maji au kumuogesha na maji yenye ubaridi kidogo pia huweza kusaidia. Mpatie vinywaji kwa wingi kuzuia asipungukiwe na maji mwilini. Homa kali kwa mtoto mdogo inaweza kuchangia mtoto kupata mashambulio. Lakini homa, hasa homa kali, inaweza kuwa dalili ya maambukizi makali mwilini. Huduma muhimu zaidi kwa mtoto mwenye homa ni kuchunguza na kutibu chanzo cha homa hiyo.

Dalili za hatari na sababu za homa
Homa na matatizo yaliyotajwa chini Yanaweza kuashiria...
Shingo kukakamaa au maumivu ya kichwa makali Homa ya uti wa mgongo
Upele mdogomdogo mwili mzima Surua
Kikohozi ambacho kinachukua muda mrefu Kifua kikuu
Maumivu ya tumbo na kuharisha au kufunga choo (au kupata choo kigumu na kwa shida), wakati mwingine kukiwa na madoa ya pinki juu ya tumbo au ubavuni. (Kama ni homa ya matumbo au taifodi,homa huongezeka hatua kwa hatua katika kipindi cha wiki 1, halafu maumivu ya tumbo ndipo huanza.) Homa ya matumbo (Taifodi).
Angalia pia Baadhi ya magonjwa hatari ya kuambukiza (kinaandaliwa).
Kusikia baridi kali au aina yote ya homa kama unaishi eneo ambapo malaria ni ugonjwa wa kawaida. Malaria
Kipimajoto kikionyesha homa ya kawaida ikianzia zaidi ya nyuzijoto 37.5 selsiasi na homa kali ikianzia zaidi ya nyuzijoto 39
Selsiasi
Farenheiti
chini sana
k a w a i d a
homa
homa kali

Malaria

Malaria imeelezewa zaidi katika Baadhi ya magonjwa hatari ya kuambukiza (kinaandaliwa). Malaria ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya vifo vya watoto katika sehemu nyingi ambazo hukumbwa sana na ugonjwa huo.

Dalili
  • Homa
  • Kusikia baridi kali au kutokwa na jasho
  • Maumivu ya kichwa, maumivu kwenye misuli, maumivu tumboni
  • Kutapika au kuharisha
Matibabu

Kila inapowezekana, pima kabla ya kuanza matibabu ya malaria. Lakini kama huwezi kufanya kipimo hicho, na malaria ni ugonjwa wa kawaida katika eneo hilo,na hakuna chanzo kingine cha homa hiyo, anza dawa za malaria mara moja.

Anemia (upungufu wa wekundu wa damu) ni ugonjwa wa kawaida miongoni mwa watoto wenye malaria. Hivyo wanapaswa pia kutumia vidonge vya madini ya chuma.

Dalili za hatari
  • Kupumua kwa shida
  • Mashambulio, kuchanganyikiwa kimawazo-kutofikiri vizuri, kupoteza fahamu, au dalili yoyote nyingine ya maambukizi kwenye ubongo (angalia Homa ya uti wa mgongo).

Dalili hizi ni tishio kwa maisha na mtoto anatakiwa msaada wa daktari haraka. Choma sindano ya atesuneti (artesunate) wakati unatafuta msaada zaidi. Kama huna atesuneti, choma sindano ya kwinini. Angalia Baadhi ya magonjwa hatari ya kuambukiza: Madawa (kinaandaliwa).

Uzuiaji

Angalia Baadhi ya magonjwa hatari ya kuambukiza (kinaandaliwa) kuhusu njia nyingi za kupunguza malaria katika familia na jamii yako.

Mtoto kitandani akiwa amekingwa na kiandarua dhidi ya mbu mkubwa
Zuia malaria kwa kutumia vyandarua na wavu wa kuzuia mbu madirishani.

Mashambulio au mtikishiko wa maungo (seizures au convulsions)

Mtoto akiwa amepigwa na shambulio

Mashambulio ni hali inayokuja ghafla, na kawaida kuchukua muda mfupi, ikijumuisha kupoteza fahamu au kuchanganyikiwa kiakili, na mara nyingi mtikishiko wa maungo. Lakini wakati mwingine mtoto hubaki amekakamaa.

Mtoto anaweza kupata mashambulio kwa sababu ya homa kali, kupungukiwa na maji mwilini, jeraha, malaria, au kwa sababu nyingine. Mashambulio ambayo hujirudia huitwa Kifafa. Mashambulio ya kurudia yameelezewa katika Matatizo ya kichwa na ubongo (kinaandaliwa).

