Hesperian Health Guides

Antibiotiki (viuavijasumu) hupambana na maambukizi

Kuwatunza watoto: Madawa

Antibiotiki ni dawa za kupambana na maambukizi kutokana na bakteria. Hazisaidii dhidi ya maambukizi virusi kama vile tetekuwanga,surua ya rubella, mafua, au homa ya kawaida. Siyo kila antibiotiki inaweza kupambana na maambukizi ya bakteria. Dawa za antibiotiki zenye muundo wa kemikali unaofanana huchukuliwa kuwa katika familia moja. Ni muhimu kuwa na ufahamu juu ya familia za antibiotiki kwa sababu kuu 2:

 1. Dawa za antibiotiki kutoka katika familia moja mara nyingi hutibu matatizo yanayofanana.
 2. Kama una mzio kutokana na dawa moja ya antibiotiki kutoka katika familia moja, utapata mzio pia kutokana na dawa za antibiotiki zingine kutoka familia hiyo. Hii inamaanisha kwamba unatakiwa kutumia dawa kutoka katika familia nyingine ya antibiotiki.

Dawa ya antibiotiki lazima itumike “kwa dozi kamilifu.” Kukatisha dozi bila kukamilisha siku zote za matibabu huweza kuyafanya maambukizi kuwa sugu zaidi.

Penisilini

Dawa kutoka familia ya penisilini ni miongoni mwa dawa muhimu zaidi katika kundi la antibiotiki. Penisilini hupambana na baadhi ya maambukizi, yakiwemo mengi ambayo husababisha usaha.

Penisilini hupimwa katika miligramu (mg) au uniti (U). Kwa penisilini G,miligramu 250 = 400,000 U.

Kwa watu wengi, penisilini ni miongoni mwa dawa salama zaidi. Kutumia zaidi ya dozi iliopendekezwa ni kupoteza fedha lakini huenda isimuathiri mtumiaji.

Usugu kwa dawa ya penisilini

Baadhi ya maambukizi yamejenga usugu dhidi ya penisilini. Hii inamaanisha kuwa zamani penisilini ilikuwa na uwezo wa kutibu mgonjwa mwenye maambukuzi haya, lakini kwa sasa haiwezi. Kama maambukizi hayatibiki na penisilini ya kawaida, antibiotiki nyingine inaweza kujaribiwa, au penisilini ya aina nyingine inaweza kusaidia. Kwa mfano, nimonia (kichomi) wakati mwingine huonesha usugu kwa penisilini. Tumia amoksilini badala yake.

MuhimuNBgrnimportant.png

Kwa ajili ya penisilini zote (ikiwemo ampisilini na amoksilini)

Baadhi ya watu wana mzio na penisilini. Mzio kiasi husababisha upele. Mara nyingi hujitokeza saa au siku kadhaa baada ya kutumia penisilini na hudumu kwa siku kadhaa.Ukitokea acha kutumia penisilini mara moja. Dawa za kupambana na mzio (Antihistamines) husaidia kupunguza muwasho. Tumbo kuvurugika na kuharisha kutokana na penisilini siyo dalili za mzio. Ingawa husababisha kero,zisiwe sababu za kusimamisha matumizi na dawa hiyo.

Kwa nadra sana, penisilini inaweza kusababisha mzio mkali sana-mlipuko wa mzio. Ndani ya dakika au saa kadhaa baada ya kutumia penisilini, mwili unaweza kututumuka,koo na midomo kuvimba, kupata tabu katika kupumua, hali ya kutaka kuzirai, na kuingia kwenye mshtuko. Hii ni hatari sana. Lazima achomwe sindano ya efedrini (adrenalin) mara moja. Wakati wote kuwa na epinefrini (epinephrine) tayari unapochoma sindano ya penisilini. Angalia Huduma ya kwanza.

Mtu yoyote ambaye amewahi kupatwa na mzio kutokana na penisilini kamwe asipewe – ampisilini, amoksilini, au aina za penisilini zingine tena,aidha kwa njia ya mdomo au sindano. Hii ni kwa sababu mzio unapotokea tena unaweza kuwa mbaya zaidi na hata kumuua. Watu wanaopata mzio kutokana na penisilini wanaweza kutumia erithromaisini au antibiotiki kama dawa mbadala.

