Hesperian Health Guides

Matibabu ya saratani

Katika sura hii:

Matibabu ya saratani hutumika kujaribu kuuponya ugonjwa na vilevile kumsaidia mgonjwa kuishi maisha marefu zaidi akiwa na unafuu.

Aina ya matibabu ya saratani hutegemea aina ya saratani inayomsumbua mgonjwa, aidha ipo sehemu moja tu ya mwili au imekwisha kusambaa sehemu zingine za mwili, na hali ya afya ya mhusika. Njia za matibabu zinaweza kuwa tiba kwa njia moja moja au njia zaidi kwa pamoja. Njia nyingine ya matibabu inaweza kutumika kama njia ya kwanza haikufanikiwa vizuri. Kuna aina 4 za matibabu ya saratani.

  1. Upasuaji — huondoa seli za saratani kutoka kwenye mwili.
  2. Tibakemikali (chemotherapy) — hutumia dawa kuua seli za saratani.
  3. Tibamionzi — hutumia mionzi yenye nguvu kubwa kuua seli za saratani.
  4. Tiba ya homoni — uhutumia dawa kusimamisha homoni ambazo huzidisha saratani.


Ingawa matibabu yanaweza kuwa na madhara ya pembeni yanayokera, matibabu haya kawaida ndiyo njia pekee ya kuangamiza saratani, inayomwezesha mtu kuendelea kupata ahueni.

Baadhi ya njia za matibabu zina gharama zaidi kuliko zingine, na baadhi hazipatikani sehemu zote. Hivyo, kwa bahati mbaya, hakuna usawa pia katika matibabu ya saratani.

Kwa jinsi saratani inavyowathiri watu kwa namna tofauti, vivyo hivyo ndivyo matibabu ya saratani yalivyo. Kwa mfano, baadhi ya watu hupatwa na madhara ya pembeni mabaya wakati wengine hukabiliana na matibabu hayo vizuri zaidi. Au tiba moja inaweza kufanikiwa kupambana na saratani kwa mtu mmoja lakini hushindwa kufanya kazi ipasavyo kwa mwingine. Matibabu pia huathiri hisia za watu na afya ya akili kwa njia tofauti.

Kutoweka kwa dalili

Matibabu ya saratani yanapofanikiwa, vipimo haviwezi tena kuonesha uwepo wa saratani mwilini. Tumetumia msemo wa ‘kutoweka kwa dalili’ badala ya ‘kupona’, kwa sababu bado kuna uwezekano wa saratani kurudi baadaye. Mtu anaweza kuwa katika hali hiyo ya kutokuwa na dalili zozote baada ya matibabu kusimamisha saratani kuongezeka, lakini kivimbe au tyuma ikabaki pale pale.

Utahitaji uchunguzi wa mara kwa mara baada ya matibabu ya saratani. Uchunguzi huu hutegemea aina ya saratani.

mwanaume akiwa na plasta kwenye shavu.

Upasuaji

Saratani inapogudulika katika sehemu moja ya mwili, kuna uwezekano wa kuiondoa kwa mafanikio kupitia upasuaji. Wakati mwingine saratani ndogo ndogo (vivimbe au tyuma) vinaweza kuondolewa katika vituo vya afya vya kawaida. Saratani zingine huhitaji kulazwa hospitalini kwa ajili ya upasuaji na mtu atahitaji muda zaidi kupata ahueni.

Wakati mwingine upasuaji hufanyika pamoja na tibakemikali (chemotherapy) au tibamionzi (radiation) kuua saratani yoyote iliobaki ambayo haikuondolewa kupitia upasuaji.

Tibakemikali

Baadhi ya saratani zinaweza kutibiwa kwa dawa. Hii ndiyo tibakemikali. Dawa za tibakemikali kawaida ni ghali ingawa nyingi zimeanza kupatikana kwa bei nafuu. Programu za kitaifa za afya zinapaswa kurahihisha upatikanaji wa dawa hizi ili watu zaidi waweze kutibiwa na kunusurika kutokana na saratani.

