Hesperian Health Guides

Saratani za kawaida

Katika sura hii:

Kila aina ya saratani ni tofauti, na ina visababishi, dalili, na njia za matibabu tofauti. Baadhi ya saratani ni rahisi kuzuiwa na kutibiwa, na zingine ni hatari sana kwa maisha. Hata katika maeneo ambapo watu wanaishi katika umasikini, aina nyingi za saratani zinaweza na zinapaswa kutibiwa.

mwanaume akikohoa.

Saratani ya mapafu

Dalili
 • Kukohoa
 • Kukohoa damu
 • Maumivu ya kifua, kawaida upande mmoja
 • Ugumu katika kupata pumzi ya kutosha


Mara mtu anapokua na dalili hizi, saratani ya mapafu inakuwa imefika kiwango cha juu.

NWTND Can Page 10-2.png

Saratani ya mapafu ndiyo saratani inayojitokeza sana kwenye jamii kuliko saratani zingine, na pia ni miongoni mwa saratani ambazo zinazuilika zaidi. Kawaida husababishwa na uvutaji, na bila kujali umevuta kwa muda gani. Kuacha uvutaji katika hatua yoyote ile hupunguza uwezekano wa kupata saratani ya mapafu. Uvutaji sigara pia husababisha aina zingine za saratani. Mtu ambaye anaishi kwenye nyumba ambapo kuna mvutaji au anafanya kazi sehemu ambapo watu huvuta pia ataathirika, hata kama yeye mwenyewe siyo mvutaji.

Aina zingine za moshi pia huchangia saratani ya mapafu. Kwa mfano, moshi wa dizeli kutoka kwenye magari, moshi kutoka viwandani, na moshi kutokana na shughuli za upikaji. Kama unavuta na pia unakaa katika mazingira ya moshi sehemu za kazi au nyumbani, uwezekano wa kupata saratani ya mapafu ni mkubwa zaidi.

Saratani ya mapafu kawaida inaua. Njia bora ya kuzuia saratani ya mapafu ni kuacha uvutaji. Kwa msaada zaidi, angalia sura ya Madawa ya kulevya, pombe na tumbaku (inaandaliwa).

Saratani za utumbo mkubwa na rektamu (njia ya haja kubwa)

Kuhusiana na aina hizi 2 za saratani ya sehemu ya chini ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula, kuna uwezekano zaidi wa kuzipata kama wanafamilia wa karibu nao wanazo. Pia hujitokeza zaidi miongoni mwa watu ambao tayari wana aina zingine za magojwa ya matumbo, kama vile vidonda ndani ya matumbo.

sura ya mtu kutoka nyuma ikionesha "utumbo mkubwa", "rektamu", na "unyeo".
tumbo mkubwa
rektamu
unyeo

Baadhi ya kiliniki huchunguza aina hizi za saratani kwa kuchukua sampuli ya kinyesi cha mtu na kupima iwapo kuna dalili za damu.

Aina hizi za saratani kujitokeza kwa kiwango kidogo kwa wanaume na wanawake ambao hutumia sana mbogamboga, matunda, nafaka ambazo hazijasindikwa, na vyakula vingine vyenye nyuzinyuzi kila siku. Unywaji mdogo wa pombe na kutovuta sigara humlinda mtu dhidi ya saratani hizi.

Dalili
 • Kinyesi cheusi au chenye damu
 • Maumivu tumboni
 • Mabadiliko katika jinsi unavyojisaidia haja kubwa: kuongezeka au kupungua kwa mara ngapi unakwenda chooni, au kuharisha au kufunga choo (kutopata choo barabara).


Anemia inaweza pia kuwa dalili. Hisia za uchovu, na kupungua uzito ni dalili za saratani hiyo inapokuwa imefikia kiwango cha juu.