Wakati wa shambulio, ondoa vitu vyote vinavyomzunguka mtoto ili asiweze kujiumiza. Mgeuze alalie upande ili asikabwe wakati anatapika. Usimkamate na kumkandamiza chini mtoto au kujaribu kukamata ulimi wake wakati wa shambulio.

  • Kwa shambulio linalotokana na malaria, tafuta msaada wa kiafya. Wakati unatafuta msaada wa daktari, mpe diazipamu (diazepam). Tibu malaria kwa kutumia dawa. Angalia Baadhi ya magonjwa hatari ya kuambukiza: Madawa (kinaandaliwa).
  • Kwa shambulio linalotokana na kupungukiwa na maji mwilini, tafuta msaada daktari. Baada ya shambulio kutoweka, mpe vinywaji vya kumuongezea maji mwilini.
  • Kwa shambulio kutokana na homa ya uti wa mgongo, tafuta msaada wa daktari.


Kama kuna uwezekano mdogo wa vyanzo hatari vya mashambulio vilivyoelezewa juu, shambulio moja tu huenda siyo tatizo (ingawa linatisha kushuhudia). Iwapo mashambulio yatajirudia, muone daktari.

Mkazo wa misuli au kukakamaa ambako kunahusiana na pepopunda (tetanasi) kunaweza kuchanganywa na mashambulio mengine. Taya hufungamana na kukaza sana, na mwili ghafla hupinda ukielekea nyuma. Jifunze kutambua mapema dalili za pepopunda (tetanasi), angalia Huduma ya kwanza.

Mvulana amelala chini mwili wake ukiwa umekakamaa na kupinda kama tao kutokana na pepopunda (tetanasi)

Homa ya uti wa mgongo

Homa ya uti wa mgongo ni nadra lakini ni ugonjwa hatari sana ambao huathiri maeneo ya ubongo na uti wa mgongo. Mara nyingi, huanza bila sababu yoyote ya wazi na homa ndiyo dalili ya kwanza. Wakati mwingine ugonjwa huo hutokana na ugonjwa mwingine kama vile kifua kikuu, surua au matibwitibwi (mumps).

Uti wa mgongo unaosababishwa na kifua kikuu unaweza kuchukua wiki kadhaa kuandama.

Dalili
  • Homa
  • Maumivu makali ya kichwa
  • Kutapika
  • Mashambulio
  • Shingo kukakamaa — mtu anashindwa kuweka kichwa chake kati ya magoti yake
  • Mtu anakuwa hataki kuguswa — jaribio tu la kumgusa mtoto humfanya aanze kulia
  • Kuogopa mwanga
  • Kukasirika kwa urahisi, uepesi kuhisi, na kufadhaika
  • Ulegevu: udhaifu, kusinziasinzia, au kupoteza fahamu
Dalili kwa mtoto mchanga

Utosi juu ya kichwa cha mtoto unaweza kuvimba na kujitokeza juu. Mtoto anaweza kuwa anatapika au kuharisha. Huenda kukawa na homa au halijoto kushuka kuliko kawaida.

Mtoto kichwa chake kikiinuliwa na shingo yake ikipinda kwa hali ya kawaida
Mtoto asiye na raha mwenye shingo na mgongo vilivyokakamaa
Shingo ya mtoto mwenye afya hupinda unapoinua kichwa chake.
Shingo ya mtoto mwenye homa ya uti wa mgongo hukakamaa. Ukinua kichwa chake, mgongo wake mzima huinuka.
Matibabu

Tafuta msaada wa daktari mara moja. Mtoto atahitaji kupewa aina mbili za antibiotiki kwa pamoja (ampisilini na seftriakzoni au ampisilini au jentamaisini. Kama homa ya uti wa mgongo ilifuatia kifua kikuu, tibu kifua kikuu pia.

Nimonia au kichomi (maambukizi ya mapafu)

Kikohozi, mafua, na matatizo ya kupumua yanaweza kuwa ya kiwango cha kawaida au laini, au kiwango kikubwa -hatari. Mojawapo ya matatizo hatari ni nimonia au kichomi, ambukizo la mapafu. Nimonia umefafanuliwa zaidi katika Matatizo ya kupumua na kukohoa (kinaandaliwa). Nimonia ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya vifo vya watoto wadogo.

Mtoto ngozi yake kifuani ikivutwa kwa ndani
Dalili
  • Kupumua haraka haraka ni miongoni mwa dalili kuu za nimonia. Kupumua haraka haraka humaanisha:
    Kwa mtoto ambaye ana saa chache baada ya kuzaliwa hadi miezi 2: zaidi ya pumzi 60 kwa dakika
    Kuanzia miezi 2 hadi 12: zaidi ya pumzi 50 kwa dakika.
    Kuanzia miezi 12 hadi miaka 5: zaidi ya pumzi 40 kwa dakika.


