Hesperian Health Guides

Kisukari

Katika sura hii:

Kisukari ni ugonjwa gani?

Chakula kinapomeng’enywa ndani ya miili yetu huingiza sukari kwenye damu yetu. Sukari hii huitwa glukozi au sukari asilia na miili yetu huitumia kupata nishati ambayo tunahitaji. Vitu vitamu hubadilika kuwa glukozi lakini na vyakula vingine pia, hasa vyakula vyenye wanga kama wali, mahindi, magimbi, viazi, na mkate au vyakula vingine kutokana na ngano.

Kisukari humaanisha kuwa na sukari nyingi mwilini kuzidi mahitaji. Tukiwa na kisukari, badala ya sukari kutuongezea nguvu au nishati, hulundikana kwenye damu na kusababisha uharibifu mwilini.

NWTND Diab Page 1-1.png Weka kipande cha mkate mweupe mdomoni na kutulia kwa dakika chache. Je unaweza kuhisi kiwango cha sukari kilichomo kwenye mkate?

Aina kuu ya ugonjwa wa kisukari ni kisukari Aina ya 2 (Type 2 diabetes). Kisukari Aina ya 2 kawaida husababishwa na kutofanya mazoezi au kutojishughulisha vya kutosha, kula vyakula ambavyo havina tija kiafya- hasa vyakula vilivyochakatwa sana, vyakula vilivyofungashwa viwandani- na ongezeko la msongo, na ukosefu wa usawa katika upatikanaji wa huduma za msingi katika maisha yetu. Kisukari ni ugonjwa usiopona, maana yake unaweza kutulia na kupungua, au unaweza kuzidi na kuwa mmbaya zaidi, lakini kamwe hautoweki kabisa.

Kuishi maisha yenye afya zaidi ukiwa na kisukari, kunahitaji udhibiti wa kiwango cha sukari kwenye damu yako. Kisukari ni hatari kwa sababu kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu yako kinaweza kusababisha matatizo kama upofu, kupoteza viungo (mikono au miguu), kupoteza uwezo wa kufanya ngono, kiharusi, au hata kifo. Unapodhibiti kiwango chako cha sukari, matatizo haya yanaweza kuepukwa, na unaweza kuendelea na maisha yenye afya na tija. Huo ndiyo ‘udhibiti’ wa kisukari.

Je, unaweza kuishi maisha yenye afya ukiwa na kisukari?

Dawa na huduma za kitabibu haziwezi kuponyesha kisukari. Lakini watu wanaweza kuwa na afya nzuri wakiwa na kisukari kama watajifunza juu ya ugonjwa huu na kuchukua hatua za kuudhibiti wao wenyewe. Mambo muhimu ambayo yanahitajika ni kula vyakula vyenye afya, kufanya mazoezi, kutunza meno na fizi katika hali ya usafi, kutunza miguu yako vizuri, kutafuta njia za kupunguza msongo, na kupumzika vya kutosha. Wakati mwingine, dawa pia huhitajika.

Wafanyakazi wa afya wanaweza kusaidia kudhibiti kisukari kwa kuvileta pamoja vikundi vya kusaidiana kujifunza juu ya ugonjwa huu na jinsi ya kujihudumia wao wenyewe.
kundi la watu likijadiliana.
Ilikuwa vigumu kuiambia familia yangu kwamba nilihitaji vyakula vyenye afya zaidi. Lakini sasa wanaona jinsi ninavyoendelea vizuri na wanaelewa kwamba kwa kubadilisha ulaji wetu afya zetu pia zitabadilika.

Dalili za kisukari

Dalili za mwanzo za kisukari kawaida huwa ni ngumu kubainisha. Wakati mwingine kunakuwa hakuna dalili yoyote. Hivyo watu wengi wana kisukari lakini hawajui.

Dalili ambazo zinaweza kutokana na kisukari
 • Kiu
 • Kukojoa mara kwa mara
 • Kutoona vizuri
 • Kukosa nguvu au kuchoka kwa urahisi
 • Vidonda ambavyo huchukua muda mrefu kupona
 • Ganzi miguuni
 • Maambukizi ya kuvu au fangasi yanayorudia kwa wanawake


Dalili hizi pia hutokana na matatizo mengine ya kiafya. Hivyo huwezi kusema kwa uhakika mtu ana kisukari kwa dalili hizi tu. Kupata uhakika, pata kipimo cha damu.

mtoto akijishikizia kwa mama yake ambaye anaonekana anaumwa.
Dalili za hatari

Kiwango cha sukari kwenye damu kinapopanda sana, husababisha:

 • Kiu kikali
 • Uchovu mkubwa na kusinziasinzia au kuchanganyikiwa
 • Kusikia njaa kila baada ya muda mfupi
 • Kupoteza uzito hata kama mtu anakula chakula cha kutosha


Mtu mwenye dalili hizi za hatari anapaswa kupimwa na kutibiwa haraka. Bila kutibiwa, anaweza kupoteza maisha kutokana na kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu. Angalia Kiwango cha sukari kwenye damu kuzidi kupita kiasi (hyperglycemia).

