Hesperian Health Guides

Zuia na kudhibiti matatizo ya kisukari

Katika sura hii:

Tunza miguu yako

Utunzaji vizuri wa miguu ni miongoni mwa mambo muhimu ya kuzingatia kwa watu wenye kisukari. Uharibifu wa neva ambao husababishwa na kisukari unaweza kuchangia kupoteza hisia au kutia ganzi kwenye miguu, na kufanya vigumu kusikia maumivu unapojeruhiwa. Kisukari pia husababisha matatizo katika uponaji wa vidonda, na kurahihisha maambukizi. Fangasi kwenye miguu (angalia sura ya Matatizo ya ngozi - inaandaliwa) zinaweza kuchangia maambukizi.

Maambukizi kwenye mguu yanaweza kuenea mguu mzima kama hayatatibiwa. Mguu unaweza kuathirika kiasi cha kuhitaji kutolewa. Lakini matunzo mazuri ya miguu na udhibiti wa sukari mwilini yanaweza kuepusha kukatwa viungo.

mwanaume akikagua mguu wake.

Kagua miguu yako kila siku

Ni vigumu kugundua kuwa umejeruhiwa kama huna hisia. Hivyo, kama utagundua kuwa sehemu za mguu wako zinaanza kufa ganzi, hakikisha unakagua mguu wako kwa kuangalia na kugusa sehemu mbalimbali kila siku. Kama huwezi kuifanya shughuli hiyo wewe mwenyewe, tafuta mtu wa kukusaidia. Baadhi ya watu hutumia kioo kujiangalia chini ya miguu. Angalia kama kuna sehemu zilizoivia, nyekundu, ngozi iliyochanika, au vidonda. Gusa na kutafuta sehemu ambazo zinaweza kuwa za vuguvugu au zimevimba, ambazo zinaweza kuwa dalili za mwanzo za maambukizi. Hakikisha pia unakagua katikati ya vidole.

Tafuta msaada wa wafanyakazi wa afya kwa kila kidonda ambacho kinaonekana kutopona au sehemu ambazo zinabaki nyekundu, zikiwa na joto au vuguvugu, au zilizovimba. Ni muhimu kutibu vidonda mapema kuepuka matatizo makubwa baadaye.

Matunzo ya majeraha kwenye mguu

Weka sehemu zilizojeruhiwa katika hali ya usafi na ukavu. Usiutumie mguu wenye jeraha kukanyagia kwa nguvu kadri iwezekanavyo. Tumia magogo ya kutembelea ili kupunguza mgandamizo kwenye vidonda.

Kidonda Kidonda chenye maambukizi
mguu wenye kidonda Kidonda chenye maambukizi

Safisha vidonda na maji safi pamoja na dawa ya kuua wadudu. Ondoa tishu zozote ambazo zimekufa. (Tishu zilizokufa huwa baridi ukizigusa na huonekana kuwa na weusi.) Kuuloweka mguu kwenye maji ya vuguvugu (siyo ya moto) husaidia katika kuondoa tishu zilizokufa. Paka mafuta ya antibiotiki na kufunika kidonda na kitambaa cha gozi (gauze) au kitambaa kingine kisafi na laini. Weka padi juu yake.

Angalia kama kuna dalili za maambukizi, kama vile kuvimba, ugumu, joto, au misitari nyekundu inayokwenda juu kutoka kwenye kidonda. Tibu maambukizi na antibiotiki kama vile tetrasakilini, doksisakilini, penisilini, au metronidazo.

Kama kidonda hakitapona kwa huduma yako binafsi na ya wengine, tafuta msaada wa wafanyakazi wa afya.

 mguu uliovalishwa viatu vya kamba (sendo)ukiwa na neno "NDIYO" na mguu usio na viatu wenye neno “HAPANA”.
NDIYO
HAPANA

Zuia majeraha ya mguu

Vaa viatu vya kawaida au viatu vya kamba (sendo), hata ukiwa ndani. Unaweza kukanyaga kitu chenye ncha kali na kutohisi maumivu.

Nawa miguu kila siku na kuikausha vizuri. Kila mara kausha katikati ya vidole.

Kila mara kagua ndani ya viatu na mikono yako kuhakikisha kuwa hakuna kitu chenye ncha kali au chenye uwezo wa kujeruhi kabla hujavivaa. Kitu chochote ambacho kinaweza kujeruhi kinapaswa kufunikwa au kuondolewa.

NWTND Diab Page 23-4.png

Kucha za vidole vya miguu

Kucha za vidole vya mguu zikirefuka kwa kuingia ndani zinaweza kukata ngozi na kusababisha maambukizi. Kata kucha na hakikisha usijeruhi kidole, au tumia tupa ili kuzuia zisirefuke sana. Kata kucha kutoka upande mmoja hadi mwingine kwenye mstari ulionyooka badala ya kufuata kizingo kuzuia kucha kurefuka na kuingia ndani nyama.

wanawake 2 wakiongea katika genge la mbogamboga.
Kula vizuri kudhibiti kisukari kutasaidia pia kuzuia shinikizo la juu la damu (tatizo la presha ya juu). Kula chumvi kidogo husaidia kudhibiti shinikizo la damu.