Matibabu

Zikigundulika mapema, saratani hizi zinaweza kutibiwa kwa njia ya tibakemikali au kuondolewa kwa upasuaji. Kutegemea na wapi ilipo na ukubwa wa sehemu ya matumbo ambayo inapaswa kuondolewa, upasuaji unaweza kujumuisha uundaaji wa unyeo bandia wa muda au wa kudumu kwa kutoboa tundu katika utumbo mpana. Katika operesheni ya uundaji wa unyeo bandia, daktari huunganisha, kwa kushona, sehemu hai ya utumbo na mlango au tundu kwenye tumbo ili kinyesi kiweze kuchepushwa kwa kukwepa sehemu ambayo saratani iliondolewa na kwenda moja kwa moja kwenye chombo, kawaida mfuko maalum nje ya mwili. Kadri stadi za matibabu na upasuaji saratani za utumbo mkubwa na rektamu zinavyozidi kuboreshwa, operesheni za uundaji wa unyeo bandia chache zinahitajika.

Saratani ya shingo ya kizazi

Saratani inapoathiri sehemu kubwa ya tumbo la uzazi (kizazi), huitwa saratani ya tumbo la uzazi. Lakini inapoathiri mlango wa tumbo la uzazi, huitwa saratani ya shingo ya kizazi. Saratani ya shingo ya kizazi ni aina ya saratani ambayo hujitokeza sana na kukua polepole. Saratani hii inatibika kama itagundulika mapema. Na kukiwa na programu nzuri za huduma ya afya, inaweza kuzuilika kabisa. Saratani ya shingo ya kizazi hujitokeza sana miongoni mwa wanawake wenye VVU kwa sababu mifumo yao ya kinga haiwezi kupambana na maambukizi vizuri. Ni muhimu sana kwa wanawake wenye VVU kupata kipimo cha saratani ya shingo ya kizazi mara kwa mara-angalau mara moja kwa mwaka, kama inawezekana.

Kirusi cha HPV, ambacho huambukizwa kupitia ngono (angalia sura Maambukizi sehemu za ukeni au umeni na matatizo mengine – inaandaliwa), ndiyo kisababishi kikuu cha saratani ya shingo ya kizazi. Kirusi hiki cha HPV kimeenea sana kiasi kwamba wanaume na wanawake wengi huambukizwa. Lakini ni baadhi ya aina za HPV tu ambazo husababisha saratani.

Shingo ya kizazi
mchoro wa sehemu ya mwili wa mwanamke ukionesha viungo vya uzazi na mshale ukielekeza kwenye ‘shingo ya kizazi’.

Chanjo dhidi ya kirusi cha HPV huzuia aina nyingi za kirusi hiki ambacho husababisha saratani (kuna aina nyingi za HPV). Programu ya chanjo kwa wasichana na wavulana wote kwenye jamii yao inaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya wanawake ambao wanapata saratani ya shingo ya kizazi, lakini haitaondoa saratani hii moja kwa moja. Uchunguzi na kuibainisha mapema ndiyo muhimu zaidi ili iweze kutibika mapema. Vyote 2 –uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi na matibabu yake ni rahisi kufanyika na kwa mafanikio makubwa.

Saratani ya shingo ya kizazi hujitokeza sana miongoni mwa wanawake wenye VVU kwa sababu mifumo yao ya kinga haiwezi kupambana na maambukizi vizuri. Ni muhimu sana kwa wanawake wenye VVU kupata kipimo cha saratani ya shingo ya kizazi mara kwa mara-angalau mara moja kwa mwaka, kama inawezekana.

Dalili

Mwanzoni, saratani ya shingo ya kizazi haina dalili ambayo inaonekana wazi. Baadaye, kunaweza kuwa na damu ikitoka ukeni wakati wa tendo la ngono, au wakati wote nje ya hedhi. Kama saratani haitatibiwa, inaweza kusababisha maumivu - kwanza mgongoni sehemu ya chini au kwenye nyonga, na baadaye chini miguuni sehemu ya nyuma.

