Hesperian Health Guides

Dawa za kisukari kwa njia ya sindano

Kisukari: Madawa

Insulini


Insulini ni homoni ambayo huzalishwa katika kongosho na huusaidia mwili kuchakata sukari kwenye vyakula. Ni muhimu kwa ajili ya uhai, na kama mwili hauwezi kuzalisha homoni hiyo, kemikali ya insulini hutumika badala yake. Watu wote wenye kisukari Aina ya 1 watahitaji kutumia dawa ya insulini kwa maisha yao yote kama miili yao haiwezi kuzalisha homoni hiyo. Katika hali hii, dawa za kumeza kama vile metformin au dawa za sulfo zinakuwa hazitoshelezi. Hivyo, insulini inaweza kuwa ndiyo njia pekee ya kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu.

Insulini lazima itolewe kwa njia ya sindano. Inaweza kuwa katika vichupa vidogo, na unaweza kutumia sindano kuandaa dozi sahihi. Insulini inaweza pia kuwa katika kifaa kinachofanana na kalamu ambacho hupima dozi sahihi na ni rahisi zaidi kutumia.

  • Insulini inayofanya kazi haraka: aina kuu ya insulini inayofanya kazi haraka hujulikana kama insulini ya “kawaida”. Lispro na aspart ni miongoni mwa insulini ambazo hufanya kazi haraka. Aina hii ya insulini hutumika kabla ya mlo.
  • Insulini inayofanya kazi taratibu: NPH ndiyo aina kuu ya insulini ambayo hufanya kazi taratibu lakini hukaa mwilini muda mrefu. Glargine na determir pia zinafanya kazi taratibu kwa muda mrefu. Aina hii ya insulini hutumika mara 1 au 2 kwa siku.
  • Dozi ya insulini mchanganyiko: dozi mchanganyiko wa insulini ambazo hufanya kazi taratibu lakini kwa muda mrefu na insulini ambazo hufanya kazi haraka inayotumika sana ni NPH /regular 70/30, na hutumika mara 2 kwa siku. Dozi nyingine ya insulini mchanganyiko inayotumika sana ni NPH /regular 50/50.
Madhara ya pembeniGreen-effects-nwtnd.png

Insulini inaweza kusababisha sukari kwenye damu kushuka sana na haraka mno kiasi cha kuhatarisha maisha (angalia Dharura za kisukari).

Tatizo la kuongezeka uzito linaweza kudhibitiwa kwa kula vyakula vyenye afya na kujishughulisha kimwili baada ya kuanza matumizi ya insulini.

MuhimuNBgrnimportant.png

Miongoni mwa hatari kuu kuhusiana na matumizi ya insulini ni kwamba inaweza kusababisha sukari kwenye damu kupungua mno kupita kiasi, hali ambayo ni dharura ya kitabibu.Hii inaweza kutokea zaidi kama mtu ataruka mlo, atakuwa amefanya mazoezi makubwa, au baada ya kutumia insulini nyingi kimakosa.

Ni muhimu kwa mtu ambaye anatumia insulini kuelewa jinsi ya kuitumia kwa usahihi na kutambua dalili za hatari kuashiria upungufu wa sukari kwenye damu kupita kiasi. Kama sivyo, lazima apate msaada nyumbani. Mtu ambaye tayari ana tatizo la kuona atahitaji msaada wa ziada kuhakikisha anatumia dozi sahihi.

Kama mtu atakuwa anatumia insulini zote- zinazofanya kazi taratibu na zinazofanya kazi haraka, ni muhimu sana kuelewa tofauti katika insulini hizo na kuzitumia kwa usahihi.

Jinsi ya kutumiaNBgrninject.png

Insulini inapaswa kuhifadhiwa sehemu yenye ubaridi, mbali na joto kali au ubaridi mkali. Inaweza kuhifadhiwa kwenye friji sehemu isiyo na ubaridi mkali lakini siyo kwenye friza. Kamwe usiruhusu insulini kuganda barafu.