Sindano

Penisilini mara nyingi hufanya kazi vizuri inapotolewa kwa njia ya mdomo. Sindano za penisilini zinaweza kuwa hatari. Zinaweza kusababisha mzio mkali na matatizo mengine. Tumia sindano za penisilini pale tu kunapokuwa na maambukizi makali au hatari.

Ampisilini na amoksilini


Ampisilini na amoksilini ni familia ya penisilini yenye tiba pana, maana yake ni kwamba huua aina nyingi za bakteria. Dawa hizi 2 mara nyingi ni mbadala wa nyingine.Pale ambapo ampisilini imependekezwa katika kitabu hiki, amoksilini inaweza kutumika katika nafasi yake kwa kuzingatia dozi sahihi.

Ampisilini na amoksilini ni dawa salama sana na ni msaada mkubwa kwa watoto wachanga na watoto wadogo. Ni muhimu sana katika kutibu maambukizi ya sikio. Ampisilini ni muhimu katika kutibu homa ya uti wa mgongo na maambukizi mengine makali miongoni mwa watoto wachanga. Amoksilini hutumika kwa ajili ya nimonia.

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Dawa hizi 2, lakini hasa ampisilini, huwa na tabia ya kusababisha kichefuchefu na kuharisha. Epuka kutoa dawa hizi kwa watoto ambao tayari wanaharisha - kama unaweza wapatie dawa aina nyingine ya antibiotiki.

Madhara mengine ya kawaida ya pembeni ni upele. Lakini uvimbevimbe, mithili ya malengelenge, unawowasha ambao huja na kutoweka ndani ya saa chache huenda ni dalili ya mzio kutokana na penisilini. Simamisha utoaji wa dawa hiyo mara moja na usimpe mtoto huyu penisilini tena.Matukio ya usoni yanaweza kuwa mabaya zaidi na hata kutishia maisha. Kwa baadhi ya matatizo,erithiromaisini inaweza kutumika. Upele ulioenea tambarare ukifanana kama wa surua, na kawaida huonekana wiki moja baada ya kuanza kutumia dawa na ambao huchukua siku kadhaa kutoweka, mara nyingi siyo dalili ya mzio. Lakini siyo rahisi kujua kwa uhakika iwapo upele huo unatokana na mzio au la,hivyo ni bora kusimamisha dawa.

MuhimuNBgrnimportant.png

Usugu dhidi ya dawa hizi unazidi kuenea. Kutegemea na mahali unapoishi,dawa hizi zinaweza kutofanya kazi tena dhidi ya stafilokokasi (aina ya bakteria wanaosababisha uvimbe unaotunga usaha, shigella, na maambukizi mengine.

Jinsi ya kutumiaNBgrninjectpill.png

Dawa ya ampisilini na amoksilini hufanya kazi vizuri zinapotumiwa kwa njia ya mdomo. Ampisilini inaweza pia kutolewa kwa njia ya sindano, lakini ni kwa ajili ya magonjwa makali kama vile homa ya uti wa mgongo au iwapo mtoto anatapika au hawezi kumeza.

Kama ilivyo kwa dawa zingine za antibiotiki, kila mara toa dawa angalau kwa muda i wa siku chache zilizopendekezwa hapa. Kama mtoto ataendelea kuonesha dalili za maambukizi, endelea kumpatia kiwango kile cha dawa kila siku hadi saa 24 baada ya dalili zote kutoweka Kama mgonjwa ametumia dawa kwa muda wa siku nyingi zilizopendekezwa na bado ana dalili, simamisha kumpa antibiotiki hiyo na tafuta msaada wa daktari.

Kwa watu walio na VVU, kila mara toa dawa kwa ajili ya muda wa siku zote zilizoorodheshwa. Vilevile, kiwango cha antibiotiki ambacho kinapaswa hutegemea umri na uzito wa mtu na makli ya maambukizi. Kwa ujumla, toa kiasi cha chini kwa mtoto mwembamba au kwa maambukizi yasiyo makali sana, na kiasi cha juu kwa mtoto mwenye uzito mkubwa zaidi au dhidi ya maambukizi makali sana.

