Hesperian Health Guides

Uzazi wa mpango: Kutumia vidonge vya majira

Vidonge vya kutumia kwa njia ya mdomo kudhibiti uzazi

Vidonge vingi vya kudhibiti uzazi hujumuisha homoni 1 au 2 zinazofanana na homoni ambazo hutengenezwa na mwili wa mwanamke. Homoni hizi zinaitwa estrojeni na projestini.

Vidonge vya kudhibiti uzazi au vidonge vya majira huja vikiwa na nguvu tofauti za kila homoni na pia huuzwa chini ya majina ya kibiashara tofauti. Aina 3 za kwanza ambazo zimeoneshwa hapa chini zina homoni ya estrojeni na projestini (angalia vidonge mseto), na aina ya 4 vina homoni moja tu ya projestini (angalia vidonge vidogo).

Aina ya homoni ya estrojeni inayotumika sana huitwa ethinyl estradiol. Dozi ya kawaida ni makrogramu 35. Kiasi cha kawaida cha homoni ya projestini kwenye vidonge mseto ni miligramu 0.1.

Wanawake wanaotumia vidonge vya majira kawaida hupata hedhi ya kila mwezi kidogo kuliko kama wangepata bila kutumia vidonge vya majira. Hili linaweza kuwa jambo zuri, hasa kwa wanawake wenye tatizo la upungufu wa wekundu wa damu (anemia). Lakini kama mwanamke hapati hedhi ya kila mwezi au hupata hedhi nyepesi (kidogo) mno kwa miezi kadhaa na hapendezwi na madhara haya ya pembeni, anaweza kujaribu aina nyingine ya vidonge vya majira vyenye kiasi kikubwa zaidi cha homoni ya estrojeni.

Vidonge vyote vya majira hufanya kazi vizuri zaidi kudhibiti mimba kama vitatumiwa katika muda ule ule kila siku. Utaratibu huo hurahihisha mwanamke kukumbuka kumeza kidonge. Ni muhimu hasa kutumia vidonge vidogo (vyenye homoni moja ya projesti tu ) katika muda ule ule kila siku kwa sababu kwa kidonge hiki, kuna uwezekano mkubwa wa kupata mimba kama mwanamke atasahau kumeza hata kidonge kimoja tu.

Kwa paketi ya vidonge vya siku 28, tumia kidoge 1 kila siku na kuanza paketi nyingine baada ya kumaliza ya kwanza. Paketi ya siku 28 inaweza kuwa na vidonge 21 vyenye homoni na vidonge 7 vilivyobaki vikiwa havina homoni. Vidonge hivi 7 ni kwa ajili ya kukumbusha kumeza kidonge kila siku. Baadhi ya paketi za siku 28, hata hivyo, zina vidonge vyenye homoni tu. Kwa paketi ya vidonge 21, tumia kimoja kila siku na baada ya hapo subiri hadi siku 7 kabla ya kuanza paketi nyingine (isipokuwa kama unatumia vidonge mfululizo ili upate vipindi vichache vya hedhi).

VIDONGE MSETO VYENYE DOZI ZA HOMONI AMBAZO HUBADILIKA BADILIKA
Vidonge hivi hujumuisha mchanganyiko wa homoni za estrojeni na projestini ambazo hubadilika badilika kipindi chote cha mwezi mzima. Kwa vile kiasi cha homoni hubadilika, ni muhimu kutumia vidonge vyote kama ilivyopangwa.
Baadhi ya majina ya kibiashara: Gracial, Logynon, Qlaira, Synphase, Trinordiol, Trinovum, Triquilar, Triphasil


VIDONGE MSETO VYENYE DOZI ZA HOMONI AMBAZO HAZIBADILIKI: HOMONI ZOTE MBILI ZA ESTROJENI NA PROJESTINI
Vidonge mseto hivi hujumuisha estrojeni (kawaida makrogramu 35) na projestini (kawaida miligramu 0.1). Paketi ya siku 28 inakuwa na vidonge 21 vyenye homoni na 7 ambavyo havina chochote ila kwa ajili ya kukumbusha kumeza kidonge kila siku. Paketi ya vidonge 21 inakuwa na vidonge vyote vyenye homoni. Kiasi cha kila homoni ni sawa kwa vidonge vyote 21 kwenye paketi.
Baadhi ya majina ya kibiashara: Alesse, Cilest, Diane, Femoden, Gynera, Harmonet, Norinyl, Ortho-Novum, Ovysmen


VIDONGE MSETO VYENYE DOZI ZISIZOBADILIKA: PROJESTINI ZAIDI NA ESTROJENI KIDOGO
Vidonge hivi vina kiasi kikubwa cha projestini (miligramu 0.15 ) na kiasi kidogo cha estrojeni (makrogramu 30 ). Paketi ya siku 28 ina vidonge 21 vyenye homoni na 7 havina chochote ila kwa ajili ya kukumbusha kumeza kidonge kila siku. Paketi ya vidonge 21 ina vidonge vyote vyenye homoni. Kiwango cha homoni ni sawa katika vidonge vyote 21 katika aina zote 2 za paketi. Vidonge hivi vinaweza kufanya kazi vizuri zaidi kwa mwanamke ambaye hupata hedhi nzito kila mwezi au wanaopata maumivu kwenye maziwa kabla ya hedhi kuanza.
Baadhi ya majina ya kibiashara: Lo-Femenal, Lo/Ovral, Microgynon, Microvlar, Nordette


VIDONGE VYENYE HOMONI YA PROJESTINI TU (VIDONGE VIDOGO)
Vidonge hivi vina homoni moja tu ya projestini na huwa katika paketi ya vidonge 28. Vidonge vyote kwenye paketi vina kiwango cha homoni ya projestini sawa.
Baadhi ya majina ya kibiashara: Femulen, Microlut, Micronor, Micronovum, Neogest, Microval, Ovrette, Exluton