Kwa mtu yoyote ambaye anatumia dawa za kisukari, kipimo cha tone la damu kwa ajili ya sukari kinaweza kuonesha ni kwa ufanisi gani dawa, au dozi mahsusi ya dawa inavyofanya kazi. Kawaida mtu huanza na dozi ya chini, halafu dozi huongezwa kidogo kidogo. Hivyo vipimo zaidi kuliko kawaida hufanyika wakati wa kuanza dawa mpya ili kusaidia kupata dozi ambayo inafanya kazi vizuri zaidi.

KWA KISUKARI AINA 1: Watu ambao wana kisukari Aina 1 wanahitaji insulini kila siku kuendelea kuwa na afya. Insulini inayofanya kazi taratibu inahitajika kutuliza hali ya mtu usiku mzima na kesho yake siku nzima, na mtu huyu atajifunza jinsi ya kurekebisha dozi ya insulini inayofanya kazi haraka kutegemea na milo na wakati anapokuwa anafanya mazoezi. Wafanyakazi wenye uzoefu watamsaidia mtu mwenye kisukari na familia yake kutambua aina za insulini na dozi ambayo inafanya kazi vizuri zaidi.

KWA KISUKARI AINA 2
Watu wenye kisukari Aina 2 mara nyingi huanza kwa kutumia insulini inayofanya kazi taratibu kwa njia ya sindano mara moja kila siku, aidha dozi hiyo ya sindano peke yake au kama nyongeza kwa dawa zingine za kumeza kama vile metformin au dawa za sulfo.

Dozi za kuanzia za insulini inayofanya kazi taratibu zinapaswa kuwa za chini, kama vile uniti 10. Kama utaanza na sindano moja ya NPH, inapaswa kutolewa usiku. Lakini kwa sababu NPH hudumu mwilini saa 12 tu, watu wengi huitumia mara 2 kwa siku kuepuka kiwango cha sukari kubadilika ghafla.

Mfanyakazi wa afya anaweza kukuongezea kidogo kidogo kiasi cha insulini inayofanya kazi taratibu hadi sukari kwenye damu itakaposhuka na kukaa vizuri. Mara sukari kwenye damu inapofikia kiwango kizuri, utaendelea kutumia dozi hiyo hiyo kila siku. Inaweza kuchukua wiki kadhaa kupata dozi iliyo sahihi.

Sukari kwenye damu inaweza kuwa katika kiwango kizuri muda wa asubuhi, lakini kuwa katika kiwango cha juu baada ya kula. Kama hali hii itatokea, mtu anaweza kuhitaji insulini inayofanya kazi haraka kama vile insulini ya kawaida ikitolewa kabla ya mlo. Insulini inayofanya kazi haraka inapaswa kuanza kutolewa katika dozi ndogo, takriban uniti 4. Kawaida huanza kutolewa mara moja kwa siku kabla ya mlo mkubwa zaidi wa siku, lakini baadhi ya watu watahitaji kuitumia kabla ya kila mlo. Insulini ya kawaida inapaswa kutumika dakika 30 kabla ya kula. Kupima sukari kwenye damu yako mara kwa mara mwanzoni kutamsaidia mfanyakazi wa afya kurekebisha dozi yako ya insulini inayofanya kazi haraka, ili kupata kiasi sahihi ambacho unahitaji.

Dozi mchanganyiko ya insulini ni mbadala mwingine kwa watu ambao wanahitaji zaidi ya insulini inayofanya kazi taratibu. Kwa mfano, NPH /Regular 70/30 hutolewa mara 2 kwa siku, dakika 30 kabla ya mlo wa asubuhi na dakika 30 baada ya mlo wa jioni.

Dalili za kuzidisha dozi ya insulini

Dalili za hatari za kiwango cha sukari kwenye damu kushuka sana ni pamoja na matatizo katika kutembea, kujisikia mchovu, uoni hafifu, kuchanganyikiwa, kupoteza fahamu au mashambulio. Kama mtu ana fahamu, anahitaji kula kitu chenye sukari haraka na baada ya hapo kupata mlo kamili. Kama mtu amepoteza fahamu, weka sukari kidogo au asali chini ya ulimi wake na endelea kumpa kidogo kidogo hadi atakapoamuka na kuweza kujihudumia.Ukurasa huu ulihuishwa: 05 Jan 2024