Hesperian Health Guides

Kisukari: Madawa

Kisukari: Madawa

Dawa za kisukari aina ya 2 kwa njia ya mdomo

Metformin


Dawa ya Metformin husaidia insulini inayozalishwa mwilini kufanya kazi vizuri zaidi, na pia hupunguza uzalishaji wa sukari kwenye ini. Dawa hii hufaya kazi vizuri kwa watu wenye kisukari Aina 2 ambao hawawezi kudhibiti kisukari chao kupitia mabadiliko katika ulaji na mazoezi. Lakini haitumiki kwa watu wenye kisukari Aina 1. Bei yake ni nafuu kuliko dawa zingine za kisukari, haisababishi sukari kwenye damu kupungua kupita kiasi, na haisababishi kuongezeka uzito. Metformin wakati mwingine hutolewa pamoja na matibabu mengine ya kisukari (dawa za sulfo au insulini).

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Kuharisha, kichefuchefu, tumbo kusokota, gesi, na ladha mbaya ya mate mdomoni. Inasaidia kutumia metformin pamoja na chakula ili kupunguza madhara hayo ya pembeni. Kawaida, madhara yake ya pembeni huwa siyo makubwa na hutoweka baada ya wiki 1 au 2 baada ya kuanza dawa au dozi inapoongezwa. Kama madhara ya pembeni yataendelea, jaribu dozi ya chini au dawa tofauti.

MuhimuNBgrnimportant.png

Mtu ambaye amepungukiwa na maji mwilini, au ana maambukizi makubwa anapaswa kusimamisha matumizi ya metformin hadi atakapopata nafuu.

  • Watu wenye matatizo ya figo wanapaswa kupimwa damu kujua hali ya figo zao kabla hawajaanza dawa ya metformin.
  • Watu wenye matatizo madogo ya figo wanapaswa kupewa dozi ndogo ya metformin (isiyozidi miligramu 1000 kwa siku).
  • Watu wenye matatizo makubwa ya figo hawapaswi kutumia dawa ya metformin.


Watu wenye matatizo makubwa ya moyo, ini, au ambao ni watumiaji wakubwa wa pombe kwa kawaida hawapaswi kutumia dawa ya metformin.

Mtu mwenye kisukari Aina 2 ambaye atafanyiwa upasuaji au kupigwa eksirei zinazotumia rangi hapaswi kutumia dawa ya metformin siku 1 kabla na siku 2 baadaye. Hii ni muhimu kuzuia tatizo hatari la ongezeko la kiwango cha asidi ya lactic (lactic acidosis) kwenye damu ambayo huathiri utendaji wa viungo mbalimbali mwilini na kusababisha matatizo makubwa ya kiafya.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png

Kwa mtu yeyote ambaye anatumia dawa za kisukari, kipimo cha kiwango cha sukari kwenye damu kwa kuchunguza tone la damu huweza kuonesha jinsi gani dawa, au dozi mahsusi ya dawa, inavyofanya kazi. Kawaida, mtu huanza na dozi ya chini na baada ya hapo dozi huongezwa taratibu-kidogo kidogo. Hivyo ili kusaidia kutafuta dozi ambayo inafanya kazi vizuri zaidi, vipimo zaidi kuliko kawaida vinapaswa kufanyika kila inapoanzishwa dawa mpya ya kisukari.

Metformin huwa katika vidonge vya miligramu 500, 850, au 1000, na vinapaswa kutumika pamoja na chakula.

NWTND bag arrow.png
Kwa watu wazima, kawaida mtu huanza na miligramu 500 mara 1 kwa siku, pamoja na mlo wa jioni.

Kama viwango vya sukari bado viko juu, dozi inaweza kuongezwa kuanzia wiki inayofuata kwa kutumia kidoge chenye dawa zaidi au kwa kugawa dozi hiyo na kuitumia zaidi ya mara 1 kwa siku.

Kwa mfano:

wiki 1: Tumia miligramu 500 AU
Tumia ½ ya kidonge cha miligramu 850 kila usiku

wiki 2: kutumia miligramu 850 kila siku, tumia ½ ya kidonge cha miligramu 850 na mlo wa asubuhi na ½ ya kidonge cha miligramu 850 na mlo wa jioni AU
Kutumia miligramu 1000 kila siku, tumia miligramu 500 na mlo wa asubuhi na miligramu 500 na mlo wa jioni kila siku.