Watoto wote hupumua haraka wanapokua wanalia. Jaribu kumtuliza mtoto. Atakaposimamisha kulia, weka mkono wako kwenye tumbo lake kusikia iwapo linapanda na kusuka. Tazama na kusikiliza pumzi ngapi anaingiza ndani kila dakika.

  • Homa
  • Kikohozi
  • Ngozi ya kifuani kuvutwa ndani kila anapoingiza pumzi
  • Kukosa hamu ya kula
Matibabu

Kama unaamini kwamba mtoto huyu mdogo anaweza kuwa na nimonia, mtibu kwa kutumia amoksilini na kotrimozazo (Cotrimoxazole) mara moja.

Mpe vinywaji kwa wingi na pia chakula.

Mtoto anapaswa kuanza kupata nafuu ndani ya siku 2. Kama hapati nafuu, huenda kuna sababu nyingine, mathalan kifua kikuu, athma, au maambukizi ya minyoo ambayo yameenea hadi kwenye mapafu yake. Hali yake ikizidi kuwa mbaya, hasa kama anapumua kwa shida, anapoteza ufahamu, au amepata shambulio, tafuta msaada wa daktari haraka. Mtoto huenda atahitaji sindano za ampisilini na seftriakzoni (au ampisilini na jentamaisini kama ni chini ya mwaka 1).

Uzuiaji

Kitu chochote ambacho huathiri mapafu hurahihisha maambukizi sehemu hiyo. Moshi hudhoofisha mapafu na kuchangia ongezeko la nimonia. Kama kuna wavutaji tumbaku kwenye kaya, wanapaswa kila mara kuvutia nje ya nyumba mbali na watoto.

Jiko lenye bomba la kutoa nje moshi litasaidia kukinga mapafu ya wasichana na wanawake ambao kawaida ndiyo wapishi wakuu wa chakula, na watoto walioko karibu nao.

Nimonia na utapiamlo

Watoto wengi ambao hufariki kutokana na nimonia huwa wana utapiamlo. Utapiamlo hudhoofisha sana miili yao kiasi cha kushindwa kupambana na maambukizi.

Mtoto mwenye utapiamlo akiombaomba mtaani

Kila mtu hupumua vizuri watoto wanapopata chakula cha kutosha chenye afya kila siku.


Kikohozi

Kikohozi cha kawaida husababishwa na mafua kiasi, na mara nyingi dawa haziwezi kusaidia. Mtulize mtoto kwa chai tamu yenye vuguvugu, mvuke, au kwa kumbeba tu na kumfanya ajisikie vizuri. Anapaswa kupata nafuu ndani ya kipindi cha wastani wa wiki 1.

Dalili za kihohozi hatari
Dalili Huenda ni...
Kukohoa kwa wiki 2 au zaidi, kupungua uzito, na homa Tuberculosis.
Angalia Matatizo ya kupumua na kukohoa (kinaandaliwa).
Kukohoa kukiambatana na kupumua haraka haraka Nimonia
Kikohozi kikavu usiku wakati mtoto haonekani kuumwa (hasa kukiwa na sauti yenye mlio kama filimbi). Athma au Pumu.

Angalia Matatizo ya kupumua na kukohoa (kinaandaliwa).

Kifua (kukohoa kwa sauti nzito)

Kukohoa kwa sauti nzito au kikohozi ambacho huchukua muda mrefu kukiwa na sauti inayokoroma kinaweza kuwa kifua. Unaweza pia kusikia mlio wenye sauti ya juu mtoto anapovuta pumzi ndani.

Kifua husababishwa na maambukizi katika njia ya hewa kooni. Dawa za antibiotiki mara nyingi hazisaidii. Kuvuta mvuke au kumtoa mtoto nje usiku ili aweze kuvuta hewa nzuri iliyopoa kunaweza kusaidia kidogo.

Wakati mwingine, koo huvimba sana kwa ndani na kusababisha mtoto kupata shida anapopumua. Sikiliza pumzi zake na mpeleke kwenye kituo cha afya iwapo unafikiri hapati hewa ya kutosha. Kuna dawa ambazo zinaweza kupunguza uvimbe.

Mtoto akikohoa kwa nguvu kiasi cha kutokwa na machozi

Kifaduro

Kifaduro huanza kama mafua – kukiwa na homa, kutokwa na kamasi laini puani na kukohoa. Baada ya wiki 1 au 2, kikohozi huongezeka. Mtu huanza kukohoa kwa milipuko ya nguvu ya ghafla ambayo haiwezi kuzuilika, ikifuatia na kukohoa mfululizo kwa muda kadhaa. Akianza kukohoa, hukohoa kwa nguvu kiasi cha kumsababishia kutapika. Baada ya milipuko ya kukohoa kwa nguvu, mtu huhangaika kupata hewa. Anapovuta hewa ndani, sauti ya mlio wa juu kama filimbi inaweza kusikika.

