Hesperian Health Guides
Uzazi wa mpango
HealthWiki > Toleo Jipya: Mahali Pasipo na Daktari > Uzazi wa mpango
Sura hii inajadili njia mbalimbali za kuzuia mimba au kupanga muda wa kupata mimba nyingine. Njia zote ambazo zimeelezewa katika sura hii hutumika sehemu zote duniani.
Yaliyomo
Kwa nini uzazi wa mpango?
Kuna njia nyingi salama na zenye uhakika za kuzuia mimba, au kukusaidia kuchagua lini upate mtoto na idadi ya watoto ungependa kuzaa. Unaweza kupata njia za kuzuia mimba zenye gharama nafuu au zisizo na malipo kabisa kutoka kliniki za uzazi wa mpango katika mazingira yako ya kawaida. Uzazi wa mpango hujulikana pia kama kama njia ya kudhibiti uzazi. Haijalishi maneno gani ambayo yanatumika, uzazi wa mpango una manufaa mengi:
- Kuzaa idadi ndogo ya watoto ni bora zaidi kwa afya ya mwanamke kuliko kuzaa watoto wengi. Kwa kutumia njia ya uzazi wa mpango, unaweza kuamua lini mwili wako uko katika hali nzuri kiafya kubeba mimba.
- Kuvuta subira katika uzazi na kuacha muda wa kutosha kati ya mtoto mmoja na mtoto mwingine hukuwezesha kuwaandalia watoto utakaowazaa maisha ya uhakika, na kukupa muda zaidi, nguvu, na fedha kwa ajili ya kuwahudumia watoto ambao tayari unao.
- Kuamua kama unataka kupata watoto na lini, bila watu au mtu mwingine kukuamrisha kupata mimba au usipate mimba: kuchukua hatamu ya maisha yako.
- Kufurahia tendo la kukutana kimwili bila kuwa na wasiwasi wa kupata mimba kama wewe na mwenzako hamtaki au hamjawa tayari kupata mtoto.
- Uzazi wa mpango huwasaidia wanawake kuepuka utoaji mimba usiyo salama, tatizo ambalo husababisha vifo vya maelfu ya wanawake kila mwaka.
Uzazi wa mpango, tendo la ngono, mimba — wakati mwingine ni mambo magumu kuyazungumzia. Kitabu cha Hesperian kijulikanacho kama Juhudi za afya kwa wanawake (Health Actions for Women) kimependekeza njia za kuwawezesha wanaume na wanawake kuuzungumzia uzazi wa mpango na masuala mengine ya afya ya wanawake.
Baadhi ya watu hupenda kuzaa watoto wengi-hasa watu wa kawaida na mara nyingi wenye hali duni (baadhi ya watoto kufariki wakiwa wadogo) kwa sababu watoto husaidia kufanya kazi na kuwatunza wazazi wao wanapozeeka.
Hali ni tofauti katika nchi zenye mgawanyo mzuri wa rasilimali na manufaa yatokanayo. Mahali ambapo ajira, makazi, na huduma za afya vinapatikana kwa urahisi zaidi, na mahali ambapo wanawake wana fursa sawa na wanaume kielimu, ajira, na katika kuendesha maisha yao, watu mara nyingi huchagua kuwa na familia ndogo. Sababu ni kwamba, kwa kiasi fulani, hawahitaji kuwa tegemezi kwa watoto wao kiuchumi, na wana imani kubwa zaidi kuwa watoto wao wataishi maisha bora kiafya, kijamii na kiuchumi.
Watu hutumia njia za uzazi wa mpango ikiwa:
- Inatolewa kwa gharama nafuu au bila malipo.
- kuna njia za uzazi wa mpango tofauti ili watu waweze kuchagua njia ipi inayowafaa.
- hakuna mtu anayeshinikizwa au kulaghaiwa kutumia njia hiyo ya uzazi wa mpango.
- wanaume wanaelewa na kuamini manufaa ya uzazi wa mpango, na kuwasikiliza wanawake wanachotaka.
- mtu yeyote ambaye anataka kutumia uzazi wa mpango anaweza kuipata huduma hiyo kwa urahisi, wakiwemo vijana au watu wazima, ambao wameolewa na hawajaoa au kuolewa, na watu wenye ulemavu.
Uzazi wa mpango ni kwa ajili ya nani ?
Baadhi ya watu hufikiri kuwa uzazi wa mpango ni kwa ajili ya wanawake walioolewa tu. Lakini wanawake wengi ambao wameoolewa na hawajaolewa hufanya tendo la ngono, na wengi wanataka kufurahia tendo hilo bila kuwa na wasiwasi au uoga wa kupata mimba. Vilevile, wanawake mara nyingi huwa hawana maamuzi ya mwisho juu ya tendo la ngono. Baadhi hushinikizwa au kulazimishwa. Hata hivyo, bila uzazi wa mpango, mwanamke yeyote, aliyeolewa au hajaolewa, mwenye umri mdogo au mkubwa, anaweza kupata mimba. Ukiwa mfanyakazi wa afya au katika nafasi yotote ya uelimishaji, ni muhimu kueneza elimu ya uzazi wa mpango kwa wanawake wote.
Unapaswa pia kutafuta njia za kuwapa elimu wanaume juu ya uzazi wa mpango. Baadhi ya njia za uzazi wa mpango, mfano kondomu, huhitaji azma ya wanaume. Na mara nyingi mwanaume hutarajiwa kuchangia uamuzi juu ya njia ya uzazi mwenzi wake atakayoitumia. Kuwasiadia wanaume kuelewa manufaa au faida za uzazi wa mpango huwasaidia kuondokana na wasiwasi wao juu ya njia husika na kuelewa jinsi uzazi wa mpango unavyowasaida pia.
Kuwapa elimu wanaume juu ya uzazi wa mpango pia humrahihishia mwanamke kuongea na mume au mwenzi wake juu ya uzazi wa mpango na na kuamua njia ipi watumie. Kama mwanaume bado hataki kutumia uzazi wa mpango hata baada ya kujifunza na kuelewa faida zake, mwanamke atahitaji kuamua iwapo anapaswa kuendelea kuitumia katika hali kama hiyo. Kuna njia ambazo mwanamke anaweza kutumia bila mwanaume kujua.
Elezea jinsi ya kutumia njia mbalimbali za uzazi wa mpango kwa usahihi na kuwa mkweli juu ya madhara yake ya pembeni. Sababu kuu ya wanawake kuacha kutumia njia ya uzazi wa mpango ni kutokana na kero ya madhara yake ya pembeni. Lakini kama atajua mapema juu ya madhara hayo, anaweza kuwa tayari kuendelea na njia hiyo hadi madhara yatakapopungua au kuachagua njia nyingine inayomfaa zaidi.
Kuwasaidia vijana
Vijana wanaweza kuanza mahusiano ya kimapenzi au hata kingono kabla hawajajua jinsi ya kuzuia kupata mimba. Jamii zinaweza kuwasaidia vijana kupata taarifa ambazo wanahitaji ili kufanya maamuzi sahihi. Shule zinaweza kuwapatia vijana elimu ya afya ambayo inajumuisha suala la mimba. Vijana pia wanaweza kufundishwa kuwa walelimishaji rika na muda maalum unaweza kupangwa kwenye kliniki na sehemu zingine ili kuwapatia vijana unasihi na nyenzo za kuzuia mimba.