Uchunguzi

Saratani ya shingo ya kizazi ni nadra kuua kama ikigundulika mapema. Programu za uchunguzi ambazo huwapima wanawake wote mara kwa mara ni rahisi kuanzisha, hata kwenye kiliniki ndogo vijijini. Kila mojawapo ya vipimo 3 tofauti kwa ajili ya saratani ya shingo ya kizazi kina manufaa yake:

daktari akimfanyia mwanamke kipimo cha nyonga.
Vipimo vya saratani ya shingo ya kizazi vinaweza kufadhaisha kidogo, lakini havisababishi maumivu.
 • Kukagua kwa macho au kipimo cha siki (vinegar test), (kuangalia shingo ya kizazi baada ya kupaka siki au Lugol’s iodine). Kipimo hiki kina gharama ndogo sana, hakihitaji maabara, na ni rahisi kujifunza. Wakati mwingine seli zenye afya huonekana kuwa na hitilafu, hivyo kama hilo litatokea vipimo vingine hutumika kuhakiki matokeo. Kujifunza jinsi ya kufanya ukaguzi kwa kuangalia kwa macho, angalia Kitabu cha Wakunga, ambacho kinapatikana kutoka Hesperian.
 • Kipimo cha Pap (Pap smear). Kipimo cha Pap kinaaminika sana lakini kinaweza kutobainisha saratani hiyo kila mara. Hivyo kipimo kinapaswa kurudiwa kila miaka 3 au karibu na hapo.
 • Kipimo cha HPV. Hiki ni kipimo kwa ajii ya kirusi cha HPV ambacho husababisha saratani ya shingo ya kizazi. Kipimo hiki kinaweza kufanyika peke yake, au pamoja na kipimo cha Pap, au baada ya Pap kuonesha kama kuna saratani.
Matibabu

Saratani za shingo ya kizazi zikigundulika mapema ni miongoni mwa saratani ambazo hutibika kwa mafanikio zaidi. Baadhi ya matibabu ni rahisi na gharama yake ni nafuu kiasi kwamba huweza kufanyika kwenye kiliniki na mfanyakazi aliyepitia mafunzo, mara baada ya uchunguzi kuibainisha saratani.

 • Tibabaridi (Cryotherapy) hugandisha sehemu ya shingo ya kizazi (seviksi) kwa kutumia dioksidi ya kaboni au gesi ya nitrous oxide. Ugandishaji huua seli zenye hitilafu na kuzizuia kuendelea kugeuka saratani. Tibabaridi haina maumivu na ni salama. Tibabaridi ina gharama nafuu na ni rahisi kwa wafanyakazi wa afya na wakunga kujifunza kuitoa. Angalia Kitabu cha Wakunga, kinapatikana kutoka Hesperian.
 • Utaratibu wa upasuaji wa LEEP (Loop electrosurgical excision procedure) ni utaratibu wa upasuaji wa kutoa tishu yenye hitilafu kutoka kwenye shingo ya kizazi. Utaratibu wa LEEP hutumia waya laini wenye umbo la kitanzi unaopitisha umeme, kuondoa sehemu ya shingo ya kizazi yenye seli zenye hitilafu. Utaratibu wa LEEP unahitajika kama eneo lenye seli zenye hitilafu kwenye shingo ya kizazi ni kubwa, au linafika hadi ndani ya mlango wa shingo ya kizazi.
 • Utaratibu wa upasuaji kwa kisu (Cold knife conization). Utaratibu huu hutumia kisu cha upasuaji kuondoa sehemu kubwa ya shingo ya kizazi kama eneo ambalo limeonekana kuathiriwa na saratani ni kubwa sana. Upasuaji huu hufanywa na mtaalam. Upasuaji kwa kisu husababisha uwezekano mkubwa wa mimba kuharibika au matatizo mengine mwanamke huyu atakapopata ujauzito siku za usoni.


Kama saratani imefikia hatua mbaya sana, inaweza kuhitaji kuondoa kabisa mji wa mimba (uterasi) kwa njia ya upasuaji. Hii itaondoa kabisa uwezekano wa kupata ujauzito tena, lakini huongeza uwezekano wa kunusurika saratani.

