Hesperian Health Guides

Kuwatunza watoto

Katika sura hii:

Mtoto akila kwa furaha
Mtoto akioga
Mtoto akipewa chanjo
Ckakula chenye virutubishi,usafi wa mwili na mazingira, na chanjo dhidi ya magonjwa ya kawaida kwa watoto ni kama walinzi ambao huwalinda watoto dhidi ya maambukizi na kuwaweka katika hali nzuri ya kiafya.

Wazazi na wafanyakazi wa afya wanaweza kujifunza zaidi juu ya lishe kutoka Lishe bora hutengeneza afya bora, usafi wa mwili na mazingira kutoka Maji na usafi wa mazingira: Funguo za kudumishaji afya, na kuhusu chanjo mbalimbali kutoka Chanjo (kinaandaliwa) ili kuzuia idadi kubwa ya magonjwa miongoni mwa watoto.

Hasa kwa watoto, punje 1 ya kinga ni muhimu zaidi kuliko punje 12 za tiba.


Chakula chenye virutubishi

Chakula cha kutosha chenye virutubishi ndiyo ufunguo kwa ukuaji na afya ya mtoto. Lishe bora hutengeneza afya bora kinahusu jinsi gani wewe na watoto wako mnaweza kupata lishe bora, hata kama uwezo wenu wa kifedha ni mdogo. Pia kinaelezea matibabu ya utapiamlo miongoni mwa watoto na watu wazima. Unaweza kuwapatia watoto wachanga na watoto wengine vyakula bora zaidi kwa kuzingatia mwongozo ufuatao:

Mama akimnyonyesha mtoto wake

Kwa miezi 6 ya kwanza

Maziwa ya mama yana kila kitu ambacho mtoto mchanga anahitaji na yanapaswa kutolewa kila mara mtoto atakapohitaji kunyonya: kila saa 3 au 4 wakati wa mchana, na mara chache kidogo wakati wa usiku. Usimpe mtoto mchanga maji, juisi au uji hadi atakapoota meno ya kwanza ambayo huota anapofikisha wastani wa miezi 6. Vinywaji hivi vinaweza kusababisha watoto wadogo kuharisha.

Bonyeza hapa kwa taarifa zaidi juu ya unyonyeshaji.

Kuanzia miezi 6 hadi 12 (mwaka 1)

Huu ni umri ambapo watoto wengi huanza kuugua kutokana na lishe duni. Ili kulinda afya ya mtoto, endelea kumpatia maziwa ya mama, na pia kuanza kumpatia vyakula vinavyofaa kulikiza mara kadhaa kwa siku. Anza na chakula cha aina 1 au 2, kama vile uji wa kawaida au chakula kikuu cha kawaida cha familia, kikiwa na mafuta kidogo au mafuta ya kuongezea.

Mama akimsaidia mtoto wake kula vipande vidogo vidogo vya ndizi.

Baada ya muda mfupi, muongezee vyakula vingine vyenye virutubishi, vikiwemo:

  • Vyakula vyenye protini mara moja kwa siku au zaidi: maharagwe yaliyopikwa vizuri yakalainika au mlo wa maharagwe yaliyosagwa, mayai, bidhaa za maziwa au nyama ya samaki iliyopikwa na kupondwapondwa.
  • Mbogamboga: mbogamboga zilizopikwa vizuri zikiwemo boga, njegere, karoti, mboga za kijani, nyanya, au vyakula vyote vyenye rangi ya chungwa au kijani ambavyo huliwa sehemu unayoishi.
  • Matunda: vipande vidogo vya matunda kama vile embe, papai,ndizi, au zabibu.

Baada ya mwaka wa kwanza

Endelea kunyonyesha kwa miaka 2 au zaidi.

mtoto mdogo akila chakula kutoka kwenye bakuli kwa kutumia kijiko

Pia mpatie vyakula vyenye virutubishi mbalimbali ambavyo mtu mzima anapaswa kula: wanga, protini, mbogamboga na matunda. Watoto wanapaswa kula angalau mara 4 au zaidi kwa siku. Wanahitaji hata kula zaidi hasa kwa sababu hawanyonyeshwi tena.

Wasichana wanahitaji chakula cha kutosha sawa na wavulana. Wasichana na wavulana ambao hupata chakula cha kutosha chenye virutubishi hukua wakiwa wenye afya nzuri. Chakula husaidia pia akili kukua-ili mtoto aweze kufikiri, kujifunza na kucheza.

Watoto wanapaswa kuwa kama kuku: kudonoadonoa wakati wote.


NWTND cfc Page 3-3a.png

Chupa

Chupa na chuchu za mpira siyo salama kwa sababu ya ugumu wa kuvitunza katika hali ya usafi unaohitajika. Kawaida hubeba vijidudu vya magonjwa ambavyo husababisha kuharisha. Iwapo unataka kumlisha mtoto kama mama yake amekwenda kazini, kwa mfano, mpatie maziwa ya mama yaliyokamuliwa na kuhifadhiwa vizuri kwa kutumia kikombe na kijiko kisafi. Watoto wachanga na wengine wanaowazidi kamwe wasitumie chupa. Kitendo cha kuwapatia watoto wakubwa zaidi juisi, uji, au maziwa kwenye chupa huloweka meno yao laini kwenye sukari kwa muda mrefu sana na ni chanzo cha kawaida cha meno kuoza (kuwa na vijishimo). Watoto wanaweza kujifunza kwa urahisi kunywa kwa kutumia vikombe.

