Saratani ni tatizo gumu kwa kila mtu, lakini ni gumu zaidi kwa watu maskini. Watu wenye hali duni au ambao hawapati huduma za msingi wako katika hatari kubwa ya kupatwa na saratani, kwani huishi mahali ambapo uchafuzi wa mazingira umekithiri. Hufanya kazi hatarishi, na hukabiliwa na msongo zaidi. Kula mchanganyiko wa vyakula vizuri (matunda na mbogamboga kutoka shambani, protini, na nafaka ambazo hazijasindikwa) vinaweza kusaidia kuzuia saratani, lakini baadhi ya watu hawawezi kumudu kula vizuri. Na watu wenye hali duni kawaida hawawezi kumudu gharama za uchunguzi wa afya, dawa, na huduma za afya zenye uwezo wa kubainisha na kutibu saratani zao.
Kwa sababu zote hizi, tunaweza kusema umasikini na ukosefu wa usawa katika upatikanaji huduma huchangia tatizo la saratani.
Kampuni za utengenezaji dawa kwa ajili ya saratani kawaida hazina masilahi na afya ya watu, lakini lengo lao kuu ni kutengeneza faida. Mwaka 2014, mkuu wa kampuni ya maarufu ya dawa ya Bayer pharmaceutical company alisema kuwa dawa yao mpya ya saratani ni ghali sana na siyo kwa ajili ya watu wa India, lakini ni kwa “wagonjwa katika nchi za magharibi (Ulaya na Marekani) ambao wanaweza kumudu bei yake”.
Dawa za saratani za kuokoa maisha zinapaswa kupatikana kwa kila mtu, siyo kuwa chanzo cha faida.