Kifaduro ni mateso kwa mtu yeyote, lakini ni mateso makubwa zaidi kwa watoto. Mtoto mdogo chini ya mwaka 1 anaweza kupoteza maisha kwa kukohoa mfululizo. Watoto wachanga mara nyingi hawapati kifaduro cha kawaida, hivyo inakuwa vigumu kujua kama wana maambukizi haya.

Matibabu
  • Pumzika ili usichochee kukohoa.
  • Nyonyesha zaidi au mpatie vinywaji vya ziada na chakula.
  • Kama mtoto atapoteza uzito au anaonekana kupumua kwa shida,tafuta msaada wa daktari.

Njia bora zaidi ya kuwalinda watoto dhidi ya kifaduro ni kuhakikisha wanapatiwa chanjo ya kifaduro. Angalia Chanjo (kinaandaliwa).

Kifua kikuu

Kifua kikuu huwaathiri watoto kuliko watu wazima. Kwa mtoto mwenye kikohozi ambacho kimechukua wiki 2 au zaidi, hasa kama kuna homa au kama kuna mtu yeyote kwenye kaya ambaye anaweza kuwa na kifua kikuu, angalia Matatizo ya kupumua na kukohoa (kinaandaliwa).

Sauti yenye mlio kama filimbi wakati wa kupumua

Sauti hii ya juu yenye mlio kama filimbi husikika wakati wa kupumua. Sauti hii husababishwa na mbano ndani ya mapafu au kooni na inaweza kuandamana na mafua au tatizo kubwa zaidi. Iwapo sauti hii inaendelea kujirudia tena na tena, huenda tatizo ni athma au pumu. Inaweza pia kuwa dalili ya kifua kikuu, hasa kama sauti hii inasikika zaidi upande mmoja wa kifua. Angalia Matatizo ya kupumua na kukohoa (kinaandaliwa).

Mafua

Mtoto akipiga chafya Mtoto kutokwa na kamasi laini puani, maumivu kooni, au kikohozi hutoweka iwapo atapumzika vya kutosha, kupatiwa vinywaji kwa wingi, na chakula cha kutosha. Mtoto atapata nafuu bila dawa. Dawa za antibiotiki hazina faida yoyote juu ya mafua.Mafua mara nyingine huchangia maambukizi ya sikio au koo lenye vidonda likiambatana na homa.

Maambukizi ya sikio

Iwapo mtoto mchanga au mtoto mwenye umri mkubwa zaidi atakuwa anajikuna sikio na kulia, huenda sababu ni ambukizo sikioni. Maambukizi sikioni hutokea sana miongoni mwa watoto, hasa baada ya kuugua mafua. Sehemu ya ndani ya pua imeunganishwa na sehemu ya ndani ya sikio. Hivyo ni rahisi kwa vijidudu vya magonjwa kuvuka kupita sehemu hiyo fupi inayounganisha viungo hivyo.

Dalili
  • Mtoto mwenye umri mkubwa zaidi anaweza kukuambia kwamba sikio lake linauma.
  • Mtoto mchanga hulia au hupangusa masikio yake au sehemu za pembeni kichwani.
  • Huenda kukawa na homa, ukosefu wa hamu ya kula, kupata usingizi kwa tabu, au mtoto kuonekana anahangailka kwa ujumla.
Matibabu
vipande 2 vya karafu au kitunguu swaumu kwenye jagi la mafuta

Ambukizo la sikio linaweza kuambatana na maumivu makali sana na kusababisha mtoto kulia na kutoa machozi mengi. Lakini kama mtoto ana afya na lishe nzuri, mara nyingi ambukizo hilo huweza kutoweka lenyewe. Dawa ya asetaminofeni (acetaminophen) inaweza kusaidia kupunguza maumivu.

Unaweza kujaribu karafu au kitunguu swaumu , tiba ya nyumbani ambayo pia inaweza kusaidia. Loweka vipande viwili vya karafu au kitunguu swaumu kwenye mafuta yaliyotengenezwa kutokana na mbogamboga, yakae hadi kesho yake. Halafu weka matone ya mafuta machache kwenye sikio mara kadhaa kwa siku.

Lini unapaswa kutumia antibiotiki?
Mtu akitumia karatasi iliyosokotwa kutoa usaha kutoka kwenye sikio la mvulana
Toa usaha kwa kutumia utambi wa karatasi laini au kitambaa kisafi kilichosokotwa.

