Hesperian Health Guides
Majeraha na ajali
Majeraha ya kawaida kwa watoto mara nyingi yanaweza kuzuilika.
Yaliyomo
Kukabwa au kupaliwa
Kukabwa ni tatizo hatari kwa watoto chini ya miaka 2. Kama mtoto atakuwa anakohoa au anaweza kutoa sauti, angalia kwa karibu iwapo atakohoa nje kile alichomeza. Kama mtoto hawezi kukohoa au kutoa sauti, haraka mpigepige mgongoni polepole na kubonyeza mara kadhaa kifuani kwa kutumia kiganja cha mkono wako. Au kwa mtoto wa mwaka 1, bonyeza mara kadhaa tumboni kulazimisha kukitoa. Angalia Huduma ya kwanza.
Vipande vya chakula vyenye umbo la mduara ndiyo chanzo kikuu cha matukio ya kukabwa kwa watoto wadogo. Epuka kuwapa watoto vitu vigumu vyenye utamu wa sukari, nafaka, punje kubwa,vipande vinene vya nyama au jibini, au vya mbogamboga mbichi. Chakula cha watoto wadogo kinakuwa salama zaidi kinapopikwa vizuri na kusagwa au kukatwakatwa katika vipande vidogo.
Kula sumu
Sumu zote, vikiwemo viuatilifu, na dawa za kufanyia usafi nyumbani zinapaswa kuwekwa juu kwenye shelfu au kufungiwa kwenye kabati. Kwa taarifa zaidi juu ya kushughulikia matukio mbalimbali ya sumu, angalia Huduma ya kwanza.
Kuzama
Mtoto anaweza kuzama katika bwawa, shimo la maji machafu, au hata kwenye ndoo iliyojaa maji. Watoto wadogo wanapaswa kuangaliwa kwa karibu wanapokuwa karibu na maji. Watoto wenye umri mkubwa zaidi , hasa wakiume, mara nyingi huzama kwa sababu ya kutochukua tahadhari wanapokua wanaogelea kwenye maji yenye mawimbi makali au yenye kina kirefu. Kuhakikisha usalama wa njia zinazopakana na maji na kupita juu ya madaraja, na kuwafundisha watoto wote kuogelea, ni muhimu katika kuilinda jamii.
Kuungua
Ajali za kuungua zinaweza kuzuiwa kwa kuwaweka watoto mbali na majiko, sehemu zenye joto kali na sufuria na vifaa vingine vya kupikia, moto,na taa. Lakini majeraha ya moto yanapotokea, ni muhimu kuyatibu haraka, kupunguza maumivu na kuzuia maambukizi, ambayo yanaweza kuwa makali baada ya kungua. Baadhi ya majeraha ya moto hayaumi sana kwa sababu neva ndani ya ngozi zinakuwa zimeathirika. Hata bila maumivu, majeraha hayo yanapaswa kutibiwa. Kuhusu jinsi ya kuyatibu, angalia Huduma ya kwanza.
Ajali za vyombo vya usafiri
Helmeti pamoja na mikanda ya kujifunga kwenye viti vinaweza kuzuia majeraha mengi na vifo kutokana na ajali za baisikeli, na magari. Kwa kuzifanya barabara kuwa salama kwa watembea kwa miguu na waendesha baisikeli, majeraha mengi zaidi na vifo vinaweza kuepukika.
Vurugu
Vurugu na unyanyasaji wa watoto ni tatizo kubwa lililoenea sana na lenye uwezo wa kusababisha madhara ya kudumu kwa mtoto-siyo tu kimwili , lakini pia kwenye fikra na moyo wa mtoto. Ni wajibu wa watu wazima wote kuwalinda watoto dhidi ya unyanyasaji. Ili kujifunza jinsi ya kutambua dalili za unyanyasaji na kupata taarifa zaidi juu ya swala hili gumu, soma Vurugu (kinaandaliwa).