Vyakula vinavyotamaanisha lakini vyenye virutubishi kidogo (junk food)

Cola, chipsi na vitu vitafunwa vilivyokolezwa sukari havistahili

Keki, vitu vitamu vya kumumunya vyenye asili ya pipi au peremende, chipsi, soda, na baadhi ya vyakula ambavyo husindikwa viwandani vina faida ndogo kilishe. Hukolezwa sukari kupita kiasi, chumvi, mafuta, na kemikali, badala ya virutubishi vya kutosha. Kula sana vyakula hivyo husababisha meno kuoza na huchangia shinikizo kubwa la damu, ugonjwa wa kisukari, na matatizo mengine ya kiafya baadaye katika maisha.

Iwapo vinapatikana kwa urahisi, watoto wanaweza kudai wapatiwe vyakula hivyo kutokana na ladha yake nzuri. Tukiwa wazazi na wafanyakazi wa afya, ni wajibu wetu kuwalinda watoto wasijenge tabia ya kula vyakula hivyo.

Mtoto akiomba chakula, mpatie matunda ambayo hayajakaa muda mrefu tangu yavunwe kutoka shambani, vitu vyenye asili ya karanga, maziwa ya mtindi, uji, au kitu kingine chochote chenye virutubishi ambacho hakijaongezewa sukari. Wafundishe watoto kuwa vyakula vya kawaida (au vya asili) vyenye virutubishi pia ni vitamu. Tabia ya kula vyakula vyenye afya zitawasaidia watoto kwa maisha yao yote.

Watoto hukua vizuri wakiwa na afya na nguvu kwa kula vyakula halisi —siyo vyakula vinavyotamaanisha lakini vyenye virutubishi kidogo (junk food).


Msichana akinawa mikono kwenye kibeseni na sabuni

Usafi wa mwili na mazingira

Wanawishe watoto mikono kabla ya kula na mara kadhaa kila siku. Matatizo ya kuharisha, homa, mafua na magonjwa mengine husababishwa na vijidudu ambavyo husambazwa kutoka kwenye mikono ya mtoto hadi mdomoni (na watoto kawaida huingiza sehemu ya mikono yao mdomoni !). Kunawa mikono huzuia vijidudu ambavyo vimejikusanya mikononi kuingia mdomoni na kusababisha magonjwa. Kunawa husaidia kulinda afya ya watoto.

Kukata kucha

Waogeshe watoto kila siku. Tunza kucha zao zikiwa fupi ili uchafu usijikusanye chini yake.

Watoto na watu wazima wanahitaji sehemu safi na salama kwa ajili ya kujisaidia kila siku. Bila hivyo, vinyesi na vijidudu vya magonjwa ndani yake vitasambaa kila mahali. Kwa kujenga vyoo kwa ajili ya familia yako au na majirani zako au jamii yako, utakuwa umesaidia kuzuia ugonjwa wa kuhara. Maji na usafi wa mazingira: Funguo za udumishaji afya kimebeba mapendekezo mengi ya kina kwa ajili ya kuboresha usafi wa mazingira na kuzuia kuharisha miongoni mwa watoto.

Chanjo na madawa

Chanjo husaidia kuwakinga watoto dhidi ya magonjwa mengi hatari ya utotoni kama vile surua, pepopunda (tetanasi), polio, na kifua kikuu. Kutoa chanjo ni rahisi zaidi, gharama yake ni nafuu na matokeo yake ni zaidi kuliko jitihada zozote za kumsaidia mtoto ambaye tayari anaugua au anakaribia kufa. Kuwapatia chanjo watoto ni miongoni mwa njia muhimu zaidi za kulinda afya zao.

Angalia Chanjo (kinaandaliwa) kwa ajili ya orodha ya chanjo muhimu na ratiba ya utoaji wa chanjo hizo.

Hakikisha watoto wako wanapata chanjo zote za msingi.


Mvulana akimsaidia mdogo wake kupiga mswaki

Njia zingine za kulinda afya ya watoto

  • Linda meno ya watoto kwa kupiga mswaki. Usiwape vitu vingi vya kula au kumumunya, pipi, au vinywaji vilivyokolezwa sukari. Bonyeza hapa kwa ajili ya taarifa zaidi juu ya vyakula vinavyotamanisha lakini vyenye virutubishi kidogo (Junk food).
  • Nyonyesha. Unapompatia vyakula vingine na vinywaji, tumia kikombe au kijiko kisafi, siyo chupa na chuchu za mpira ambavyo ni vigumu kutakaswa wakati wote.
  • Usiruhusu watoto wagonjwa au wenye vidonda,upele au ukurutu, chawa, au mba kulala kitanda kimoja au kushirikiana nguo au taulo na watoto wengine. Watibu watoto hao haraka kwa sababu maambukizi hayo husambaa kwa urahisi kutoka mtoto mmoja hadi mwingine.
Watoto wakiwa wamelala kwenye kitanda chenye kiandarua cha kuzuia mbu
  • Tumia kiandarua kuzuia mbu. Ondoa vidimbwi au maji mengine yote ambayo hayatembei ili mbu wasiweze kuzaliana. Weka wavu kwenye milango na madirisha yanayobaki wazi muda mrefu.
  • Usiruhusu nguruwe, mbwa na kuku -na vijidudu waliowabeba – kuingia ndani ya nyumba.
Sw NWTND cfc Page 5-3.png
Ndiyo
Hapana
  • Kama kuna minyoo, mpe dawa ya kutibu minyoo kila baada ya miezi 3 hadi 6, kuanzia anapofikisha umri wa mwaka 1.
  • Ili kujikinga na maambukizi ya minyoo ya safura, watoto wanapaswa kuvaa viatu au ndara na wasitembee pekupeku.