Kutibu tatizo hilo kwa kutumia amoksilini au kotrimozazo (cotrimoxazole) linaweza kuwa wazo zuri kwa mtoto ambaye tayari ana hali mbaya kiafya. Watoto kama hawa hupata ugumu kupambana na maambukizi. Hivyo wanapopata maambukizi masikioni, huwa yanachukua muda mrefu kupona. Maambukizi ya sikio ambayo huchukua muda mrefu au ambayo hurudia mara kawa mara yanaweza kusababisha uziwi. Kila mara tumia antibiotiki iwapo:

  • Sikio linatoa usaha au damu.
  • Ambukizo la sikio halionyeshi dalili za kuanza kupungua baada ya siku chache.
  • Mtoto mchanga wa miezi 6 au chini ya hapo ana ambukizo.
Dalili za hatari

Tafuta msaada wa daktari kwa dalili yoyote kati ya zifuatazo:

NWTND cfc Page 19-1.png
Uviaji na uvimbe nyuma ya sikio unaweza kuwa dalili ya maambukizi hatari ya mfupa mmojawapo unaobeba sikio.
  • Maumivu kwenye mfupa nyuma ya sikio
  • Maumivu ya kichwa, kizunguzungu, au shambulio
  • Ulegevu (uchovu mkubwa au udhaifu)
  • Kupoteza uwezo wa kusikia vizuri, na uziwi
Uzuiaji

Wakati mwingine mtoto anaweza kuigiza kitu ndani ya sikio lake. Jaribu kusafisha sikio kwa kutumia bomba la sindano (bila sindano yake), iliyojazwa mchanganyiko wa maji na haidrojeni peroksaidi (hydrogen peroxide) nusu kwa nusu au siki (vinegar). Au kama utakuwa makini sana ili usijeruhi sehemu ya ndani ya sikio, unaweza kutoa kitu hicho sikioni kwa kutumia kibanio kidogo. Kinyume chake, epuka kuingiza kitu chochote kwenye sikio la mtu yeyote. Unaweza kuingiza vijidudu vya magonjwa kwenye sikio, au bila kukusudia kutoboa ngoma ya sikio. Hata mkwaruzo mdogo kwenye ngoma ya sikio unaweza kusababisha maambukizi.

Mwanamke akimnyonyesha mtoto wake

Watoto walionyonyeshwa hupata maambukizi kidogo ya sikio ukilinganisha na wale ambao hawakunyonyeshwa.


kielelezo cha vifindo ambavyo vimevimba
vifindo

Vidonda kooni

Vidonda kooni kawaida hutokana na mafua. Koo linaweza kuonekana jekundu kwa ndani na kutoa maumivu mtoto anapojaribu kumeza chakula. Vifindo (vifindo 2 ambavyo huonekana kama uvimbe katika kila upande nyuma ya koo) vinaweza kuongezeka ukubwa na kutoa maumivu au hata kujaa usaha.

Matibabu
  • Mpe juisi za matunda kwa wingi, chai na vinywaji vingine.
  • Mfundishe mtoto kusukutua kwa kutumia maji ya vuguvugu yenye chumvi. (Koroga chumvi ½ kijiko cha chai kwenye glasi ya maji).
  • Mpe parasetamo kupunguza maumivu.

Kwa koo lenye vidonda, dawa za antibotiki hazitasaidia na hazipaswi kutumika. Lakini aina moja ya vidonda vya kooni miongoni mwa watoto ambayo husababishwa na maambukizi ya bakteria ya streprotokokasi ni hatari na hupaswa kutibiwa kwa kutumia penisilini.

Dalili ya vidonda vya kooni ambavyo husababishwa na bakteria (ya streprotokokasi)
  • Uvimbe na usaha sehemu ya nyuma ya koo
  • Uvimbe au maumivu kwenye matezi shingoni na chini ya masikio
  • Homa
  • Hakuna kikohozi au kutokwa kamasi

Kama mtoto ana dalili hizi 3 au 4, huenda vidonda kwenye koo lake vimetokana na maambukizi ya bakteria za streprotokokasi. Anapaswa kutibiwa na penisilini au amoksilini ya vidonge kwa siku 10, au kupewa sindano 1 ya penisilini benzathini (benzathine penicillin). Utaratibu wa kimaabara wa kuotesha vimelea vinavyosabaisha maambukizi kooni (throat culture) ndiyo njia ya uhakika zaidi ya kujua chanzo cha vidonda vya kooni. Utaratibu huu unapaswa kutumika pale unapowezekana.