AMOKSILINI (MATUMIZI KWA NJIA YA MDOMONI)
Kwa maambukizi mengi miongoni mwa watoto
Toa miligramu 45 hadi 50 kwa kila kilo kwa siku, ikigawanywa katika dozi 2 kwa siku. Kama huwezi kumpima mtoto, mpe dozi kulingana na umri:
Chini ya miezi 3: toa miligramu 125, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Miezi 3 hadi miaka 3: toa miligramu 250, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Miaka 4 hadi 7: toa miligramu 375, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Miaka 8 hadi 12: toa miligramu 500, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Zaidi ya miaka 12: toa miligramu 500 hadi 875, mara 2 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Kwa ajili ya Nimonia
Toa miligramu 80 kwa kilo kila siku, dawa ikiwa imegawanywa katika dozi 2 kwa siku kwa siku 3. Kama watu wengi katika eneo lako wana VVU, wape dozi ya amoksilini kwa siku 5. Kama huwezi kumpima mtoto, mpe dozi kwa kuzingatia umri:
Miezi 2 hadi 12: mpe miligramu 250, mara 2 kwa siku kwa siku 3 hadi 5.
Miezi 12 hadi miaka 3: mpe miligramu 500, mara 2 kwa siku kwa siku 3 hadi 5.
Miaka 3 hadi 5: mpe miligramu 750, mara 2 kwa siku kwa siku 3 hadi 5.
AMPISILINI (KWA NJIA YA MDOMO)
Mpe miligramu 50 hadi 100 kwa kila kilo kwa siku, zikigawanywa kwenye dozi 4 kwa siku. Kama huwezi kumpima mtu, mpe dozi kulingana na umri wake:
Chini ya mwaka 1: mpe miligramu 100, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Mwaka 1 hadi 3: mpe miligramu 125, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Miaka 4 hadi 7: mpe miligramu 250, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Miaka 8 hadi 12: mpe miligramu 375, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Zaidi ya miaka 12: mpe miligramu 500, mara 4 kila siku kwa siku 7.
AMPISILINI (KWA NJIA YA SINDANO)
Matumizi ya ampisilini kwa njia ya sindano ni kwa ajili ya magonjwa makali, au kama mgonjwa anatapika au hawezi kumeza.
Choma miligramu 100 hadi 200 kwa kilo, zikigawanywa katika dozi 4 kila siku. Kama huwezi kumpima mtu, mpe dozi kwa kuzingatia umri wake:
Chini ya mwaka 1: choma miligramu 100, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Mwaka 1 hadi 5: choma miligramu 300, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Miaka 6 hadi 12: choma miligramu 625, mara 4 kila siku kwa siku 7.
Zaidi ya miaka 12: choma miligramu 875, mara 4 kila siku kwa siku 7.

Kumtibu mtoto wakati unampeleka hospitali choma sindano 1 ya mchangayiko wa dawa zifuatazo kwenye msuli au mshipa. Choma sindano kwenye mshipa tu kama umefundishwa vya kutosha kufanya hivyo, kama hapana choma kwenye msuli. Angalia Dawa, vipimo, na matibabu (kinaandaliwa)

AMPISILINI NA SEFTRIAKZONI

Changanya kichupa cha poda ya ampisilini cha miligramu 500 na mililita 2.1 za maji yaliyotakaswa. Hii itatengeneza mchanganyiko wenye ukali wa miligramu 500 kwa kila mililita 2.5.

Changanya kichupa cha poda ya dawa ya seftriakzoni gramu 1 kwa ajili ya sindano na mililita 3.5 za maji yaliyotakaswa. Hii itatengeneza mchanganyiko wenye ukali wa gramu 1 kwa kila mililita 4.

MuhimuNBgrnimportant.png
Usitoe Sefriakzoni kwa watoto chini ya mwezi 1.


AMPISILINI Choma miligramu 50 kwa kila kilo ya mwili, mara 4 kwa siku kwa angalau siku 5.
NA
SEFTRIAKZONI: Choma miligramu 100 kwa kila kilo ya mwili, mara 1 kwa siku angalau kwa siku 5.


Kama huwezi kumpima mtoto, toa dozi kulingana na umri:

Mwezi 1 hadi 12: choma mililita 2 za ampisilini mara 4 kwa siku, NA
mililita 2 za seftriakzoni mara 1 kwa siku, angalau kwa siku 5.
Mwaka 1 hadi 3: Choma mililita 3 za ampisilini mara 4 kwa siku, NA
mililita 4 za seftriakzoni mara 1 kwa siku angalau kwa siku 5.
Miaka 4 had 5: Choma mililita 5 za ampisilini mara 4 kwa siku, NA
mililita 6 za seftriakzoni mara 1 kwa siku angalau kwa siku 5.

