Hesperian Health Guides

Juhudi za jamii dhidi ya kisukari

Katika sura hii:

Wakati mtu mmoja mmoja ndiye anayepata kisukari na anaweza kufanya mabadiliko kuboresha afya yake, mabadiliko ambayo yanaweza kuzuia watu wengi zaidi wasipate kisukari yanapaswa kufanyika tu katika ngazi ya jamii. Kwa mfano, mtu mmoja anaweza kuchagua aina ya vyakula gani atakavyoweka mdomoni mwake, lakini uchaguzi wake una ukomo kwani unategemea vyakula gani vinapatikana katika eneo lake na unafuu wa bei. Mtu mmoja anaweza kutaka kufanya mazoezi zaidi, lakini hawezi kulazimisha eneo jirani kuwa salama kwa ajili yake kufanya mazoezi. Ni bora zaidi kuziweka familia na jamii pamoja kubadili mambo ambayo yanachangia kisukari au kuzidisha zaidi madhara ya ugonjwa huo.

Walinde watoto wachanga na watoto wadogo

Wamama na watoto wanapaswa kupatiwa lishe bora ili wasipatwe na kisukari. Wavulana na wasichana pia wapatiwe vyakula vyenye virutubishi vya kutosha. Watoto wanaopata utapiamlo wangali tumboni na wenzao wakati wa umri wa utotoni huwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kupata kisukari baadaye. Epuka kuwapa watoto sukari, pipi, au vyakula vingine visivyo na manufaa kiafya.

Boresha upatikanaji wa vyakula vyenye afya

wanawake 2 wakipika.
mwanamke akihudumia bustani.

Katika kuongeza aina tofauti za vyakula, wingi, na unafuu wa bei ya vyakula vyenye afya kwenye jamii yako:

  • Andaa darasa la mapishi kufundisha juu ya ulaji wenye afya. Watu wakiona kuwa vyakula vyenye afya vina ladha nzuri na kujifunza jinsi ya kuviandaa, watapenda kuvitumia.
  • Saidia kuendeleza utamaduni wa kula vyakula vya asili vyenye afya. Kama vyakula ambavyo vinapendwa sana kwenye jamii havina tija kiafya, ni bora zaidi kupunguza matumizi yake. Chagua vile vyenye manufaa zaidi kiafya na kuwaomba wazee kwenye jamii kutoa elimu jinsi ya kuviandaa.
  • Tumia shule kuwashirikisha watoto katika kuzalisha, kupika, na kula vyakula vyenye afya. Vyakula ambavyo vinatolewa shuleni vinaweza kutengenezwa kutokana na nafaka za kawaida, matunda, na mbogamboga. Simamisha uuzaji wa vyakula vsivyo na tija kiafya na vinywaji vilivyokolezwa sukari kwa watoto ndani na karibu na shule.
  • Anzisha sehemu za bustani za jamii mahali ambapo watu wanaweza kupanda mbogamboga, matunda na vyakula vingine vyenye virutubishi ambavyo huchukua muda mfupi kukomaa. Hata kuzalisha chakula kidogo chenye virutubishi vingi kunaweza kuleta mabadiliko katika ulaji wako. Baadhi ya watu kwenye majiji hupanda mazao maghorofani, kwenye veranda au ndani ya viwanja ambavyo havitumiki.
  • Hamasisha vikundi vya wakulima au wazalishaji chakula kuhakikisha upatikanaji wa chakula chenye afya kwa watu wote, na wakulima waweze kupata soko la uhakika kwa ajili ya mazao yao. Kwa taarifa zaidi juu ya miradi ya chakula, angalia Mwongozo kwa Jamii juu ya Afya ya Mazingira.

Tengeneza sehemu za kufanyia mazoezi na michezo

Katika sehemu za mjini, watu wanaweza kutokuwa na maeneo salama ya kufanyia mazoezi. Jamii zinapaswa kushirikiana kujenga viwanja vya mpira, sehemu za kuchezea mpira wa vikapu na netiboli, na viwanja vya kuchezea. Maeneo haya kawaida hupata umaarufu kama makutano ya jamii.

kundi la watu likiwa kwenye mjadala.