Visipotibiwa, vidonda vinavyosababishwa na bakteria kooni hugeuka kuwa ugonjwa hatari wenye maumivu makali ambao hujulikana kama homa ya rumatizimu (rheumatic fever).

Homa ya rumatizimu (rheumatic fever)

Homa ya rumatizimu hutokana na maambukizi ya bakteria kooni ambayo husababisha vidonda vikali vyenye maumivu kooni. Tatizo hili huwaathiri sana watoto wenye umri kati ya miaka 5 na 15. Kama mtoto ana baadhi ya dalili zifuatazo wiki 2 hadi 3 baada ya kuugua vidonda kooni, homa ya rumatizimu huenda ndiyo kisababishi:

  • Maumivu kwenye maungio, hasa kwenye kifundo cha mkono na kifundo cha mguu
  • Maungio yaliyovimba, yakiwa yamegeuka kuwa na rangi nyekundu na joto kali
  • Homa
  • Vipele vidogovidogo vyenye muundo wa nusu mduara au mduara kamili, au uvimbe chini ya ngozi, kwenye mikono, au miguuni, lakini siyo usoni
  • Kushindwa kudhibiti mwenendo wa sehemu mbalimbali mwilini ukiwemo uso miguu, au mikono
  • Udhaifu mwilini, pumzi fupifupi, maumivu ya kifua

Mtoto akiwa amevimba maungio ambayo yanatoa joto kali

Kama unafikiri mtoto ana homa ya rumatizimu, mpe penisilini kutibu maambukizi. Tafuta msaada wa daktari. Homa ya rumatizimu inaweza kuharibu na kudhoofisha moyo. Tatizo hili hujulikana kama rumatizimu ya moyo (rheumatic heart disease) na unaweza kumsababishia mgonjwa ulemavu na hata kifo kabla ya muda wake.

Mtoto akiwa amefungua wazi kinywa chake

Dondakoo

Dondakoo ni ugonjwa hatari sana ambao huanza na vidonda au maumivu kooni na homa ya kiasi. Baada ya siku chache,utando wa kijivu au mweupe unaweza kuonekana sehemu ya nyuma ya koo. Mara nyingi, sauti ya mtoto hubadilika, shingo huvimba,na pumzi yake hutoa harufu mbaya. Uvimbe na utando wa kijivu au mweupe unaweza kufanya upumuaji kuwa mgumu au kushindikana.

Matibabu
  • Tafuta msaada wa daktari. Dawa za kupambana na sumu inayotokana na maambukizi zinaweza kusaidia.
  • Mpe erithromaisini au penisilini.
  • Sukutua maji ya vuguvugu yaliyochanganywa na chumvi kidogo.
  • Vuta pumzi ya mvuke ili kurahihisha upumuaji.

Kama utando sehemu ya nyuma ya koo utazidi kuongezeka kiasi kwamba mtoto anaanza kupata shida katika kupumua,uondoe kwa kutumia kitambaa kisafi.

Dondakoo huzuilika kwa urahisi kwa chanjo ya DPT. Hakikisha watoto wako wanapata chanjo hiyo dhidi ya dondakoo.

Surua

Mtoto akiwa na upele mdogomdogo usoni na kifuani

Dalili za kwanza za surua ni homa, kamasi laini, macho mekundu na yenye maumivu, na kikohozi. Dalili hizi huanza wastani siku 10 baada ya kuwa karibu na mtu ambaye anaugua surua. Kinachofuata ni vidonda mdomoni na kuharisha. Mwisho, upele huonekana nyuma ya masikio na kwenye shingo, na kusambaa hadi usoni na mwilini, na baada ya hapo mikononi na miguuni.

Matibabu

Mtoto mwenye surua anaweza kupata nafuu ndani ya siku 5 hadi 10 kama utamsaidia kunywa, kula na kupumzika:

  • Mpe vinywaji kwa wingi. Kama anaharisha au ana dalili yoyote ya kupungukiwa na maji mwilini, mpe kinywaji maalum cha kumuongezea maji.
  • Endelea kunyonyesha kama bado yuko katika umri wa kunyonya. Muwezeshe kunywa kila mara na kadri atakavyotaka. Kama atapata shida kunyonya mwenyewe, mpe maziwa ya mama yaliokamuliwa kwa kutumia kijiko.
  • Mpatie vyakula vidogovidogo mara nyingi kila siku. Kama ana matatizo ya kumeza matonge ya chakula, jaribu supu mbalimbali, uji na juisi za matunda.
  • Mpe parasetamo au ibrofeni (ibuprofen) kupunguza maumivu na homa.
  • Mpe vidonge vya vitamini A.