Kwa watu wazima wengi, metformin hufanya kazi vizuri wanapotumia jumla ya miligramu 1000 hadi 2000 kila siku, nusu asubuhi na mlo wa asubuhi na nusu jioni na mlo wa jioni.

Inawezekana pia kutumia metformin mara 3 kila siku (pamoja na mlo wa asubuhi, mlo wa mchana na mlo wa jioni. Kwa mfano:

Kutumia jumla ya miligramu 1500 kwa siku: tumia miligramu 500 na mlo wa asubuhi, miligramu 500 na mlo wa mchana, na miligramu 500 na mlo wa jioni kila siku.
Zaidi ya miligramu 2000 kwa siku mara nyingi haisaidii.
Kamwe usitoe zaidi ya miligramu 2550 kwa siku.
Dawa ya metformin inapotumiwa na mtoto, daktari au mfanyakazi wa afya mwenye uzoefu huelekeza na kufuatilia kiwango cha dozi.

Dawa zingine ambazo zinaweza kusaidia

Dawa za sulfo na insulini ni dawa ambazo wakati mwingine hutumika badala ya, au pamoja na metformin.

Dawa za sulfo (Sulfonylureas)


Dawa za sulfo (sulfonylureas) ni kundi la dawa tofauti kwa ajili ya watu wenye kisukari Aina 2. Husaidia kongosho kutengeneza insulini zaidi na kuuwezesha mwili kutumia insulini vizuri zaidi. Aina moja ya dawa za sulfo hufanya kazi haraka kudhibiti kiwango cha sukari ambacho kimepanda kupita kiasi, lakini zinapaswa kutumika mara 2 tu kwa siku. Aina nyingine ya dawa za sulfo hufanya kazi taratibu lakini hudumu muda mrefu mwilini. Hivyo, isipokuwa kama inahitajika dozi kubwa zaidi, kawaida dozi yake hutumika mara 1 kwa siku.

Dawa za sulfo zinaweza kutumika peke yake au pamoja na matibabu mengine ya kisukari (metformin au insulini) kudhibiti viwango vya sukari kwenye damu vizuri zaidi. Ufanisi wake unaweza kupungua kama mtu amekaa na kisukari Aina 2 kwa muda mrefu.

Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Dawa ya sulfo inaweza kushusha sukari kwenye damu kupita kiasi haraka sana na kusababisha tatizo la upungufu wa sukari mwilini (angalia Hypoglycemia), hasa kama mtu hajala baada ya kutumia dawa, au amefanya mazoezi sana kuliko kawaida. Hatari hii inaweza kujitokeza zaidi kuhusiana na aina ya dawa za sulfo ambazo hufanya kazi taratibu kama vile glibenclamide (glyburide) na chlorpropamide kwa sababu hudumu muda mrefu mwilini.

  • Ongezeko la hamu ya kula na uzito ni miongoni mwa madhara ya pembeni ambayo yanaweza kutokea. Ulaji wenye afya na kupata mazoezi ya kutosha vinaweza kusaidia kuzuia hali hiyo.
  • Kunywa pombe wakati unatumia dawa za sulfo, hasa chlorpropamide, huweza kusababisha kutapika.
  • Kwa baadhi ya watu, dawa za sulfo husababisha upele mwilini au kudhurika rahisi kutokana na jua.
MuhimuNBgrnimportant.png

Watu wenye ugonjwa wa figo au ini, au ambao kawaida ni watumiaji wa pombe wanapaswa kutumia dawa za sulfo kwa uangalifu.

Kwa watu wenye umri mkubwa zaidi (zaidi ya miaka 65) au watu wenye ugonjwa wa figo, ni salama kutumia dawa za sulfo zinazofanya kazi haraka, kama vile glipizide, na kuanza na dozi ya chini zaidi, kuzuia sukari ya damu kupungua kupita kiasi.

Dawa ya sulfo haiwezi kutumika kwa watu wenye kisukari Aina 1 au kwa watu ambao wana mzio na dawa hizo.

Isipokuwa glibenclamide (glyburide), wanawake wajawazito wanapaswa kuepuka kutumia dawa za sulfo isipokuwa kama hakuna dawa nyingine.

Watoto wenye kisukari Aina 2 kawaida hawapewi dawa za sulfo.