AU

AMPISILINI NA JENTAMAISINI

Changanya kichupa cha poda ya ampisilini cha miligramu 500 kwa ajili ya sindano na maji yaliyotakaswa mililita 2.1. Hii itatengeneza mchanganyiko wenye ukali wa miligramu 500 kwa kila mililita 2.5.

Tumia kichupa cha jentamaisini cha miligramu 2 ambayo haijapunguzwa makali yenye kiwango cha mililita 40 kwa kila mililita.

MuhimuNBgrnimportant.png

Jentamaisini ni antibiotiki kali sana kutoka kundi la aminoglycoside. Inaweza kutolewa tu kwa njia ya sindano au kwenye mshipa wa damu kwa njia ya dripu. Dawa hii inaweza kuharibu figo na uwezo wa kusikia, na hivyo inapaswa kutumika tu kwa dharura wakati msaada wa daktari ukitafutwa. Jentamaisini inapaswa kutolewa kwa kuzingatia dozi yake sahihi kwa ukamilifu.

Kama mtoto anaonekana kupungukiwa na maji mwilini (mdomo umekauka sana au hakojoi) mpe kinywaji maalum cha kuongeza maji mwilini hadi atakapopata nafuu kabla hujampa jentamaisini. Angalia Maumivu tumboni, kuhara, na minyoo na jinsi ya kutoa kinywaji cha kuongeza maji mwilini.

Kwa watoto wachanga wenye umri chini ya wiki 1
AMPISILINI: Choma miligramu 50 kwa kilo, mara 2 kwa siku kwa angalau siku 5,
NA
JENTAMAISINI: Choma miligramu 5 kwa kilo, mara 1 kwa siku angalau kwa siku 5.

Usitoe kwa zaidi ya siku 10.

Kwa watoto wachanga wa umri wa wiki 1 hadi mwezi 1
AMPISILINI: Choma miligramu 50 kwa kilo, mara 3 kwa siku angalau kwa siku 5,
NA
JENTAMAISINI: Choma miligramu 7.5 kwa kilo, mara 1 kwa siku angalau kwa siku 5.

Usitoe kwa zaidi ya siku 10.

Kwa watoto wadogo na watoto wachanga zaidi ya mwezi 1
AMPISILINI: Choma miligramu 50 kwa kilo, mara 4 kwa siku angalau kwa siku 5,
NA
JENTAMAISINI: Choma miligramu 7.5 kwa kilo, mara 1 kwa siku angalau kwa siku 5. Usitoe kwa zaidi ya siku 10.

Ni salama zaidi kutoa dozi sahihi ya jentamaisini kulingana na uzito wa mtoto lakini kama huwezi kumpima mtoto uzito, toa dozi kwa kuzingatia umri kama ifuatavyo:

Mwezi 1 hadi 4: choma sindano ya ampisilini mililita 1.5 mara 4 kwa siku, NA
Mililita 0.5 hadi 1 ya jentamaisini mara 1 kwa siku, angalau kwa siku 5.
Miezi 4 hadi 12: choma mililita 2 za ampisilini mara 4 kwa siku, NA
jentamaisini mililita 1.5 mara 1 kwa siku, angalau kwa siku 5.
Mwaka 1 hadi 3: choma ampisilini mililita 3 mara 4 kwa siku, NA
Jentamisini mililita 2 mara 1 kwa siku angalau kwa siku 5.
Miaka 4 hadi 5: choma mililita 5 za ampisilini mara 4 kwa siku, NA
Jentamaisini mililita 3 mara 1 kwa siku angalau kwa siku 5.

Usitoe kwa zaidi ya siku 10.

Penisilini kwa njia ya mdomo, penisilini V, penisilini VK


Penisilini kwa njia ya mdomo (badala ya njia ya sindano) inaweza kutumika kwa ajili maambukizi ya wastani na maambukizi yasiyo makali sana, yakiwemo:

 • Vidonda kooni vikiandamana na homa kali
 • Maambukizi ya sikio
 • Sinusitisi-uvimbe katika uwazi unaowasiliana na pua kutoka ‘vyumba’ vingine vinavyohifadhi hewa ndani ya mifupa ya kichwa (sinusi)
 • Homa ya rumatizimu
 • Nimonia

Hata kama ulianza kwa kuchoma penisilini kwa ajili ya maambukizi makali, unaweza kuanzisha matumizi ya penisilini kwa njia ya mdomo pale mgonjwa atakapoanza kupata nafuu. Kama ugonjwa hautaanza kupungua ndani ya siku 2 au 3, fikiria kumuanzishia antibiotiki nyingine na kutafuta msaada zaidi wa daktari.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png

Ili kuusaidia mwili kutumia dawa vizuri, tumia penisilini kabla hujala, angalau saa 1 kabla au saa 2 baada ya chakula.

