Hesperian Health Guides

Kuzuia njaa

Katika sura hii:

Unaweza kusaidia jamii yako kujiandaa kukabiliana na njaa au maafa kwa kulima mazao ya chakula, kuyahifadhi vizuri na kujenga utaratibu wa majirani kusaidiana.

Kulima mazao ya chakula

Popote unapoishi, unaweza kulima mazao ya chakula. Kuzalisha chakula chako mwenyewe ni miongoni mwa njia bora zaidi za kupata lishe yenye afya, na kukusaidia angalau kupata chakula unapokuwa huna fedha ya kununua chakula.

Watu wakipalilia mbogamboga kwenye bustani iliyotengenezwa katika eneo la wazi katikati ya majengo ya ghorofa ya makazi

Wakazi kwenye majiji wanaweza kupanda mazao yao ya chakula kwenye paa maghorofani, katika maeneo ya wazi, kwenye viungu au viroba vilivyojazwa udongo na kunin’ginizwa dirishani. Mimea kidogo kwenye chungu inaweza kutokupa chakula cha kutosha lakini ni kianzio. Watoto nao hupenda kupanda mimea na kuihudumia. Hii ni stadi muhimu kuwafundisha na kuendeleza. Ungana na majirani kutengeneza bustani katika eneo la wazi na hata kufanya zaidi.

Kama tayari umeanza kilimo, lakini sana sana unalima mazao ya kibiashara kama vile pamba, kahawa, mpunga, au mahindi, panda pia mbogamboga kwa ajili ya familia au wanajamii wenzako. Au jenga bwawa dogo la kufugia samaki. Kama mazao yako ya kibiashara yataathirika au bei kuporomoka, hutakosa chochote kwa ajili ya kula.

Kwa mawazo zaidi juu ya namna ya kuzalisha chakula chako mwenyewe, angalia Kitabu cha Hesperian: Mwongozo kwa Jamii juu ya Afya ya Mazingira Sura 15.

Boresha uzalishaji wako

Ngombe akila majani na kuzalisha mbolea
 • Rutubisha udongo kwa kutumia mbolea ya wanyama na mboji. Mbolea za kibiashara na kemikali huongeza uzalishaji kwa miaka michache, lakini pia huharibu udongo na kuchafua vyanzo vya maji. Mbolea za asili kama vile samadi na mboji husaidia kurutubisha udongo kwa muda mrefu. Kwa bustani ndogo ya nyumbani, weka taka zako kutokana na chakula kwenye chombo ili ziweze kuoza na kutengeneza mboji ambayo unaweza kutumia kurutubisha udongo.
Mwanamke akimwaga maji kwenye ndoo iliyotundikwa juu, ikiwa na bomba 2 za kutoa maji kwenye ndoo kuelekea kwenye bustani
Matobo madogo kwenye bomba huruhusu maji kutoka polepole kama matone na kuingia kwenye udongo.
 • Tumia maji kwa uangalifu. Jaribu kuvuna maji ya mvua. Kama unaweza kupata bomba refu la maji, tengeneza msitari wa matobo madogo madogo kumwagilia kila mmea badala ya kupoteza maji mengi kwa kuyahifadhi kwenye mabwawa makubwa ya umwagiliaji.
NWTND Nut Page 31-1.png
Mwaka huu ni mahindi. Mwaka ujao ni maharagwe.


 • Panda mazao tofauti kila msimu wa kilimo ili kuzuia magonjwa na kuimarisha udongo.
 • Panda mbaazi au maharagwe. Vyakula hivi vina virutubishi vingi na huimarisha udongo kadri vinavyokua.
Mwanaume akitumia bomba lililounganishwa na tenki mgongoni mwake kunyunyizia mazao.
Kama una bomba la kunyunyizia, lisafishe vizuri, halafu weka ndani mafuta ya mbogamboga (vegetable oil) kidogo na maji. Changanya vizuri kabla ya kunyunyizia ili kuua wadudu waharibifu.


