Hesperian Health Guides

Kufunga uzazi kabisa, upasuaji

Katika sura hii:

Kwa wale ambao hawataki kuzaa watoto wengine tena, ufungaji uzazi kabisa ni salama, na huhitaji upasuaji mdogo kwa wanawake na wanaume. Katika nchi nyingi, huduma hii hutolewa bila malipo. Ulizia kwenye kituo cha afya au hospitalini juu ya huduma hii. Ufungaji uzazi hautoi kinga dhidi ya maambukizi yanayoenezwa kupitia ngono, vikiwemo VVU.

Kwa wanawake, upasuaji huu hujumuisha kufunga mirija ya kusafirisha mayai ya uzazi. Njia moja wapo ni kukata sehemu ndogo karibu na kitovu ili mirija kutoka kwenye mifuko ya mayai (mahali mayai huzalishwa) iweze kukatwa na kufungwa. Kawaida upasuaji huu mdogo hufanyika kwenye chumba cha daktari bila kumweka mwanamke usingizini. Upasuaji huu hauna madhara juu ya vipindi vya hedhi ya mwanamke au uwezo wake wa kufanya tendo la ngono, na badala yake unaweza kuongeza starehe katika tendo hilo kwa sababu mwanamke anakua hana wasiwasi tena juu ya kupata mimba.

Kwa wanaume, upasuaji wa kufunga uzazi hujulikana kama vasekitomi. Vasekitomi inaweza kufanyika kwa urahisi na haraka katika chumba cha daktari au kwenye kituo cha afya bila kumweka mwanaume usingizini. Upasuaji huu tena ni salama zaidi na hukamilika haraka kuliko wa mwanamke. Mapumbu au makende hayatolewi na upasuaji hauna madhara yoyote juu ya uwezo wa mwanaume kufanya tendo la ngono, au starehe inayohusiana. Shahawa za mwanaume hutoka kama zamani, lakini bila mbegu za kiume ndani yake.

mwili wa mwanamke ukionesha mahali upasuaji kwa ajili ya kufunga uzazi hufanyika.
Sehemu ndogo hukatwa hapa
mwili wa mwanaume ukionesha mahali upasuaji kwa ajili ya kufunga uzazi hufanyika.
Sehemu ndogo hukatwa hapa ili mirija kutoka kwenye makende ya mwanaume iweze kukatwa na kufungwa.