Hatari kubwa kutokana na surua ni kwamba inaweza kuchangia maambukizi ya magonjwa mengine ambayo ni hatari zaidi. Hii ni kawaida kwa watoto ambao wana lishe duni au wanaumwa kutokana na VVU au ugonjwa mwingine. Kuwa mwangalifu kwa matatizo yafuatayo na kuyatibu haraka:

  • Kuharisha: Tibu kwa kutumia kinywaji maalum cha kuongeza maji mwilini. Tafuta msaada zaidi iwapo mtoto hatapata nafuu ndani ya siku 1 au 2.
  • Ambukizo la sikio: Ambukizo la sikio kutokana na surua linaweza kusababisha uziwi. Tibu mara moja maumivu yoyote ya sikio na amoksilini na kotrimozazo (cotrimoxazole).
  • Uoni hafifu: Surua inaweza kuchangia upofu. Zuia tatizo hili kwa kuwapa watoto wote wenye surua vitamini A.
  • Nimonia au kichomi: Kama mtoto ana surua, anapumua haraka kuliko kawaida, au kama anapata shida kupumua, mtibu kwa ajili ya nimonia.
  • Homa ya uti wa mgongo: Tafuta msaada wa daktari kama mtoto ataonekana kuchanganyikiwa, ana maumivu makali ya kichwa, anapata shambulio, au anapoteza ufahamu. Bonyeza hapa kwa taarifa zaidi juu ya Homa ya uti wa mgongo.
Uzuiaji

Watoto wote wanapaswa kuchanjwa dhidi ya surua. Angalia Chanjo (kinaandaliwa). Kama mtoto mmoja atapata surua, unaweza kuwakinga watoto wengine katika familia au shuleni iwapo watapatiwa chanjo haraka. Hakikisha mtoto mwenye surua anabaki nyumbani na, ikiwezekana, mbali na dada na kaka zake ambao hawajambukizwa. Hata hivyo, ndugu zake hao nao wanaweza kuwa tayari wameambukizwa hata kama wanakuwa bado hawajaanza kuonesha dalili za surua. Hivyo, ni bora zaidi nao wakabaki nyumbani hadi itakapothibitika kuwa wote ni salama. Hii itasaidia kuzuia maambukizi kuenea katika jamii. Unaweza kupata maambukizi ya surua mara moja tu katika maisha, baada ya hapo unakuwa na kinga.

Surua aina ya Rubella

Mwanamke mjamzito akijaribu kumhimiza mama mwenye mtoto ambaye anaonekana kuwa na upele kukaa mbali
Rubella husababisha madhara makubwa kwa mtoto aliye tumboni mwa mama yake. Wanawake wajawazito wanapaswa kukaa mbali sana na watoto ambao wanaugua rubella.
Dalili
  • Homa ya wastani, chini ya nyuzijoto 38.3° sentigredi au nyuzijoto 100° farenheiti.
  • Upele kiasi ambao huanzia usoni na kuenea mwili mzima.
  • Matezi ya limfu (lymph nodes) nyuma ya masikio na nyuma ya shingo na kichwa kuvimba.

Miongoni mwa watoto na vijana ,madhara ya rubella ni nafuu yakilinganishwa na ya surua. Rubella hupungua yenyewe baada ya siku 3 au 4.

Kwa wanawake, rubella inaweza kusababisha vidonda kwenye magoti, kifundo cha mkono,na kwenye vidole.

Njia pekee ya uhakika ya kumlinda mwanamke mjamzito dhidi ya rubella ni kuwapatia chanjo watoto wote kwenye jamii.


Tetekuwanga

Tetekuwanga husababisha homa isiyo kali, na madoa yenye wekundu yanayowasha. Madoa hayo kawaida huanzia sehemu kuu ya mwili na kuenea usoni, mikononi, na miguuni. Baadaye hugeuka kuwa vipele au viuvimbe vyenye maji maji ambavyo hutoweka ghafla na kuacha mabaka ya vidonda. Tetekuwanga kawaida huondoka baada ya wiki 1. Lakini ukunaji wa vipele hivyo huruhusu vijidudu na uchafu kuingia chini ya ngozi na kuweza kusababisha maambukizi kwenye ngozi.

Vuta mawazo ya mtoto aache kujikuna sana. Tunza kucha zake zikiwa fupi na usafi wa mikono yake. Au mvalishe glovu au soksi mikononi. Punguza muwasho kwa kutumia kitambaa kilicholowekwa kwenye mchanganyiko uliopikwa wa unga wa shayiri na maji. Dawa ya kupambana na mzio kama vile krofeniramin (chlorpheniramine) inaweza pia kusaidia kutuliza muwasho.