Pima shinikizo la damu

Kila mtu mwenye kisukari anapaswa kupimwa shinikizo la damu (presha), na kila mtu mwenye shinikizo la damu anapaswa kupimwa kisukari. Kama kilivyo kisukari, shinikizo la juu la damu husababisha uharibifu kwa moyo, mishipa ya damu, figo, na sehemu zingine za mwili. Hivyo kama una vyote 2 –kisukari na shinikizo la juu la damu, uwezekano wa kupata ugonjwa wa moyo, kiharusi, ugonjwa wa figo, au matatizo mengine makubwa ya kiafya ni mkubwa zaidi kuliko kuwa aidha na kisukari au shinikio la damu peke yake.

Shinikizo la damu la kawaida ni chini ya 140/90 mmHg (angalia sura: Ugonjwa wa moyo - inaandaliwa). Kama shinikizo la damu iko juu, jaribu kuishusha kwa kuushughulisha mwili - kwa mfano kufanya mazoezi yanayostahili, kupunguza msongo, na kula vyakula vyenye afya zaidi. Hatua hizo pia husaidia kudhibiti kisukari.

Dawa inayoitwa ACE Inhibitors husaidia kushusha shinikizo la damu na inaweza pia kuzuia tatizo la figo kushindwa kufanya kazi. Kundi lingine la dawa inayoitwa statins husaidia kupunguza kiasi cha kolestro kwenye damu, na kupunguza uwezekano wa matatizo ya moyo au kiharusi kutokea kwa watu wenye kisukari. Kwa taarifa zaidi juu ya dawa ambazo husaidia kushusha shinikizo damu na kolestro, angalia sura: Ugonjwa wa moyo - inaandaliwa.

NWTND Diab Page 24-2.png

Acha uvutaji

Watu wanaovuta hupata kisukari kwa urahisi zaidi. Na watu wenye kisukari wanaovuta hupata matatizo mengine makubwa ya kiafya kuliko wale wasiovuta. Uvutaji tumbaku huharibu viungo zaidi mwilini na siyo mapafu tu. Huziba mzunguko wa damu na kuongeza shinikizo la damu. Uvutaji ni hatari sana kwa watu wenye kisukari kiasi kwamba kuacha kuvuta ni muhimu zaidi hata kuliko kupunguza kiwango cha sukari kwenye damu yako. Angalia sura Madawa ya kulevya, pombe na tumbaku (inaandaliwa) kwa msaada zaidi jinsi ya kuacha uvutaji.

NWTND Diab Page 25-1.png

Uwezo wa kuona

Kiwango cha sukari kwenye damu kikipanda sana huweza kusababisha uoni hafifu. Tatizo hili kawaida hutoweka mara baada ya sukari kwenye damu kurudi kwenye kiwango salama. Hata hivyo, kisukari kinaweza kusababisha uharibifu wa kudumu kwa msihipa ya damu kwenye macho, na kuchangia, taratibu, kupoteza uwezo wa kuona au kupofuka kabisa. Mtu mwenye kisukari anapaswa kupimwa macho angalau mara moja kwa mwaka, au mara kwa mara kama tayari ana tatizo la macho. Kama uharibifu wa mishipa ya damu kwenye macho utagundulika mapema, unaweza kutibiwa na mtaalam wa macho na kuzuia kupoteza uwezo wa kuona.

mwanaume akisafisha meno yake.

Utunzaji wa mdomo

Kisukari huzidisha maambukizi ya fizi ambayo pia huzidisha kisukari. Watu wenye kisukari wanapaswa kupiga mswaki angalau mara 2 kwa siku, kwa kutumia mswaki na dawa ya meno au kijiti cha mwarobaini. Njiti za meno pia zinaweza kusaidia kusafisha katikati ya meno. Kwa taarifa zaidi jinsi ya kuzuia maambukizi ya fizi, angalia sura: Matatizo katika meno na fizi (inaandaliwa).

Mtu mwenye kisukari anaweza kumuona daktari wa meno kwa ushauri zaidi. Kila mara hakikisha unamfahamisha daktari wa meno kuwa una kisukari.

Chanjo

Watu wenye kisukari wanapaswa kupata chanjo za mara kwa mara kuzuia magonjwa kama vile homa ya mafua (influenza) na nimonia, kwa vile yanaweza kusababisha hali mbaya zaidi kwa mtu mwenye kisukari.


Ukurasa huu ulihuishwa: 20 Mei 2017