Hesperian Health Guides
Vitamini na viongeza madini mwilini (mineral supplements)
HealthWiki > Toleo Jipya: Mahali Pasipo na Daktari > Kuwatunza watoto > Vitamini na viongeza madini mwilini
Vitamini A, retino (retinol)
Kuzuia uoni hafifu wa usiku na zerofthalmia
Katika maeneo ambapo matatizo ya uoni hafifu usiku na zerofthalmia (kukauka na kuongezeka ukubwa wa konea) yameenea sana, watu wanahitaji zaidi matunda ya njano na mbogamboga za kijani, pamoja na vyakula kutokana na wanyama kama vile mayai na maini. Kwa kuwa vyakula hivyo mara nyingi havipatikani – angalau kwa muda mfupi–ni bora kuwapatia watoto na mama zao matone ya vitamini A mwilini kila baada ya miezi 6.
Kawaida huwezi kupata Vitamini A inayozidi kiwango ambacho mwili unahitaji kutoka kwenye chakula. Lakini kuzidisha vidonge vya vitamini au mafuta ni hatari. Usitumie zaidi ya kiwango ambacho kimependekezwa.
Kwa watoto wadogo, unaweza kusaga vidonge na kuchanganya unga na maziwa kidogo ya mama. Au kata kidonge aina ya kapsuli na kukamulia majimaji yaliyomo mdomoni mwa mtoto.
Kuzuia upungufu wa vitamin A mwiliniZaidi ya mwaka 1: toa uniti 200,000 kwa mdomo mara moja. Rudia baada ya miezi 6.
Kwa akina mama: toa uniti 200,000 kwa mdomo ndani ya wiki 6 baada ya kujifungua. Vitamini A itamkinga mama na pia kumfikia mtoto kupitia maziwa ya mama.
Vitamini A huzuia nimonia na upofu, matatizo 2 ya kawaida yanayohusiana na surua.
Zaidi ya mwaka 1: toa uniti 200,000 kwa njia ya mdomo, mara 1 kila siku kwa siku 2. (Kama mtoto alipata dozi ya vitamini A katika miezi 6 iliyopita, mpe dozi hii kwa siku 1 tu.)
Iwapo mlengwa ana hali mbaya sana ya lishe au tayari ameanza kupoteza uwezo wake wa kuona, rudia dozi ya vitamini A baada ya wiki 2.
Zinki (Zinc)
Madini ya zinki husaidia watoto wanaoharisha kupata nafuu haraka. Madini hayo yanapaswa kutolewa pamoja na kinywaji cha kuongeza maji mwilini.
Zaidi ya miezi 6: toa miligramu 20, mara 1 kila siku kwa siku 10 hadi 14.
Madini ya chuma, ferasi salfeti, ferasi glukoneti (iron, ferrous sulfate, ferrous gluconate)
Vyongeza madini ya chuma husaidia katika kutibu au kuzuia matukio mengi ya upungufu wa wekundu wa damu mwilini. Matibabu kwa kutumia vyongeza madini ya chuma kawaida huchukua angalau miezi 3.
Vyongeza madini ya chuma hufanya kazi vizuri vinapotumiwa pamoja na vitamini C (aidha kwa kula matunda na mbogamboga, au kutumia kidonge cha vitamini C).
Vyongeza madini ya chuma wakati mwingine huvuruga tumbo na ni bora kutumiwa na chakula. Vilevile, vinaweza kusababisha shida katika kupata choo hasa kwa watu wazima, na kufanya kinyesi kuonekana cheusi.
Kunywa viongeza madini ya chuma vinavyomiminika huyafanya meno kuonekana meusi. Kunywa kwa kutumia mrija au piga meno mswaki baada yakunywa.
Hakikisha dozi ni sahihi. Ukizidisha hugeuka sumu. Usitoe viongeza madini ya chuma kwa watu walioathirika sana kilishe. Subiri hadi afya zao zirudi ndipo uwape madini ya chuma.
Miundo tofauti ya viongeza madini ya chuma huwa na ujazo tofauti wa madini hayo. Kwa mfano, kidonge cha ferasi salfeti chenye miligramu 300 huwa na miligramu 60 za madini ya chuma. Lakini kidonge cha ferasi glukoneti chenye miligramu 325 huwa na miligramu 36 za madini ya chuma. Hivyo, soma maelekezo kwenye kifungashio cha vidonge vyako, chupa ya dawa (au karatasi ya taarifa juu ya dawa), au taarifa juu ya viongeza madini ya chuma vingine kujua kiwango cha madini ya chuma kilichomo.
KUZUIA upungufu wa wekundu wa damu (anemia) miongoni mwa akina mama wajawazito na wanaonyonyeshaDOZI YA FERASI SALFETI KWA UMRI | |||
KUNDI LA UMRI | KIASI GANI KATIKA KILA DOZI | VIDONGE VYA MILIGRAMU 300 VINGAPI | JUMLA YA MADINI YA CHUMA |
Chini ya miaka 2 | Miligramu 125 za ferasi salfeti | Tumia sairapu ya madini ya chuma, au saga ¼ kidonge cha ferasi salfeti chenye miligramu 300 kwenye maziwa ya mama | Toa kiasi cha kutosha kutoa miligramu 25 za madini ya chuma |
Miaka 2 hadi 12 | Miligramu 300 za ferasi salfeti | Kidonge 1 cha ferasi salfeti chenye miligramu 300 | Toa kiasi cha kutosha kutoa miligramu 60 za madini ya chuma |
Zaidi ya miaka 12 | Miligramu 600 za ferasi salfeti | Vidonge 2 vya ferasi salfeti vyenye miligramu 300 | Toa kiasi cha kutosha kutoa miligramu 120 za madini ya chuma |