Hesperian Health Guides
Njia ya kitanzi
Kitanzi cha kuzuia uzazi ni kidude kidogo cha plastiki, au plastiki na shaba, ambacho huwekwa kwenye kizazi cha mwanamke na mtaalam wa afya. Kitanzi huzuia mbegu za kiume kurutubisha yai la uzazi, na pia huzuia yai kutojibanza kwenye ukuta wa tumbo la uzazi. Kwa taarifa zaidi juu ya jinsi ya kufunga kitanzi, angalia Sura ya 21 ya Kitabu cha wakunga (A Book for Midwives), ambacho kinapatika kutoka shirika la Hesperian.
Njia ya kitanzi ina kiwango kikubwa cha ufanisi, na kitanzi kinaweza kukaa ndani ya kizazicha mwanamke kwa muda kuanzia miaka 5 hadi 12, kutegemea na aina ya kitanzi. Kitanzi hakitoi kinga dhidi ya maambukizi yanayopitia ngono vikiwemo VVU.
Kitanzi ni njia salama kwa wanawake ambao wamewahi kupata ujauzito na wale ambao hawajawahi kupata mimba. Kitanzi kinaweza kuingizwa kwenye kizazi cha mwanamke wakati wote ule anapokuwa hana ujauzito, na akiwa hana maambukizi ukeni au maambukizi yanayopitia ngono. Kitanzi kinaweza pia kuondolewa na mtalaam wa afya wakati wowote ule. Baada ya kuondolewa, mwanamke anaweza kupata mimba bila kuchelewa.
Mara baada ya kuingizwa kwenye kizazi, siyo rahisi kitanzi kutoka lakini inawezekana. Mara moja kwa mwezi, unaweza kukagua kama kamba za kitanzi ambazo huninginia kutoka kwenye mlango wa kizazi bado zipo kwa kuingiza kidole ndani ya uke wako na kuzigusa (lakini siyo kuzivuta). Kama huwezi kuzigusa au kama unafikiri kitanzi kimetoka, tumia kondomu au epuka kufanya ngono hadi utakapopata uchunguzi wa mtaalam wa afya.
Madhara ya pembeni ambayo yanaweza kutokea kutokana na matumizi ya njia ya kitanzi
Madhara ya pembeni ya kawaida ni hedhi kuwa nzito zaidi, ikiambatana na maumivu zaidi kuliko kawaida. Hali hii inaweza kuumiza lakini siyo hatari na taratibu hupungua baada ya miezi michache. Baadhi ya aina za vitanzi vina homoni ya projestini, ambayo husaidia kupunguza kero na damu ya hedhi. Kitanzi chenye projestini kinaweza kusababisha madhara ya pembeni yanayofanana na ya vidonge vidogo vya majira.
Nani hapaswi kutumia kitanzi
- Wanawake wenye saratani ya mlango wa kizazi au tumbo la uzazi. Wanawake wenye saratani ya matiti hawapaswi kutumia kitanzi chenye projestini, lakini wanaweza kutumia kwa usalama kitanzi chenye shaba.
- Wanawake wanougua kisonono, klamidia, au maambukizi sehemu ya nyonga (kwenye kinena). Kwa taarifa zaidi juu ya ugonjwa wa kisonono na klamidia, angalia Matatizo na maambukizi sehemu za ukeni na umeni (kinaandaliwa).
- Kwa taarifa zaidi juu ya maambukizi sehemu ya nyonga, angalia "Maambukizi Sehemu ya Nyonga (Pelvic Infection)" katika Maumivu Tumboni, Kuhara na Minyoo.