Hesperian Health Guides

Kudhibiti sukari kwenye damu kwa kutumia dawa

Katika sura hii:

Jifunze jinsi ulaji, mazoezi, na dawa vinavyoweza kuusaidia mwili wako kuzuia sukari kwenye damu kupanda sana kiasi cha kukufanya kujisikia vibaya, au kupatwa na dharura (sukari kwenye damu kuzidi kupita kiasi). Dawa za kisukari husaidia kupunguza kiwango cha sukari kwenye damu na hata zaidi, lakini kiasi kikubwa cha insulini au cha dawa za sulfo kinaweza kusababisha tatizo la upungufu wa sukari mwilini. Kama utatumia dawa, unapaswa kupima kiwango cha sukari kwenye damu yako mara kwa mara hadi utakapojua kitu gani huwa kinasababisha sukari kupanda. Kwa njia hiyo unaweza kujua iwapo unadhibiti kisukari chako vizuri.

Kupima sukari kwenye damu yako

Kama ilivyoelezwa kwenye Vipimo vya Kupimwa kisukari, vipimo vya damu vinaweza kutumika kubainisha kisukari. Watu pia hutumia vipimo vya damu kudhibiti kisukari. Kutumia kifaa cha kupima sukari kwenye damu (glukomita) na kutumia kipimo cha A1C ni njia 2 za kufuatilia kiwango cha sukari kwenye damu. Njia hizo 2 hutoa taarifa tofauti, lakini zote husaidia.

Glukomita ni kifaa rahisi ambacho huonesha kiwango cha sukari kwenye damu dakika hiyo unapopima. Ni bora zaidi kupima muda tofauti wa siku ili kuona iwapo matokeo ya vipimo yanabadilika kabla na baada ya mlo, na kutoka siku moja hadi nyingine. Unaweza kupima:

 • Kabla ya mlo. Kiwango kizuri ni kati ya 4.4 - 7.2 mmol/l (80 - 130 mg/ dl).
 • Saa 2 baada ya mlo. Kiwango kizuri ni chini ya 10 mmol/l (180 mg/dl).

Katika kupima, weka tone la damu kutoka kwenye ncha ya kidole kwenye kipande cha karatasi maalum cha kupimia na kiwango cha sukari kitaoneshwa kwenye glukomita. Kutegemea na glukomita, unaweza kuelekezwa kuweka kipande cha karatasi maalum cha kupimia kwenye glukomita kabla ya kuongeza tone la damu kwenye kipande hicho (angalia chini), au unaweza kuelekezwa kuweka tone la damu kwanza kwenye kipande cha kupimia.

Kidole kinatobolewa kidogo na sindano kutoa damu.
kidole chenye tone la damu kikigusa kipande cha kupimia.
Tumia sindano au lancet kupata tone moja la damu litakalokwenda kwenye kipande cha kupimia. Kwa glukomita ya aina hii, chomeka kwanza kipande cha kupimia, baada ya hapo gusa kidole chako chenye damu kwenye ncha ya kipande cha kupimia.
mwanamke akiwa katika chumba cha kusubiria kukiwa na bango ukutani linalosema "Kundi la Kisukari Leo.”

Baadhi ya watu wana kifaa cha glukomita nyumbani kwao na wanaweza kujipima mara kwa mara. Wengine hutumia glukomita kwenye kiliniki ya karibu au kwenye kikundi cha kusaidiana cha wenye kisukari. Glukomita inaweza kutumiwa na watu wengi kwa usalama. Lakini usitumie sindano au kifaa cha kutobolea kwa zaidi ya mtu mmoja kutoa damu- kinaweza kueneza VVU na magonjwa mengine kupitia damu.

Kipimo cha A1C (glycosylated hemoglobin test) kinapatikana tu kwenye kliniki au kituo cha afya au hospitali. Kipimo hiki hukupa wastani wa kiwango cha sukari kwenye damu kwa miezi iliopita. Hivyo kinaonesha jinsi unavyokidhibiti kisukari chako kwa ujumla, na siyo kwa siku husika tu. Kwa watu wenye kisukari, kiwango kizuri ni chini ya 8.0%. Kama kipimo hiki kinapatikana, jaribu kupima angalau mara 1 au 2 kwa mwaka.

Daktari au mfanyakazi wa afya au programu ya kisukari inaweza kutumia namba tofauti kidogo kwa ajili ya hali yako binafsi. Kitu muhimu unachohitaji ni kuuelewa mwili wako, mambo yanayoathiri kiwango chako cha sukari na kiwango gani kinakufanya ujisikie vizuri zaidi.

