Hesperian Health Guides

Njia za asili za uzazi wa mpango

Katika sura hii:

Unyonyeshaji

mwanamke akimnyonyesha mtoto, mwanaume akiwa amemweka mkono begani.

Mwanamke anapokua ananyonyesha, mwili wake huzalisha homoni ambazo huzuia ujauzito kwa miezi kadhaa. Unyonyeshaji unategemewa katika kuzuia mimba pale ambapo:

  • Mtoto ana umri chini ya miezi 6.


NA

  • Utakuwa unampa maziwa ya mama tu, bila chakula au kinywaji kingine, na unamnyonyesha mtoto wako mara kwa mara, mchana na usiku.


NA

  • Bado hujapata hedhi ya kila mwezi baada ya kujifungua.


Mara utakapoanza kumpa mtoto wako vyakula vya watoto au kurudia kupata hedhi tena, unyonyeshaji hautaweza kukusaidia tena kuzuia mimba.

Kuelewa siku za kuweza kupata mimba (kuhesabu siku)

Mwanamke anaweza kupata mimba tu wakati wa siku zake za rutuba, pale yai la uzazi kutoka kwenye mfuko wa mayai linapoachiwa na kuanza safari kupitia mirija ya uzazi likielekea kwenye tumbo la uzazi (kizazi au mji wa mimba). Safari hii huchukua siku kadhaa na hufanyika mara moja kwa mwezi. Kwa kuepuka ngono katika kipindi hiki cha rutuba, mwanamke anaweza kuzuia mimba. (Au kama wenzi wanatafuta ujauzito, wanaweza kufanya ngono katika kipindi hiki kuongeza uwezekano wa mimba kutunga.)

Njia ya kuhesabu siku iweze kufanya kazi, mwanamke anapaswa kuwa anapata hedhi zake kwa mpangilio unaofanana, na anapaswa kutunza vizuri kumbukumbu za hatua muhimu katika mzunguko wake wa hedhi. Mwanaume anapaswa kuwa tayari kusaidia katika kufanikisha njia hii, kwa sababu wakati wa siku za mwanamke za rutuba, wanatakiwa kuepuka kufanya ngono inayohusisha mwingiliano wa kimwili wa ume kwenye uke. Wanaweza kufanya aina zingine za ngono, au wanaweza kutumia kondomu kila wakati wa kipindi cha rutuba ya mwanamke.

Hii inaweza kuwa njia nzuri kwa mwanamke ambaye anataka kudhibiti idadi ya watoto alionao. Lakini wakati mwingine, mzunguko wa hedhi hubadilika bila kutarajiwa. Watu mara nyingi hawatunzi kumbukumbu au kufuatilia mzunguko huo, na hivyo ni jambo la kawaida kupata mimba wakati wa kutumia njia hii. Njia ya kuhesabu siku haitoi kinga dhidi ya magonjwa yanayoambukizwa kupitia ngono vikiwemo VVU, ambavyo vinaweza kuenezwa wakati wote wa mzunguko wa hedhi ya mwanamke.

Jinsi ya kutumia njia ya kuhesabu siku

mwanamke akihesabu kwenye vidole vyake na kutafakari.
Nilianza hedhi siku 8 zilizopita, hivyo hatuwezi kufanya ngono leo, au kwa siku 10 zijazo. Ni bora niende kwa dada yangu.

Hesabu idadi ya siku za mzunguko wako wa hedhi kwa miezi kadhaa. Anza kuhesabu siku ya kwanza ya kuona damu ya hedhi. Siku ya mwisho ya mzunguko huo ni siku ya mwisho kabla ya kuona damu ya hedhi tena. Kama una idadi ya siku zinazofanana, na mzunguko wako una kati ya siku 26 na 32, njia ya kuhesabu siku inaweza kufanya kazi kwako.

Mara baada ya kuhesabu mzunguko wako wa hedhi kwa miezi kadhaa na una uhakika kwamba hedhi yako huja kwa mpangilio wa siku zile zile, basi unaweza kuanza kutumia njia hii. Epuka kufanya ngono kuanzia siku ya 8 hadi siku ya 19 ya kila mzunguko wa hedhi. Au tumia kondomu katika siku hizo.

Unapaswa kuendelea kutunza kumbukumbu ya hesabu ya siku na tarehe za kila mzunguko ili njia hii iweze kufanya kazi. Kama mzunguko wako wa hedhi utabadilika, tumia njia nyingine hadi mzunguko wako utakaporudia mpangilio unaofanana kwa miezi kadhaa.

Mwili wa mwanamke huzalisha ute au utando telezi unaofanana na kamasi wakati wa siku zake za rutuba ili kusaidia mbegu za kiume kuingia kwenye kizazi au tumbo la uzazi. Hivyo kukagua ute huu kila siku kunaweza kusaidia kujua lini mwanamke yuko katika kipindi chake cha rutuba.

NWTND FP Page 18-2.png
NWTND FP Page 18-3.png
Ute au utando telezi kama kamasi = rutuba Ute mweupe, kavu, unanata na kuganda = siyo wakati wa rutuba

Kuchomoa ume, kumwaga nje

Mwanaume kuchomoa ume wake kutoka kwa mwanamke, mbali na uke kabla hajaachia shahawa, husaidia kuepusha mimba. Hii inawezekana kama mwanaume ana uwezo wa kujidhibiti na ana azma ya kufanya hivyo. Njia hii haifai kwa wanaume ambao huachia shahawa bila kutarajia. Hata kama mwanaume atachomoa ume, shahawa kidogo zenye mbegu za kiume zinaweza kupenya na kusababisha mimba. Hivyo, njia hii huenda siyo nzuri kwa watu wenye uhakika kuwa hawataki mimba. Vile vile, kuchomoa ume hakutoi kinga dhidi ya maambukizi yanayopitia kwenye ngono.

Ngono bila kuingiliana kimwili

NWTND FP Page 19-1.png

Kuna njia nyingi za kuwa karibu na mwenzi, kupata raha ya kingono, na kuonesha mapenzi zaidi ya ngono ya kawaida. Baadhi ya wenzi hufanya ngono kwa njia ya mdomo. Huwezi kupata mimba kwa njia hii. Wengine hufanya ngono kwa njia ya haja kubwa. Hii pia haiwezi kusababisha mimba. Lakini unaweza kuambukizwa magonjwa ya ngono vikiwemo VVU, kupitia ngono kwa njia hizo. Kutumia mikono yako kumpa mwenzi raha ya kingono ni salama sana. Haiwezi kusababisha mimba na kueneza maambukizi yanayopitia ngono.