Saratani ya kibofu

Kuna sababu kuu 3 za saratani ya kibofu:

 • Uvutaji.
 • Kuathiriwa na kemikali zenye sumu, kawaida sehemu za kazi, viwandani na migodini. Kwa mfano, saratani ya kibofu hujitokeza sana miongoni mwa wafanyakazi wanaotengeneza au kushughulika na vyuma, rangi, mpira (rubber), ngozi, nguo, kapeti, saruji, na plastiki. Pia hujitokeza sana miongoni mwa wafanyakazi migodini, mafundi umeme, na wengine ambao hushughulika na kemikali na moshi wake.
 • Kichocho (angalia sura Magonjwa mengine hatari, inaandaliwa). Katika maeneo mahali ugonjwa huu umeenea, hiki ndicho chanzo kikuu.
Dalili
 • Damu kwenye mkojo.
 • Kutoa mkojo kwa kasi sana, au mara nyingi zaidi.
 • Maumivu mgongoni upande mmoja, sehemu ya chini, juu kidogo ya katikati ya mfupa wa nyonga, au kwenye msamba (kati ya unyeo na ukeni au korodani).
 • Kukojoa kwa shida, lakini watu wengi wenye saratani ya kibofu huwa hawana maumivu wanapokuwa wanakojoa.


Dalili hizi pia ni dalili za matatizo mengine ya kibofu. Angalia sura Matatizo katika ukojoa (inaandaliwa).

Matibabu

Saratani ya kibofu kawaida hutibiwa kwa njia ya upasuaji kuondoa kivimbe au tyuma, au sehemu ya kibofu ambayo imeathirwa na saratani. Tibakemikali pia inaweza kutumika kukifanya kivimbe kunywea kabla ya upasuaji, au kuzuia saratani kurudi baada ya upasuaji. Kama kivimbe ni kikubwa sana, kibofu kizima kinaweza kuondolewa kwa njia ya upasuaji.

Saratani ya kibofu inaweza kurudi. Uchunguzi wa ziada mara kwa mara unahitajika baada ya matibabu kuhakikisha kuwa saratani hairudi.

Saratani ya ini

Saratani ya ini ni hatari hasa na ugonjwa mgumu kutibika. Hujitokeza sana miongoni mwa wanaume.

ini la mwanaume likioneshwa na mshale.
Ini
Dalili

Kawaida haina dalili. Hata hivyo, karibu kila mtu mwenye saratani ya ini amewahi kuugua ugonjwa wa homa ya ini (hepatitis) au sirosisi-ini kuharibiwa kwa sababu ya matumizi makubwa ya pombe au kwa sababu ya ugonjwa. Hivyo mtu mwenye saratani ya ini anaweza kuwa na dalili za ugonjwa wa ini:

 • Umanjano (rangi ya manjano kwenye ngozi na machoni)
 • Maumivu tumboni sehemu ya juu kulia
 • Tumbo kuvimba
 • Kusikia uchovu kila mara
Uzuiaji

Saratani hii ni ngumu kutibika, lakini chanjo ya homa ya ini (hepatitis B) husaidia kuzuia matukio mengi. Angalia taarifa juu ya homa ya ini (hepatitis).

Kuzuia sirosisi ambayo inasababishwa na pombe, epuka kunywa zaidi ya kipimo 1 au 2 vya pombe kwa siku. Kama tayari unaugua ugonjwa wa ini, mathalan homa ya ini (hepatitis), unaweza kupunguza hatari ya kupata saratani ya ini kwa kutokunywa pombe kabisa.

Saratani ya matiti

Saratani ya matiti ni miongoni mwa saratani zinazowaathiri sana wanawake ingawa wanaume nao wanaweza kupata saratani ya matiti. Inapogundulika mapema, saratani ya matiti inaweza kutibika kwa mafanikio. Inaweza kutibiwa kwa upasuaji, tibamionzi, tibakemikali, tiba ya homoni, au baadhi ya njia hizo kwa pamoja.

Mtu yoyote anaweza kujifunza kuchunguza matiti kwa ajili ya vivimbe au dalili isiyo ya kawaida. Vivimbe vyenye asili ya saratani kawaida huwa vigumu, havina maumivu, umbo lake huwa na manundu, na huwa halitembei chini ya ngozi. Chunguza kila titi kwa wakati. Uchunguzi zaidi kwa njia ya eksirei au kwa njia ya mashine inayonasa mawimbi ya sauti ndogo mwilini, ambayo hayawezi kusikika kwa sikio la kawaida (ultrasound), unaweza kubainisha kama kivimbe kina uwezo wa kuwa saratani. Lakini utahitaji biopsi (uchunguzi wa kwa darubini wa tishu iliokatwa kutoka mwili-hai) ili kuwa na uhakika.

