Hesperian Health Guides

Kupunguza maumivu makali ya saratani

HealthWiki > Toleo Jipya: Mahali Pasipo na Daktari > Kupunguza maumivu makali ya saratani

Katika sura hii:

Maumivu ya saratani yanaweza kusababishwa na saratani yenyewe au matibabu yake. Kwa mfano, watu wanaopata tibakemikali wanaweza kupata maumivu mdomoni.

Kadri saratani inavyozidi, maumivu yanayosababishwa na saratani yanaweza kuongezeka na kuwa makali zaidi. Dawa zenye nguvu za kupunguza maumivu kama vile mofini au kodeini (morphine or codeine) hutuliza maumivu kwa mafanikio zaidi, na dozi ya dawa hizi inaweza kuongezwa kuanzia kiwango cha chini hadi cha juu ili iweze kufanya kazi vizuri.

Kwa sababu dawa hizi zinaweza kujenga tabia ya kutaka kuzitumia wakati wote, dawa zenye nguvu za kupunguza maumivu (zenye asili ya kutia usingizi-narcotics) mara nyingi hazipatikani. Serikali na wafanyakazi wa afya kwa nia njema hudhibiti matumizi yake kwa kuogopa kuchangia matumizi mabaya na tabia ya ulevi wa dawa hizi. Hali hii husababisha mateso zaidi yasiyostahili kwa watu wanaoteseka na saratani na magonjwa mengine yasiyopona. Dawa hizi zimeorodheshwa kwenye orodha ya Dawa za Msingi ya Shirika la Afya Duniani lakini juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha zinapatikana kwa watu wenye saratani na wengine wanaoteseka na maumivu makali. Tunapaswa kupambana na unyanyapaa kuhusiana na dawa hizi, na kutambua umuhimu wake katika kupunguza maumivu kama haki ya binadamu.

Njia zingine za kutuliza maumivu ya saratani au matibabu ya saratani ni pamoja na akupancha (tiba ya visindano), ukandaji na usuguaji sehemu za mwili, na kufanyiwa mazoezi ya viungo mbalimbali vya mwili.

Huduma kwa ajili ya siku za mwisho wa uhai

Kuna saratani ambazo haziwezi kupona, bila kujali unaishi wapi au unatumia fedha kiasi gani. Ingawa mgonjwa hatapona saratani, mtazamo chanya utasaidia kuinua moyo na kuboresha siku za mwisho za mtu mwenye saratani, na hata kuleta unafuu kiasi kwa wapendwa wake. Kuwa na mtazamo chanya kunaweza kumsaidia mtu kupata nguvu zinazohitajika kila siku, hata kama atakuwa anapata matibabu au la.

wanafamilia wakiwa wamezunguka kitanda cha mwanamke anayekaribia kufa.

Kwa saratani ambazo haziwezi kupona, hatimaye utakuja wakati ambapo inakuwa wazi kwamba kifo kinakaribia. Hatua hii inapofika, msaidie ngonjwa na wale wanaompenda kuelewa kinachoendelea, na kujiandaa. Mkumbushe kwamba utakuwepo kwa ajili yake kwa maisha yake yaliyobaki hadi siku ya kifo. Anaweza kuhitaji matibabu kupunguza maumivu, na huduma yenye upendo kumpa faraja na urahisi katika kufariki. Angalia sura ya Kuwahudumia wagonjwa (inaandaliwa) kwa taarifa zaidi juu ya kumhudumia mtu wakati anafariki.