 • Epuka viuatilifu. Viuatilifu ni sumu. Huua wadudu waharibifu na kusaidia mazao kwa muda mfupi, lakini pia huwadhuru watu wanaovigusa na kuvitumia. Ndege na wanyama wadogo ambao husaidia kudhibiti wadudu pia wanaweza kudhurika. Bila ndege hao, wadudu waharibifu wataongezeka na kuharibu mazao zaidi. Baada ya muda, wadudu waharibifu wanaweza kujenga usugu dhidi ya dawa na kustahimili hata viuatilifu kali zaidi. Kemikali hizi ghali ni hatari na yafaa kuziepuka kila inapowezekana.


Kunyunyizia mimea na sabuni isiyo kali inaweza kusaidia kuwadhibiti wadudu bila kutumia viuatilifu vyenye sumu kali. Hata mafuta ya kula viwandani ambayo yametengenezwa kutokana na mbogamboga (vegetable oil) yana uwezo wa kuua aina nyingi za wadudu waharibifu.

Hifadhi vizuri chakula chako

Kuzalisha chakula tu hakutasaidia kuondoa njaa na kuboresha hali ya lishe ndani ya familia au jamii iwapo kitaachwa na kuharibika au kuliwa na wadudu waharibifu. Kukausha, kuhifadhi katika achali (pickling), kupaka chumvi, na kuchachusha ni njia za asili za kutunza chakula kikiwa salama kwa ajili ya kula baada ya mwisho wa msimu.

Kwa nafaka na maharagwe

 • Kausha na kuhifadhi nafaka mara baada ya kuvuna. (Kuviacha shambani huchangia upotevu mkubwa.)
 • Hifadhi nafaka mahali pakavu, juu ya udongo,ardhi na kwenye vyombo ambavyo vimefungwa na kukazwa. Kwa ajili ya mavuno makubwa, unaweza kujenga banda lililoinuliwa kama kwenye kielelezo kifuatacho. Mavuno kidogo yanaweza kuhifadiwa kwenye mapipa salama na vyombo vingine ambavyo vimefunikwa vizuri.
Kichanja cha miti , kikiwa na vizuizi katika kila miguu
vizuizi
Safisha eneo husika kuondoa majani na vitu vingine vilivyopo juu. Wanyama wadogo huvutiwa na mabaki ya chakula, na maeneo yenye giza yaliyojitenga mahali ambapo wanaweza kujenga makazi. Ondoa vitu hivyo kwenye mazingira husika.Tunza vyombo vya kuhifadhia nafaka vikiwa vimefungwa na ziba matobo yoyote haraka. Wanyama wadogo wana uwezo wa kupenya na kupita kwenye matundu madogo.

Tunza vyombo vya kuhifadhia nafaka juu ya ardhi.Wanyama wadogo wana uwezo wa kupanda. Ondoa kitu chochote ambacho kinagusa chombo cha kuhifadhia nafaka na kuweka vizuizi kwenye miguu.

Fuga mbwa na paka kuzuia wanyama wadogo wasisogelee.
 • Katika sehemu kadhaa nchini India, wakulima huchanganya majani ya mwarobaini na nafaka zinazohifadhiwa. Mwarobaini ni kiuatilifu cha asili na salama na hufukuza wadudu. Nchini Cameroon, wakulima huhifadhi njegere kavu kwenye vyungu vya udongo na kuchanganya na majivu yatokanayo na mimea. Majivu huzuia wadudu kuingia. Katika maeneo mengine, maharagwe makavu huhifadhiwa kwenye mafuta. Hizi ni njia nzuri sana na salama kwa ajili ya kuhifadhi nafaka na maharagwe na kutunza chakula chako kwa ajili ya matumizi ya baadae.
 • Nafaka zilizoota kuvu zinapaswa kuangamizwa. Uoto wa kuvu una sumu ndani yake.
Samaki waliotundikwa kwenye mti na kamba wakikaushwa na moto

Ukaushaji

Samaki, matunda, nyama, na mbogamboga zilizokaushwa zinaweza kukupatia vitamini, madini na protini unapokuwa huwezi kupanda au kuzalisha vyakula hivyo. Kausha vyakula haraka zaidi juu ya ardhi kuzuia vumbi kuingia. Kikapu chenye kina kifupi au ungo, waya wa kufugia kuku, au aina ya wavu mgumu wa chuma ambao unaruhusu hewa kupita chini yake, huwezesha chakula kukauka haraka. Funika vyakula wakati wa kukausha kwa kutumia kitambaa chepesi ili kuzuia wadudu na uchafu.