NWTND Diab Page 19-2.png

Dawa za kisukari

Dawa haziwezi kuponya kisukari. Lakini baadhi ya dawa zinaweza kushusha na kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu. Pia baadhi ya mitishamba husaidia.

Watu wengi huanza kudhibiti ugonjwa wa kisukari Aina ya 2 bila kutumia dawa. Ulaji wenye afya, mazoezi, na dawa za mitishamba kawaida huwa zinatosha kushusha kiwango cha sukari kwenye damu ili mtu aweze kuwa na afya. Kama ulaji wenye afya, mazoezi zaidi, na dawa za mitishamba hazitasaidia kupunguza dalili, dawa za kisasa zinaweza kutumika kuzuia sukari isipande sana, na pia kuzuia matatizo mengine ya kiafya yasijitokeze. Wakati mwingine mfanyakazi wa afya anaweza kukuelekeza kutumia dawa zote mbili kwa pamoja au, baada ya muda kukubadilishia dozi au dawa ambayo unapaswa kutumia.

Dawa zinapaswa kutumika kwa kuzingatia maelekezo ya mfanyakazi wa afya na wakati sahihi. Hakikisha wanafamilia wanaelewa madhara ya kawaida ya pembeni ya dawa na wafanye nini wakati wa dharura. Na kumbuka: dawa ni sehemu tu ya mkakati wa kujihudumia. Bado unahitaji kula vyakula vyenye afya na na kuushughulisha mwili wako unapokuwa unatumia dawa za kisukari.

Metformin

Metformin ni dawa inayotumika sana kwa ajili ya kisukari na ndiyo chaguo bora zaidi kwa watu wengi. Metformin kawaida hutumika mara 2 kwa siku. Unapoanza metformin, inaweza kusababisha mvurugano tumboni na kuharisha. Hali hii kawaida hutoweka ndani ya wiki 1 hadi 2 na inaweza kuepukwa kwa kutumia dawa hiyo kwa wakati mmoja na chakula. Kama madhara ya dawa ya pembeni yatakuwa mabaya sana au kutopungua baada ya muda, mfanyakazi wa afya anaweza kusimamisha dawa hiyo au kupunguza dozi. Watu wenye ugonjwa wa figo au ini hawapaswi kutumia metformin.

Sulfonylureas (Dawa za sulfo)

Dawa za Sulfonylurea (sulfo), kama vile glibenclamide, glipizide, na tolbutamide, kawaida hutumika mara 1 hadi 2 kwa siku kabla ya chakula.

Hatari ya dawa za sulfo ni kwamba zinaweza kusababisha viwango vya sukari kwenye damu kushuka sana kupita kiasi, na matokeo yake ni pamoja na kizunguzungu, udhaifu mwilini, kuzirai, kutetemeka, kutokwa jasho, au hata kifo. Kama dalili yoyote mojawapo itaanza, kula kitu kitamu haraka kupandisha sukari mwilini. Hakikisha wanafamilia wanazijua dalili hizo na wafanye nini kusaidia.

Katika kuzuia kiwango cha sukari kwenye damu kisishuke kupita kiasi wakati unatumia dawa za sulfo:

 • Usikose kula milo yako. Kama hujala, usitumie dawa ya sulfo.
 • Kula vyakula vya protini na vyakula vingine vyenye virutubishi kwa ajili ya mlo wa asubuhi (kifungua kinywa).
 • Kula chakula zaidi kama unafanya kazi ngumu za kimwili, mazoezi, au michezo.
 • Weka karibu akiba ya juisi ya matunda, pipi, au sukari kwa sababu unaweza kuanza kujisikia uchovu au kizunguzungu.


Kama sukari kwenye damu itakuwa inashuka sana mara kwa mara, mfanyakazi wa afya anaweza kusimamisha dawa au kupunguza dozi.

Madhara ya pembeni mengine ambayo yanaweza kutokana na dawa za sulfo ni kuongezeka uzito. Unapaswa kuwa makini zaidi na ulaji wako na mazoezi, au kubadilisha dawa za sulfo na kuanza kutumia metformin au insulini. Baada ya mtu kutumia dawa za sulfo kwa muda mrefu zinaweza kushindwa kufanya kazi vizuri katika kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu. Kama hii itatokea, ongea na mfanyakazi wa afya.