Toa miligramu 25 hadi 50 kwa kilo kila siku, ikigawanyika katika dozi 4, kwa siku 10. Kama huwezi kumpima mtoto, toa dozi kwa kuzingatia umri:
Chini ya mwaka 1: toa miligramu 62.5, mara 4 kila siku kwa siku 10.
Mwaka 1 hadi 5: toa miligramu 125, mara 4 kila siku kwa siku 10.
Miaka 6 hadi 12: toa miligramu 125 hadi 250, mara 4 kila siku kwa siku 10.
Zaidi ya miaka 12: toa miligramu 250 hadi 500, mara 4 kila siku kwa siku 10.
Kwa ajili ya maambukizi makali, zidisha kiwango cha dozi kilichoelezewa juu mara 2.
Kwa ajili ya homa ya rumatizimu
Watoto: toa miligramu 250, mara 2 kila siku kwa siku 10.
Watu wazima: toa miligramu 500, mara 2 kila siku kwa siku 10.

Dawa ya penisilini kwa ajili ya sindano, penisilini G


Tiba ya penisilini kwa njia ya sindano inapaswa kutumika kwa ajili ya maambukizi makali,yakiwemo:

 • pepopunda (tetanasi)
 • nimonia kali
 • vidonda vyenye maambukizi makali
 • mfupa uliochana ngozi na kujitokeza nje
 • kaswende


Penisilini kwa ajili ya sindano huwa katika mifumo tofauti. Tofauti kubwa ni muda ambao aina ya penisilini husika huchukua kuonesha matokeo na kudumu mwilini:kuna inayofanya kazi haraka lakini haidumu muda mrefu mwilini; inayofanya kazi na kudumu mwilini kwa muda wa kati;na inayofanya kazi polepole lakini hudumu mwilini muda mrefu.

Jinsi ya kutumiaNBgrninject.png

PENISILINI YA PROKENI (PROCAINE PENICILLIN) PROKENI BENZIPENISILINI (PROCAINE BENZYLPENICILLIN) - huanza kufanya kazi na kudumu mwilini kwa muda wa kati au wastani.

Choma kwenye msuli tu, siyo kwenye mshipa wa damu.

Toa uniti 25,000 hadi 50,000 kwa kilo kila siku. Usitoe zaidi ya uniti 4,800,000. Kama huwezi kumpima mtoto, toa dozi kwa kuzingatia umri:
Miezi 2 hadi miaka 3: choma uniti 150,000, mara 1 kila siku kwa siku 10 hadi 15.
Miaka 4 hadi 7: choma uniti 300,000, mara 1 kila siku kwa siku 10 hadi 15.
Miaka 8 hadi 12: choma uniti 600,000, mara 1 kila siku kwa siku 10 hadi 15.
Zaidi ya miaka 12: choma uniti 600,000 hadi 4,800,000, mara 1 kila siku kwa siku 10 hadi 15.

Usitumie kwa watoto wachanga chini ya miezi 2 isipokuwa kama hakuna aina nyingine yoyote ya penisilini au ampisilini. Kama hii ndiyo njia pekee iliyopo, choma uniti 50,000, mara 1 kila siku kwa siku 10 hadi 15.

Kama ni kwa ajili ya maambukizi makali kwa umri wowote ule, zidisha dozi iliyoelezewa juu mara 2. Usitoe zaidi ya uniti 4,800,000 kwa siku.

Dozi ya penisilini ya prokeni ikiunganishwa na penisilini nyingine inayotibu baada ya muda mfupi (short acting penicillin) ni sawa na penisilini ya prokeni peke yake.

BENZATHINI, BENZAIPENISILINI (BENZATHINE BENZYLPENICILLIN, BENZATHINE PENICILLIN ) – hufanya kazi polepole lakini hudumu mwilini muda mrefu
Choma kwenye msuli tu, siyo kwenye mshipa wa damu.

