Hesperian Health Guides

Dharura za kisukari

Katika sura hii:

Kuna aina 2 za dharura ambazo zinaweza kuwapata watu wenye kisukari. Dharura kutokana na upungufu mkubwa wa sukari mwilini (hypoglycemia) hutokea kwa mtu ambaye anajua ana kisukari na anatumia dawa au insulini kukidhibiti. Dharura hii husababishwa aidha na kutumia kiasi kikubwa cha dawa au insulini, au kula kidogo kuliko kawaida. Dharura ya upugufu mkubwa wa sukari mwilini inaweza kutokea bila tahadhari. Lakini kwa kuchukua hatua haraka, unaweza kumsaidia mtu aliyepungukiwa sana na sukari mwilini kupona.

Dharura kutokana na kiwango cha sukari kwenye damu kuzidi kupita kiasi (hyperglycemia) kawaida hutokea baada ya mtu kuwa amepata dalili za tahadhari hata kama mtu huyu hajui kwamba ana kisukari.

Kama una kisukari, vaa bangili yenye maneno kuwa una kisukari, au beba kadi ambayo inaonesha kuwa: “Nina kisukari.” Weka jina la dawa yoyote ambayo huwa unatumia kwenye kadi au bangili pia. Hii itasaidia watu wengine kukusaidia kama huwezi kujihudumia au wakati wa dharura. Elimisha wanafamilia wako na wengine juu ya dalili za hatari za kisukari na nini cha kufanya.

Kama mtu ana tatizo kutokana na kisukari lakini huna uhakika kama tatizo limetokana na kiwango cha sukari kwenye damu kupungua au kuzidi, mtibu kama vile sukari kwenye damu imepungua (mpe sukari kidogo) wakati ukitafuta msaada wa daktari.

Upungufu wa sukari mwilini (hypoglycemia)

Hali hii inaweza kutokea tu kwa mtu ambaye anatibu kisukari chake na dawa. Sukari kwenye damu inaweza kushuka sana kama ametumia dozi kubwa ya insulini kupita kiasi au dawa nyingine ya kisukari, hajala chakula cha kutosha, amefanya mazoezi makubwa mara moja, anakaa muda mrefu bila kula - kati ya mlo na mlo, au anatumia pombe. Kama mtu amepata matatizo ya kupungukiwa na sukari mwilini, msaidie kupata njia bora ya kudhibiti kisukari chake. Asikae muda mrefu bila kula chakula au ale vyakula vyenye afya ili kupunguza dharura hizi.

Mtu mwenye tatizo la upungufu wa sukari mwilini anaweza kuanza kujisikia hovyo hovyo, kutokwa na kijasho, au kutetemeka, halafu ghafla kuwa goigoi, kuchanganyikiwa, kupatwa na wasiwasi, au hali ya kuudhika. Kwa dalili hizi za mwanzo, analazimika kula mara moja. Kama hatafanya hivyo, hali yake itazidi kuwa mbaya zaidi. Kuwa mwangalifu na dalili za hatari zifuatazo:

Dalili za hatari
 • Matatizo katika kutembea
 • Kujisikia mdhaifu au mchovu
 • Uoni hafifu
 • Kuchanganyikiwa au utendaji usio wa kawaida (unaweza kufikiria amelewa)
 • Kupoteza fahamu
 • Mashambulio
Matibabu

Kama ana fahamu, haraka mpe sukari: juisi ya matunda, pipi, au glasi ya maji yaliyochanganywa na vijiko vya sukari kadhaa vitamsaidia. Anapaswa kula mlo kamili mara baada ya hapo pia. Kama unaweza kumpima sukari na glukomita, utajua kama matibabu yanafanikiwa. Kama bado amechanganyikiwa au hajaanza kujisikia vizuri dakika 15 baada ya kumpa sukari, tafuta msaada wa daktari.

Kama hana fahamu, weka sukari kidogo au asali chini ya ulimi wake. Endelea kumpatia kidogo kidogo. Huwa inachukua muda kwa mwili kufyonza sukari. Atakapoamuka, unaweza kumuongezea zaidi. Pata mtu wa kukaa karibu naye kwa saa 3 au 4 kuhakikisha kuwa dalili za hatari hazirudi.

Sukari kwenye damu kuzidi kupita kiasi (hyperglycemia)

Mtu mwenye kisukari anaweza kuwa na sukari nyingi sana kwenye damu kama atakula chakula kingi, hafanyi mazoezi kama kawaida, ana ugonjwa au maambukizi, hatumii dawa yake ya kisukari, au amepungukiwa na maji mwilini. Hali hii inaweza kumtokea mtu yeyote hata kama hajajua kuwa ana kisukari. Kabla dharura hizi hazijatokea, dalili zifuatazo zinaweza kuashiria kuwa mtu ana kisukari, au aina ya kisukari alichonacho inahitaji matibabu tofauti:

Dalili
 • Kusikia kiu na kunywa maji sana
 • Kukojoa kila baada ya muda mfupi
 • Kutoona vizuri
 • Kupungua uzito


Kama mtu hatapa matibabu ya kudhibiti sukari nyingi kwenye damu, kiwango hicho kinaweza kufikia hatua ambayo ni hatari zaidi na kusababisha kuzimia na hata kifo. Unaweza kunusuru maisha ya mtu mwenye tatizo la sukari kuzidi kupita kiasi kwa kutafuta msaada haraka kila unapoona dalili za hatari zifuatazo:

Dalili za hatari
 • Mapigo ya moyo kwenda mbio
 • Pumzi ambayo ina harufu inayofanana na ya matunda
 • Ngozi kavu
 • Maumivu tumboni, kichefuchefu, kutapika
 • Shinikizo la chini la damu
 • Kuchanganyikiwa
 • Pumzi nzito za haraka haraka
 • Kupoteza fahamu
Matibabu

Mpeleke mtu mwenye dalili hizi za hatari kwenye kituo cha afya haraka. Kama ana fahamu, mpe maji mengi ya kunywa, lakini kiasi kidogo kidogo kila baada ya muda.

Kama una uhakika ana sukari nyingi kwenye damu, na tayari umepima sukari yake kwenye damu na glukomita, na unajua dozi yake ya insulini, mpe insulini kidogo wakati unatafuta msaada. Lakini kama huna uhakika kwamba tatizo ni sukari kupanda, usimpe insulini. Kumpa insulini mtu ambaye sukari kwenye damu imeshuka kunaweza kusababisha kifo.


Ukurasa huu ulihuishwa: 20 Mei 2017