Matatizo yanayosababishwa na kisukari ambacho hakijadhibitiwa

Kama kisukari kimeachwa bila kutibiwa kwa miezi au miaka, kiwango kikubwa cha sukari kinaweza kuharibu viungo, neva na mishipa ya damu. Hali hii husababisha matatizo makubwa mwilini ambayo yanaweza kuchangia madhara ya kudumu au hata kifo.

mwanamke.
kiharusi (kupooza)
upofu
maambukizi ya fizi, kupoteza meno
mshtuko wa moyo
figo kushindwa kufanya kazi
kupoteza hamu ya ngono, maumivi wakati wa tendo la ngono
kwa wanaume: kupoteza uwezo wa kusimamisha ume
kwa wanawake: maambukizi ya kuvu au fangasi ukeni
maambukizi kwenye ngozi ambayo hayaponi, vidonda
ganzi au maumivu

Kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu kinaweza kusababisha uharibifu wa neva. Watu wengi wenye viwango vya juu vya sukari kwenye damu huanza kuhisi maumivu miguuni au miguu hufa ganzi. Viwango vya juu pia husababisha matatizo kuhusiana na mzunguko wa damu ambayo yanaweza kuchangia vidonda kwenye ngozi kuchukua muda mrefu kupona. Mtu pia anaweza kuchoka haraka. Kiwango cha juu cha sukari kwenye damu kinaweza pia kuchangia uharibifu wa macho na figo, na kusababisha viungo hivyo visifanye kazi vizuri au kuacha kufanya kazi.

Matatizo haya yote huzidishwa na:

Kuwa na tatizo la presha ya juu (shinikizo la damu la juu) husababisha moyo wako kufanya kazi na kusukuma damu kwa shida, uharibifu kwa viungo vingine, na viwango vya sukari kwenye damu kupanda sana kuliko kawaida. Uvutaji sigara husababisha shinikizo la juu la damu na huchangia uwezekano zaidi wa kupatwa na mshtuko wa moyo na kiharusi (angalia sura: Ugonjwa wa moyo - inaandaliwa). Ni muhimu kwa mtu mwenye kisukari kuacha uvutaji na kupunguza kiwango chake cha shinikizo la damu.

Lakini kisukari hakipaswi kusababisha matatizo hayo. Kwa kula vyakula vyenye afya, kupata mazoezi ya kutosha, na kupunguza msongo, unaweza kusaidia kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu yako. Maambukizi ya mdomoni na miguuni yanaweza kuzuiwa kwa urahisi kwa kujifunza njia chache za kutunza miguu yako, meno, na fizi.

Aina za kisukari

Kuna aina 3 za kisukari:

Kisukari Aina ya 1 kawaida huwapata watu wenye umri mdogo na huja haraka sana. Sababu ya kisukari Aina ya 1 haijulikani. Lakini hakijaenea sana kama Aina ya 2.

Kama mtoto au kijana atasikia kiu mara kwa mara, uchovu, au kupungua uzito ingawa anakula vizuri, mpime haraka. Kama ana kisukari Aina 1, anahitaji matibabu haraka.

Kisukari Aina 1 humaanisha kwamba mhusika hawezi kuchakata sukari vizuri. Ili aweze kuendelea kushi atahitaji kupatiwa homoni inayoitwa insulini kila siku kwa maisha yake yote. Atahitaji insulini na vifaa vyake, na elimu na msaada wa jinsi ya kuvitumia kwa usahihi.
mwanaume akijichoma sindano kwenye tumbo lake.
Tumbo ni sehemu ya kawaida ya kuchoma sindano ya insulini.

Kisukari Aina ya 2 kawaida huanzia katika umri wa utu uzima na kuendelea polepole, lakini watu wenye umri mdogo nao wanaweza kukipata. Watu wengi wana kisukari aina ya 2 na aina hii ya 2 ndiyo inazungumziwa sana katika sura hii.

Watu wanaokula sana vyakula vyenye sukari na wanga ambavyo vimechakatwa viwandani na kubadili sana asili yake, na ambao hawapati mazoezi ya kutosha wana uwezekano mkubwa wa kupata kisukari Aina ya 2. Vivyo hivyo watu wenye vitambi vikubwa, ambao ndugu zao wana kisukari, au wamepitia vipindi virefu vya njaa.

Matibabu ya kisukari Aina ya 2 huanza na ulaji wenye afya, kuongeza mazoezi ya viungo, na kupunguza msongo. Watu wenye kisukari Aina ya 2 wanaweza kunufaika na baadhi ya dawa au dawa za mitishamba.
wanawake 2 wakingalia bango.
Una hofu juu ya kisukari?
Njoo usikilize mhadhara wa mtaalam wa afya leo usiku juu ya kisukari.
Kiliniki ya jamii

Kisukari cha mimba ni aina ya kisukari Aina ya 2 ambacho huwapata wanawake wenye mimba. Mwanamke mwenye kisukari cha mimba anakuwa na kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu yake na pia mtoto wake aliye tumboni. Baada ya kujifungua, kiwango cha sukari katika damu yake kinaweza kupungua na kurudia hali yake ya kawaida, au mwanamke anaweza kupatwa na kisukari Aina 2.

Wamama wenye kisukari cha mimba wanaweza kupata ujauzito wenye matatizo na watoto wao huwa wanakuwa wakubwa sana kwenye tumbo, na kusababisha ugumu katika kujifungua. Mwanamke mwenye kisukari anapaswa kujifungilia hospitali kwa sababu huenda akahitaji upasuaji. Mtoto anaweza kuzaliwa akiwa na kiwango cha sukari kikubwa au kidogo kwenye damu, au na matatizo ya kupumua.

Kisukari cha mimba mara nyingi hudhibitiwa kwa ulaji wenye afya na wakati mwingine kwa dawa au mitishamba.

Wanawake wengi wenye kisukari wanaweza kuzaa watoto wenye afya.
NWTND Diab Page 5-2.png


Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Jan 2024