Hesperian Health Guides

Saratani nyingi zinaweza kuzuilika

HealthWiki > Toleo Jipya: Mahali Pasipo na Daktari > Saratani nyingi zinaweza kuzuilika

Katika sura hii:

Mambo mengi tofauti yanaweza kusababisha saratani, na kawaida hakuna njia yoyote ya kujua kama kitu gani kilisababisha saratani hiyo isipokuwa kwa:

Saratani zingine nyingi zinaonekana kutokana na kuathiriwa na muunganiko wa vitu hatari kadhaa.

Ingawa hatuwezi kuzuia saratani zote, tunaweza kupunguza hatari ya kupata saratani kwa kudhibiti mambo ambayo yanachangia saratani.

mwanaume na mwanamke wakivuta sigara mtoto mdogo akiwa amepakatwa.

Epuka moshi na uvutaji

  • Uvutaji tumbaku ni miongoni mwa sababu kubwa za saratani duniani. Uvutaji husababisha saratani ya mapafu na pia saratani ya utumbo mkubwa, kibofu, na shingo. Huchochea magongwa ya moyo, kiharusi, maambukizi kwenye mapafu, na vidonda vya tumbo, na wanawake wajawazito wakivuta au kupumua ndani moshi wa sigara wa watu wengine, kuna uwezekano mkubwa vichanga vyao kuugua au kuzaliwa vikiwa vidogo sana. Kuacha uvutaji hupunguza hatari ya saratani kwa mvutaji, bila kuzingatia una umri gani unapoacha uvutaji, na hulinda familia, wakiwemo watoto, na marafiki pia. Angalia sura ya Madawa ya kulevya, pombe na tumbaku (inaandaliwa) kwa taarifa zaidi jinsi ya kuacha uvutaji.
  • Moshi kutokana na kupikia ndani huongeza uwezekano wa saratani na magonjwa mengine ya mapafu. Kutengeneza jiko lisilotoa moshi au jiko ambalo hutoa moshi kidogo na kuutoa nje kupitia bomba (inaandaliwa) hupunguza uwezekano wa saratani kwa familia nzima. Angalia kitabu
  • Uchafuzi kutoka viwandani, magari madogo na magari ya mizigo husababisha saratani. Pale watu wanapopandisha madai yao na sheria zikaunga mkono madai yao, uchafuzi wa mazingira unaweza kupungua na saratani pia.
  • Kufanya zazi katika mazingira yenye moshi ni hatari. Kama wewe na wafanyakazi wenzako mnaweza kumshawishi kiongozi kazini kuboresha mfumo wa kuingiza na kutoa hewa, au angalau kuwapatia vifaa vya kuvaa puani na mdomoni kujikinga, afya yenu itakuwa bora zaidi.
mwanaume akinywa pombe kutoka kwenye chupa.

Punguza unywaji wa pombe

Kunywa zaidi ya glasi 1 au 2 za pombe kwa siku huchangia uwezekano wa kupata saratani mbalimbali. Saratani ya matiti, saratani ya ini, saratani ya tumbo na matumbo, na saratani ya mdomoni na kooni zote zinaweza kuhusishwa na unywaji pombe. Kunywa kidogo kunaweza pia kuokoa fedha zaidi kwa ajili ya chakula na mahitaji mengine ya familia. Angalia sura Madawa ya kulevya, pombe na tumbaku (inaandaliwa) kwa taarifa zaidi juu ya kuacha pombe.

