Hesperian Health Guides

Kisukari kama fursa ya pili

Katika sura hii:

Kisukari ni ugonjwa hatari lakini unaweza kudhibitiwa. Udhibiti wa kisukari huwapa watu fursa ya kufanya mabadiliko chanya ili waweze kuishi maisha yenye afya, uchangamfu na tija.

Bila kujua jinsi ya kudhibiti kisukari chako, maisha yanaweza kuwa magumu sana. Lakini kwa kupata misaada na maarifa yanayostahili, watu wanaweza kuwa na afya zaidi kuliko siku za nyuma. Kwa sababu afya yao inategemea hali yao ya kisukari, kinapodhibitiwa wanaweza kuanza kushughulika na mambo mengine muhimu katika maisha yao na jamii zao. Watu ambao wamefanikiwa kukidhibiti kisukari wanaweza kusaidia kupigania lishe bora kwa jamii, mishahara bora, kusimamisha uchafuzi wa mazingira na kemikali zenye sumu, kudai usalama ili watu waweze kutembea kwa miguu, au mambo mengine ambayo yanaweza kuwasaidia kushughulisha miili yao, kula vizuri zaidi, na kupunguza msongo katika maisha yao.

Unaweza kuishi na kisukari

NWTND Diab Page 26-1.png

Watu wenye kisukari wanapaswa kubadili jinsi wanavyokula na kuishi.Ufuatao ni ushauri wa kuwasaidia kufanya mabadiliko:

  • Anza na mabadiliko madogo madogo. Kwa mfano, badala ya kuacha utumiaji wa vinywaji vilivyokolezwa sukari mara moja, jaribu kupunguza matumizi ya vinywaji hivyo taratibu. Kupunguza taratibu kiasi cha sukari unayokula au kuongeza kiasi cha mazoezi ni rahisi kutekeleza na kuna uwezekano mkubwa utazoea na kuendelea na utaratibu huo.
  • Amua mwenyewe unataka kubadili nini. Weka lengo kama vile kutembea zaidi, kupunguza uvutaji au kutovuta kabisa, au kuweza kucheza na wajukuu zako.
  • Tafuta msaada. Familia, marafiki, au watu wengine wenye kisukari wanaweza kukusaidia kufanya mabadiliko. Vikundi vya watu wenye kisukari na madarasa au kliniki za kisukari huunganisha watu wenye kisukari ili waweze kusaidiana.
  • Tafuta msaada kwa matatizo ya kisaikolojia. Ni jambo la kawaida kwa watu wenye kisukari kuogopa maisha ya baadaye, kuhuzunika juu ya kuugua mara kwa mara, au kuwa na hasira juu ya mabadiliko yanayohitajika. Hisia za uchungu, huzuni, au kukosa matumaini vinaweza kumzuia mtu mwenye kisukari kufanya mabadiliko ambayo yanahitajika au ambayo anataka kufanya. Ni muhimu kuzungumzia hisia hizi na watu wengine wa karibu wenye weledi, na kujifunza njia za kuishi vizuri kwa matumaini. Kwa taarifa zaidi juu ya huzuni na matatizo mengine ya kisaikolojia, angalia sura Afya ya akili (inaandaliwa).
  • Tafuta sababu zako za kutaka kuwa na afya bora zaidi. Unataka kufanya nini na unataka kujisikia vizuri namna gani? Kwa mfano, fikiria familia yako na kwa nini unataka kuendelea kuishi ukiwa mwenye afya ya kukuwezesha kuwasaidia wanafamilia kwa muda mrefu zaidi. Malengo chanya hukusaidia kufanya mabadiliko na kuendelea vizuri.
Ukurasa huu ulihuishwa: 20 Mei 2017