Mbogamboga kawaida zinapaswa kupikwa kidogo kabla ya kukaushwa. Kausha mbogamboga na matunda vizuri lakini bakisha unyevu wa kutosha ili visipoteze ladha kabisa. Nyama na samaki vinaweza kukaushwa juu ya moto.

Tunza vyakula vilivyokauka sehemu zenye giza na ubaridi, kwenye mifuko au vyombo vilivyofunikwa vizuri.

Shirikiana na majirani

Familia ikipokea chakula kutoka benki ya chakula, wakati wengine wakila pembeni kwenye meza

Baadhi ya jamii zina utamaduni wa kusaidiana chakula hasa kwa wale walio katika hali ngumu. Kwa mfano, familia zinapokwenda kwenye ibada, huenda na nafaka kiasi kuwagawia wengine. Kiasi kidogo kidogo cha nafaka kutoka familia nyingi huzaa nafaka nyingi ambayo inaweza kuhifadhiwa. Halafu, familia kadhaa zinapokosa mavuno ya kutosha msimu unaofuata, nafaka iliyohifadhiwa inaweza kutolewa kwa familia hizo. Baadhi ya makundi yameanzisha “benki za mchele” rasmi mahali ambapo familia huweka kiasi cha mchele wakati wa mavuno kwa ajili ya kuwakopesha watu wanaohitaji wakati wa msimu wa kiangazi.

Ufumbuzi kutoka ndani ya jamii kwa tatizo la njaa katika jamii husika

Jiji la Belo Horizonte nchini Brazil linapambana kukomesha njaa na umasikini kwa watu wake na wakulima wengine wanaoishi karibu. Miaka ya 1990, serikali ya jiji hilo ilitangaza chakula kuwa haki ya binadamu, na kuanzisha programu ya kufanikisha haki hii. Kwa mfano:

 • Kutoa huduma ya chakula chenye lishe bora kwa wanafunzi.
 • Watu wenye hali duni kuweza kupokea msaada wa chakula cha msingi chenye virutubishi kila wiki.
 • Migahawa mikubwa 3 katika viunga vya jiji hilo hutoa huduma ya mlo wa kawaida wenye virutubishi kwa gharama nafuu. Wateja wa kawaida wanaweza kutoa mapendekezo jinsi ya kuboresha huduma hii.
watu wakinunua na kuuza matunda na mbogamboga kwenye soko lenye shughuli nyingi
 • Jiji hununua matunda na mbogamboga kwa ajili ya programu zake za huduma ya chakula moja kwa moja kutoka kwa wakulima wadogo wanaoishi karibu na jiji. Jiji pia lilianzisha masoko ya wakulima mahali ambapo wakulima wanaweza kuuza vyakula vyao kwa bei inayofaa. Hii huwawezesha wakulima kubaki kweye ardhi yao kwani hawalazimiki kuhamia mjini. Pia husaidia kuhakikisha upatikanaji wa matunda na mbogamboga nzuri ambazo zinavunwa moja kwa moja kutoka shambani kwa watu waishio jijini.
 • Bei ya vyakula vikuu katika masoko makuu jijini hufuatiliwa. Halafu bei hizi hubandikwa kwenye maeneo ya umaa na kutangazwa kupitia radio na televisheni ili watu waweze kujua mahali pa kupata bei iliyo bora zaidi. Masoko ya binafsi pia hulazimika kuweka bei zinazowavutia wateja. Programu hizi zimechangia kuboresha, kwa kiwango kikubwa na haraka, afya za watu wa Belo Horizonte. Idadi ya vifo vya watoto ilipungua kwa nusu tangu programu hizi kuanzishwa.


Dawa pekee haikidhi kudhibiti minyoo kwa muda mrefu. Usafi binafsi na usafi wa jamii pia ni muhimu. Maambukizi ya minyoo yanaweza kuenea kwa urahisi miongoni mwa wanafamilia. Hivyo iwapo mojawapo ana minyoo, ni vyema kutibu familia nzima.