Dalili za kuzidisha dawa (dozi)

Dalili za hatari za upungufu wa sukari kwenye damu ni pamoja na matatizo katika kutembea, kujisikia mdhaifu, matatizo katika kuona, kuchanganyikiwa, kupoteza fahamu, au mashambulio. Kama mtu ana fahamu, mpe kitu kitamu ale haraka na mlo kamili haraka iwezekanavyo. Kama hana fahamu, weka sukari au asali chini ya ulimi wake na endelea kumpa kidogo kidogo hadi atakapoamuka na kuweza kula mwenyewe.

Mwingiliano na dawa zingine

Dawa zingine zinaweza kutofanya kazi vizuri kama mtu atakuwa anatumia pia dawa za sulfo. Na kama mtu anatumia insulini, baadhi ya dawa za sulfo zinaweza kutomsaidia. Ongea na mfanyakazi wa afya juu ya dawa zote ambazo unatumia.

Jinsi ya kutumiaNBgrnpill.png

Kwa mtu yoyote ambaye anatumia dawa za kisukari, kipimo cha tone la damu kwa ajili ya sukari kunaweza kuonesha dawa au dozi inafanya kazi kwa ufanisi gani. Kawaida, mtu huanza na dozi ya chini na baada ya hapo dozi hupandishwa pole pole. Hivyo vipimo zaidi kuliko kawaida hufanyika wakati wa kuanza dawa mpya kusaidia kujua dozi ipi inafanya kazi vizuri zaidi.

Dawa za sulfo ni kwa ajili ya watu wazima wenye kisukari Aina ya 2.

  • Tumia dawa ya sulfo dakika 30 kabla ya kula. Ni muhimu kula baada ya kutumia dawa hii kwa sababu kama hutakula sukari kwenye damu yako inaweza kupungua sana kupita kiasi hadi kufikia kiwango hatarishi.
  • Kama unakula vizuri na kutumia dawa kama inavyotakiwa lakini sukari kwenye damu yako ikabaki juu, ongea na mfanyakazi wa afya. Unaweza kuhitaji kubadilishiwa dozi au dawa.
  • Matibabu ya dawa za sulfo kawaida huanza na dozi ndogo ambayo hutumika mara 1 kwa siku kabla ya mlo wa asubuhi. Dozi hupandishwa polepole katika muda wa wiki kadhaa kama kiwango cha sukari kwenye damu kitabaki juu.


Kila dawa ya sulfo kwa watu wazima hutolewa katika dozi tofauti. Mtu huanza na dozi ya chini na hupimwa siku kadhaa baadaye kujua kama imeshuka vya kutosha. Kama atahitaji dozi kubwa zaidi, dozi yake itaongezwa.

Baada ya wiki moja, atapimwa tena na dozi inaweza kurekebishwa kama itahitajika. Dozi kubwa ya sulfo ni hatari sana. Hivyo dozi hubadilishwa kidogo kidogo tu kila mara.

GLIBENCLAMIDE (GLYBURIDE)

Dawa ya Glibenclamide ni dawa kutoka kundi la sulfo ambayo hufanya kazi polepole na kawaida huwa katika vidonge vya miligramu 1.25, 2.5, na 5.

NWTND bag arrow.png
Dozi ya kuanzia kawaida ni kati ya miligramu 1.25 na miligramu 5, mara 1 kila siku, kabla ya mlo wa asubuhi.

Kama itahitajika, dozi inapaswa kuongezwa. Watu wengi hustahimili vizuri dozi kati ya miligramu 2.5 na 10 kila siku. Kama unatumia miligramu 10 au zaidi kila siku, ni kawaida kugawa dozi ya siku 1 mara 2, na kutumia mara 2 kwa siku, nusu ya kwanza mara moja kabla ya mlo wa asubuhi, na nusu ya pili mara moja kabla ya mlo wa jioni.

Kwa mfano:

NWTND bag arrow.png
Kutumia miligramu 10 kila siku: tumia kidonge cha miligramu 5 kabla ya mlo wa asubuhi na kidonge cha miligramu 5 kabla ya mlo wa jioni.
NWTND bag arrow.png
Kutumia miligramu 15, tumia vidong 3 vya miligramu 2.5 na mlo wa asubuhi na vingine 3 vyenye miligramu 2.5 kabla ya mlo wa jioni. Usitumie zaidi ya miligramu 20 katika siku moja.


