Hesperian Health Guides
Dawa za minyoo
Dawa tu hazitoshi kuondoa minyoo mwilini au kudhibiti maambukizi yake kwa muda mrefu. Usafi wa mtu binafsi na jamii kwa ujumla pia unahitajika. Maambukizi ya minyoo yanaweza kuenea kwa urahisi miongoni mwa wanafamilia. Hivyo mwanafamilia 1 anapokuwa na minyoo, ni muhimu kutibu familia nzima.
Yaliyomo
Mebendazo
Mebendazo hufanya kazi dhidi ya safura, askarisi, trikurisi (trichuris au whipworm), na mchangouzi (pinworm au threadworm). Pia husaidia dhidi ya trikinosisi (trichinosis) lakini siyo sana. Ingawa kawaida haina madhara ya pembeni, mara chache huenda kukawa na maumivu tumboni au kuharisha iwapo mgonjwa ana minyoo mingi mwilini.
Epuka mebendazo wakati wa miezi 3 ya kwanza ya ujauzito kwa sababu inaweza kumuathiri mtoto aliyeko tumboni. Usitoe kwa mtoto mwenye umri chini ya mwaka 1.
toa kidonge 1 cha miligramu 500, mara 1 tu.
Albendazo
Albendazo inafanana na mebendazo, lakini huwa ni ghali zaidi. Hufanya kazi dhidi ya safura, askarisi, trikinosisi, mchangouzi (pinworm au threadworm), na aina nyingine ya michango -strongloidi (strongyloides). Madhara ya pembeni ni nadra sana.
Epuka albendazo katika miezi 3 ya kwanza ya ujauzito kwani inaweza kumuathiri mtoto aliyeko tumboni. Usitoe kwa watoto chini ya mwaka 1.
Zaidi ya miaka 2: toa miligramu 400, mara 1. Rudia ndani ya wiki 2 kama itahitajika.
Pamoti, pamoti pirante (Pyrantel pamoate), Epirante emboneti (pyrantel embonate)
Pirante (pyrantel) hufanya kazi dhidi ya mchangouzi,safura,na askarisi, lakini inaweza kuwa ghali. Mara chache husababisha kutapika, kizungunguzungu, au maumivu ya kichwa. Usitoe kwa mtu yeyote ambaye pia anatumia piperazini (piperazine)- dawa nyingine ya minyoo.
Kwa ajili ya mchangouzi: toa dozi 1, subiri wiki 2, halafu toa dozi nyingine.
Chini ya miaka 2: toa miligramu 62 (¼ ya kidonge cha miligramu 250).
Miaka 2 hadi 5: toa miligramu 125 (½ kidonge cha miligramu 250).
Miaka 6 hadi 9: toa miligramu 250 (kidonge 1 cha miligramu 250).
Miaka 10 hadi 14: toa miligramu 500 (vidonge 2 vya miligramu 250).
Zaidi ya miaka 14: toa miligramu 750 (vidonge 3 vya miligramu 250).
Kwa ajili ya Tegu (tape worm)
Kuna aina kadhaa za tegu. Dawa ya prazikante (Praziquantel) au niklosamidi (niclosamide) kutibu aina zote 2. Kama maambukizi ya tegu yamefika kwenye ubongo au yanasababisha mashambulio, mgonjwa atahitaji kupewa albendazo na dawa za kupambana na mashambulio, na anapaswa kupata msaada haraka.
Prazikante (Praziquantel)
Prazikante inaweza kusababisha uchovu, kizunguzungu, maumivu ya kichwa, hamu ya kula kupungua, na kichefuchefu. Lakini madhara ya pembeni hayo ni nadra kama dozi ndogo itatumika kutibu tegu.
Miaka 4 hadi 7: toa miligramu 150 (¼ kidonge), mara 1 tu.
Miaka 8 hadi 12: toa miligramu 300, mara 1 tu.
Zaidi ya miaka 12: toa miligramu 600, mara 1 tu.
Kwa ajili ya tegu dogo (dwarf tapeworm au H. nana)
Miaka 4 hadi 7: toa miligramu 300 hadi 600 (½ kidonge hadi kidonge 1) kwa dozi.
Miaka 8 hadi 12: toa miligramu 600 hadi 1200 kwa dozi.
Zaidi ya miaka 12 : toa miligramu 1500 kwa dozi.
Niklosamidi (Niclosamide)
Niklosamidi hupambana na tegu waliopo kwenye matumbo, lakini siyo vifuko vya mayai ya tegu nje ya matumbo.
Tumia niklosamidi baada ya chakula kidogo cha asubuhi. Vidonge vinapaswa kutafunwa vizuri na kumezwa. Dozi inaweza kutofautiana kutegemea aina ya tegu. Hivyo mtaalam wa afya karibu nawe anaweza kutoa pendekezo zuri. Kama sivyo, tumia dozi ifuatayo: Tafuna vizuri na kumeza dozi zifuatazo. Kama ni mtoto mdogo ambaye hawezi kutafuna, saga kidonge na kuchanganya na maziwa ya mama kidogo au chakula.
Miaka 2 hadi 6: toa gramu 1 (miligramu 1000), mara 1 tu.
Zaidi ya miaka 6: toa gramu 2, mara 1 tu.