Hesperian Health Guides

Jitahidi kula vya kutosha unapokuwa mgonjwa

Katika sura hii:

Uponaji kutokana na magonjwa mengi hakuhitaji chakula maalum. Chakula ambacho kinafaa kiafya ni kile kile-unapokuwa mzima au unapokuwa unaumwa.

Mwanaume mwenye furaha na afya nzuri akila karoti, na mwanaume asiye na furaha amekonda na afya yake siyo nzuri
Mtu mwenye lishe bora ana mwili wenye nguvu ambao unaweza kupambana na maambukizi. Mtu mwenye lishe duni anaweza kuugua mara kwa mara.

Unapokuwa mgonjwa, usikwepe chakula. Chakula kitakusaidia kupata nafuu.


Virusi vya UKIMWI-VVU

Watu wenye VVU wanahitaji kula zaidi kama walivyokua wanakula kabla ya kuugua ili waweze kupata nguvu za kutosha kupambana na maambukizi. Kula mara nyingi zaidi kila siku. Hakikisha unakula protini, mbogamboga, matunda, na mafuta ambavyo vyote vinahitajika kukupa nguvu na kupambana na maambukizi. Kama ilivyo kwa watu wengine, watu waishio na VVU wanahitaji kufanya mazoezi. Hata kutembea kila siku huiweka misuli yako katika hali nzuri ya kufanya kazi na moyo wako kusukuma damu vizuri.

Unapokuwa mgonjwa kutokana na VVU, vidonda mdomoni, mdomo kukauka, vidonda kooni, kichefuchefu, au kukosa hamu ya kula-vyote vinaweza kusababisha matatizo katika kula. Angalia Huduma kwa wagonjwa (kinaandaliwa) kwa mawazo zaidi kuhusu jinsi ya kula vya kutosha unapokuwa ukijisikia vibaya.

Bahati mbaya, hakuna vyakula maalum vyenye uwezo wa kuponya VVU. Ni dawa tu ambazo zinaweza kudhibiti VVU angalia VVU na UKIMWI (kinaandaliwa).

Mawe (gallstones) na ugonjwa wa kibofu cha nyongo (gallbladder disease)

Kula sana vyakula vilivyokaangwa na mafuta mengi huchangia matatizo ya nyongo. Chemsha, pika kwa mvuke, au oka chakula badala ya kukaanga. Kula zaidi mbogamboga ambazo zimevunwa kutoka shambani na matunda pia, bonyeza hapa.

Msichana akimpelekea bakuli ya chakula mwanamke mgonjwa ambaye ameshika tumbo lake

Kuharisha

Usiache kula chakula unapokuwa na tatizo la kuharisha. Kuacha kula hakusaidii tatizo kuondoka; badala yake kunaweza kuzidisha utapiamlo na maji kupungua mwilini( hatari kuu za kuharisha). Bonyeza hapa kwa taarifa zaidi juu ya kuharisha.

Hakikisha vijidudu vya magonjwa havingii kwenye chakula chako

Kulinda usalama wa chakula kwa kunawa mikono yako kabla ya kukigusa na kukiosha chakula chako, kuzuia wadudu na kukitunza katika hali yenye usafi na usalama ni baadhi ya njia za kukulinda dhidi ya magonjwa ya tumbo na kuharisha, angalia Maji na usafi wa mazingira.

Kichefuchefu au maumivu mdomoni

Huduma kwa wagonjwa (kinaandaliwa) kinapendekeza njia za kuendelea kuupatia mwili virutubishi hata kama unajisikia kuumwa sana kiasi cha kushindwa kula.