Hesperian Health Guides
Kwa nini watu wengi wana kisukari?
Hadi nifike nyumbani muda unakuwa umeenda sana, inakuwa rahisi zaidi kununua chakula ambacho tayari kimeandaliwa. |
Burger hushibisha haraka na bei yake ni nafuu, tunaweza kula hapa kila siku! |
Kawaida ajira nyingi za mjini na maisha ya mjini kwa ujumla hayahitaji watu kutembea sana kwa mguu. Mara nyingi huketi muda mrefu wanapokuwa kazini, au hula vyakula visivyo na afya ambavyo vimechakatwa sana. |
Mazingira Mapya, Maisha Mapya
Miaka 10 iliyopita, Amilcar na Serena walitoka kijijini kwao kwenda jijini kutafuta kazi.
Kwa namna moja, maisha sasa ni rahisi. Badala ya shuruba ya kulima na kuvuna mazao shambani siku nzima, Serena anafanya kazi kwenye kiwanda. Huketi siku nzima akishona nguo. Amilcar anafanya kazi ya ufagiaji katika stesheni ya treni.
Walipokuwa kijijini, walitembea kila mahali. Walipo sasa jijini, kutembea kwa mguu ni hatari, hivyo hupanda basi. Amilcar zamani alikuwa anacheza mpira saa za jioni. Siku hizi mara nyingi huenda kwenye baa ya karibu na kuangalia michezo kwenye televisheni, angalau kupata burudani.
Ulaji wao umebadilika pia. Badala ya kula chakula wanacholima au kukusanya kutoka shambani, siku hizi hununua chakula ambacho kimekwisha kutayarishwa, na vinywaji vyenye sukari kutoka kwa wachuzi mitaani, au vyakula vilivyofungashwa kutoka grosari. Vyakula hivi vina ladha nzuri. Hupatikana haraka na kwa urahisi. Lakini vyakula vingi ambavyo vimechakatwa viwandani vina kiwango kikubwa cha sukari na kemikali.
Serena na Amilcar wote wanaongezeka uzito na kuota vitambi. Misuli yao haina nguvu kama zamani walipokuwa wanafanya kazi shambani. Katika wiki ya upimaji kisukari kwa umaa iliyofanyika eneo lao, Amilcar aligundulika kuwa na kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu yake, na Serena tayari ana kisukari na anakabiliwa na maumivu ya neva kwenye miguu.
Mfanyakazi wa afya katika zoezi hilo la upimaji alimsaidia Serena kuandaa ratiba ya mazoezi ya kutembea haraka haraka kuzunguka kiwanda chao na wafanyakazi wenzake, kila siku baada ya chakula cha mchana. Alimshauri Amilcar kuwa anakunywa maji badala ya vinywaji vilivyokolezwa sukari.