Tibakemikali inaweza kutumika:

  • Kusimamisha saratani kusamba sehemu zingine za mwili.
  • Kupunguza kasi ya ukuaji wa saratani au kuifanya kunywea.
  • Kuiua saratani.
mwanamke akipatiwa dripu wakati mwanaume amempakata mtoto akiwa anangalia.

Wakati mwingine tibakemikali ndiyo tiba pekee inayohitajika, lakini kawaida hutumika pamoja na tiba ziingine. Kwa mfano, tibakemikali inaweza kutumika kuifanya saratani kunywea ili iwe rahisi kuiondoa kwa upasuaji. Au inaweza kutumika baada ya tibamionzi kuua saratani yoyote itakayokuwa imebaki.

Dawa za tibakemikali huwa katika miundo tofauti. Zinaweza kuwa kama vidonge au kama kimiminika kinachotumika kwa njia ya mdomo. Mara nyingi, dawa za tibakemikali hutolewa kupitia mshipa kama dripu. Ni kawaida pia kutumia zaidi ya dawa moja ya tibakemikali.

Kila baada ya muda gani tibakemikali huhitajika, na kwa muda gani, hutegemea aina ya saratani na dawa ya tibakemikali inayotumika. Hutegemea pia jinsi mwili wako unavyoitikia matibabu hayo, mwitikio ambao hutofautiana kati ya mtu na mtu. Tibakemikali inaweza kutolewa kila siku, kila wiki, au kila mwezi, lakini kawaida kuna kipindi cha kupumzika katika ratiba za matibabu kuruhusu mwili kupumzika na kupata ahueni.

Tibakemikali ni nzuri kwa kuua seli za saratani, lakini pia huathiri seli zenye afya. Seli zenye afya kawaida hupata ahueni na kurudia hali yake, lakini tibakemikali huuchosha mwili. Tibakemikali kawaida husababisha madhara ya pembeni yafuatayo:

  • Kichefuchefu (angalia Kusaidia kupunguza kichefuchefu).
  • Muwasho ndani ya pua na mdomo. Huenda ukajitokeza wekundu, vidonda, na wakati mwingine maumivu mdomoni na kooni. Uwezo wa mtu kuhisi ladha sahihi unaweza kubadilika, na anaweza kuhisi ladha ya chakula kuwa ya chuma au chungu kwa ujumla au hata tamu tamu. Kupunguza vidonda mdomoni, sukutua mdomoni mara kadhaa kila siku mchanganyiko wa: kikombe 1 cha maji safi au ambayo yamechemshwa na kupoozwa ili kubaki vuguvugu, ¼ kijiko cha chai cha magadi soda (baking soda), na ⅛ kijiko cha chai cha chumvi. Halafu baada ya kusukutua suuza mdomo na maji safi.
  • Uchovu. Pumzika pale utakapojihisi kutaka kupumzika. Matembezi ya dakika 15 kila siku yanaweza kukusaidia kupata nguvu. Inasaidia kunywa maji mengi na vinywaji vingine.
  • Kupoteza nywele. Tibakemikali huua seli za saratani na seli zingine zinazokua haraka. Nywele zitaota tena baada ya kuhitimisha matibabu.


Madhara ya pembeni yanaweza kuzidi kuwa mabaya zaidi siku chache baada ya matibabu, lakini huendelea kupungua taratibu.
Chukua tahadhari na afya yako wakati unapata matibabu kwa tibakemikali:

  • Pumzika kila unapojisikia.
  • Kula vyakula vyenye afya.
  • Epuka pombe, kwani inaweza kuathiri matibabu yako kwa tibakemikali na ini.

Tibamionzi (radiotherapy)

Kama ilivyo tibakemikali, tibamionzi huua seli za saratani na seli zingine zinazokua haraka. Tibamionzi inaweza kutumika kuondoa saratani, au kupunguza kasi na kukua kwa saratani. Tibamionzi inaweza kutumika peke yake au pamoja na upasuaji au tibakemikali.