Ongoza juhudi za kuielimsha jamii

Elimisheni jamii ili kuiwezesha kufahamu kisukari ni ugonjwa gani, kinatokana na nini, kinasababisha matatizo gani, na kwa nini. Wahimize wanajamii kueleza shuhuda zao juu ya kisukari, kupeana maarifa, na kuuliza maswali. Wanaweza kuamua kuanza kula vyakula vyenye afya au kufanya mazoezi pamoja.

Masuala mengine ya kujadili na kuyafanyia kazi ni pamoja na uchafuzi wa maji na hewa, na masuala ya kiuchumi au kisiasa ambayo yanaweza kuwa yanachangia msongo kwa watu binafsi na jamii.

Andaa upimaji wa kisukari kwa makundi

Siku maalum za upimaji wa kisukari ni fursa nzuri kwa watu kujua iwapo wana kisukari, hata kama hawana dalili. Wapime watu wenye dalili za hatari au ambao wana umri wa zaidi ya miaka 40 na wana wanafamilia wenye kisukari.

Kwa ajili ya vipimo kwa makundi, kipimo cha mkojo kinaweza kuwa ndiyo njia rahisi zaidi. Vipimo vya damu pia ni muhimu lakini vinapaswa kufanyika pale ambapo mtu hajakula chochote kwa siku hiyo, vizuri zaidi kifanyike asubuhi kabla ya mlo wa asubuhi. Kupata kipimo cha mkojo, haijalishi kama mtu amekula, lakini mpimaji anapaswa kuandika muda ambao kipimo kinafanyika, na mlengwa mara ya mwisho amekula saa ngapi, kwa sababu sukari kawaida hupanda baada ya chakula. Angalia zaidi juu ya upimaji.

Vikundi vya kusaidiana

Kikundi cha kusaidiana ni kikundi cha watu ambao hukutana mara kwa mara (mfano mara moja kwa wiki au wiki mbili) kusaidiana. Kikundi cha kusaidiana kinaweza kuanzishwa katika ujrani mmoja, shule, kanisa, au sehemu ya kazi-popote pale ambapo watu wanaweza kutaka kuanzisha kikundi cha kusaidiana. Wakati mwingine mfanyakazi wa afya, tabibu, au mwalimu anaweza kuanzisha na kushiriki katika kikundi cha kusaidiana. Baadhi ya vikundi huomba kukutana na wafanyakazi wa afya na wataalam wengine mara chache tu.

Watu wenye kisukari hukutana pamoja kupeana maarifa ambayo wamejifunza katika kujihudumia, kujadili mambo ambayo ni magumu, na kujisikia kuwa jamii mmoja. Watu ambao wamegundua ghafla kuwa wana kisukari wanaweza kunufaika kutokana na kukutana na wenzao, ambao wamekuwa wakiishi na kisukari kwa muda. Vikundi vya kusaidiana vinaweza kujadili changamoto mbalimbali, kupika na kula pamoja kama familia baada ya kugundua kuwa mtu mmoja mmoja anahitaji kubadili ulaji wake ili aweze kuwa na afya nzuri. Kikundi kinaweza kuanzisha miradi ya kuboresha afya ya jamii nzima kwa manufaa ya kila mtu. Kikundi cha kusaidiana pia kinaweza kukua na kudumu kwa miaka mingi kama washiriki wataona kinawasaidia.

wanawake 3 wakiweka bango lenye ujumbe "Mjadala wa leo: Jinsi kisukari chetu kinavyotuathiri."

Juhudi zingine za jamii

kundi la watu likiwa limebeba mabango ambayo yanasema "Tunza maji yetu katika hali ya usafi na salama!", na "Tunataka maji yetu ya kawaida yawe safi na salama siyo maji yako ya chupa."
  • Himiza idara ya afya, mahospitali, vituo vya afya na wafanyakazi wa afya kutoa huduma za upimaji bila malipo kwa watu ambao wanaweza kuwa na kisukari, na kuhakikisha kuwa dawa na vifaa vya kupima sukari vinapatikana kwa gharama nafuu.
  • Pigania maji safi ili kupunguza gharama za kutegemea maji ya chupa au vinywaji vilivyokolezwa sukari ambavyo siyo vizuri kiafya.
  • Simamisha uchafuzi wa mazingira na kemikali za sumu kuanzia kwenye vyanzo, mfano viwandani.
  • Punguza matumizi ya viuatilifu.



Ukurasa huu ulihuishwa: 20 Mei 2017