Tetekuwanga inaweza kuzuilika kwa chanjo (angalia Chanjo - kinaandaliwa). Kama ulipata chanjo hiyo au umewahi kuugua ugonjwa wa tetekuwanga,ugonjwa huo hauwezi kukupata tena.

Ukurutu

Ukurutu hutokana na maambukizi ya bakteria na kusababisha upele unowasha ubavuni, viganjani, mikononi, miguuni, au kwenye uume. Ugonjwa huu huwapata sana watoto. Kwa taarifa zaidi juu ya Ukurutu na magonjwa mengine ya ngozi angalia Ngozi, kucha, na matatizo ya nywele (kinaadaliwa).

Matumbwitumbwi (Mumps)

Mtoto mwenye uvimbe kwenye taya lake upande mmoja wa uso.

Ugonjwa huu huanza na homa, kuchokachoka, maumivu ya kichwa, au na kupoteza hamu ya kula. Maumivu yanaweza kutokea unapofungua mdomo wako au kula. Ndani ya siku 2, uvimbe laini hujitokeza chini ya masikio kwenye pembe la taya. Uvimbe unaweza kuanzia upande mmoja na baada ya hapo kuenea upande wa pili.

Matumbwitumbwi hutoweka bila tiba baada ya wastani wa siku 10. Iwapo uvimbe hautatoweka, huenda kukawa na tatizo lingine. Utapiamlo na VVU (angalia VVU na UKIMWI - kinaadaliwa) pia vinaweza kusababisha uvimbe wa tezi za limfu chini ya masikio, unaofanana na matumbwitumbwi ambao huchukua muda mrefu.

Kwa nadra,maambukizi ya matumbwitumbwi huenea hadi kwenye masikio na ubongo. Tafuta msaada wa daktari mara moja iwapo mtu mwenye ugonjwa wa matumbwitumbwi ataonesha dalili za ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo au matatizo ya usikivu.

Matumbwitumbwi yanaweza kuzuiwa kwa chanjo (angalia Chanjo -kinaadaliwa).

Polio

Mtoto akiwa na magogo 2 ya kutembelea

Polio ni ugonjwa hatari. Huanza kama mafua, kukiwa na homa,kuharisha,kutapika, na maumivu ya misuli. Kawaida mtoto hupata nafuu haraka. Lakini kwa baadhi ya watoto, polio huathiri misuli.

Watoto hao huanza kudhoofu, kawaida katika mguu mmoja. Wakati mwingine mguu hupooza. Ukibaki katika hali ya kupooza, utakuwa mwembamba na mdogo, wakati mguu mwingine ukiendelea kuongezeka. Iwapo utaona mtoto anapata shida kutembeza mwili wake au sehemu ya mwili (kupooza), tafuta msaada wa daktari mara moja.

Polio inauma sana. Dawa ya asetaminofeni (acetaminophen) au ibrofeni (ibuprofen) inaweza kusaidia. Pia kuloweka mkono au mguu husika kwenye maji ya moto pia huweza kusaidia. Mazoezi ya mara kwa mara ya kiungo husika ni muhimu na hupunguza madhara ya kupooza kutokana na ugonjwa huu. Angalia Sura ya 7 kuhusu Watoto wenye Ulemavu Vijijini.

Uzuiaji

Chanja watoto wote dhidi ya polio. Kampeni za chanjo zimefanikiwa sana kiasi cha kuitokomeza polio katika maeneo mengi ya dunia. Iwapo watoto wote watachanjwa,ugonjwa wa polio utatokomea kabisa.

VVU na UKIMWI

VVU hudhoofisha kinga za mwili dhidi ya magonjwa, na kurahihisha uvamizi wa magonjwa mbalimbali yakiwemo nimonia (kichomi), kifua kikuu,na kuhara. Ni muhimu kuchunguza mapema haraka iwezekanavyo iwapo mtoto ana VVU.

Iwapo jibu lako ni “ndiyo” kwa swali lolote kati ya haya yafuatayo,tafadhali soma VVU na UKIMWI (kinaadaliwa).

  • Maambukizi ya VVU ni tatizo la kawaida mahali unapoishi?
  • Wewe ni baba au mama na unaweza kuwa na VVU?
  • Unamhudumia mama mjamzito ambaye anaweza kuwa na VVU?
  • Unamhudumia mtoto ambaye anaweza kuwa na VVU?
  • Unamhudumia mtoto mdogo ambaye ukuaji wake unasuasua na huugua zaidi kuliko watoto wengine?

Dawa za kupunguza makali ya VVU zinaweza kumsaidia mtoto mwenye VVU kuishi maisha marefu na yenye afya.