Insulini

Insulini hutolewa kwa njia ya sindano. Hii ndiyo njia ya haraka zaidi ya kushusha sukari kwenye damu. Uchomaji wa sindano ya insulini unaweza kuibua woga mwanzoni, lakini taratibu watu hujifunza na hatimaye kuzoea jinsi ya kujichoma. Watu wenye kisukari Aina 1 wanahitaji insulini kuweza kuishi.

Insulini ni homoni ambayo mwili wako hutengeneza ili kudhibiti sukari kwenye damu yako katika kiwango kizuri. Watu wenye kisukari Aina 1 hawatengenezi insulini yoyote. Wale wenye kisukari Aina ya 2 hawatengenezi kiasi cha kutosha. Kuna hadithi za uwongo nyingi juu ya insulini. Insulini haisababishi upofu, haizidishi kisukari, na haimfanyi mtu kujenga tabia ya kuendelea kuitumia. Insulini hukusaidia kudhibiti kisukari chako na kuishi maisha yenye afya zaidi.

Kuna aina tofauti za insulini. Ipo aina ya insulini ambayo hufanya kazi mwilini taratibu lakini kwa muda mrefu, na hutakiwa kutumiwa mara 1 au 2 kwa siku kudhibiti sukari kwenye damu katika kiwango kizuri mchana na usiku. Aina nyingine ya insulini huanza kufanya kazi baada ya muda mfupi na hutakiwa kutumiwa kabla ya kula chakula ili chakula hicho kisipandishe sana kiwango cha sukari kwenye damu.

Hatari moja ya insulini ni kwamba inaweza kushusha kiwango cha sukari kwenye damu kupita kiasi. Mtu anaweza kuchanganyikiwa, kupatwa na kizunguzungu, kupoteza fahamu, na hata kufariki kutokana na kiwango kikubwa cha insulini. Zuia viwango vya sukari kushuka kupita kiasi kwa njia ile ile inayotumika kwa dawa za sulfo, kwa kula milo yako yote na kuweka karibu vitu vitamu kama vile pipi na vinywaji vyenye sukari kwa ajili ya dharura.

Kama utatumia insulini, kifaa cha glukomita cha nyumbani kitakusaidia kufuatilia kiwango cha sukari mara kwa mara na kuhakikisha kisishuke sana. Kama huna kifaa hiki cha glukomita, ni bora zaidi kutumia dozi ya chini ya insulini kuzuia sukari kwenye damu kushuka kupita kiasi. Bila njia ya kupima, ni heri sukari kwenye damu kuzidi kidogo kuliko sukari kushuka sana.

Kama una glukomita nyumbani, fuatilia viwango vya sukari wakati unapotumia insulini kuhakikisha visishuke kupita kiasi. Kama huna kifaa cha kupimia, ni bora zaidi kutumia dozi ndogo ya insulini kuzuia sukari kwenye damu kushuka hadi kiwango hatarishi.

sindano na kichupa cha insulini. ‘Kalamu’ ya insulini.
Watu wengi hutumia sindano kuchoma insulini Insulini pia huja katika muundo wa ‘kalamu’ maalum mahali sindano huchomekwa kwa ajili ya kila sindano inayochomwa. Kifaa hiki ni rahisi kutumia lakini ni ghali zaidi.

Insulini lazima ihifadhiwe katika hali yenye ubaridi. Kama hakuna friji, itunzeni kwenye bakuli ya maji yenye ubaridi na mbali na jua.

Baadhi ya dawa za mitishamba zinaweza kusaidia kushusha sukari

Waulize wataalam wa tiba za asili dawa gani za mitishamba zinapatikana katika eneo lako kwa ajili ya kupunguza sukari kwenye damu, njia bora zaidi za kuzitumia, na kama ni salama kuzitumia sambamba na insulini na dawa zingine.

Duniani kote, wataalam wa tiba za asili wamegundua vyakula na dawa za mitishamba ambazo zinaweza kusaidia kupunguza sukari kwenye damu. Ifuatayo ni mifano kadhaa:

 • Bitter melon
 • Uwatu (Fenugreek)
 • Fenugreek
 • Berberine
NWTND Diab Page 21-3.png
 • Mdalasini
 • Nopal (cactus)
 • Binzari ya manjano
NWTND Diab Page 21-5.png
 • Siki
 • Forosadi (Mulberry)
 • Mate tea
Sw NWTND Diab Page 21-4.png
 • Tangawizi
 • Gymnema
 • Bitter leaf
 • Majani ya mlonge
NWTND Diab Page 21-6.png


Ukurasa huu ulihuishwa: 20 Mei 2017