Hesperian Health Guides

Saratani miongoni mwa watoto

HealthWiki > Toleo Jipya: Mahali Pasipo na Daktari > Saratani miongoni mwa watoto

Saratani haijitokezi sana katika umri wa utoto. Ikijitokeza, aina ya saratani ambazo huwakumba sana watoto ni saratani ya damu (leukemia) na uvimbe(tyuma) kwenye ubongo. Kwa ujumla, saratani za watoto hutibiwa na kupona kwa urahisi zaidi kuliko za watu wazima.

Saratani nyingi miongoni mwa watoto siyo rahisi kubainishwa. Kawaida dalili siyo bayana, kama vile kuendelea kupungua uzito, maumivu ya kichwa pamoja na kutapika hasa saa za asubuhi, uvimbe wa muda mrefu au maumivu, homa za muda mrefu, au mavilio au kutokwa na damu kusio kwa kawaida. Zote hizi zinaweza kuwa dalili za matatizo mengine — baadhi yanaweza kuwa matatizo makubwa, na mengine siyo makubwa. Kama mtoto ana tatizo lolote la kiafya ambalo limechukua muda mrefu, anatakiwa kuchunguzwa afya yake na daktari au mfanyakazi wa afya.

mtoto mwenye shavu ambalo limevimba.

Saratani ya Burkitt lymphoma

Hasa katika maeneo ya Afrika, saratani ambayo hujitokeza sana ni saratani ya Burkitt lymphoma. Huanza kama bonge usoni, kwenye taya ya juu au chini. Tofauti na matumbwitumbwi (mumps), au tezi ambazo huvimba mara nyingi kuhusiana na VVU, ni upande mmoja tu wa uso ambao huvimba na huvimba haraka sana. Uvimbe unaweza kuongezeka mara 2 katika siku moja. Hauna maumivu, ingawa siku za mwanzoni unaweza kusababisha kutojisikia vizuri. Meno karibu na uvimbe hutoka katika naf asi yake au kulegezwa. Saratani hii inaweza kufikiriwa kimakosa kuwa jipu la jino.

Saratani ya Burkitt lymphoma hutibiwa kwa tibakemikali. Matibabu yanapoanza mapema, kawaida hufanikiwa zaidi.