Mashine za tibamionzi huachia miali/mionzi yenye nguvu kubwa kuua seli za saratani. Tibamionzi inaweza kuwa tiba nzuri iwapo saratani itagundulika mapema, kabla ya kuenea sehemu zingine mwilini. Hii ni kwa sababu, tofauti na tibakemikali, tibamionzi hulenga sehemu mahsusi ya mwili na haitibu mwili mzima. Matibabu kwa tibamionzi yanaweza kuondoa saratani mwilini kwa muda au kuiondoa kabisa.

mwanamke akiwa kwenye mashine ya tibamionzi.


Tibamionzi haina maumivu. Utalazwa kwenye meza ya matibabu chini ya mashine ya tibamionzi kwa dakika 15 hadi 30. Idadi ya matibabu na mara ngapi hutolewa hutegemea na aina ya saratani na ukubwa wa kivimbe (tyuma).

Madhara ya kawaida ya tibamionzi:

  • Uchovu. Pumzika kila unapojisikia. Matembezi ya dakika 15 kila siku yanaweza kukupa nguvu zaidi. Pia kunywa maji mengi na vinywaji vingine.
  • Kupoteza hamu ya chakula. Inaweza kuwa rahisi zaidi kula milo midogo mingi kuliko milo mikubwa michache. Kama unapata maumivu wakati wa, au baada ya kula, jaribu supu au vyakula laini ambavyo ni rahisi kumeza.
  • Mabadiliko ya ngozi. Ngozi juu ya sehemu iliotibiwa inaweza kugeuka pinki au nyeusi zaidi. Inaweza pia kuanza kuuma, kuhisi moto, kuwa kavu au kuwasha, kuonekana imeanza kuvimba, au kuanza kuota upele au malengelenge.
  • Kichefuchefu (angalia Kusaidia kupunguza kichefuchefu).


Madhara ya pembeni yatatoweka baada ya muda.

Jitunze vizuri wakati wa matibabu ya tibakemikali:

  • Pumzika kila unapojisikia.
  • Kula vyakula vyenye afya kama vile matunda na mbogamboga, vyakula vya protini, na nafaka ambao hazijasindikwa.
  • Kutunza ngozi ya sehemu iliotibiwa. Taratibu safisha ngozi hiyo kila siku. Epuka kitu chochote ambacho kinaweza kusababisha muwasho kwenye ngozi kama vile mavazi yanayobana, poda, au manukato.
  • Linda ngozi yako dhidi ya jua kwa kuvaa kofia na mavazi yasiobana ambayo yanafunika mwili mzima.

Tiba ya homoni

NWTND Can Page 7-1.png

Dawa ambazo huathiri homoni za mwilini zinaweza kusababisha kivimbe au tyuma kunywea, au kupunguza kasi ya ukuaji. Hii inaitwa tiba ya homoni. Dawa hizi kawaida huwa katika muundo wa vidonge, lakini baadhi hutolewa kupitia sindano. Tiba ya homoni inaweza kutolewa pamoja na tiba ya saratani moja au zaidi: upasuaji, tibakemikali, au tibamionzi.

Madhara ya pembeni ambayo yanaweza kutokea:

  • Uchovu
  • Kuongezeka uzito
  • Matatizo katika kutunza kumbukumbu au usahaulifu
  • Mabadiliko ya hisia au huzuni
  • Kuhisi joto kali ghafla, na kutokwa na jasho
  • Kukosa hamu ya ngono

Kusaidia kupunguza kichefuchefu

Kuhisi kichefuchefu kunaweza kuwa moja wapo ya madhara ya pembeni ya tibakemikali au tibamionzi. Pamoja na kukufanya kujisikia vibaya, kama kichefuchefu hakitakuzuia kula, utapata lishe ya kutosha. Kliniki au kituo cha afya cha karibu kinaweza kuwa na dawa za kupunguza kichefuchefu. Baadhi ya watu watahitaji kujaribu dawa tofauti kabla hawajapata ile inayoweza kuwasaidia. Pia jaribu njia zingine za kupunguza kichefuchefu zifuatazo ili kupata nafuu wakati wa siku na wiki ambazo utakuwa unapata matibabu hayo:

  • Kula mkate mkavu, chapati kavu, au nafaka zingine kwa ajili ya kutuliza tumbo lako. Epuka chakula chochote ambacho hukufanya ujisikie vibaya zaidi, hasa vyakula vilivyokaangwa au vyenye viungo vingi.
  • Kula milo midogo mingi badala ya milo 2 au 3 mikubwa, na kunywa, kila baada ya muda mfupi, kiasi kidogo kidogo cha vinywaji. Pia itasaidia kunywa kiasi kikubwa cha maji kuliko kawaida.
  • Kaa wima kwa muda mara baada ya kula badala ya kulala chini.
NWTND Can Page 8-1.png
  • Tumia tiba asili ya kubonyeza sehemu mbalimbali mwilini ya kurekebisha presha (acupressure) ili kupunguza kichefuchefu. Bonyeza sehemu ya ndani kwenye mkono wako iliyooneshwa kwenye picha, ukitembeza kidole chako katika miduara midogo. Bonyeza kwa nguvu lakini siyo kiasi cha kuumiza. Kama tiba hii inaelekea kusaidia, utaanza kusikia nafuu baada ya dakika chache.
NWTND Can Page 8-2.png
  • Kunywa chai ya majani ya mnanaa (mint) au tangawizi. Kutengeneza chai ya mnanaa, weka kijiko cha chai 1 cha majani ya mnanaa kwenye kikombe cha maji yanayochemka. Ruhusu majani kutulia kwa dakika chache kabla ya kunywa. Kutengeneza chai ya tangawizi, chemsha tangawizi iliyopondwa au kukatwa katika vipande vidogo kwenye maji angalau kwa dakika 15.
  • Mahali marijuana au bangi inaruhusiwa kisheria, baadhi ya watu huitumia kupunguza kichefuchefu au kumfanya mtu apate hamu ya kula.


Katika siku ya matibabu, baadhi ya watu hula kitafunwa au mlo mdogo kabla ya kutibiwa. Kwa wengine, kula au kunywa kitu chochote kabla au mara baada ya kutibiwa huwafanya kujisikia vibaya na hivyo huepuka utaratibu huo. Wakati wa matibabu, jaribu kutafuna kipande cha tangawizi kama kichefuchefu kitaanza. Baada ya matibabu, subiri angalau saa 1 kabla ya kula au kunywa chochote.

Tiba zingine za saratani

Kuna njia nyingine nyingi ambazo watu hujaribu kutumia kuponya saratani au angalau kupunguza madhara yake. Njia hizi zinajumuisha uponyaji kwa njia ya kiroho, hipnosisi taamuli (meditation), mitishamba, vyakula maalum, mazoezi ya kimwili, tibasindano au akupancha (tiba kwa kuchomachoma pini maalum maeneo mahsusi mwilini), na uchuaji au usuguaji mwili kuleta ahueni (massage). Mara nyingi njia hizi husaidia watu wanaopata tibakemikali au tibamionzi kwa sababu husaidia mwili kupata nafuu haraka na kupunguza madhara kutokana na saratani au tiba ya saratani. Pata ushauri wa daktari juu ya njia zipi ambazo zinaweza kwenda pamoja vizuri. Njia hizi zinaweza kupunguza wasiwasi au msononeko au huzuni ambavyo huwapata watu wengi wanaougua saratani na hivyo zinaweza kuwafanya kujisikia vizuri zaidi. Na zinaweza kumsaidia mtu kujisikia angalau vizuri kiasi kama anaelekea kufariki kutokana na saratani, kama hapati tena matibabu, au kama ameamua kutopata matibabu mengine tena. Hakuna njia yoyote miongoni mwa njia hizi ambayo imethibitika kuponya saratani.

Kwa bahati mbaya, kuna watu, wakiwemo madaktari, ambao hutumia fursa ya matumaini au kukata tamaa kwa watu wanaougua saratani kudai kuwa wana tiba maalum au za siri ambazo zinaweza kuponya saratani. Vibaya zaidi, kwa sababu ya ahadi hizi za uongo, watu hupoteza fedha zao au huchelewa kuanza matibabu ambayo yangeweza kuwasaidia zaidi.