Watoto chini ya kilo 30, au mwaka 1 hadi 7: choma uniti 300,000 hadi 600,000, mara 1 kwa wiki. Kwa ajili ya maambukizi ambayo siyo makali, sindano 1 inaweza kutosha.
Watu wazima na watoto wenye uzito zaidi ya kilo 30, au umri zaidi ya miaka 8: choma uniti milioni 1.2. Kwa maambukizi yasiyo makali, sindano 1 inaweza kutosha.

Vidonda kooni ambavyo vimeambatana na homa kali, mpe sindano 1 ya dozi iliyoelezwa juu.
Kwa aliye na homa ya rumatizimu, choma dozi iliyoelezwa juu mara 1 kila kipindi cha wiki 4. Endelea na tiba hii kwa miaka 5 hadi 10 ili kuzuia ugonjwa wa rumatizimu ya moyo.
Kwa ajili ya kaswende miongoni mwa watoto wachanga, choma uniti 50,000 kwa kilo mara 1.

Madawa zingine za antibiotiki

Erithromaisini (erythromycin)


Erithromaisini hufanya kazi dhidi ya maambukizi mengi kama ilivyo penisilini na inaweza kutumika na watu ambao wana mzio na penisilini. Kwa maambukizi mengi inaweza kutumika kama mbadala wa tetrasaikilini. Inaweza pia kutumika kutibu dondakoo na kifaduro.

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Erithromaisini mara nyingi husababisha kichefuchefu na kuharisha, hasa miongoni mwa watoto.Usitumie kwa zaidi ya wiki 2 kwani inaweza kusababisha ugonjwa wa manjano.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png
Toa miligramu 30 hadi 50 kwa kilo, ikiwa imegawanywa katika dozi 2 hadi 4 kila siku.
Watoto wachanga hadi mwezi 1a: toa miligramu 62, mara 3 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Mwezi 1 hadi miaka 2: toa miligramu 125, mara 3 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Miaka 2 hadi 8: toa miligramu 250, mara 3 kila siku kwa siku 7 hadi 10.
Zaidi ya miaka 8: toa miligramu 250 hadi 500, mara 4 kila siku kwa siku 7 hadi 10.

Kwa maambukizi makali, zidisha dozi iliyoelezewa juu mara 2.

Kotrimozazo (Cotrimoxazole), salfamethozazo (sulfamethoxazole) na trimethoprimu (trimethoprim), TMP-SMX


Muunganiko huu wa dawa hizi 2 za antibiotiki siyo ghali na hupambana na maambukizi mengi. Ni dawa muhimu kwa watu wenye VVU na inaweza kuzuia maambukizi mengi ambayo hutokana na VVU. (Angalia VVU na UKIMWI kinaadaliwa).

MuhimuNBgrnimportant.png

Epuka kutoa kotrimozazo kwa watoto wachanga chini ya wiki 6 na wajawazito ambao wapo katika miezi yao 3 ya mwisho kabla ya kujifungua. Mzio hutokea sana kuhusiana na dawa hii. Dalili za mzio ni homa, kupumua kwa shida, au upele. Simamisha dawa hii ya kotrimozazo kama mtoto atatokwa na upele au kama unafikiri huenda kuna mzio.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png

Kotrimozazo hutengenezwa ikiwa na nguvu tofauti za dawa 2 zilizomo ndani. Hivyo inaweza kuwa, kwa mfano 200/40 (ikimaanisha miligramu 200 za salfamethozazo (sulfamethoxazole) na miligramu 40 za trimethoprimu (trimethoprim) au 400/80 au 800/160. Wakati mwingine dozi huelezewa tu kwa kiasi cha trimethoprimu (trimethoprim) kilichomo ndani (namba ya pili).

Kwa aina nyingi za maambukizi
Wiki 6 hadi mezi 5: toa salfamethozazo (sulfamethoxazole) miligramu 100 + trimethoprimu (trimethoprim) miligramu 20, mara 2 kwa siku kwa siku 5.
Miezi 6 hadi miaka 5: toa miligramu 200 za salfamethozazo (sulfamethoxazole) + miligramu 40 za trimethoprimu (trimethoprim), mara 2 kwa siku 1.
Miaka 6 hadi 12: toa salfamethozazo miligramu 400 + trimethoprimu miligramu 80, mara 2 kwa siku 5.
Zaidi ya miaka 12: toa salfamethozazo miligramu 800 + trimethoprimu miligramu 160, mara 2 kwa siku 5.