Jilinde dhidi ya maambukizi na tafuta matibabu mapema

  • Bakteria H. pylori, ambayo husababisha vidonda vya tumbo, inaweza pia kusababisha saratani ya tumbo kama haitatibiwa. Kama una vidonda vya tumbo ambavyo hupotea na kurudi, pata matibabu kwa kutumia dawa zilizoelezewa sehemu za “Kidonda” na kwenye “Kutibu kidonda” katika Maumivu tumboni, kuhara, na minyoo.
  • Homa ya ini, Hepatitis B na C, zinaweza kusababisha saratani ya ini. Ipo chanjo ya homa ya ini, hepatitis B, na zote 2 hepatitis B na C zinaweza kuzuilika kwa kutumia kondom wakati wa tendo la ngono na kutotumia sindano ambazo zimekwisha kutumika. Angalia kwa taarifa zaidi juu ya homa ya ini.
  • Kirusi cha HPV (human papilloma virus), ambacho huambukizwa kupitia ngono, husababisha saratani ya shingo yaa kizazi kwa wanawake na baadhi ya saratani zingine miongoni mwa wanaume na wanawake. Ipo chanjo ya kuzuia maambukizi ya kirusi cha HPV.
  • VVU huchangia ueneaji wa baadhi ya saratani, hasa saratani ya Kaposi sarcoma, non-Hodgkin’s lymphoma, na saratani ya shingo yaa kizazi. Unaweza kujikinga dhidi ya VVU kwa kutumia kondom wakati wa ngono na kukataa kutumia sindano ambazo zimekwisha kutumika.

Lishe bora hutengeneza afya borah

Tabia za ulaji zinaweza kuchangia au kuzuia saratani. Kula nafaka ambazo hazijasindikwa, na mbogamboga na matunda ambayo yametoka shambani kila siku husaidia kukukinga dhidi ya saratani nyingi na magonjwa mengine. Angalia "Jinsi ya kula vizuri unapokuwa na uwezo mdogo". Kuhifadhi nafaka na maharagwe sehemu ambayo inapitisha hewa vizuri huzuia uharibifu kutokana na kuvu inayosababisha saratani ya ini.

Upatikanaji wa huduma za afya

Watu wanapokuwa wanapata huduma bora za afya, wanakuwa na afya bora na hupunguza hatari ya saratani. Upatikanaji wa huduma za afya pia husaidia kubainisha mapema saratani, hali ambayo huwezesha matibabu kufanikiwa zaidi.

Epuka mgusano na kemikali zenye sumu au mazingira yake

Maelfu ya kemikali hutengenezwa na kutumika viwandani na katika kilimo, na baadaye huachiwa na kuingia kwenye hewa tunayopumua, maji tunayokunywa, na chakula tunachokula. Baadhi ya kemikali hizi ni hatari kwa afya yetu, zikiwemo zile ambazo husababisha au kuchangia saratani. Kwa bahati mbaya hakuna sheria ambayo inalazimisha kemikali kuthibitishwa kuwa ni salama kabla ya kuanza kutumika, hivyo mara nyingi tunachelewa kugundua hatari ya kemikali hizo. Ongezeko la matumizi ya kemikali hizo duniani ni sababu mojawapo ya kuongezeka kwa kiwango cha saratani. Njia muhimu za kujilinda dhidi ya kemikali na saratani ni pamoja na:

  • Kuichukulia kemikali yoyote kuwa hatari hadi itakapothibitishwa kuwa siyo hatari.
  • Epuka matumizi ya viuatilifu na kemikali za kufanyia usafi, au kutumia vyombo ambavyo vinaweza kuwa viliwahi kutumika kuhifadhi kemikali.
  • Kutochoma taka za plastiki au taka zingine (hii huachia moshi wenye sumu kwenye hewa tunayopumua).
  • Kama huwezi kumshawishi kiongozi wako kazini kubadili na kuanza kutumia kemikali salama kazini, jaribu kuepuka kuzigusa au kupumua hewa, moshi au majivu yake. Vaa glovu, kifunika pua na mdomo, na mavazi maalum ya kujikinga, na nawa mikono yako mara kwa mara ili kemikali zisingie kwenye chakula chako au mdomo wako.
  • Himiza serikali zihakikishe mitambo ya nishati na viwanda vinashughulikia vizuri taka wanazozalisha ili wasisababishe uchafuzi wa mazingira. Kwa taarifa zaidi juu ya uhamasishaji jamii dhidi ya uchafuzi wa mazingira na kemikali, angalia Mwongozo wa Jamii juu ya Afya ya Mazingira, ambacho pia kinapatikana kutoka Hesperian.
Kielelezo cha njia ya uchafuzi kutoka kiwandani hadi kuingia kwenye mwili wa mama ambaye ananyonyesha Uchafuzi wa viwanda hatimaye huingia milini mwetu. Kusimamisha uchafuzi kutachangia saratani kupungua.

Tutakapothamini maisha ya binandamu kuliko faida, saratani itapungua.