Hesperian Health Guides

Kisukari aina ya 2 husababishwa na nini?

Katika sura hii:

Mazingira yasiyo salama kiafya huchangia sana kisukari Aina ya 2. Watu wengi huugua kisukari kwa sababu ya kula zaidi vyakula vingi vilivyochakatwa sana viwandani ambavyo huingizwa kwenye jamii zao, na mabadiliko yasiyo ya kiafya katika mitindo yao ya maisha. Sababu za kisukari ni pamoja na:

mtoto akinunua chakula dukani.
Badala ya kununua pipi leo, nunua ndizi au embe.

Vyakula visivyo na tija kiafya

Vinywaji vilivyokolezwa sukari, pipi na vyakula vilivyochakatwa sana, na unga wa nafaka zilizokobolewa, mfano sembe, vyote huongeza sukari kwenye damu, na pia kuufanya mwili kujenga tabaka la ziada la mafuta. Vyakula vilivyochakatwa sana na kufungashwa kwa namna ya kuvutia vinaweza kuwa vigumu kuepukwa. Wakati mwingine bei yake huwa nafuu zaidi, na katika majiji kawaida hupatikana zaidi kuliko vyakula vyenye afya kutoka shambani. Lakini vyakula hivi vilivyochakatwa sana huchangia uwezekano wa kupata kisukari na matatizo mengine ya kiafya.

Kutoushughulisha mwili wako vya kutosha

Watu wanaofanya kazi mashambani, wanaotembea vya kutosha, wanaofanya kazi za mikono au kucheza michezo ya viungo, huchoma sukari ya ziada kwenye damu yao kama mafuta. Lakini watu wanaokaa au kusimama sehemu moja muda wao wote siku nzima hawachomi sukari ya kutosha. Hivyo sukari nyingi hubaki kwenye damu yao.

mwanaume amebeba maboksi mgongoni yaliyoandikwa " Kelele za Bosi", "Mazingira Mapya”>
Msongo unapoongezeka, unaweza kuathiri afya yako.

Msongo

Watu wanapokua na msongo mkubwa kila mara, miili yao huing’ang’ania sukari badala ya kuiachia kutumika. Hii husababisha kiwango cha sukari kwenye damu kuongezeka.

Mafuta kuzunguka tumbo

Kiuno kikubwa au kiribatumbo huongeza uwezekano wa watu kupata kisukari.

Wanafamilia wenye kisukari

Kisukari kinaweza kuriithiwa. Kuna uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa huo iwapo miongoni mwa familia yako kuna watu wenye kisukari.

Utapiamlo

Kama watu hawatapata chakula cha kutosha, miili yao itang’ang’ania sukari wanayokula. Hii inaweza kuanza katika umri wa utotoni au hata mtoto angali bado tumboni.

NWTND Diab Page 7-1.png

Kuzeeka

Watu wenye umri mkubwa zaidi wana uwezekano zaidi wa kupata kisukari.

Kemikali

Baadhi ya kemikali huathiri uwezo wa miili yetu kutumia sukari. Kemikali zinaweza kutufikia kupitia sehemu za kazi, kupitia uchafuzi ndani ya jamii zetu, au kwa sababu huongezwa kwenye chakula au bidhaa zingine ambazo tunatumia.

Jinsi kemikali hatari zinavyochangia kisukari

Sambamba na chakula tunachokula na jinsi tunavyoishi, baadhi ya kemikali huchangia kisukari. Kufanya kazi, kula, kunywa, au kupumua ndani ya mazingira yenye kemikali hatari zifuatazo huongeza uwezekano wa kupata kisukari:

  • Dioksini (Dioxins) huzalishwa katika utengenezaji wa viuatilifu na karatasi, na kutokana na kuchoma plastiki.
  • PCB ni aina ya kemikali ambazo hutumika viwandani kwa ajili ya ufunikaji wa kuhami (insulation) na ulainishaji wa mitambo.
  • Phthalates kawaida hupatikana kwenye krimu za kupaka kwenye ngozi na mafuta.
  • Bisphenols hupatikana kwenye chupa za plastiki ambazo hutumika kwa ajili ya kufungasha maji, juisi na soda.
  • Madini tembo kama vile risasi, zebaki, aseniki, na cadmium, huachiwa kwenye mazingira kupitia shughuli za uchimbaji na usafishaji mafuta, uchimbaji madini, na baadhi ya viwanda.
  • Viuatilifu hutumika kuua wadudu au magugu.


Njia bora zaidi ya kujikinga dhidi ya kemikali hizi ni kutozitumia. Kama kuna kemikali hatari kazini kwako na huwezi kumshawishi mkuu wako wa kazi kubadili na kutumia kemikali zilizo salama zaidi, jiepushe kupumua moshi au harufu yake au kuzigusha. Vaa kifaa cha kukinga pua na mdomo na mavazi mengine ya kuukinga mwili, na kunawa mikono yako mara kwa mara ili zisiingie kwenye chakula chako au mdomoni.

mwanaume akiwa amevaa kinga mdomoni na puani akinyunyizia mimea viuatilifu.

Kila mahali tumezungukwa na kemikali hatari. Jitahidi kula vyakula ambavyo havijanyunyiziwa viuatilifu. Jaribu kutafuta dawa za kufanyia usafi nyumbani na bidhaa za kutunza mwili zenye kiwango kidogo cha kemikali hatari au ambavyo havina kabisa.

Uchafuzi wa maji, hewa na chakula na viuatilifu ni changamoto kubwa sana. Changamoto hii inaweza kutatuliwa tu pale jamii itakaposhinikiza wenye viwanda, na serikali kuhakikisha sheria za usalama kuhusiana na viwanda na mazingira zinatekelezwa.

Kwa taarifa zaidi juu ya kulinda chakula chetu, maji, ardhi na hewa, angalia Mwongozo kwa Jamii juu ya Afya ya Mazingira.



Ukurasa huu ulihuishwa: 20 Mei 2017