GLIMEPIRIDE

Glimepiride ni miongoni mwa dawa za sulfo ambazo zinafanya kazi taratibu na kawaida huwa katika vidonge vya miligramu 1, miligramu 2, na miligramu 4.

NWTND bag arrow.png
Dozi ya kuanzia ni kati ya miligramu 1 na miligramu 2, mara 1 kila siku, kabla ya mlo wa asubuhi.

Kama itahitajika, dozi inaweza kuongezwa. Watu wengi hupata maendeleo mazuri na dozi kati ya miligramu 1 na miligramu 4 kila siku, ikitumika mara 1 kila siku. Usitumie zaidi ya miligramu 8 katika siku moja.


GLIPIZIDE

Glipizide ni dawa ya sulfo ambayo inafanya kazi haraka na kawaida huwa katika vidonge vya miligramu 5, na miligramu 10.

NWTND bag arrow.png
Dozi ya kuanzia kawaida ni miligramu 2.5, mara 1 kila siku, kabla ya mlo wa asubuhi. Kama ni kuanza na dozi ya miligramu 2.5 kila siku, tumia ½ kidonge cha miligramu 5.

Kama itahitajika, dozi inaweza kuongezwa. Watu wengi hupata maendeleo mazuri na dozi ya kati ya miligramu 2.5 na miligramu 20 kila siku. Kama unatumia dozi ya miligramu 10 au zaidi kwa siku, ni kawaida kugawa dozi ya siku katika nusu na kutumia mara 2 kila siku, nusu mara moja kabla ya mlo wa asubuhi, na nusu nyingine mara moja kabla ya mlo wa jioni.

Kwa mfano:

NWTND bag arrow.png
Kutumia dozi ya miligramu 10 kila siku: tumia kidonge cha miligramu 5 kabla ya mlo wa asubuhi na kingine cha miligramu 5 kabla ya mlo wa jioni.


Usitumie zaidi ya miligramu 20 katika siku moja.

GLICLAZIDE na GLICLAZIDE MR

Dawa ya gliclazide huwa katika miundo 2.

Dawa ya gliclazide ya kawaida huwa katika vidonge vya miligramu 80.

NWTND bag arrow.png
Dozi ya kuanzia kawaida ni kati ya miligramu 40 na 80, mara 1 kila siku, kabla ya mlo wa asubuhi. Kama unaanza na dozi ya miligramu 40 kila siku, tumia ½ kidonge cha miligramu 80.

Kama itahitajika, dozi inaweza kuongezwa. Watu wengi hupata maendeleo mazuri na dozi ya miligramu kati ya 40 na miligramu 240 kila siku. Kama unatumia dozi ya miligramu 160 au zaidi kwa siku, ni kawaida kuigawa dozi ya siku katika nusu na kutumia mara 2 kila siku: nusu ya kwanza mara moja kabla ya mlo wa asubuhi, na nusu ya pili mara moja kabla ya mlo wa jioni. Kwa mfano:

NWTND bag arrow.png
Kutumia dozi ya miligramu 160 kila siku: tumia kidonge cha miligramu 80 kabla ya mlo wa asubuhi na kingine cha miligramu 80 kabla ya mlo wa jioni.


Usitumie zaidi ya miligramu 320 katika siku moja.

Gliclazide MR (iliyorekebishwa) huwa katika vidonge vya miligramu 30 na ina dozi tofauti na gliclazide ya kawaida. Dozi ya kuanzia kwa kawaida ni miligramu 30 za gliclazide MR kila siku.

Kama itahitajika, dozi inaweza kuongezwa. Watu wengi hupata maendeleo mazuri na dozi ya miligramu kati ya 30 na miligramu 120 kila siku kabla ya mlo wa asubuhi. Kama unatumia gliclazide MR, usitumie zaidi ya miligramu 120 katika siku moja.

CHLORPROPAMIDE

NWTND bag arrow.png
Dozi ya kuanzia kwa kawaida ni kati ya miligramu 100 na 250 kila siku, kabla ya mlo wa asubuhi.

Kama itahitajika, dozi inaweza kuongezwa. Watu wengi hupata maendeleo mazuri na dozi ya miligramu kati ya 100 na miligramu 500 mara 1 kila siku kabla ya mlo wa asubuhi.

Usitumie zaidi ya miligramu 750 katika siku moja.Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Jan 2024