mwanamke akifanya uchunguzi wa titi lake.
Uchunguzi makini wa titi huchukua dakika kadhaa. Mwanamke au daktari kwa mpangilio hugusa na kusugua kwa nguvu kila pointi kwenye titi kabla ya kwenda pointi nyingine. Huhisi kitu chochote ambacho siyo cha kawaida kama vile kivimbe, sehemu ambayo inaanza kugandamana na kuwa gumu, au mabadiliko ya rangi. Fanya hivi kwa titi lote na chini ya mkono.


Hakuna mengi ya kufanya katika kuzuia saratani ya titi, ingawa kula vizuri, kuepuka pombe na sigara, na kupata mazoezi ya mara kwa mara husaidia. Unyonyeshaji pia husaidia kutoa kinga.

Saratani ya tumboni

NWTND Can Page 16-2.png
Dalili
 • Maumivu tumboni
 • Kupungua uzito
 • Matatizo katika kumeza
 • Kitu kama vile tungamo au rundo ambacho unaweza kuhisi na kugusa tumboni
 • Choo cheusi (kinaweza kuonekana kama lami)

Sababu kuu ya saratani ya tumboni ni maambukizi ya bakteria anayejulikana kama H. pylori, ambaye ndiyo chanzo kikuu cha vidonda vya tumbo. Ingawa H. pylori huongeza hatari ya saratani ya tumboni, mambo mengine pia huchangia uwezekano wa saratani ya tumboni, kama vile uvutaji sigara, kula sana nyama zilizosindikwa, nyama nyekundu, vyakula vilivyokaangwa sana, na vyakula ambavyo vimehifadhiwa kwa chumvi.

Saratani nyingi za tumboni ni ngumu kutibika kwa mafanikio. Ni bora zaidi kuzuia saratani hizi. Ulaji wa matunda, mbogamboga mbichi, na nafaka ambazo hazijasindikwa kila siku hutoa kinga kiasi.

Saratani ya tezi dume

Wanaume wana tezi dume, sehemu ya chini kidogo na kibofu, ambayo huongezeka ukubwa kadri wanavyozeeka. Saratani ya tezi dume kawaida hukua polepole na inaweza kuchukua miaka kadhaa ndiyo iweze kusababisha matatizo. Kama ilivyo kwa saratani zingine, matibabu ya saratani ya tezi dume hufanikiwa zaidi saratani inapogundulika mapema. Hata saratani ya tezi dume ambayo imeenea inaweza kutibiwa kwa mafanikio. Saratani ya tezi dume hujitokeza zaidi miongoni mwa wanaume wenye umri zaidi ya miaka 65, na wale wenye umri mkubwa zaidi wenye saratani hiyo huishi nayo hadi kifo, mara nyingi kikisababishwa na mambo mengine.

Dalili

Saratani ya tezi dume inaweza kutoonesha dalili zozote katika hatua za mwanzo. Wanaume wengi huwa hawajui wanayo hadi inapogundulika wakati wa uchunguzi wa kitabibu.

Dalili kubwa ni matatizo katika kukojoa, lakini hili linaweza pia kusababishwa na tezi dume kuongezeka ukubwa ambako hakuhusiani na saratani. Jambo hili ni kawaida kwa wanaume wenye umri mkubwa.

Sababu za kumuona mfanyakazi wa afya:

 • Matatizo katika kuanza kutoa mkojo au kusimamisha mkojo.
 • Hisia za kutaka kukojoa kila baada ya muda mfupi, hasa usiku
 • Maumivu au hisia za kuungua wakati wa kukojoa
 • Damu kwenye mkojo au shahawa
 • Maumivu makali na ya mara kwa mara sehemu ya chini mgongoni, tumboni, kiunoni, au sehemu za nyonga


Kipimo maalum cha damu cha PSA (prostate-specific antigen) kinaweza kusaidia kubainisha kuwepo kwa saratani ya tezi dume. Kiwango cha juu cha PSA humaanisha uwepo wa saratani ya tezi dume, lakini kinaweza pia kumaanisha tezi kupanuka au kupata maambukizi (angalia sura Matatizo katika kukojoa, kinaadaliwa).

Matibabu

Jinsi saratani ya tezi dume itakavyotibiwa (upasuaji, tibamionzi, tibakemikali, tiba ya homoni, au mchanganyiko wa tiba hizi) hutegemea aina ya seli za saratani, kama zimeenea, umri wako na afya kwa ujumla, na upendeleo wako. Baadhi ya saratani za tezi dume huota polepole mno na matibabu pekee yaliyopo ni kuchunguzwa afya mara kwa mara.

Saratani ya ngozi

Saratani za ngozi hujitokeza sana miongoni mwa watu wenye ngozi nyepesi nyeupe, na ni nadra miongoni mwa watu wenye ngozi nyeusi, lakini inaweza kumpata mtu yoyote. Huwapata mara nyingi watu wazima ambao walipata majerahajua mabaya walipokuwa watoto.

Kuna aina kuu 2 za saratani ya ngozi. Saratani ya ngozi aina ya Non-melanoma, ndiyo hujitokeza sana, na inatibika kwa urahisi kwa sababu huota polepole na inaweza kuondolewa na mfanyakazi wa afya. Aina ya pili, melanoma, ndiyo hatari zaidi kuliko saratani za ngozi zote.

mwanaume akiwa na kidonda kwenye pua na juu ya shavu.
mwanaume akimvalisha mtoto mvulana kofia.
Saratani aina ya non-melanoma kawaida huonekana kama kivimbe chekundu au cha pinki ambacho kinakua polepole, kidonda, au ganda la kidonda usoni au sehemu nyingine kwenye ngozi. Saratani hizi zinaweza kukatwa na kuondolewa kama zitaendelea kukua kwa sababu husambaza saratani ndani ya mwili.

Melanoma ni aina ya saratani ya ngozi ambayo hukua haraka na ni hatari. Inapaswa kutibiwa mara moja bila kuchelewa. Kwanza eneo lililoathirika hukatwa na kutolewa nje. Matibabu mengine yanaweza kuhitajika kama saratani itakuwa imeenea sehemu zingine za mwili.

Dalili za saratani ya melanoma ya ngozi

Melanoma huonekana tofauti na baka jeusi kwa kigezo kimoja au zaidi:

NWTND Can Page 18-2.png Umbo lake lina sura isiyo ya kawaida-siyo mduara au wala umbo wa yai
NWTND Can Page 18-3.png Mwisho wake pembeni hakujasawazika-kuna manundu
NWTND Can Page 18-4.png Huwa na rangi tofauti katika baka moja
NWTND Can Page 18-5.png Hubadilika ukubwa, rangi, au umboe
Uzuiaji

Walinde watoto, hasa wenye ngozi laini nyeupe, kwa kutumia kofia, nguo ambazo zinafunika mikono na miguu, na mafuta ya kuwakinga dhidi ya madhara ya miali ya jua.

Kama huwa unafanya kazi juani au sehemu za nje, funika ngozi yako na vaa kofia.

Saratani ya Kaposi sarcoma

Hii ni saratani ya ngozi ambayo huwaathiri baadhi ya watu ambao wameambukizwa na VVU. Saratani ya Kaposi sarcoma hudhihirishwa na vivimbe au vidoa vyekundu, vyenye rangi ya udongo, au zambarau ndani ya mdomo au sehemu yoyote kwenye mwili.

Dalili

Madoa yasiyo na maumivu ambayo huonekana kama mavilio kuzunguka au ndani ya mdomo, au sehemu yoyote kwenye mwili. Madoa au mavilio hayo kawaida hayana maumivu, isipokuwa yanapopasuka au kutobolewa.

Matibabu

Muone daktari au mfanyakazi wa afya mwenye uzoefu na suala la VVU. Dawa za kupunguza VVU kuzaliana (ARV) husaidia kuzuia aina hii ya saratani kwa watu wenye VVU, na kuanza matibabu ya ARV huweza kusaidia kudhibiti isiongezeke. Wakati mwingine saratani ya Kaposi sarcoma hutibiwa kwa tibakemikali, au na dawa zingine.